Prime
Motsepe sawa! Kuna somo moja zito kwa TFF
SHIRIKISHO la Soka la Afrika (CAF), linapitia katika kipindi kigumu baada ya uamuzi wa Machi 17 wa Bodi ya Rufaa ya chombo hicho kuivua Senegal ubingwa wa Afrika baada ya kuridhika na hoja za Morocco kuwa wachezaji wa wapinzani wao katika fainali ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) walitoka uwanjani bila ridhaa ya mwamuzi.
Katika fainali hiyo iliyofanyika Januari 18 jijini Rabat, mwamuzi Jean-Jacque Ndala aliipa Morocco penalti katika dakika ya mwisho ya mchezo, uamuzi ambao ulipingwa na wachezaji wa Senegal kiasi cha kuamua kutoka uwanjani. Ni Sadio Mane pekee alisalia uwanjani na ndiye aliyetuma mtu kwenda vyumbani kuwaambia wenzake warejee uwanjani.
Iliwachukua kati ya dakika 15 hadi 17 kurejea uwanjani na kumruhusu Brahim Diaz kupiga mkwaju wa penalti ambao hata hivyo uliokolewa na kipa na katika muda wa nyongeza Senegal ikafunga bao la ushindi.
Kwa sheria za mpira wa miguu, Ndala alitakiwa amalize mchezo baada ya wachezaji wa Senegal kutoka uwanjani bila ridhaa yake. Lakini katika hali ya kushangaza, mwamuzi huyo alisubiri kwa takriban dakika 17, jambo lililoifanya Morocco kutumia suala hilo kama hoja kuu kwa mujibu wa kifungu namba 82 cha kanuni za CAF na hivyo kustahili adhabu inayotajwa kwenye kifungu cha 84 ambayo ni kupokonywa ushindi na mpinzani kunufaika kwa kupewa mabao matatu.
Hili ni sakata kubwa na fedheha kwa mpira wa miguu wa Afrika; kwanza kwa sababu ya mazingaombwe ya refa Ndala ya kusubiri kwa muda mrefu bila kufanya uamuzi wa kumaliza mchezo, pili kwa sababu tukio hilo lilitokea katika hatua ya juu ya michuano mikubwa kuliko yote ya CAF, na tatu kwa sababu ya uamuzi wa kupindua matokeo ya mechi ambayo mwamuzi aliona ilikuwa muhimu ifikie mwisho na kanuni kuu ya soka ni uamuzi wa refa kuwa wa mwisho.
Matukio yaliyotokea kuelekea kumalizika kwa mchezo huo yanatia shaka na yale yaliyotokea kuelekea Bodi ya Rufaa kufikia uamuzi pia yanatia shaka.
Ungetegenea katika hali hiyo, rais wa CAF, Patrice Motsepe asakamwe kila upande kuwa anahusika katika kila kasoro kuanzia siku ya fainali ambayo ilikuwa na matukio mengi ya ajabu likiwemo la taulo la kipa hadi uamuzi wa kuivua Senegal ubingwa.
Lakini hakuna lawama zinazoelekezwa kwake bali jinsi shirikisho hilo lilivyoshughulikia kilichotokea.
Katibu Mkuu wa CAF, Veron Mosengo-Omba, ambaye alikuwa akidaiwa kushikilia cheo hicho kinyume cha katiba baada ya kuvuka umri wa miaka 61 akaachia ngazi Machi 17 bila kueleza sababu za uamuzi huo. Hata hivyo, anatuhumiwa kufanya mabadiliko ya watu muhimu kwenye vyombo huru vya haki siku chache kabla ya Bodi ya Rufaa kukutana.
Pia kumeibuka tuhuma nyingi kuwa kuna harufu ya rushwa katika kufikia uamuzi wa kuivua Senegal ubingwa na shinikizo la kutaka uchunguzi ufanyike.
Motsepe, raia wa Afrika Kusini na mmoja wa mabilionea wakubwa Afrika amekuwa mtulivu na hajaonyesha kutetereshwa na janga hilo la aina yake katika soka Afrika na duniani kwa ujumla.
Badala yake, amekuwa akitumia mikutano na waandishi wa habari kueleza umuhimu wa kufuata taratibu na kuheshimu uamuzi wa vyombo halali vya CAF na vya michezo kwa ujumla.
Motsepe hajaonyesha hata chembe ya wasiwasi dhidi ya Bodi ya Rufaa, zaidi ya kuonyesha ni jinsi gani CAF ilifuata taratibu zinazotakiwa katika kushughulikia matukio yaliyotokea siku ya fainali baada ya mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ambaye ni Msenegali kujiondoa katika kikao cha kuadhibu matukio hayo kutokana na maslahi binafsi ya kitaifa.
Motsepe pia ameunga mkono uamuzi wa Senegal kukata rufaa Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), akisema hiyo ni hatua muhimu katika kuheshimu vyombo vya maamuzi vya michezo na kwamba CAF itatekeleza uamuzi wa chombo hicho chenye makao yake makuu jijini Laussane, Uswisi.
Mbali na kutotoa kauli tata kuhusu sakata hilo, Motsepe amefanya ziara nchini Senegal ambako alikutana na rais wa nchi hiyo, Bassirou Diomaye pamoja na viongozi wa soka akiwahakikishia kuwa CAF iko tayari kutoa ushirikiano kamili kwa chombo chochote au serikali itakayotaka kufanya uchunguzi wa kuwepo kwa rushwa katika sakata hilo.
Alisema rushwa ipo si katika mchezo wa mpira wa miguu pekee, bali sehemu nyingi na wameshaelezwa jinsi uovu huo ulivyokuwepo awali na jinsi walivyoushughulikia.
Mbali na Senegal, Motsepe pia amefanya ziara nchini Morocco ambako pia alitarajiwa kukutana na rais wa shirikisho la soka pamoja na viongozi muhimu wa serikali kuzungumzia sakata hilo.
Kwa kifupi, Motsepe ameonyesha njia ya jinsi viongozi wetu wanavyotakiwa kufanya wakati kunapotokea matatizo ambayo pengine yamesababishwa na vyombo vyao vya maamuzi au watendaji wake.
Kujitokeza mbele ya waandishi wa habari na kutoa maneno tata kunazidisha ugumu wa tatizo, hasa kila upande unapotafsiri kauli hizo kwa mitazamo tofauti.
Tumeona jinsi sakata la kuahirishwa kiholela kwa mechi ya Simba na Yanga kulivyoibua kauli nyingi tata na kusababisha ugomvi huo udumu kwa takriban miezi mitatu. Kibaya zaidi ni viongozi wa juu kugeuzwa kuwa sehemu ya tatizo, hadi nao kuitwa kwenye vikao vya usuluhishi.
Wakati Motsepe anajiweka juu ya tatizo na kuchukua hatua za kutumia busara kutuliza hali kwa kufanya ziara katika nchi zinazohusika na sakata hilo, hakukuwepo na juhudi zozote zz viongozi wa mpira wa miguu kukutana na viongozi wa Simba na Yanga katika vikao tofauti ili kutafuta suluhu au kueleweshana umuhimu wa kuheshimu uamuzi wa vikao halali.
Badala yake, viongozi wa juu ndio wakatuhumiwa kuhusika katika kupanga njama dhidi ya upande mmoja, hali iliyosababisha wasiwe na ushawishi wa kumaliza tatizo hilo ndani ya duru za soka hadi mamlaka za juu za nchi zilipoingilia kati.
Motsepe ameonyesha imani na vyombo vya uamuzi vya ndani ya CAF na nje, jambo ambalo ni muhimu kwa afya ya CAF na mpira wa miguu barani Afrika. Maana yake ni kwamba hata kama Bodi ya Rufaa ilikosea, bado familia ya mpira ina sehemu nyingine ya kurekebisha makosa hayo.
Hii inajenga imani kwamba vyombo vya haki vya CAF viko huru na havielekezwi kufanya uamuzi kwa kadiri ya utashi wa viongozi wa juu. Ni mara ngapi Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka (TFF), imetuhumiwa kufanya uamuzi kwa utashi wa mabosi wao? Ni mara ngapi Kamati ya Uchaguzi imetuhumiwa kuelekezwa kuengua wagombea fulani?
Kama Motsepe angekuwa anavielekeza vyombo vya CAF kufanya uamuzi kwa utashi wake, leo hii asingekuwepo pale kwa jinsi soka la Afrika lilivyo na mizengwe. Angekuwa ameshapelekewa tuhuma nyingi na baadhi ya watu wangejitoa mhanga kueleza ni jinsi gani alihusika katika uamuzi.
Tunahitaji aina hii ya viongozi kuanzia katika ngazi za chini za uongozi wetu. Mpira wa miguu umezuia wadau kwenda mahakamani kwa ahadi kuwa utaunda vyombo imara na huru vya haki. Ni lazima ahadi hiyo itekelezwe. Lakini kikubwa zaidi ni busara na weledi wa kiongozi wa juu kunapotokea tatizo kama hilo la fainali ya AFCON.
Kwa kifupi, Motsepe ameonyesha mfano wa viongozi bora wenye weledi katika soka barani Afrika.