Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hizi ndizo kanda zenye ushawishi TFF

TFF Pict

Muktasari:

  • Iliwekwa bayana kwamba wapigakura wa uchaguzi huo ni wajumbe 83 kulingana na uwakilishi kuanzia klabu 16 zinazoshiriki  Ligi Kuu Bara, wajumbe 52 wa vyama 26 vya soka vya mikoa na wajumbe 15 kutoka vyama vitano wanachama wa TFF.

JANA katika mfululizo wa makala maalumu za Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) utakaofanyika Agosti 16 jijini Tanga ilielezwa ukweli juu ya wapigakura wa uchaguzi huo.


Iliwekwa bayana kwamba wapigakura wa uchaguzi huo ni wajumbe 83 kulingana na uwakilishi kuanzia klabu 16 zinazoshiriki  Ligi Kuu Bara, wajumbe 52 wa vyama 26 vya soka vya mikoa na wajumbe 15 kutoka vyama vitano wanachama wa TFF.


Pia iliainishwa wajumbe hao 83, miongoni mwao wapo 47 ambao ndio wahusika wa kuidhinisha na kuwadhamini (endosment)  wagombea 25 waliojitokeza kuwania uchaguzi wakiwamo wagombea sita wa urais na 19 wanaowania nafasi sita za ujumbe wa kamati ya utendaji.

Wakati huu wadau wakiendelea kusikilizia wagombea waliofanikiwa kupenya katika hatua ya mapingamizi kabla ya kwenda katika usaili ili kupitishwa kwa uchaguzi huo wakitanguliwa na kampeni itakayohitimishwa Agosti 15, leo gazeti hili linaendelea kukudadavulia mbio za uchaguzi huo.

Linaangazia kanda zenye nguvu na zinazobeba kwa asilimia kubwa uchaguzi huo ambao rais wa sasa wa TFF, Wallace Karia alijitokeza kuchukua na kurudisha fomu za kutetea nafasi hiyo kwa mara nyingine.


KANDA SITA

Baada ya marekebisho yaliyofanywa na Shirikisho la Soka Kimataifa (Fifa), juu ya muundo wa mkutano mkuu wa TFF, ulileta mgawanyo mpya wa kanda ukilenga kupunguza gharama za uendeshaji wa mikutano hiyo.

Awali mkoa mmoja ulikuwa ukihesabika kama kanda, lakini baada ya marekebisho ambayo yalizua maneno mengi uliwafyeka watu kushiriki kwenye mkutano huo.

Baada ya marekebisho hayo katiba ya TFF ibara ya 84 ikazitambulisha kanda sita zilizogawanywa kwa mikoa inayokaribiana.


HALI ILIVYO

Kanda ya Kwanza ni lle yenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Mtwara na Lindi ikiwa na lengo la kurahisisha mawasiliano ya karibu kwa wenyeviti wa mikoa hiyo.

Kanda ya Pili inaundwa na mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara ilhali Kanda ya Tatu ikiundwa na mikoa ya Mbeya, Songwe, Ruvuma, Iringa na Njombe.

Kanda  ya Nne inahusisha mikoa ya Dodoma, Singida, Simiyu na Shinyanga wakati ile ya tano ikiwa na mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara na Geita huku kanda ya sita na ya mwisho ikiwa na mikoa ya Kigoma, Tabora Rukwa na Katavi.


KANDA MOTO

Licha ya kwamba kanda zote ni sawa kulingana na mgawanyo, lakini katika sanduku la kura kuna kanda zinazoonekana za moto na zenye nguvu kubwa ya kufanya uamuzi kwa wagombea.

Kanda zinazotajwa kuwa na nguvu kubwa ni ile ya kwanza na ya tatu. Kanda ya kwanza inatajwa ndio ‘baba lao’. Hii sio kwa sababu ya kuwa karibu na makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania, bali ni kutokana na idadi ya mikoa iliyo nayo na ushawishi mkubwa ilionao katika soka la Tanzania.

Inaelezwa kwamba mikoa hiyo ina ushawishi mkubwa hata kwa wapigakura pale wanapotaka jambo lao lipite au lifanyiwe kazi na mamlaka za soka kwa haraka, sawa na ilivyo kwa kanda ya tatu, lakini idadi ya mikoa mitano kila moja inabeba kura nyingine kwani kwa mujibu wa kanuni ya kila mkoa huwakilishwa na wajumbe wawili - maana kanda hizo zina kura 20.

Kanda nyingine nne kila moja ina mikoa minne ikibeba kura nane kwa kila moja na kama mgombea atakubalika kupitia kanda hizo mbili zenye nguvu kisha akaungwa mkono angalau na kanda hata mbili tu na kuambulia nyingine za vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu -  basi nafasi ya kushinda ni kubwa zaidi.

Hata hivyo, bado kanda zote na wapigakura wengine wa uchaguzi wana nguvu ya uamuzi ya kuweka viongozi wapya wa kuliongoza shirikisho hilo na hiyo ndio inayosubiriwa kwa hamu Agosti 16 jijini Tanga ili TFF ikapate safu mpya ya uongozi kwa ajili ya miaka minne ijayo kabla ya kuitishwa uchaguzi mwingine.