Hawa wakitajwa, yametajwa mabao 2025
Muktasari:
- Hakuna kitu kinachokwaza mashabiki wa soka kama kutazama mechi inayomalizika kwa matokeo ya 0-0. Mashabiki wanataka mabao. Kutokana na hilo, ndio maana kuna mastaa hao wamejitengenezea majina makubwa kutokana na uhodari wao wa kusukumia mipira nyavuni.
LONDON, ENGLAND: RAHA ya mechi, mabao. Hicho ndicho kinachofanya mashabiki wengi kwenda kwenye viwanja vya soka, kutazama ufundi wa kutikisa nyavu, jinsi makipa wanavyoteswa na kufanywa kuwa bize kuokota mipira kwenye nyavu za magoli yao.
Hakuna kitu kinachokwaza mashabiki wa soka kama kutazama mechi inayomalizika kwa matokeo ya 0-0. Mashabiki wanataka mabao. Kutokana na hilo, ndio maana kuna mastaa hao wamejitengenezea majina makubwa kutokana na uhodari wao wa kusukumia mipira nyavuni.
Sambamba na hilo la wafungaji wa mabao, kuna kundi jingine pia linahusudiwa kwenye soka, wakali wa kupiga pasi za mabao (asisti). Kwenye hilo, wapo mastaa ambao ni hodari kwa kufunga mabao na kuasisti, wakihusika kwenye kuleta mchango mkubwa kwa timu zao.
Makala haya yanahusu mastaa walihusika kwenye mabao mengi kwa timu zao za klabu kwa mwaka huu wa 2025 kwa maana ya kufunga na kuasisti.
1. Lionel Messi - mabao 62 (amefunga 42 + asisti 20)
Bado ameendelea kuwa tishio akiwa na umri wa miaka 38. Supastaa, Lionel Messi amefunika mastaa wote wa soka kwa kuchangia mabao mengi mwaka huu wa 2025. Kwenye ngazi ya klabu, mkali huyo amechangia mabao 62 huko Inter Miami ndani ya mwaka huu, akifunga mara 42 na kupiga pasi za mabao kwa maana ya asisti mara 20.
2. Harry Kane - mabao 55 (amefunga 44 + asisti 11)
Straika, Harry Kane anashika namba mbili kwenye orodha hii, lakini akiwa namba moja kwa Ulaya kutokana na mchango wake wa mabao kwa mwaka 2025. Kwenye mabao 44 aliyofunga tangu mwaka huu uanze, 23 amefunga katika msimu huu wa 2025-26. Fowadi huyo wa Bayern Munich amehusika kwenye mabao 55, akifunga 44 na kuasisti mara 11.
3. Kylian Mbappe - mabao 54 (amefunga 48 + asisti 6)
Staa huyo Mfaransa, Kylian Mbappe anaongoza kwa kufunga mabao ndani ya mwaka huu wa 2025, akitupia nyavuni mara 48 katika mechi 51. Hata hivyo kwenye orodha ya wachezaji waliochangia mabao mengi anashika namba tatu, kutokana na mchango wake kwa klabu ya Real Madrid kuwa mabao 54, akifunga 48 na kuasisti mara sita.
4. Vangelis Pavlidis - mabao 50 (amefunga 37 + asisti 13)
Tangu alipojiunga na Benfica mwaka jana, Vangelis Pavlidis amekuwa na wastani wa kuchangia bao kwenye timu hiyo kila baada ya dakika 94.3. Na ndio maana haishangazi kuona anashika namba moja kwenye mbio za Kiatu cha Dhahabu kwenye ligi ya Ureno, Primeira Liga. Staa huyo amehusika kwenye mabao 50, akifunga 37 na asisti 13.
5. Peeter Phanthavong - mabao 50 (amefunga 30 + asisti 20)
Kwa sasa anakipiga kwenye kikosi cha Ezra FC inayoshiriki Lao League 1, Peeter Phanthavong amekuwa na mwaka mzuri kabisa, akiwa na umri wa miaka 19 tu, lakini ni hatari akihusika katika mabao mengi mwaka 2025, akihusika katika mabao 50, akifunga mara 38 na kuasisti mengine 20 katika kuisaidia klabu yake kufikia malengo ya msimu.
6. Kevin Hernandez- mabao 48 (amefunga 43 + asisti 5)
Fowadi huyo wa Puerto Rico, Kevin Hernandez amekuwa kwenye kiwango bora sana cha kufunga mabao kwa mwaka huu akitumikia kikosi chake cha Puerto Rico SSC. Kwenye ligi pekee yake kwa msimu wa 2025-26, amefunga mabao 19 katika mechi 14, huku akiwa tayari ameshafunga hat-trick tatu ndani ya muda huo. Amehusika kwenye mabao 48, akifunga 43 na kuasisti matano.
7. Xherdan Shaqiri - mabao 46 (amefunga 24 + asisti 22)
Xherdan Shaqiri amekuwa kwenye kiwango bora kabisa tangu aliporejea kwenye klabu yake ya zamani ya FC Basel mwaka 2024. Alishinda ubingwa wa ligi na Kombe la Uswisi msimu uliopita, akimaliza msimu wa 2024-25 akiwa kinara wa mabao na asisti wa Basel. Ameendelea na moto wake kwa msimu wa 2025-26, huku kwa mwaka huu akihusisha kwenye mabao 46.