Ile shughuli ya magwiji ndo leo!
LILE pambano la kufungulia msimu mpya wa 2025-26, linapigwa leo jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Simba na Yanga zinakutana kwa mara nyingine likiwa ni pambano la 11 tangu mwaka 2001 michuano hiyo ilipoasisiwa kwa lengo la kufungulia msimu mpya wa mashindano.
Katika mechi 10 za awali kwa timu hizo kukutana katika Ngao ya Jamii, ikiwamo nusu fainali ya msimu uliopita, kila moja imeshinda mara tano na kupoteza tano vilevile.
Lakini rekodi zinaonyesha kuwa kwa muda wa miaka 20 ya kuchezwa kwa mechi hizo za Ngao, ni klabu nne tu zilizowahi kutwaa, Simba ikiongoza kwa kubeba mara 10 ikifuatiwa na Yanga (8), kisha Azam FC na Mtibwa Sugar zikifuata kila moja ikitwaa mara moja.
Hata hivyo, wakati Simba inaongoza kwa kutwaa mara nyingi taji hilo, Yanga ndio inayoonekana kuwa timu iliyopoteza fainali nyingi zaidi za michuano hiyo ikiwa ni mara saba kati ya mechi 15 ilizocheza, ikifuatiwa na Azam iliyopoteza sita kati ya mechi saba ilizocheza.
Simba yenyewe inashika nafasi ya tatu kwa kupoteza mechi nyingi ikiwa ni nne kati ya 14 ilizocheza huku Mtibwa ikishika mkia kwa kupoteza mechi mbili kati ya tatu ilizocheza.
Tofauti na hisia za mashabiki wengi wa soka hususani wa Simba na Yanga kuamini kwamba timu inayoshinda Ngao ya Jamii basi ina nafasi kubwa ya kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara, hata hivyo mambo ni kinyume kulingana na rekodi za michuano hiyo.
Kuna wakati timu moja inachukua Ngao ya Jamii, lakini ikachemsha katika Ligi Kuu na hata Kombe la FA, lakini kuna nyakati flani bahati huwa inawabeba walioanza kunyakua Ngao kwa kumalizia mataji yaliyosalia kama ilivyofanya Yanga msimu uliopita, ilipokomba kila kitu kuanzia Ngao ya Jamii, Kombe la Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho (FA) na Kombe la Muungano.
Hapa chini ni miaka minane ambayo ilishuhudiwa bingwa wa Ngao ya Jamii akichemsha kubeba ubingwa wa Ligi, kitu ambacho mashabiki wa Simba na Yanga wanapaswa kwenda uwanjani kulishuhudia pambano la leo, lakini wasiamini moja kwa moja kama mambo yatawanyookea kiulaini.
2001
Yanga ilifanya kweli kwa kuinyoa Simba kwa mabao 2-1 katika pambano la msimu wa kwanza wa michuano hiyo, lakini mwisho wa msimu timu hiyo ilichemsha kubeba ubingwa wa Ligi Kuu, kwani taji la lilienda kwa Wekundu wa Msimbazi.
Simba ilimaliza msimu kwa pointi 31 katika hatua ya Nane Bora (enzi hizo Ligi ikiendeshwa kwa mtindo huo) kupitia mechi 14, ilihali mabingwa wa Ngao, Yanga walimaliza katika nafasi ya nne wakashindwa hata kushiriki Ligi Kuu ya Muungano kwani Mtibwa na Moro United ndizo zilizokuwa katika 3 Bora.
2002
Huu ndio uliokuwa msimu wa pili wa Kombe la Tusker, michuano iliyokuwa maarufu enzi hizo ikitumiwa kama Ngao ya Jamii.
Katika mechi ya fainali, Simba iliinyamazisha Yanga kwa kuifunga mabao 4-1 katika mechi iliyojaa vurugu baada ya Madaraka Selemen ‘Mzee wa Kiminyio’ kuumiliki mpira kwa mkono kabla ya kufunga na kuibua twimbili mbele ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na kusababisha aliyekuwa Rais wa Yanga, Tarimba Abbas kufungiwa na FAT.
Kilichotokea katika Ligi Kuu ni kwamba Yanga ilitwaa ubingwa kwa kumaliza msimu ikiwa kileleni mwa msimamo wa Nane Bora kwa pointi 26, dhidi ya 25 ilizokuwa nazo Simba iliyoshika nafasi ya pili.
2005
Baada ya mechi ya Ngao kutofanyika 2004, mwaka uliofuata yaani 2005 mechi ilipigwa ikibeba jina la fainali ya Kombe la Tusker lililofanyika kwa mara ya mwisho na Simba ilishinda tena kwa mabao 2-0, lakini bingwa wa Ligi Kuu aliibuka Yanga iliyomaliza na pointi 61, huku Simba ikiwa ya tatu.
Mshindi wa pili aliyekuwa akiifukuzia Yanga alikuwa ni Moro Utd aliyemaliza na pointi 58.
2009
Baada ya mechi za Ngao kutochezwa kabisa kwa misimu mitatu mfululizo, mwaka 2009 michuano hiyo ilirejea tena na Mtibwa kuibuka washindi kwa bao 1-0, ikiifunga Yanga, lakini katika Ligi Kuu ikiendeshwa kwa mtindo wa kuunganisha miaka yaani 2009-2010, Simba ndio walioibuka wababe.
Wekundu hao walimaliza kileleni wakiwa hawajapoteza mechi yoyote na kuandika rekodi ya kutwaa ubingwa wakishinda mechi 20 na kutoka sare mbili na kuvuna pointi 62 kupitia mechi 22, huku Mtibwa ikimaliza ya nne, nyuma ya Yanga na Azam zilizokuwa katika Tatu Bora.
2012
Msimu huu wa 2012-2013, Simba ilianza kwa kishindo kwa kutwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Azam FC kwa mabao 3-2, lakini katika Ligi Kuu Bara, bingwa aliibuka Yanga.
Yanga ilibeba ubingwa huo wa Ligi kwa kumaliza ikiwa na pointi 60, sita zaidi na ilizokuwa nazo Azam iliyokuwa ya pili, huku Simba ikimaliza ya tatu kwa alama 45, ikizidiwa pointi 15.
2013
Watetezi wa Ligi katika msimu wa 2013-2014, Yanga walianza msimu kwa kuvaana na Azam katika Ngao ya Jamii na kweli mambo yalitiki kwa kushinda kwa bao 1-0, lakini katika Ligi Kuu mambo yaliwaendea harijojo.
Bingwa wa msimu huo katika Ligi Kuu alikuwa ni Azam FC iliyotwaa bila kupoteza mchezo ikiifikia rekodi ya Simba ya 2009-2010.
Azam ilimaliza na pointi 62 kupitia mechi 26, wakati Yanga ilimaliza ya pili ikiwa na pointi 56 nyuma ya mabingwa hao wapya ambao hilo lilikuwa taji la kwanza na la mwisho kwao katika Ligi Kuu Bara.
2016
Huu ulikuwa msimu wa saba ambao bingwa wa mechi ya Ngao ya Jamii alichemsha kubeba ubingwa wa Ligi Kuu na safari hii ilikuwa ni Azam FC iliyobeba taji hilo kwa kuichapa Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-1.
Dakika 120 za pambano hilo zilishuhudiwa timu hizo zikitoka sare ya 2-2 na katika kupigiana matuta, Azam ikaibuka kidedea.
Hata hivyo, katika Ligi Kuu mambo yalienda kombo kwa Azam kwani bingwa wa msimu huo wa 2016-2017 alikuwa ni Yanga. Yanga ilibeba ubingwa wa Ligi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kwani ililingana pointi na Simba kila moja ikiwa na 68, huku Azam ilikuwa ya nne nyuma ya Kagera Sugar.
2023
Msimu wa nane ambao ulishuhudiwa bingwa wa Ngao anapishana na Kombe la Ligi Kuu ilikuwa ni 2023-2024 baada ya Simba kutwaa Ngao ya Jamii kwa penalti 3-1 mbele ya Yanga mechi iliyopigwa Mkwakwani, Tanga baada ya dakika 120 kumalizika kwa suluhu.
Hata hivyo, mwisho wa msimu, Yanga ilifanya kweli ikibeba ubingwa kwa pointi 80 kupitia mechi 30, huku Simba iliyochekelea mapema kubeba Ngao ikimaliza ya tatu nyuma ya Azam na kuchomolewa kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kushiriki mfululizo.