FIFA yawalinda wanasoka wa kike wanapopata mimba
Muktasari:
- Katika Ibara ya 18(7) ya Shirikisho la Mpira wa Dunia (FIFA) (Regulations on the Status and Transfer of Players) iliyoanzishwa mwaka 2020 na kuanza kutumika Januari 1 2021 inampa mchezaji mwanamke haki ya likizo ya uzazi ya angalau wiki 14 pamoja na malipo ya theluthi mbili ya mshahara wake wa mkataba na endapo kama sheria ya kitaifa au makubaliano ya pamoja yanaweka masharti yenye manufaa zaidi yatatakiwa kuzingatiwa.
ELIMU duni ya uelewa kwa wanasoka wa kike ya kuijua sheria ya FIFA inayolinda haki zao pindi wanapopata ujauzito na baada ya kujifungua imetajwa kuchangia wengi wao kukatiza ndoto zao na kujikuta wanaishi majuto.
Katika Ibara ya 18(7) ya Shirikisho la Mpira wa Dunia (FIFA) (Regulations on the Status and Transfer of Players) iliyoanzishwa mwaka 2020 na kuanza kutumika Januari 1 2021 inampa mchezaji mwanamke haki ya likizo ya uzazi ya angalau wiki 14 pamoja na malipo ya theluthi mbili ya mshahara wake wa mkataba na endapo kama sheria ya kitaifa au makubaliano ya pamoja yanaweka masharti yenye manufaa zaidi yatatakiwa kuzingatiwa.
Ibara mpya ya 18 ya FIFA inasisitiza mchezaji atakuwa na haki ya kurejea katika shughuli za soka baada ya kukamilika kwa likizo yake ya uzazi klabu iliyomuajiri itakuwa na wajibu wa kumrejesha na kumpatia msaada wa kutosha na endelevu wa kitabibu pia mchezaji atapewa fursa ya kumnyonyesha mtoto mchanga au kukamua maziwa.
Mbali na FIFA sheria nyingine ni ya ajira na mahusiano kazini Na. 6 ya mwaka 2004; ambayo sasa ni Sura ya 366 Toleo lililorekebishwa mwaka 2019 kifungu cha 37 (1 na 2) kinasema itakuwa kinyume cha sheria kwa mwajiri kusitisha ajira ya mfanyakazi isivyo haki.
KAULI YA SPATA
Kutokana na kanuni ya 71(2) inayosema mchezaji yeyote wa Ligi Kuu anapaswa kuwa mwanachama wa Chama cha Wachezaji wa Mpira wa Miguu Tanzania (SPATA) kabla ya kukamilisha usajili wake kwenye klabu ya Ligi Kuu.
Katibu msaidizi wa SPATA Abeid Kasabalala anasema kutokana na kanuni hiyo wanashauri wachezaji wote kabla hawajasaini mikataba na klabu wanapaswa kuipeleka katika ofisi hizo ili ipitiwe na wanasheria ili kuweka vipengele vya kulinda haki zao.
“SPATA mwaka jana 2025 tulifanya semina ya kutoa elimu kwa wachezaji wa mpira wa wanawake zaidi ya mara sita tulikuwa na wawakilishi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) maana kulikuwa na malalamiko ya unyanyasaji wa kingono pia kulikuwa na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) vilizungumzwa vitu vingi vya kuvifanyia kazi ikiwemo na suala la mimba” anasema Kasabalala na kuongeza;
“Tunashauri kila mchezaji awe na mwanasheria wake wa kumsaidia kuchambua mkataba itakuwa rahisi hata kuingiza katika mkataba wake sheria ya FIFA pia ili klabu ifaidike na mchezaji anufaike mchezaji anapoanza kucheza akiwa na umri wa miaka 18 angalau aitumikie klabu miaka mitatu baada ya hapo atakuwa amefikisha umri wa miaka 21 umri ambao anaweza akawa anaanzisha familia pia nasisitiza viongozi wa timu wawe wanawapa elimu ya maisha wachezaji wasije wakazeeka bila watoto.”
KAULI YA TFF
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Evance Mgeusa anasema kitu kinachotakiwa kufanyika kwa wachezaji ni uelewa mpana kabla ya kusaini mikataba yao ili likitokea tatizo inakuwa rahisi kusaidika.
“Kuna Chama cha Soka la Wanawake Tanzania (TWFA) kabla hawajasaini mikataba yao waende ili wakasaidiwe kuweka baadhi ya vipengele muhimu ambavyo vitakuwa msaada pindi wanapopata changamoto lakini pia kuna maajenti wa FIFA ambao wakiwasimamia katika mikataba yao hawatakuwa wanapitia hali za kukata tamaa” anasema katibu huyo na kuongeza;
“Wengi wao wanasaini mikataba ili mradi wapate pesa za kula lakini inakuwa haina vipengele vyakuwalinda TFF tunapokea mikataba yao ambayo wamemalizana na timu zilizowaajiri.
“Kuna wengine wakipata mimba wanarudi katika mikoa waliyotokea kwani wanakuwa hawana uelewa wa nini kifanyike wen gine wana washauri wazuri wa kuwaambia nendeni TFF mkashitaki kabla sijawa katibu nimefanya kazi kwenye kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji nilikuwa naona kesi nyingi za aina hiyo.”
WANACHOSEMA ZFF
Katibu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) Hussein Ahmada Vuai anasema :”Mashirikisho ya mpira wa miguu nchini kama tutakubaliana tuitumie sheria ya kipolisi ambayo kabla ya askari kuanzisha familia kuna muda wanapewa wa kuitumikia serikali ukitumikia muda huo ndipo wanaweza wakaoa au kuolewa ipo hivyo pia katika jeshi ikiwa ni moja ya sharti lao kubwa.
Anaongeza:”Sheria hiyo ikitumika itasaidia klabu zilizowaajiri kunufaika kwa maana wanaposajili mchezaji inakuwa inamlipa na inategemea huduma yake ili haki zipatikane kwa pande zote mbili basi itumike sheria hiyo, vinginevyo itahitajika mjadala mpana kuhakikisha kila kitu kinakwenda kama kinavyotakiwa.”