GARI LIMEWAKA: Wachezaji na kocha waliowasha Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Lakini si timu pekee zinazopambana kuonekana. Wachezaji nao wameanza kujitambulisha, hasa wale waliosajiliwa katika dirisha lililopita na ambao hawakuhitaji muda mrefu kuzoea mazingira mapya.
UTAMU wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2026/27 umeanza kushika kasi, huku kila timu ikipambana kujitengenezea nafasi nzuri katika mbio za mafanikio.
Lakini si timu pekee zinazopambana kuonekana. Wachezaji nao wameanza kujitambulisha, hasa wale waliosajiliwa katika dirisha lililopita na ambao hawakuhitaji muda mrefu kuzoea mazingira mapya.
Baadhi yao wameanza kwa moto mkubwa, wakikonga nyoyo za mashabiki na kuthibitisha kwa vitendo kwamba viongozi waliopambana kuwasajili hawakufanya makosa.
Wapo waliokuja kama nyota wakubwa, wengine majina yao hayakuwa na kelele nyingi, lakini ndani ya uwanja wameanza kuonyesha tofauti.
Hawa hapa ni wachezaji nane na kocha mmoja walioanza msimu kwa moto, wakitoa ishara kwamba mambo yao yanaweza kuwa makubwa zaidi kadri ligi itakavyoendelea.
OBREY CHIRWA – GEITA GOLD
Chirwa amefika Geita Gold akitokea Kagera Sugar, lakini hakuhitaji muda mrefu kuwaonyesha waajiri wake wapya thamani yake.
Mshambuliaji huyo wa Zambia tayari amefunga mabao manne akianza maisha yake Geita Gold kwa moto mkubwa.
Msimu uliopita Chirwa alifanya makubwa akiwa Kagera Sugar akifunga mabao 18 na kuwa mmoja wa wafungaji bora wa Ligi ya Championship huku akisaidia timu hiyo kurejea Ligi Kuu.
Wakati baadhi wakijiuliza kwa nini Kagera Sugar ilimuacha mshambuliaji huyo, Chirwa mwenyewe amekuwa jibu la swali hilo.
Alipokutana na waajiri wake hao wa zamani, aliwaadhibu kwa kufunga mabao mawili katika ushindi wa Geita Gold wa mabao 6-2.
PETER SHALULILE – YANGA
Usajili wa mshambuliaji Peter Shalulile kwenda Yanga ulikuwa miongoni mwa uliotikisa zaidi kutokana na historia yake katika soka la Afrika Kusini.
Mshambuliaji huyo wa Namibia alitua Jangwani akitokea Mamelodi Sundowns, ambako alikuwa amejijengea jina kubwa na kufanya makubwa kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Hakuchelewa kuanza kulipa. Katika mchezo wake wa kwanza tu aliweka mpira wavuni na hadi sasa amefikisha mabao mawili, huku akiwa ametoa pia asisti moja katika mechi nne za mwanzo dhidi ya Namungo, Coastal Union, JKT Tanzania na Pamba Jiji.
Mwanzo huo umemsaidia kushusha presha iliyokuwa juu yake kutokana na ukubwa wa jina lake.
Sasa kinachosubiriwa Jangwani ni mwendelezo, kwani matarajio kwa Shalulile ni makubwa.
IBRAHEEM JABAAR – SIMBA
Simba ilipomleta Ibraheem Jabaar kutoka Stellenbosch ya Afrika Kusini, matarajio yalikuwa makubwa.
Kiungo huyo wa Nigeria ameanza kuthibitisha mapema kwamba Wekundu wa Msimbazi hawakukosea kumleta.
Jabaar alionyesha uwezo wake katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, kabla ya kuendeleza kiwango hicho kwenye Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar na Pamba Jiji.
Bahati mbaya, alianza kukosa mechi baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja katika mchezo dhidi ya Pamba Jiji.
Kabla ya tukio hilo, alikuwa ameonyesha uwezo mkubwa katika eneo la kiungo na kuwapa mashabiki wa Simba sababu ya kuamini kuwa wamepata mchezaji anayefaa.
OSCAR MWAJANGA – MBEYA CITY
Jina lake huenda halina kelele kubwa kama mastaa wengine, lakini Mwajanga ameshaanza kufanya kazi yake uwanjani.
Mshambuliaji huyo wa Mbeya City tayari amefunga mabao matatu, akionyesha mapema kwamba Wagonga Nyundo hawakukosea kumleta.
Mwajanga alijiunga na Mbeya City akitokea Tanzania Prisons, iliyoshuka daraja na msimu huu kushiriki Ligi ya Championship.
Akiwa chini ya kocha Salum Mayanga, mshambuliaji huyo ameanza kuonyesha umuhimu wake katika kikosi hicho.
Mabao yake mawili yalikuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Fountain Gate, ushindi uliompa nafasi zaidi ya kuzungumziwa.
NATHANIEL CHILAMBO – SIMBA
Simba ilipata suluhisho la haraka katika upande wa kulia wa ulinzi baada ya kumsajili beki Nathaniel Chilambo kutoka Azam FC.
Chilambo alifika wakati Shomari Kapombe akiwa nje kwa majeraha na David Kameta ‘Duchu’ akikosa baadhi ya mechi kutokana na adhabu ya kadi nyekundu.
Badala ya kuonekana kama mbadala wa muda, Chilambo ameanza kuonyesha kwamba anaweza kuwa chaguo la kudumu.
Mbali na kucheza kama beki wa kulia, ameonyesha uwezo wa kuingia katikati ya uwanja na kusaidia eneo la kiungo.
Kiwango chake cha mwanzo kimewashusha presha mabosi wa Simba na sasa ushindani wa namba katika eneo hilo umeanza kuwa mkubwa.
HENRI STANIC – AZAM FC
Azam FC nayo imepata mchezaji mpya aliyeanza kuonyesha thamani yake mapema.
Beki huyo raia wa Ubelgiji alisajiliwa kutoka Stellenbosch ya Afrika Kusini na anacheza Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza.
Licha ya Azam kuruhusu mabao matano katika mechi nne za mwanzo, Stanic ameonyesha kiwango kinachotia matumaini.
Tayari ameshatwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi, aliyopata katika ushindi wa Azam wa 2-1 dhidi ya TRA United, mchezo ambao matajiri hao wa Chamazi walimaliza wakiwa pungufu.
Mwanzo wake unaonyesha kwamba Stanic anaweza kuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi hicho kadri msimu unavyoendelea.
ALBERT KANGWANDA – YANGA
Kumwacha Kangwanda kwenye orodha hii kungekuwa kosa.
Winga huyo wa Zambia amekuwa miongoni mwa wachezaji wapya walioanza kwa kishindo ndani ya kikosi cha Yanga.
Tukio lake kubwa la kwanza lilikuwa kwenye dabi dhidi ya Simba, ambapo kichwa chake kiliipa Yanga ushindi wa 1-0 na kutwaa Ngao ya Jamii.
Kama hiyo haitoshi, Kangwanda alikuwa tayari amefunga mabao mawili na kutoa asisti mbili katika Ligi Kuu kabla ya mchezo wa jana.
Hiyo inamfanya kuwa amehusika moja kwa moja katika mabao manne.
Lakini si mabao na asisti pekee vinavyomfanya Kangwanda azungumzwe.
Kasi yake, uwezo wa kuwatoka mabeki na akili yake anapokuwa na mpira vimeifanya Yanga ipate silaha nyingine katika eneo la pembeni.
JONATHAN SOWAH – SINGIDA BLACK STARS
Mshambualiaji Sowah amerejea katika klabu iliyompa jukwaa la kujitambulisha nchini Tanzania na ameanza safari yake ya pili akiwa na moto uleule.
Msimu uliopita, Sowah aliitumikia Simba katika kipindi kilichozungukwa na changamoto, huku akifunga mabao matatu kabla ya kuachana na klabu hiyo.
Lakini kabla ya kwenda Simba, alikuwa ameitumikia Singida Black Stars na ndani ya miezi sita tu akaifungia timu hiyo mabao 13.
Alionekana kuwa mmoja wa washambuliaji waliokuwa na kasi kubwa ya kufunga.
Sasa amerejea Singida na ameanza kuonyesha kwamba huenda mazingira hayo ndiyo yaliyomfaa zaidi.
Sowah tayari amefunga mabao matatu, akitoa ishara kwamba safari yake ya pili Singida inaweza kuwa na hadithi nyingine kubwa.
MANQOBA MNGQITHI – YANGA
Kama kuna mtu aliyeanza kwa presha kubwa, lakini akageuza hali ndani ya muda mfupi, basi ni kocha wa Yanga, Manqoba Mngqithi.
Baada ya kuanza kwa kipigo katika kilele cha Yanga Day, Mngqithi alijibu kwa vitendo.
Akaichapa Simba kwenye Ngao ya Jamii na kuipa Yanga taji la kwanza msimu huu.
Hakuishia hapo.
Katika Ligi Kuu, Yanga imeendelea na moto huo, ikikaa kileleni huku ikikimbizana na Simba. Katika mechi nne za mwanzo, timu zote zilikuwa zimeshinda michezo yote kabla ya Yanga kukutana na Fountain Gate jana.
Kinachompa Mngqithi nguvu ni namna timu yake ilivyoanza kufunga.
Katika mechi nne za mwanzo, Yanga ilikuwa imefunga mabao 13, huku ikiruhusu mawili tu.
Kwa kulinganisha, Simba ilikuwa imefunga mabao saba katika mechi zake nne za kwanza na kuruhusu mabao mawili.
Yanga ya Mngqithi imeonekana kuwa na nguvu katika kushambulia na kukaba, huku ikianza kuonyesha dalili za kuwa moja ya timu hatari zaidi msimu huu.
Kwa sasa, ni wazi mabosi wa Yanga wana sababu ya kuamini hawakukosea kumleta kocha huyo raia wa Afrika Kusini.