Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Feliche: Ngumi zimenijengea nyumba na kunivusha mipaka

Muktasari:

  • Alianza ngumi mwaka 2016, akiwa na miaka 20, bila hata kufahamu kwamba mchezo huo ungekuja kuwa sehemu kubwa ya maisha yake. Leo ana miaka 30, ana watoto wawili na amefanikiwa kucheza mapambano mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

MIAKA kumi ndani ya mchezo wa ngumi si safari nyepesi, hasa kwa mwanamke anayelazimika kupambana na wapinzani ulingoni, mitazamo ya jamii, changamoto za familia na wakati mwingine kukosa wadhamini. Hata hivyo, kwa bondia Feliche Mashauri, safari hiyo imekuwa na mafanikio yaliyobadilisha maisha yake, ikiwemo kujenga nyumba yake Boko, kusafiri nje ya nchi na kujijengea jina katika mchezo huo.

Alianza ngumi mwaka 2016, akiwa na miaka 20, bila hata kufahamu kwamba mchezo huo ungekuja kuwa sehemu kubwa ya maisha yake. Leo ana miaka 30, ana watoto wawili na amefanikiwa kucheza mapambano mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

Katika mazungumzo haya, Feliche anafunguka kuhusu safari yake, mapambano yaliyompa presha, maisha ya familia, changamoto za mabondia wanawake, jeraha lililomuumiza na mipango yake baada ya kustaafu.


ALIVYOANZA NGUMI

Feliche alianza mchezo wa ngumi mwezi Aprili mwaka 2016. Safari yake haikuchukua muda mrefu kufikia hatua ya kupanda ulingoni, kwani kati ya Agosti na Oktoba mwaka huohuo, alikuwa tayari amecheza pambano lake la kwanza.

“Nilianza mwaka 2016, mwezi wa nne. Kufikia mwezi wa nane mpaka wa kumi mwaka huohuo nilikuwa tayari nimepanda ulingoni kucheza pambano langu la kwanza.”


UREMBO NA KAZI

Pambano lake la kwanza lilikuwa katika uzito wa Lightweight, kilo 62. Feliche anakumbuka kwamba mwanzoni hakuwa akichukulia ngumi kama kazi rasmi, kiasi kwamba alikuwa akienda mazoezini akiwa amevaa heleni, cheni na lipstick.

“Nilikuwa bado sijauchukulia mchezo kama kazi. Nilikuwa naenda mazoezini na heleni, cheni na lipstick. Hata nilipopanda ulingoni sikuwa najua pambano lina raundi ngapi mpaka refarii aliponiambia ni raundi nne.”€

“Raundi za mwanzo zilikuwa ngumu sana, nilichoka, lakini kocha alikuwa ananipa moyo. Niliendelea kupambana mpaka mwisho nikashinda kwa maamuzi ya majaji wote watatu.”


MSHAHARA WA KWANZA

Tofauti na watu wanaoanza mchezo kwa kutafuta umaarufu pekee, Feliche alipata nafasi ya kulipwa tangu pambano lake la kwanza. Alilipwa Sh 300,000, fedha ambazo wakati huo zilikuwa nyingi kwake na kumfanya aanze kuona uwezekano wa kujenga maisha kupitia mchezo huo.

“Nililipwa laki tatu. Kwangu wakati huo zilikuwa fedha nyingi sana, niliona kumbe naweza kufanya kitu kikubwa kupitia ngumi. Hapo ndipo nilipoanza kuona umuhimu wa kuwekeza nguvu zangu zote kwenye mchezo.”


KABLA YA NGUMI

Kabla ya kuanza kujihusisha na ngumi, Feliche alikuwa msichana wa nyumbani. Baadaye alipata ajira ya mauzo katika kampuni moja iliyokuwa ikisambaza bidhaa.

Kazi hiyo ilimsaidia kwa sababu ilikuwa na nafasi nzuri ya kupanga muda wa majukumu yake na mazoezi. Aliweza kufanya kazi na wakati huohuo kuendelea kujenga uwezo wake katika mchezo wa ngumi.

“Kabla ya ngumi nilikuwa dada wa nyumbani. Baadaye nilipata kazi ya mauzo kwenye kampuni moja ya kusambaza bidhaa. Ilikuwa kazi nzuri kwa sababu nilikuwa napata muda wa kufanya kazi na kwenda mazoezini.”€


JOY AWINO ALINIPA PRESHA

Feliche anasema hajawahi kukutana na pambano gumu sana akiwa nyumbani Tanzania, lakini pambano lililompa presha kubwa lilikuwa la ubingwa wa Eastern and Central Africa mwaka 2018/2019 dhidi ya Joy Awino kutoka Kenya.

“Pambano lililonipa mawazo sana ni la Joy Awino kutoka Kenya. Alikuwa na mwili wa mazoezi, unaona kabisa ni mpinzani mwenye nguvu. Nilijua sitakuwa na kazi rahisi.

“Nilifanya sparing nyingi na wanaume ili kujiandaa. Mwisho wa siku nilifanikiwa kushinda kwa pointi na kuchukua mkanda wa ubingwa.”€


MTIHANI  WA KWANZA ULAYA

Baada ya kutwaa ubingwa mwaka 2019, Feliche alipata fursa ya kwenda Uingereza kupambana na Nina Bradley katika pambano la Ubingwa wa Jumuiya ya Madola.

“Baada ya kushinda mkanda mwaka 2019, nilipata connection ya kwenda Uingereza kucheza na Nina Bradley. Lilikuwa pambano la raundi 10. Nilipoteza kwa maamuzi ya majaji, lakini nilicheza vizuri sana.”€

MAPAMBANO TISA NJE YA TANZANIA

Feliche anasema ameshacheza mapambano tisa nje ya Tanzania, akitaja nchi kama Uingereza kuwa miongoni mwa maeneo aliyokwenda mara nyingi zaidi, huku pia akiwahi kupambana Afrika Kusini.

“Nimecheza mapambano tisa nje ya nchi. Nimeenda Uingereza mara nne au tano na Afrika Kusini mara moja. Nimejifunza mengi kupitia safari hizo.”€


MAKOCHA TOFAUTI

Kwa sasa anafundishwa na makocha Issa na Paul, huku pia akipata maelekezo kutoka kwa makocha wa Ufilipino chini ya Kocha Rick FC.

 “Nilianza kwa Kocha Kwame na Japhet Kaseba, baadaye nikawa chini ya Kocha Kanda Kabongo. Kwa sasa nafanya kazi na Kocha Issa, Paul na makocha kutoka Ufilipino chini ya Kocha Rick.”€


NGUMI ZIMENIJENGEA NYUMBA

Feliche anasema kwa kiasi kikubwa amefanikiwa kufikia malengo aliyokuwa amejiwekea alipoanza mchezo huo. Ngumi zimemuwezesha kujenga nyumba yake eneo la Boko, kusafiri katika mataifa mbalimbali na kujipatia umaarufu ndani na nje ya Tanzania.

“Ndiyo, nimepata mafanikio mengi. Kupitia ngumi nimeweza kujenga nyumba yangu Boko, kusafiri nchi mbalimbali kama Uingereza na kupata umaarufu. Kuna mambo ambayo nilikuwa nayatamani zamani, lakini kupitia mchezo huu nimeweza kuyafikia.”€


SHIDA YA WANAWAKE IKO HAPA

Kwa mtazamo wa Feliche, changamoto kubwa inayowakabili mabondia wanawake ni kutopata kipaumbele sawa na wanaume kutoka kwa waandaaji wa mapambano. Anasema baadhi ya mapromota wanajikita zaidi katika kuandaa mapambano ya wanaume na kuwaacha wanawake wakipata nafasi chache na malipo madogo.

“Changamoto kubwa ni sisi wanawake kutokupewa kipaumbele. Mapromota wengi wanapanga mapambano ya wanaume, sisi tunabaki nyuma na hata tunapopata nafasi malipo yanakuwa madogo.”€

“Pia hatuna wadhamini wa kutosha na usaidizi kutoka serikalini na viongozi wa ngumi bado ni mdogo. Hiyo inafanya iwe vigumu kwa mwanamke kujenga maisha kupitia mchezo huu.”€


MALIPO

Anasema kiasi kinachoweza kulipwa kinategemea ofa iliyotolewa, mkataba, ukubwa wa pambano na rekodi ya bondia husika. Kwa hiyo, hakuna kiwango kimoja anachoweza kusema ndicho cha chini katika kila mazingira.

“Siwezi kutaja kiasi maalumu kwa sababu malipo ni mazungumzo. Inategemea ofa unayopewa, mkataba na rekodi yako kwenye mchezo. Kila pambano lina mazingira yake.”€


KAZI PEKEE

Kwa sasa Feliche hana ajira nyingine zaidi ya mchezo wa ngumi. Aliwahi kufanya kazi ya kuajiriwa, lakini aliamua kuacha ili aweze kupanga vizuri majukumu ya familia yake, hasa kulea watoto na kuendelea na mazoezi.

“Kwa sasa sina kazi nyingine zaidi ya ngumi. Nilishawahi kuajiriwa lakini niliona inakuwa ngumu kupanga muda wa kazi, watoto na mazoezi. Nikaamua kuachana na ajira ili nijikite zaidi kwenye ngumi na familia.”€


MTOTO WA KWANZA

Feliche tayari alikuwa ndani ya mchezo wa ngumi alipoanza kujenga familia. Alipata mtoto wake wa kwanza mwaka 2020 na wa pili mwaka 2024, hivyo sasa ni mama wa watoto wawili.

“Nilipata mtoto wa kwanza mwaka 2020 na wa pili mwaka 2024. Ni kazi ngumu sana kuwa mama halafu wakati huohuo uwe mwanamichezo. Ndiyo maana niliona ni bora kuacha kazi ya kuajiriwa ili nipate muda wa kulea watoto na kufanya mazoezi.”


KAZI NA FAMILIA

Feliche anasema kawaida huingia kambini wiki moja au mbili kabla ya pambano ili kupata utulivu, kujikita kwenye mazoezi na kuondoa vishawishi vinavyoweza kuathiri maandalizi yake.

“Watoto wanakuwa nyumbani na wazazi wangu pamoja na familia. Mimi huwa naingia kambini wiki moja au mbili kabla ya pambano ili nipate utulivu na niweze kujiandaa vizuri bila mawazo mengi.”€


MAMA BORA

Anapokuwa nyumbani ni mama wa kawaida, anavaa magauni au dera, anapika na kufanya shughuli nyingine za kifamilia. Hata hivyo, anawashauri wanamichezo wanawake kuzingatia muonekano na namna wanavyojipresent katika jamii ili wasijenge taswira inayowafanya watu washindwe kutambua upande mwingine wa maisha yao.

“Mimi nikiwa nyumbani ni mama wa kawaida kabisa. Naweza kuvaa gauni au dera, napika na kufanya shughuli zangu za nyumbani. Sio kwamba kwa sababu mimi ni bondia basi lazima niwe mkorofi.”€

 “Nawashauri wanawake wenzangu wajue kujitofautisha na maisha ya ulingoni. Hata muonekano ni muhimu kwa sababu unaweza kukusaidia kupata matangazo na kuheshimika kwenye jamii.”


MUME SIO BONDIA

Anasema baba wa watoto wake hajihusishi moja kwa moja na shughuli za mchezo wa ngumi, lakini anaelewa kazi anayofanya na anamheshimu kutokana na majukumu yake kama mwanamichezo.

“Hapana, hajihusishi na masuala ya ngumi, lakini anaelewa kazi yangu. Ananiheshimu na ananipa ushirikiano.”


KUSTAAFU

Feliche anasema anapanga kustaafu mchezo wa ngumi ndani ya miaka mitatu hadi mitano ijayo. Hata hivyo, hataki kuondoka kabisa katika mchezo huo, kwani ana malengo ya kuwa refarii au promota ili kusaidia kuinua mabondia vijana wanaoanza safari zao.

“Ninajipa miaka mitatu mpaka mitano nistaafu. Baada ya hapo ningependa kuwa refarii au promota ili niweze kusaidia vijana chipukizi kwenye mchezo huu.”€

“Kama hayo hayatakuwa yamefanikiwa, mimi ni mkufunzi wa mazoezi binafsi. Pia najua fashion design, kushona na mambo ya saluni pamoja na kusuka.”€


URAFIKI WANGU NA MABONDIA WANAWAKE NI WA SALAMU

Feliche anasema hana urafiki wa karibu na mabondia wengi wanawake, zaidi ya kusalimiana wanapokutana. Hata hivyo, anamtaja mdogo wake Jesta ambaye pia ni bondia kuwa miongoni mwa watu wa karibu katika mchezo huo.

 “Sina urafiki wa karibu sana na mabondia wengi wa kike. Tunaishia kusalimiana tu, lakini mdogo wangu Jesta ambaye naye anacheza ngumi ndiye niliye karibu naye zaidi.”


JERAHA KUBWA ZAIDI

Februari mwaka 2026, Feliche alipata jeraha kubwa la kuvunjika mfupa wa pua wakati wa mazoezi ya sparing. Jeraha hilo lilikuwa moja ya nyakati ngumu zaidi katika safari yake ya ngumi kwa sababu alilazimika kuingia tena ulingoni siku chache baadaye akiwa bado na tatizo hilo.

“Jeraha kubwa zaidi nililopata ni kuvunjika mfupa wa pua mwezi wa pili mwaka huu wakati wa sparing. Kilichoniumiza zaidi ni kwamba siku chache baadaye nililazimika kuingia ulingoni nikiwa bado na jeraha hilo na nikapoteza pambano. Hilo ni jambo ambalo sipendi hata kulikumbuka.”


MKONGWE

Feliche anasema kwa sasa ana miaka 30 na anaelekea kutimiza miaka 31. Alianza kuingia ulingoni rasmi akiwa na miaka 20, hivyo ametumia takribani miaka 10 ndani ya mchezo huo.

“Kwa sasa nina miaka 30, naelekea 31. Nilianza kuingia ulingoni rasmi nikiwa na miaka 20, kwa hiyo nina miaka 10 kwenye mchezo wa ngumi.”


ANAWAHESHIMU HAWA

Anasema hana bondia mwanaume ambaye anaweza kumtaja kama rafiki yake wa karibu sana, lakini kuna mabondia anaowaheshimu kutokana na namna walivyompokea, kumfundisha na kumsaidia katika safari yake ya mchezo wa ngumi.

“Sina rafiki wa karibu sana mwanaume kwenye ngumi, lakini kuna watu ninaowaheshimu sana kwa sababu walinipokea na kunifundisha. Hao ni Fadhili Majia, Yona Segu, Ibra Class, Abdul Ubaya, Deo Samuel na Sharifu Omari.”