Fetty Densa ataja siri ya kudumu Simba Queens
Muktasari:
- Densa ni miongoni mwa wachezaji waliodumu kwa muda mrefu Msimbazi tangu alipojiunga na Simba Queens mwaka 2019 akitokea Evergreen ya Temeke.
BEKI wa kulia wa Simba Queens, Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ amesema kujitunza, kufanya mazoezi na kuheshimu maelekezo ya makocha ni miongoni mwa mambo yanayomsaidia kudumu kwa muda mrefu katika kikosi hicho huku akiendelea kuonyesha kiwango kinachomweka kwenye ushindani wa namba.
Densa ni miongoni mwa wachezaji waliodumu kwa muda mrefu Msimbazi tangu alipojiunga na Simba Queens mwaka 2019 akitokea Evergreen ya Temeke. Umaarufu wake unatokana na uwezo wake uwanjani, huku mtindo wake wa kuvaa hijabu anapokuwa kwenye michezo ukimfanya awe miongoni mwa wachezaji wanaotambulika kirahisi katika soka la wanawake nchini.
Akizungumzia na Mwanaspoti siri ya kuendelea kuwa imara licha ya miaka mingi ya kuitumikia timu hiyo, Densa amesema kuheshimu kazi yake na kujali mwili ni sehemu muhimu ya maisha ya mchezaji anayetaka kudumu kwenye ushindani kwa muda mrefu.
“Mazoezi ni muhimu na yanasaidia. Wakati mwingine ukiwa hufanyi mazoezi unazeeka mapema,” amesema Densa, akisisitiza umuhimu wa mchezaji kuendelea kujifua ili kuuweka mwili katika hali nzuri.
Mbali na mazoezi, beki huyo amekuwa akisisitiza umuhimu wa kusikiliza na kutekeleza maelekezo ya makocha, akiamini juhudi za ziada ndizo zinazomsaidia mchezaji kuendelea kuwa bora.
Rekodi zinaonyesha Densa amekuwa sehemu ya mafanikio ya Simba Queens tangu mwaka 2019, akisaidia timu hiyo kutwaa mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu ya Wanawake katika misimu ya 2019/20, 2020/21 na 2021/22. Wakati timj hiyo sasa ikiandika historia ya kubeba mataji ya ligi mara nyingi zaidi ikichukua mara tano dhidi ya nne za JKT Queens.
Pia beki huyo alikuwa sehemu ya kikosi kilichofika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake mwaka 2022, mafanikio yaliyoiweka Simba kwenye ramani ya soka la wanawake barani Afrika.
Msimu wa 2021/22, Densa alionyesha umuhimu wake katika kikosi hicho kwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa msimu wa Ligi Kuu ya Wanawake. Mafanikio hayo yanaonyesha kudumu kwake Msimbazi si suala la miaka pekee, bali pia mchango wake katika mafanikio ya timu na uwezo wa kuendelea kushindana katika kiwango cha juu.