Prime
Huu si uchambuzi, ni uchafuzi wa soka
Kila wakati uchambuzi unachukua sura mpya. Ulianza uchambuzi halisi wa mechi za mpira wa miguu na matukio yanayoambatana nao, ukaacha sura hiyo na kuanza kuwa wa kusakama watu matumizi mabaya ya vyombo vya habari na baadaye ukachukua sura ya kutoa habari kabla ya vyombo vingine na baadaye uchambuzi wa tuhuma.
Na sasa uchambuzi umeamua kuwa wa kuchafua mchezo mzima wa mpira wa miguu.
Uchambuzi kwamba timu fulani imeamua kuwa dhaifu kwa makusudi ili ipoteze mechi, hauwezi kutetewa kwa hoja nzito kwa sababu ni vigumu kuthibitisha, hasa ukichukulia mpira ni ajira kwa wachezaji wanaosakata soka uwanjani na hivyo kitendo chochote cha kucheza chini ya kiwango ni kujiharibia soko.
Uchambuzi kuwa waamuzi na marefa wanacheza kamari na hivyo kufanya matukio fulani kwa makusudi ili washinde huko walikowekeza fedha, ni mgumu kuuthibitisha kwa hoja. Ni hisia tupu ambazo zinatolewa na mtu asiyejali athari za kile anachosema.
Lakini huu uchambuzi wa Yanga walinunua mechi dhidi ya Mbeya City FC umevuka mipaka.
Chombo makini cha habari kisingemruhusu mtangazaji, mwandishi au mchambuzi kuingia studio au chumba cha habari kuandika au kutangaza tuhuma ambazo hazijafanyiwa kazi kikamilifu kuthibitisha habari hiyo.
Chombo makini kisingeweza kuruhusu kuchapishwa au kutangazwa kwa habari isiyokamilika ambayo huyo anayeitoa anadai anao ushahidi wakati huo ushahidi ulitakiwa uthibitishwe na kuzipa nafasi pande zote mbili haki ya msingi ya kuzungumzia suala hilo kabla halijaenda hewani au kuchapishwa gazetini.
Kama ushahidi uko mfukoni, basi na hiyo habari inayochafua taasisi ilitakiwa ibakie mfukoni hadi aliyenayo atakapofanya kazi ya ziada kuthibitisha pande zote na kupata ushahidi usio na shala lolote.
Kwa mtangazaji au mwandishi makini asingepoteza muda kuichapisha au kuitangaza habari yenye tuhuma ambazo hazijafanyiwa kazi na hata mchambuzi makini angeweza kusema suala hilo litachambuliwa baada ya ushahidi wote kukamilika.
Na kwa raia mwema na makini angeweza kuripoti suala hilo kwenye taasisi inayohusika na kukomesha rushwa na kupeleka ushahidi wake ili mamlaka zikomeshe vitendo vya rushwa na kuulinda mchezo wa mpira wa miguu.
Ni kitu cha ajabu watu wanaingia studio kuchambua mechi ambayo wanadai au wana uhakika ilishachezwa nje ya uwanja. Ni watu wasio makini ndio wanaweza kupoteza muda hewani kujadili kitu ambacho ni dhahiri; kwamba matokeo yalishajulikana.
Mara ya kwanza niliposikia kocha wa Mbeya City, Mecky Maxime aliagizwa asitumie wachezaji takriban nane, nilimlaumu nahodha huyo wa zamani wa Taifa Stars kwa kukubali kuiongoza uwanjani timu isiyo na wachezaji wake wa kikosi cha kwanza. Hapo namuomba radhi sana Maxime.
Lakini nilipokuja kumsikia Maxime mwenye anazungumzia suala hilo nikagundua kumbe maagizo hayo hayakuwa kwa ajili ya mechi dhidi ya Yanga pekee, kumbe nyingine kama tatu za awali, ikiwemo dhidi ya Azam FC baada ya wachezaji hao kutorejea kambini mapema na hivyo walipewa adhabu na uongozi. Ilikuwaje mtu akalibeba suala hilo mzobemzobe na kulipa picha tofauti na kilichotokea?
Hakuna uchambuzi unajikita kwenye tuhuma ambazo hazijathibitishwa. Uchambuzi unazungumzia jambo ambalo limekamilika na si limeibuliwa tu bila ya kuwa na taarifa kamili.
Nadhani kuna haja ya mamlaka kuchukua hatua. Ninajua wamiliki wa vyombo vya habari wanajua cha kufanya kuepusha taasisi au watu bninafsi kuchafuliwa bila ya kupewa nafasi ya kujitetea.
Hata kama tuhuma hizo hazijaelekezwa moja kwa moja kwa Bodi ya Ligi (TPLB), bado kitendo hicho na vingine vingi vya kutuhumu marefa na wachezaji, kinachafua ligi na kupoteza ladha ya mchezo wenyewe.
Si ajabu kuona siku hizi hata mechi za Simba na Yanga hazijazi mashabiki zinapocheza kwenye uwanja wenye uwezo wa kuchukua mashabiki wachache kama wa ule KMC. Kwa sababu si rahisi kwa mashabiki kwenda viwanjani kuangalia mechi ambazo wanasikia zinanunuliwa.
Hivyo kuilinda ligi na kuwalinda wachezaji na waamuzi Bodi ya Ligi haina budi kuchukua hatua za kuanza kudhibiti na kukomesha vitendo ambavyo vinachafua mashindano yake, hasa Ligi Kuu ambayo ndio kioo cha mpira wetu.
Uhuru wa kuchafua watu na taasisi haupo. Uhusu wa kuchafua mashindano haupo. Bali upo uhuru wa kuibua uchafu wa taasisi au watu binafsi na kuuweka hadharani pale habari inapofanyiwa kazi na kupata ushahidi wa kutosha.
Sijui ni hatua gani zinaweza kuchukuliwa, lakini ni muhimu kwa mamlaka, hasa TPLB kuchukua hatua mapema kabla ya watu kupotea viwanjani na wadhamini kupoteza Imani na mashindano hayo makubwa kwa ngazi ya klabu nchini.