Himid Mao: Fei ndo kiungo bora Bara, ishu ya kustaafu?.
Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, kiungo huyo, ambaye aliwahi kucheza El Gaish ya Ligi Kuu Misri, amefunguka kuhusu kiwango chake, maisha ya soka na mambo anayoyaona ndani na nje ya uwanja.
KATIKA soka, wachezaji wengi hufika hatua ambayo uzoefu wao unakuwa sehemu ya thamani kubwa katika kikosi, lakini Himid Mao ‘Ninja’ bado anaendelea kupambana na vijana na wageni wanaogombea nafasi katika safu ya kiungo ya Azam FC.
Akizungumza na Mwanaspoti, kiungo huyo, ambaye aliwahi kucheza El Gaish ya Ligi Kuu Misri, amefunguka kuhusu kiwango chake, maisha ya soka na mambo anayoyaona ndani na nje ya uwanja.
Pamoja na hayo, amemtaja Feisal Salum ‘Fei Toto’ kama kiungo bora kwa sasa na namna anavyojiandaa kwa siku atakapoamua kutundika daluga.
Himid ambaye kwa sasa anakipiga Azam FC, ameweka wazi hakuna kocha mzuri atakayekuja nchini na kumweka Fei Toto benchi kutokana na kiwango anachoonyesha uwanjani.
“Feitoto si mchezaji mzawa wala wa kigeni ambaye atakosa kumtaja, ni mchezaji mzuri mwenye kipaji na bidii uwanjani,” anasema Ninja.
AKARIBIA KUSTAAFU
Akizungumzia siri ya kuendelea kuonyesha kiwango bora, Himid anabainisha kuwa hana siri zaidi ya kupenda mchezo huo na kufurahia kila dakika anayopata kuitumikia Azam FC.
Kuhusu muda wa kustaafu soka la ushindani, Himid ameweka wazi kuwa hajaweka umri maalum wa kutandika daluga, bali ataacha siku atakayosikia mwili umechoka.
“Siku nikisikia nimechoka nitaacha kucheza, lakini kwa sasa nafikiri siku yangu ya kuacha ipo karibu sana kuliko siku niliyoanza kucheza mpira,” alisema Himid.
USHINDANI WA NAMBA
Licha ya Azam FC kusajili viungo wengi wa kimataifa, Himid amemudu kupigania namba kwenye mfumo wa viungo watatu uwanjani. Ndani ya kikosi hicho kuna wachezaji kama Yahya Zayd, Sadio Kanoute, Feisal Salum ‘Feitoto’ na wengineo.
Alieleza mafanikio ya kiwango chake yanatokana na ushirikiano na kazi kubwa wanayoifanya pamoja na viungo wenzake kwenye uwanja wa mazoezi.
“Ili uwe na kiwango bora lazima uiheshimu na kuipenda kazi yako kwa maana lazima upumzike kwa wakati, ule vizuri, mazoezi sana,” anasema Ninja.
Anaongeza kuwa hakuna uchawi kwenye mpira na ili udumu kwa muda mrefu uwanjani, Himid ametoa wito wa kuuheshimu mwili kwani ndiyo ofisi ya mchezaji, pamoja na kuwaheshimu wachezaji wenzake na klabu anayoitumikia.
UFALME WA FEITOTO
Anasema ufalme wa Feitoto ndio unafanya kila dirisha la usajili kuhusishwa na timu kubwa nchini na hilo linatokana na kiwango bora anachoendelea kuonyesha.
“Nafikiri Feisal ndiye mchezaji bora wa ligi ya Tanzania kwa miaka hii ya karibuni, kiasi kwamba si kitu cha kushangaza kuona kila dirisha la usajili watu wanamtaja kumsajili kwenye klabu kubwa,” alisema Himid.
LIGI KUU
Himid anaamini Ligi Kuu imepiga hatua kubwa na kuwa na ushindani wa hali ya juu, jambo linalowavutia wachezaji wengi wa kigeni na makocha bora kuja nchini.
Anaongeza kuwa klabu nchini zimefanya kazi kubwa kuboresha miundombinu ambayo inawarahisishia kazi makocha.
TEKNOLOJIA YA FVS
Akigusia mfumo wa msaada wa video kwa waamuzi (FVS/VAR), Himid anasema umeongeza jicho la ziada kwa waamuzi, ingawa alitoa angalizo utumiwe vizuri kwa sababu tayari umeshawaumiza Azam FC msimu huu.
“Teknolojia inawasaidia lakini waangalie kwa makini kwa sababu tayari imetoa madhara kwetu,” anasema Himid.
SOKA LA WANAWAKE
Kuhusu soka la wanawake, Himid anasema ndilo eneo lililopiga hatua kubwa zaidi nchini kwa kushiriki Kombe la Dunia na michuano ya AFCON.
Alipendekeza kuwa soka la wanawake linastahili kupewa jicho kubwa na uwekezaji zaidi kama ilivyo kwa timu za wanaume.
“Licha ya Tanzania kutofanya vizuri, wadau wanapaswa kulipiga jicho soka la wanawake kwa sababu ni eneo ambalo limekuwa likifanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.”
TENISI
Nje ya soka, Himid amefichua anapenda sana mchezo wa tenisi na huwa anacheza na marafiki zake pindi anapopata nafasi, ingawa udogoni akiwa anasoma na kukua maeneo ya Magomeni kulikuwa na uchache wa viwanja vya mchezo huo.
“Kama kungekuwa na viwanja mitaa ya kwetu nafikiri ningekuwa mcheza tenisi lakini shida ni Magomeni hakuna viwanja.”
MKE WAKE
Kwenye upande wa familia, Himid anamwelezea mke wake kama nguzo muhimu sana katika maisha yake na mke mzuri humsaidia mchezaji kutuliza akili na kufanya vizuri uwanjani.
“Nisiwe muongo lakini kiwango ninachoonyesha kinatokana na utulivu wa mke wangu, namshukuru sana na nampenda.”
TABIA YAKE
Miongoni mwa tabia anazozipenda akienda dukani kununua nguo, ananunua kuanzia mbili na kuendelea.
“Mi mi niki penda kitu na weza kun unua cha aina moja hata nne au ta no, rangi hiyo hiyo na aina hiyo hiyo. Nanunua hivyo ili siku isipite miezi miwili nikajutia kuona kitu kilikuwa kizuri lakini nikajikuta nimenunua kimoja kikaja kuharibika,” alisema Himid.