Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HESABU NGUMU: Sare ya Mzizima Dabi ilivyoinogesha Yanga

MZIZIMA Pict


ILE mechi ya Mzizima Dabi ndiyo kama ulivyosikia, haikutoa mbabe baada ya Azam na Simba kumaliza dakika 90 bila kufungana, ilikuwa kali lakini kuna alama zikaachwa na vikosi vya pande hizo mbili.


Mechi hiyo iliyopigwa Jumapili ya Aprili 5, 2026 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, ilizikutanisha timu ambazo hazikuwahi kupata mshindi uwanjani hapo mara tatu zilizopita na matokeo yaliisha kwa sare ambayo rekodi hiyo imeendelea.


Sare hiyo imeifanya Simba kubaki nafasi ya pili ikifikisha pointi 35, huku Azam nayo ikiwa ya tatu na pointi 33. Kileleni kuna Yanga yenye 41.

Awali Simba ilikuwa na matumaini ya endapo ikiifunga Azam, basi katika mbio za kuifukuzia Yanga kileleni iwe kwenye mstari mzuri kwani ingebakisha pointi nne huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya TRA United.

Endapo Simba ingeichapa Azam, hesabu zao hizo zingekaa vizuri kwani ingehamishia nguvu kuichapa pia TRA na kuweka tofauti ya pointi moja na Yanga zikifukuzana hadi pale zitakapokutana Mei 3 mwaka huu katika Kariakoo Dabi ambayo pengine itaamua nani akae juu na kuchonga barabara ya ubingwa vizuri.

MZIZI 06


Lakini sare dhidi ya Azam, hesabu zimekuwa ngumu kwa Simba, hivi sasa inalazimika kuifukuza Yanga kwa mbali kidogo tofauti ya pointi zikiwa sita, hata ikiifunga TRA United, zitabaki tatu ambazo ikitokea ikashinda Kariakoo Dabi, bado itaachwa kwa tofauti ya mabao.

Hivi sasa Yanga inaongoza kwa pointi 41 huku pia ikifunga mabao 35 na kuruhusu matatu, ndiyo timu yenye mabao mengi ya kufunga na machache ya kuruhusu. Simba ina mabao 26 na imeruhusu sita. Ni timu ya pili kwa kufunga mabao mengi, pia ya tatu kuruhusu machache baada ya Yanga (3) na Azam (5).

MZIZI 01

IBENGE HAKAMATIKI

Matokeo ya mchezo huo yamempa heshima Kocha wa Azam, Florent Ibenge ambaye baada ya kuichapa Simba kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza, hajachafua heshima yake akiondoka na alama moja mzunguko wa pili.

Ibenge kwa hesabu mujarabu ni kwamba, msimu huu ameondoka na pointi nne mbele ya Simba, pia anabakiza mchezo mmoja tu wa marudiano dhidi ya Yanga kuhitimisha rekodi yake kwani hakuna timu iliyomaliza nne bora msimu uliopita ambazo ni Yanga, Simba na Singida Black Stars iliyomfunga kwenye ligi msimu huu.

Katika mechi mbili dhidi ya Singida Black Stars, Ibenge alianza na sare, kisha ushindi, huku pia dhidi ya Simba akianza na ushindi, kisha sare. Dhidi ya Yanga, ameambulia sare, bado marudiano dhidi ya vinara hao wa ligi akiifanya Azam kuwa timu ngumu kufungika msimu huu katika msimu wake wa kwanza tu.

MZIZI 02

SIMBA MBELE KUGUMU

Simba ilikuwa na mchezo mzuri kwa muda mwingi na ilimiliki mechi lakini shida ilikuwa safu yao ya ushambuliaji, kinara wao wa ufungaji mshambuliaji Seleman Mwalimu mwenye mabao sita, hakuwa na makali ya kuivunja ngome ya Azam.

Simba lazima ianze sasa kuboresha safu yao ya ushambuliaji kwa kuwa na mtu katili atakayekuja kukamilisha kazi nzuri ya viungo wa kati kwa msimu ujao hasa kwenye mechi kubwa kama hizi dhidi ya Azam na msimu huu haijafunga bao lolote mbele ya matajiri hao wa Chamazi.

MZIZI 07

MANULA KAMALIZA

Dakika 90 za mechi hiyo, Azam golini kwao walimpa kazi Aishi Manula kupambana na chama lake la zamani na jamaa akawapa majibu Simba hawakuwa sahihi kumuacha kufuatia kazi yake bora aliyoifanya kuwalinda matajiri hao wa Chamazi.

Manula alikuwa mwiba mbaya kwa Simba akifanya kazi bora nne ya kukataa nafasi ambazo wekundu hao wangezigeuza mabao, alikataa shuti la ufundi la Libase Gueye dakika ya 42, nafasi mbili za Clatous Chama na moja ya Anicet Oura.

Kipa huyo kweli alistahili tuzo ya mchezaji bora wa mchezo aliyokabidhiwa akimzidi James Akaminko ambaye naye alikuwa bora sana kwenye mechi pale katikati ya uwanja kwa kutibua na kulainisha kazi bora kwa timu yake.


MZIZI 08

Kulikuwa na matukio mawili ya Simba kupata penalti yaliyojitokeza kwenye mchezo huo na mashabiki wa wekundu hao walilia na mwamuzi Ahmed Arajiga kutoka Manyara, waliona kama ndiye aliyewakatili kwenye matukio hayo.

Kwenye tukio la kwanza lilimhusisha Gueye aliyekuwa anasukumana na beki wa Azam, Fuentes Mendoza dakika ya 29, lakini Arajiga alionekana kukaa kati akishindwa kuamua juu ya tukio hilo, wengi wanaweza kumlaumu mwamuzi huyo lakini alihitaji kupata msaada kutoka kwa msaidizi wake namba moja, Mohammed Mkono kutoka Tanga ambaye ndiye aliyekuwa kwenye nafasi sahihi ya kuona kila kitu kilichokuwa kinaendelea kwa wachezaji hao wawili lakini hakufanya hivyo.

MZIZI 05

Tukio la pili lilikuwa dakika ya 59 na baada ya mpira wa kona kupanguliwa na Manula ukamkuta beki wa Simba, Ismael Toure aliyepiga shuti kwa mguu wa kushoto na mpira kwenda kumgonga Mendoza mkononi lakini bado Arajiga alishindwa kufanya maamuzi.

Kumbuka Arajiga alirudi kuchezesha mchezo huo baada ya mara ya mwisho kuwapa penalti Simba, ilipokuwa inacheza dhidi ya Mashujaa lakini Kibu Denis alikosa, inawezekana mwamuzi huyo alipata presha kutokana na matukio ya namna hiyo.


MZIZI 09

Kipa wa Simba, Mahamadou Tanja Djibrilla Kassali Djibo alicheza dabi yake ya pili akiwa na wekundu hao, akitangulia ile dhidi ya Yanga lakini hii ya juzi alionekana kuwa na makosa machache hasa ya kutema mipira, pia miguu yake haijaweza kuhimili presha ya kupiga pasi sehemu sahihi.

Mabeki wa Simba wanatakiwa kutambua aina ya kipa waliyenaye hana ubora wa kufanya uamuzi wa kupiga pasi akiwa kwenye presha kama ambavyo nusura aipe Azam bao kwa kumpigia pasi nzuri Nassor Saadun, kama Simba inataka kuanza kujenga mashambulizi kuanzia kwa Kasali basi wamuimarishe kwanza kipa wao vinginevyo kuna siku atawaunguza.

MZIZI 10

SARE TAMU KWA YANGA

Matokeo ya mchezo huo yamewaumiza Simba lakini kwa Yanga ambao inaongoza ligi yamewafurahisha kwani, itaendelea kujitanua kwa pengo la pointi sita ingawa wekundu hao wana mchezo mmoja wa kiporo dhidi ya TRA United.

Yanga imenufaika na sare hiyo ikipunguza presha kwa wekundu hao kuzidi kuwasogelea kule juu ya msimamo ambapo hata kama Simba ikishinda dhidi ya TRA, pengo litabaki kuwa alama tatu badala ya moja kama ingeifunga Azam na TRA United.