Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gamondi wa Pacome dhidi ya Gamondi wa Fei Toto

HISIA Pict


UMEKUWA uamuzi sahihi wa wakubwa wa mpira wetu kumchagua Miguel Gamondi kuwa kocha wa Taifa Stars. Nadhani ni kibarua ambacho atakwenda nacho mpaka Januari, mwakani, wakati michuano ya Afcon itakapomalizika pale Morocco.


Taifa Stars itacheza mechi zake mbili katika Jiji la Rabat halafu nyingine itacheza katika mji mwingine. Hizi mechi mbili za Rabat katika benchi atakaa Gamondi na ni uamuzi mzuri kuwa naye kwa sasa.


Kwanza unakuwa umempata kocha ambaye anawafahamu wachezaji wake kwa kiasi kikubwa. Angekuja kocha mwingine kutoka nje kwa sasa ina maana angehitaji muda kumjua Mohamed Hussein, Shomari Kapombe, Idd Nado, Feisal Salum, Mohammed Bacca, Dickson Job, Clement Mzize na wengineo.

Gamondi anawafahamu wachezaji hawa kupitia ile timu yake ya zamani, Yanga. Anawafahamu kwa sababu kuna ambao amewafundisha, lakini anawafahamu wengine kwa sababu alikuwa anacheza dhidi yao wakiwa katika timu.

HISI 03

Si ajabu wengine alikuwa anatamani hata wangekuwa katika kikosi chake, lakini kama unavyofahamu wakubwa wa Kariakoo na ndugu yao Azam huwa hawaachiani wachezaji kirahisi.

Gamondi pia anawafahamu wachezaji wetu wanaocheza nje kwa sababu alikuwa anakwenda uwanjani kutazama mechi za Taifa Stars. Huko aliwaona kina Mbwana Samatta, Simon Msuva, Novatus Dismas na wengineo.

Faida nyingine ya kuwa na Gamondi kwa muda ni kwa sababu ataendelea kuwa kocha wa timu yake Singida Black Stars. Sio jambo geni kwa kocha wa timu ya taifa pia kuendelea kuwa kocha wa klabu yake.

Imewahi kutokea hata kwa wenzetu walioendelea. Swali la kujiuliza ni kama Gamondi ndani ya muda mfupi anaweza kubadilisha kitu kutokea pale ambapo Hemed Suleiman 'Morocco' alikuwa ameishia. Watanzania hawajaguna sana kwa Gamondi kuteuliwa kuwa kocha wa Taifa Stars kwa sababu wanaikumbuka Yanga yake.

HISI 01

Je ataweza kuifanya Stars kuwa kama Yanga yake? Na papo hapo anaweza kukutana na kesi ya msingi mbele yake. Katika miaka ya karibuni klabu zetu kubwa zimekuwa zikibebwa sana na wachezaji mahiri wa kigeni na wachache wa ndani.

Muda si mrefu tutajua tu kwamba pamoja na uhodari wake wa kufundisha labda pia Gamondi alikuwa anabebwa na kina Pacome Zouazua, Aziz Ki, Maxi Nzengeli na wachezaji wengine wa kigeni ambao wameing’arisha Yanga katika siku za karibuni.

Unaweza pia kusema kwamba hata sasa hivi anang’ara na Singida yenye kina Clatous Chama, Khalid Aucho, Elvis Rupia na wengineo. Lakini kwa Taifa Stars atakuwa amekusanyiwa kundi la wachezaji wazawa. Anaweza kutufanyia kitu?

HISI 02

Lakini, hapo hapo kitakuwa kipimo kingine cha mbinu za Gamondi katika mechi kubwa. Yanga yake katika ubora ilikuwa inawapiga watu tano tano. Nadhani hata mtani alipigwa mabao matano katika utawala wa Gamondi.

Lakini, Gamondi ana mechi tatu mkononi pale Morocco. Dhidi ya Nigeria Desemba 23, halafu dhidi ya Uganda siku mbili baada ya Krismasi Desemba 27 kisha dhidi ya Tunisia, Desemba 30. Maisha hayatakuwa rahisi sana kwake.

Atahitaji kutuonyesha namna ambavyo anaweza kushambulia na kujihami kwa sababu ni wazi kwamba atakuwa na wachezaji wagumu tofauti na wale wapinzani aliokuwa anakutana nao Yanga. Hapo hapo akumbuke kwamba ana historia fulani ya kuiweka.

HISI 06

Taifa Stars haijawahi kushinda mechi hata moja katika fainali tatu ambazo imewahi kushiriki. Tulikwenda Nigeria 1980 tulikuwa na kina Leodeger Tenga na hatukuwahi kushinda mechi. Tukaenda Misri 2019 hatukuwahi kushinda mechi. Na mwaka juzi tukaenda Ivory Coast na kina Samatta tena na hatukushinda mechi.

Pambano dhidi ya Zambia tulikaribia kushinda mechi ya kwanza pale Ivory Coast baada ya Msuva kufunga la kuongoza, lakini dakika za mwisho Patson Daka akachomoa. Gamondi anaweza kuingia katika historia kutuwezesha kushinda pambano la kwanza.

Lakini, wakati mwingine maisha yanaenda kasi. Kwa akili ya haraka haraka ya watu waliompa kibarua cha muda Gamondi ni kwamba ataishika timu mpaka mwishoni mwa michuano ya Afcon kisha atatafutwa kocha mwingine wa kudumu kwa ajili ya kutupeleka katika fainali ambazo zitafanyika nyumbani kwetu kwa ushirikiano na Uganda na Kenya.

HISI 05

Kitu ambacho hauwezi kujua ni kwamba huenda Gamondi akaifanyia mambo mazuri timu ya taifa na kuwa kocha wa kudumu huku akiachana na kibarua cha Singida Black Stars. Naamini bado kuna heshima kubwa ya kuwa kocha wa Taifa Stars kuliko  Singida.

Kama nafasi ikijitokeza na tukamkubali kama ataibadilisha Stars, basi kibarua kinaweza kwenda kwake moja kwa moja. Lakini, ni eneo lipi hasa ambalo anapaswa kulifanyia kazi? Nadhani ni lile la mbele. Stars ya karibuni imekuwa haitengenezi nafasi za mara kwa mara za ufungaji.

Wote tunafahamu namna ambavyo Samatta, Feisal, Msuva na Mzize ni wafungaji wazuri, lakini kwa Taifa Stars ufungaji umekuwa tatizo kubwa. Gamondi akifanikiwa katika hilo tu basi kuna nafasi kubwa akatuachia mtihani wa maswali kumshawishi awe kocha wa kudumu.

Kwanza ajaribu kutuweka sawa tusione tofauti ya Yanga ya Pacome na Stars ya Feisal. Akifanikiwa hilo nadhani anaweza kuzuia nafasi ya kocha mwingine anayefikiriwa kuja kuifundisha timu ya taifa.

HISI 04

Ni kazi ngumu kwa sababu wengi tunaamini kwamba hata Simba na Yanga zisingefika fainali za Shirikisho bila wachezaji wa kigeni. Gamondi atuonyeshe kwamba hahitaji wachezaji wa kigeni kufanya timu ya Tanzania kushambulia kwa kasi na mbwembwe kama Yanga ilivyokuwa inafanya.