Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Haya ndiyo madhara ya kuongeza shepu

Muktasari:

  • Unaweza kukutana na mwanamke mwenye makalio makubwa, kiuno chembamba na maumbile yanayovutia, kisha ukajikuta unatamani kuwa na mwonekano kama wake.

KILA mwanamke anatamani kuonekana vizuri na kuwa na mwonekano unaompa kujiamini anapovaa nguo anazozipenda. Hata hivyo, katika ulimwengu wa sasa wa mitindo na mitandao ya kijamii, suala la shepu limekuwa kama mashindano yasiyo rasmi.

Unaweza kukutana na mwanamke mwenye makalio makubwa, kiuno chembamba na maumbile yanayovutia, kisha ukajikuta unatamani kuwa na mwonekano kama wake.

Ndipo baadhi ya wanawake huamua kutafuta njia za mkato za kubadilisha maumbile yao, wengine wakitumia dawa za kumeza, mafuta ya kupaka, sindano na wengine kwenda mbali zaidi kwa kufanyiwa upasuaji wa kuongeza ukubwa wa makalio, matiti au sehemu nyingine za mwili.

Tatizo si kutamani kuwa na shepu nzuri, bali ni pale tamaa hiyo inapomfanya mwanamke kuweka afya yake rehani bila kujua kinachoendelea ndani ya mwili wake. Wapo wanaonunua bidhaa hizo kupitia mitandao ya kijamii bila kujua zimetengenezwa na nini, huku wengine wakijisalimisha kwa watu wasio na utaalamu wa kitabibu.

Taasisi ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) imewahi kutoa tahadhari kuhusu matumizi ya silikoni ya kuchoma mwilini kwa ajili ya kuongeza makalio na matiti, ikieleza kuwa inaweza kusababisha madhara makubwa, ikiwamo kiharusi na hata kifo. Haya ni baadhi ya madhara matano ambayo mwanamke anaweza kuyapata anapojaribu kubadilisha shepu yake kwa njia zisizo salama.

1. KUPATA MAAMBUKIZI NA VIDONDA MWILINI

Mwanamke anayefanyiwa upasuaji au sindano za kuongeza ukubwa wa makalio na matiti anaweza kupata maambukizi endapo vifaa vitakavyotumika havitakuwa safi au utaratibu wa kitabibu hautafuatwa.

Maambukizi yanaweza kusababisha maumivu, kuvimba, usaha na vidonda vinavyochelewa kupona. Katika mazingira makubwa zaidi, maambukizi yanaweza kuenea mwilini na kuhitaji matibabu ya haraka hospitalini.


2. KUPATA KIHARUSI NA KUKOSA HEWA

Hili ni moja ya madhara makubwa zaidi yanayoweza kumpata mwanamke anayechagua njia zisizo salama za kuongeza shepu.

Kwa mujibu wa FDA, sindano za silikoni zinazotumiwa kuongeza makalio au matiti hazijaidhinishwa kwa matumizi hayo. Silikoni ikiingia kwenye mishipa ya damu inaweza kusafiri kwenda kwenye mapafu, moyo au ubongo na kuziba mishipa ya damu.

Hali hiyo inaweza kusababisha matatizo ya kupumua, kiharusi na hata kifo. Jambo la kutisha ni kwamba madhara yanaweza kujitokeza mara moja au baada ya miezi na hata miaka kadhaa.


3. KUATHIRI VIUNGO VYA MWILI

Upasuaji wa kubadilisha maumbile, hasa ule wa kuhamisha mafuta kutoka sehemu moja ya mwili kwenda nyingine, unaweza kuambatana na hatari ya damu kuganda.

Kwa mfano, upasuaji wa kuongeza makalio kwa kutumia mafuta ya mwili, maarufu kama Brazilian Butt Lift (BBL), una hatari ya mafuta kuingia kwenye mishipa ya damu na kusababisha kuziba kwa mishipa hiyo.

Utafiti uliochapishwa katika jarida la kitabibu kuhusu usalama wa upasuaji wa urembo uliripoti makadirio ya vifo vinavyohusishwa na BBL kuwa kati ya kifo kimoja kwa kila upasuaji 15,000 hadi 20,000. Hii inaonyesha kuwa hata upasuaji unaofanywa kwa lengo la urembo unaweza kuwa na hatari kubwa.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

4. KUVURUGIKA KWA MFUMO WA HOMONI

Baadhi ya wanawake hutumia dawa za kumeza zinazodai kuongeza makalio, matiti au kufanya mwili uwe na maumbo fulani. Tatizo ni kwamba si kila bidhaa inayouzwa kwa madai hayo ina viambato vilivyoelezwa kwenye kifungashio chake.

Endapo bidhaa ina viambato vya homoni au kemikali nyingine zisizofaa, inaweza kuvuruga mfumo wa kawaida wa homoni mwilini.

Madhara yanaweza kutegemea aina ya dawa, kiwango kilichotumiwa na muda wa matumizi. Mwanamke anaweza kupata mabadiliko ya hedhi, chunusi, kuongezeka kwa uzito au matatizo mengine ya kiafya.

Ni muhimu kuelewa kuwa hakuna uhakika kwamba dawa za kuongeza shepu zinazouzwa kiholela zinaweza kuongeza makalio au matiti kwa usalama.

5. KUPOTEZA MUONEKANO WA ASILI

Wakati mwingine mwanamke anaweza kuingia kwenye upasuaji akitarajia kutoka na shepu aliyokuwa akiitamani, lakini matokeo yakawa tofauti kabisa.

Anaweza kupata makovu makubwa, ngozi kubadilika rangi, sehemu za mwili kutokuwa na uwiano au tishu za mwili kuharibika.

Kwa upande wa wanaotumia sindano za silikoni zisizoidhinishwa, FDA inaeleza kuwa kemikali hizo zinaweza kusambaa kutoka eneo lililochomwa na kusababisha ulemavu wa kudumu. Hata kujaribu kuziondoa kunaweza kuwa kugumu na kuhitaji upasuaji mwingine.