Prime
Hizi hapa njia za Simba kumnasa Fei Toto

Muktasari:
- Lakini ni kwamba, hata Yanga nayo inampigia hesabu kiungo mshambuliaji huyo kwa lengo la kwenda kuziba nafasi ya Stephane Aziz Ki aliyeuzwa Wydad Casablanca ya Morocco.
MASHABIKI wa Simba wanasikilizia dili la kiungo wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' kama litatiki au la, lakini presha yao ni suala la kuwepo kwa kipengele cha mkataba kati ya klabu hiyo ya Chamazi na Yanga.
Lakini ni kwamba, hata Yanga nayo inampigia hesabu kiungo mshambuliaji huyo kwa lengo la kwenda kuziba nafasi ya Stephane Aziz Ki aliyeuzwa Wydad Casablanca ya Morocco.
Sasa sikia. Kama umeshawahi kusikia msemo wa Kiswahili wa kumkaanga papa kwa mafuta yake? Basi hivyo ndivyo Yanga walivyofanya kwa Azam FC kumpata Prince Dube na ndivyo Simba wanavyojipanga kufanya kumpata Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Ni kwamba Prince Dube aliandika barua kwa uongozi wa Azam akielezea nia yake ya kuvunja mkataba na klabu hiyo na kuendelea na maisha yake sehemu aitakayo.
Klabu haikuwa na hiyana,ikamkubalia huku ikimtaka kulipa pesa ya kuvunjia mkataba kama mkataba wenyewe ulivyosema.
Mwanaspoti linajua pesa ya kuvunjia mkataba ilikuwa Shilingi 700 milioni, pesa nyingi sana ambazo Dube hakuwa nazo wakati ule kwa mujibu wa wasimamizi wake.
Akashauriwa aende kufungua kesi TFF akiukana mkataba aliokuwa ameusaini mwenyewe, akashindwa kesi.
Baada ya vuta nikuvute, Dube akalipa pesa hiyo na kuwa huru....akaenda Yanga.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba watu wa karibu wa Yanga walimlipia Dube pesa hiyo.
Na wao hawakutoa pesa hiyo katika akaunti zao, bali akaunti za Azam Media, kampuni dada ya Azam.
Yanga ina mkataba na Azam Media wa maudhui, unaoiingizia klabu hiyo Shilingi 200 milioni kwa mwezi.
Mwanaspoti linachojua ni kwamba walichofanya ni kwenda Azam Media kuomba wapewe kwa mkupuo mmoja pesa za miezi minne ya mbele, yaani Shilingi 800 milioni.
Walipopata pesa hizo, wakampa Dube akalipe deni lake...akawa huru. Azam Media na Azam ni mali ya tajiri mmoja, Said Salim Bakhresa.
Kwa hiyo Yanga walimnasa mchezaji wa Azam kwa kutumia pesa za Azam...walimkaanga papa kwa mafuta yake.
Hiki ndicho watu wa karibu wa Simba walichoshauri uongozi kifanyike pia kwa Fei Toto. Wanafainali hao wa Kombe la Shirikisho Afrika, pia wana mkataba na Azam Media kama ule wa Yanga...yaani wa kupata Shilingi 200 milioni kwa mwezi.
Na wao wako kwenye mchakato wa ndani kwenda kuomba wapewe kwa mkupuo mmoja pesa za miezi kadhaa mbele, ili wamnunue Fei Toto. Hizo ni za ndani sana.
Wakifanikiwa kufanya hivyo basi watakuwa wamemnunua Fei Toto kwa pesa ya Azam wenyewe...wamekaanga papa kwa mafuta yake.
Kuna mjadala wa ndani baina ya timu hizo kwani kuna fungu Simba walipata kwa ushiriki wao wa Kombe la Shirikisho. Hivyo kuna namna ambayo kimakubaliano Simba watalazimika kusubiri hadi mwezi wa ujao upite, ndio dili lao na Azam litengamae kwa maana ya kupewa fungu.
Wasiwasi wao ni kwamba, je, Fei Toto ataendelea kuwa anapatikana sokoni hadi wakati huo? Kiuhalisia ni kwamba lolote linaweza kutokea.
Jambo jingine linaloleta ugumu kwa sasa ni mkataba wenyewe wa mauzo ya Fei Toto kati ya Yanga na Azam.
Kuna kipengele cha Yanga kupata Shilingi 1 bilioni kutoka Azam FC endapo mchezaji huyo atauzwa kwenda Simba.
Mmmoja wa vigogo wa Azam Fc anasema; “Na Azam hawawezi kuwa wajinga eti wamuuze Fei Toto kwa Shilingi 1 bilioni halafu zote wawape Yanga. Kimsingi ni kwamba hata kugawana sawasawa hawawezi kukubali...yaani kumuuza Fei Toto kwa Sh 2 bilioni halafu moja wawape Yanga na wao wabaki na moja.”
“Wao wanaamini kwamba wamemuongezea thamani Fei Toto kwa kuwekeza pesa nyingi kwake tangu ajiunge nao. Kwa hiyo hawawezi kugawana sawa sawa na timu yoyote...lazima wao wazidi.
Na kama ni hivyo basi maana yake Simba wanatakiwa watafute zaidi ya bilioni mbili....kazi kubwa sana,”alidokeza mmoja wa vigogo wa usajili wa Azam FC.
Hivyo, kutokana na njia hiyo kuwa ngumu, wamekubaliana ndani wafanye tena kama Yanga.
Simba wachukue dau wampe Fei Toto mwenyewe avunje mkataba, badala ya kumnunua. “Akishavunja, akawa mchezaji huru...halafu wao wamchukue. Na wakifanya hivyo watakuwa wameisaidia Azam FC kukikwepa kile kipengele,”kilisema chanzo chetu cha kuaminika.
“Kwa sababu hapo mchezaji atakuwa hajauzwa, bali yeye mwenyewe kavunja mkataba,”aliongeza. Hivi ndivyo Yanga walivyofanya kwa Prince Dube, au PSG kwa Neymar kutoka Barcelona.
Habari zinasema kwamba katika mkataba wa mauziano ya Dube kati ya timu yake ya Zimbabwe ya Highlanders na Azam, kulikuwa na kipengele cha klabu hiyo kulipwa zaidi ya Shilingi 100 milioni endapo Dube atauzwa.
Lakini kwa kuwa hakuuzwa bali alivunja mkataba yeye mwenyewe, Azam haikuwajibika kuwalipa Highlanders. Kipengele kikaisha kikawaida.
Na za ndani kabisa zinasema kwamba ndivyo itakavyokuwa endapo Simba watapita njia ya Yanga. Kwa hiyo Simba wanaendelea na kuomba tu, Feitoto asisaini mkataba mpya na Azam FC, na kusiwe na klabu nyingine kuja kuharibu dili lao kabla ya Agosti.