Gego afichua Aucho anavyogeuka mwalimu ndani ya uwanja
Muktasari:
- Furaha yake haiishii hapa. Anafurahia kupata namba kikosini na zaidi anafurahia kucheza sambamba na wajina wake, Khalid Aucho, pacha wake mpya na mtu ambaye alikuwa akimuangalia kama kioo.
KIUNGO mkata umeme wa Singida Black Stars, Khalid Habib 'Gego' ni mtu anayefurahia mengi katika soka lake kwa sasa. Ana furaha kuiwezesha timu yake kufuzu hatua ya makundi la Kombe la Shirikisho la Afrika ikiwa ni mara yao ya kwanza wanashiriki michuano hiyo ya CAF.
Furaha yake haiishii hapa. Anafurahia kupata namba kikosini na zaidi anafurahia kucheza sambamba na wajina wake, Khalid Aucho, pacha wake mpya na mtu ambaye alikuwa akimuangalia kama kioo.
"Ilikuwa ni ndoto lakini sasa ni uhalisia. Nilishawahi kuzungumza na wewe (mwandishi) kuwa namkubali sana Aucho, ni mchezaji ambaye nilikuwa namtazama uwanjani kama darasa, lakini sasa nacheza naye katika kikosi kimoja, najisikia vizuri.
"Nafurahi nacheza na mchezaji kiongozi uwanjani, kuna vitu vinaongezeka kwangu. Pengine hakuna ambaye anaweza kunielewa, lakini tangu nimeanza kucheza sambamba naye kuna vitu vimeongezeka kwenye uchezaji wangu."
KAMA BAHATI
Gego na Aucho ni pacha bora ndani ya kikosi cha Singida Black Stars tangu msimu huu umeanza kama anavyofunguka kocha mkuu Miguel Gamondi ambaye ameliambia Mwanaspoti kuwa anafurahishwa na muunganiko wa haraka baina ya wawili hao huku akikoshwa na uwezo wa Gego kuwa ni kijana mpambanaji.
"Kabla sijatua Bara nimekutana na wachezaji wengi wa kigeni bora kwenye michuano ya Mapinduzi Cup na sasa nakipiga soka Ligi Kuu na naendelea kukutana na viungo wazuri, lakini kwangu hadi sasa Aucho ndiye mchezaji bora.
"Aucho ni kiungo mzuri. Ana vitu vingi bora ambavyo kwa namna moja ama nyingine nilikuwa nikijifunza kutoka kwake sasa nacheza naye timu moja, amekuwa akinielekeza mengi na kuwa sehemu ya kuniaminisha kuwa mimi ni bora nitafika mbali," anasema Gego.
Anasema kipaji kikubwa na uzoefu alionao Aucho aliyetua Singida msimu huu akitokea kwa mabingwa mara nne mfululizo wa Ligi Kuu Bara Yanga, usingetarajia kumuona akiwa hana ujivuni akiwa ni msikivu na mwepesi wa kufundisha vitu vingi wenzake.
Tangu Gego ametua ndani ya Singida Black Stars ambayo ilikuwa na nyota wengi eneo hilo, ameendelea kuwa muhimili kikosi cha kwanza akimuondoa Kelvin Nashon ambaye alihudumu kwa muda na sasa anaitumikia Pamba Jiji.
FEI TOTO NEMBO YA ZANZIBAR
Ubora wa kiungo wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' umekuwa kivutio kwa mastaa wa ndani na hata wale wanaokuja Tanzania kucheza soka la kulipwa na zaidi kwa wachezaji kutoka Kisiwani Zanzibar alipozaliwa nyota huyo wamekuwa wakifunguka kuhusu ubora wake kama anavyothibitisha Gego.
"Kuna wachezaji wengi wazawa wanacheza nafasi ninayocheza mimi (kiungo), lakini kwangu kioo changu ni Fei Toto. Ni mchezaji ambaye hakubali kushindwa lakini pia haridhiki kutokana na kile anachokifanya siku hadi siku," anasema na kuongeza;
"Ubora wake na mafanikio anayoyapata Bara yamekuwa kivutio na kichocheo kwa wachezaji wanaoibuka na waliopo kuendelea kupambana ili kufikia alipo yeye sasa."
Gego anasema hakuna aliyekuwa anaamini kwenye ushindani alionao Fei Toto dhidi ya mastaa wa kigeni wanaocheza Ligi Kuu hivyo kutokana na makubwa anayoyafanya anazidi kuipaisha Zanzibar na kufungua milango ya wachezaji wengine kupata nafasi.
HAPA UTAMPENDA
"Mimi sio kiraka, lakini kutokana na kuchagua kazi ya soka kuwa ajira yangu, endapo kocha ataamua kunichezesha katika nafasi tofauti na kiungo naweza kucheza kwa kufuata maelekezo, lakini mimi ni bora zaidi na nafurahia kucheza nikiwa eneo la kiungo," anasema na kuongeza;
"Kiungo naweza kucheza chini na juu na sasa nimekuwa nikitumika zaidi chini ndani ya Black Stars, ila nilipokuwa KMKM nilikuwa nikicheza juu namba nane na nilipopata nafasi za kufunga na nilikuwa nazitumia vyema."
SIMU MOJA TU
Mastaa wengi wa Kizanzibar wanaocheza Ligi Kuu Bara wameibuliwa kupitia michuano ya Mapinduzi Cup na hilo pia limetokea kwa Gego ambaye amejiunga na Singida Black Stars katika dirisha kubwa msimu huu.
"Baada ya michuano ya Mapinduzi kwisha nilipokea simu moja kutoka kwa kiongozi ambaye sitaweka wazi jina lake, akaniambia kuhusiana na kunihitaji ili niweze kucheza timu yake, nikamwambia mimi bado nina mkataba hivyo anatakiwa azungumze na viongozi wa KMKM," anasema na kuongeza;
"Nilikuwa na mkataba wa mwaka mmoja nilipomweleza hayo alirudi kwa viongozi wangu na kumalizana nao na mimi ndipo nilipokaa nao mezani kwa lengo la kumalizana nao katika maslahi binafsi na sasa naitumikia Singida Black Stars."
Gego anasema matamanio makubwa kwake yalikuwa ni kuja kucheza Ligi Kuu Bara ambapo pia ni njia yake kutoka kwenda kusaka mafanikio mengine nje ya Tanzania.
NAMBA 4, 9 FRESHI
Sio kila mchezaji anavaa jezi namba kwa maana fulani. Kwa upande wa Gego yeye ni tofauti.
"Navaa jezi namba 4 kwasababu ndio namba niliyopewa baada ya kukuta haina mtu ndani ya Singida Black Stars. Pia kwenye maisha yangu ya mpira siamini katika kuvaa namba fulani ya jezi. Mimi yoyote navaa," anasema na kuongeza;
"Hata namba moja ingekuwa inavaliwa na wachezaji wa ndani ningevaa pia nyingine. Zote naweza kuvaa hadi tisa ambayo inatajwa kuwa ina mkosi, mimi naweza kuivaa kikubwa nipate nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza."