Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

FVS kidonge kichungu kumeza, tutaweza kuvumilia?

HISIA Pict


TULIHITAJI VAR yetu na ghafla TFF wametuletea kitu kinachoitwa Football Video Support kwa kifupi chake ni FVS. Kaka yangu Crescentius Magori baada ya pambano dhidi ya Pamba akadai wataiandikia barua Bodi ya Ligi kwa ajili ya kuangalia maboresho. Nadhani alikuwa amevurugwa kidogo na kinachoendelea dhidi ya Simba kwa sasa.


Simba imecheza mechi tatu mfululizo ikiwa pungufu. FVS imefanya kazi nzuri dhidi yao. Sio kwao. Dhidi yao. Ilianzia katika pambano la kwanza David Kameta ‘Duchu’ alilambwa kadi nyekundu kwa mchezo hatarishi dhidi ya David Luhende wa Kagera Sugar.


Mechi ya pili Ibraheem Jabaar akarusha kiwiko cha makusudi kwa mchezaji wa Pamba, Abdulkarim Yunus. FVS ikafanya kazi yake. Ilimchanganya Magori, lakini kadi nyekundu ilikuwa sahihi.


Kufikia hapo Jabaar alipaswa kuwaomba msamaha wachezaji wenzake aliowapa kazi ngumu uwanjani. Lakini pia alipaswa kuwaomba msamaha mabosi wake na mashabiki. Halafu mwishowe kabisa nadhani Magori angemkata nusu ya mshahara wake ili liwe onyo kwake na wachezaji wengine ambao wanapaswa kujua kwamba tumeingia katika zama mpya.

Halafu Antony Mligo akanaswa akiwa amecheza rafu mbaya kwa mchezaji wa Singida Black Stars, Yusuph Khamis pale Singida. Mashabiki wa Simba wamechanganyikiwa na FVS mpaka sasa.

Sio kwamba inawaonea, hapana. Wao kama walivyo watani zao nadhani hawajazoea sana haki katika mechi zao hasa hizi za ndani. Kihistoria na kwa rekodi wao ndio wamekuwa wakipata upendeleo zaidi dhidi ya timu ndogo.

HISI 01

Kama hali ikiendelea hivi nadhani wakubwa wataendelea kuumbuka na kuichukia FVS. Mzoea vya kunyonga vya kuchinja haviwezi. Tulitaka wenyewe mfumo huu wa kuondoa makosa ya kibinadamu katika soka letu, lakini nahisi kuna watu wameanza kuguna. Kwangu huu ni wakati sahihi wa kuleta haki ambayo italeta ushindani mkubwa katika soka letu. Hapo awali tulikuwa na haki feki.

Msimu uliopita bao la Peter Shalulile katika pambano dhidi ya Coastal Union lingeweza kuhesabika kisha tukasingizia makosa ya kibinadamu, lakini majuzi limekataliwa. Uzuri ni kwamba mwamuzi msaidizi alishaona kuwa ni offside (la kuotea). Kama asingeona na FVS isingekuwepo si ajabu leo tungekuwa tunalumbana kuhusu FVS. 

Penalti ambayo Pamba walipewa dhidi ya Simba tumezoea kuona Simba na Yanga wakipewa bila hata marudio ya FVS hayajaingia. Wadogo huwa hawapewi penalti kama zile dhidi ya wakubwa. Mwamuzi alipokwenda katika televisheni nadhani alihisi angeweza kuumbuka na hatimaye baada ya miezi mingi tukakuta wadogo wanapewa penalti dhidi ya wakubwa. Penalti ambayo iliwarudisha mchezoni.

HISI 02

Hata hivyo, mfumo wa FVS unahitaji tu uvumilivu wa kawaida. Anayelia leo anaweza kucheka kesho na anayecheka leo anaweza kulia kesho. Simba wana bahati tu kwamba wametengeneza timu imara ambayo haitetereki sana mchezaji mmoja akilambwa kadi nyekundu uwanjani.

Nimekumbuka tu kwamba kama mfumo huu ungeingia mapema, basi rafiki zangu kina Juma Nyosso na Kevin Yondani wangekuwa wanalamba umeme katika dakika ya nne tu ya mchezo. Alichofanya Jabaar kilikuwa kitu cha kawaida tu kwao enzi wakicheza soka la ushindani. Kurukia washambuliaji mateke ya migongoni ilikuwa ni kitu cha kawaida kabisa kwao. Kwa sasa nadhani ubabe wa kijinga uwanjani utapungua.

FVS sio tu inaweza kuchukiwa na wakubwa hapo mbeleni, lakini nahisi inaweza hata kuchukiwa na waamuzi. Na wao kwa kiasi kikubwa wataumbuka.

Zamani walikuwa wanajificha katika kivuli cha makosa ya kibinadamu, lakini kwa sasa hawataweza tena kujificha katika kichaka hicho. Wana nafasi ya kwenda katika televisheni kuangalia marudiano na kuchukua uamuzi mpya.

Wasiwasi wangu ni kwamba timu zimepewa nafasi chache za kutumia FVS.

Mara nne tu. Lakini vipi kama timu ikionewa mara saba hadi nane? Kuna uwezekano mwamuzi akagundua kwamba timu fulani imemaliza nafasi zake nne na baada ya hapo akaanza kuwagandamiza kwa makusudi akiamini kwamba hawana nafasi tena ya matukio yao kwenda kuangaliwa katika mfumo wa FVS.

HISI 03

Labda tungerudi katika mfumo wa VAR ambapo kila tukio lenye utata linarudiwa bila ya kujali idadi yake. Haki ni haki. Ikiwezekana itolewe mara nyingi zaidi kadri uvunjifu wa sheria unapojitokeza.

Hauwezi kuhukumu mara nne kisha ukawa ukomo wa haki. Bodi ya Ligi waliangalie hili kwa mara nyingine ingawa naelewa kwamba walikuwa wana nia njema kuweka matukio manne wakihofia upotezwaji wa muda.

Vyovyote ilivyo huenda FVS watakuwa wameleta jibu la swali maarufu ambalo nimekuwa nikijiuliza mara kwa mara. Je waamuzi wetu hawajui sheria vyema, wanapendelea au wanahongwa? FVS huenda ikatupa jibu sahihi zaidi.

Tutajua dhamira zao za kweli pale ambapo watakuwa wanaenda katika marudio ya televisheni. Wapo wengine ambao wataibua kichekesho pale ambapo wataendelea kusimamia uamuzi wa ovyo licha ya dunia nzima kuona kwa usahihi tukio fulani.

Kitu kingine ambacho kinapaswa kurekebishwa ni nani ana mamlaka ya kumwambia mwamuzi akaangalie tukio husika. Wakati mwingine kocha anakuwa mbali na eneo la tukio kiasi kwamba haoni kwa usahihi kilichotokea.

Bado wachezaji walio karibu wana nafasi ya kumwambia mwamuzi akaangalie marudio ya tukio husika. Sidhani kama kocha wa Pamba aliona kiwiko kilichorushwa na Jabaar wa Simba. Wakati yeye akiwa Magharibi kiwiko kilikuwa kimerushwa Mashariki mwa uwanja. Tutegemee pia kwamba FVS itatupunguzia ule mkeka mrefu unaotolewa na Kamati ya saa 72.  

Kuna mambo yatakuwa yanamalizwa ndani ya dakika 90 badala ya kusubir FVS. Kuna timu ambazo zilikuwa zinanufaika na mkeka wakati zingeweza kuanza adhabu mule mule uwanjani.

Mfano ni kosa la Ibrahim Hamad ‘Bacca’ kumpiga mtu teke kwa makusudi pale Morogoro kungekuwa na FVS ina maana wapinzani wa Yanga wangenufaika mapema kwa Yanga kucheza pungufu.

Hata hivyo, Bacca aliendelea kucheza dakika zote na akaanza kutumikia adhabu yake mechi iliyofuata baada ya mkeka wa kumfungia kutoka.

 Zamani ina maana Jabaar angemaliza mechi halafu akafungiwa baadaye. Pamba wasingenufaika na mkeka huo. Shukrani kwa sasa kuna watu wanaanza kupata machungu ndani ya dakika 90. Kuanza kutumikia adhabu mechi inayofuata ni kuwapa walioadhibiwa muda wa kujipanga.

Tunategemea pia kwamba Azam TV watakuwa wamejipanga kuonyesha mechi zote ‘live’ ili kila mechi ipate haki ya kuamuliwa kwa FVS. Tuna tatizo la msingi la kudhani sheria nyingj zipo kwa ajili ya Simba na Yanga tu. Sio kweli. Tuangalie haki pia katika mechi za JKT dhidi ya Namungo, Kagera Sugar dhidi ya Geita Gold na nyinginezo.

Na hapo hapo jambo jingine muhimu ni uwepo wa kamera nyingi ambazo zinaweza kuamua mambo kwa urahisi. Kuna ‘angle’ ambazo hata mwamuzi akienda katika televisheni anaweza asiambulie kitu kama sisi watazamaji.

Anaweza kufanya vitu kwa hisia tu. Yanga wamewahi kukataliwa bao la Shalulile kwenye mashindano ya CAF, lakini mpaka sasa hatujui kama kweli alizidi au hakuzidi. Ni kwa sababu ya kamera zenyewe.