Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fei Toto wa 2024 sio huyu wa 2025

PUMZI Pict

Muktasari:

  • Taarifa za ujio wa Stars Afrika Kusini zilipokewa kwa shangwe na kuifanya ziara hiyo kusubiriwa kwa hamu kubwa kwa sababu ya kitu kimoja tu, uwepo wa Feisal Salum, Feitoto.

MWANZONI mwa mwezi Juni, timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ilifanya ziara maalumu Afrika Kusini. Ikiwa huko ilicheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya wenyeji Afrika Kusini na ikashiriki mashindano ya COSAFA kama mwalikwa.


Taarifa za ujio wa Stars Afrika Kusini zilipokewa kwa shangwe na kuifanya ziara hiyo kusubiriwa kwa hamu kubwa kwa sababu ya kitu kimoja tu, uwepo wa Feisal Salum, Feitoto.


Mchezaji huyo amekuwa akihusishwa na kujiunga na Kaizer Chiefs, ambayo ndiyo klabu kubwa na yenye mashabiki wengi zaidi nchini humo. Kwa hiyo ujio wake uliwaweka mashabiki wengi kwenye hali ya kusubiri kumwona 'mchezaji wao ajae'. Vyombo vya habari vikaisherehesha ziara ya Stars kutokana na Feitoto na kuifanya kuwa kubwa sana. Ni sawa na kilichotokea kwa Hispania mwaka 1982.

Nchi hiyo ilikuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia na mabingwa watetezi Argentina walitarajiwa kuja na kijana wao wa ajabu, Diego Maradona. Mchezaji huyo aliyekuwa gumzo Amerika Kusini alishamalizana na Barcelona akitokea Boca Juniors ya Argentina.

PUM 01

Kwa hiyo mashabiki wa Barcelona walimsubiri kwa hamu sana mchezaji wao mpya wamwone kwenye mashindano hayo.

Hicho ndicho kilichotokea kwa Feitoto na ziara ya Stars Afrika Kusini. Kile kilikuwa kipimo cha watu nchini humo kumwona huyo anayeitwa Feitoto, je yaliyomo yamo? Siku ikafika na Stars ikiwa na Feitoto ikashuka kwenye dimba la Peter Mokaba, mjini Polokwane.

Baada ya mchezo huo ulioisha kwa sare ya 0-0, mijadala nchini humo ikawa tofauti. Wachambuzi wengi na hata mashabiki wa kawaida wakamkataa Feitoto, Nyota wa zamani wa Orlando Pirates na Mamelodi Sundowns, Lebohang Mokoena ambaye sasa ni mchambuzi, alisema bayana Feitoto atahitaji muda mrefu sana kuweza kuendana na mikikimikiki ya ligi ya Afrika Kusini. Kwenye mitandao ya kijamii, watu wengi waliikanya Kaizer Chiefs kutowekeza kwa Feisal kwa sababu hakuwa na uwezo uliodhaniwa.

Yafuatayo ni baadhi ya maoni ya watu baada ya mchezo ule. 'Feisal was last seen singing a national anthem (Feisal Salum mara ya mwisho alionekana akiimba wimbo wa Taifa). Shabiki huyu alimaanisha Feitoto hakuonekana kabisa kwenye mechi, tangu aonekane wakati anaimba wimbo wa Taifa, kabla mechi haijaanza.

PUM 02

Signing this chap is tantamount to signing Andile Mpisane..better to sign son of the soil Andile Mpisane (Kumsaini huyu kijana ni sawa tu na kumsaini Andile Mpisane...ni kumsaini mzawa Andile Mpisane).

Shabiki huyu aliamini uwezo wa Feitoto unalingana na wachezaji wao wa ndani kama Andile Mpisane wa Royal AM FC.

If Selepe wasn't born Salum would've fooled us 🚮 (Endapo Selepe asingezaliwa, Salum angetudanganya). Shabiki huyu alimlenga Simphiwe Selepe wa Orlando Pirates, kijana wa miaka 20 ambaye ni gumzo kubwa sana Afrika Kusini.

Number 6 of Tanzania was quiet the entire game🐄🤣😂😅(Namba 6 wa Tanzania alikuwa kimya mechi yote). Namba sita ndiyo jezi aliyovaa Feitoto siku hiyo.

PUM 03

His gloves appeared more than him 😭😭😭 (Glovu zake zilionekana mara nyingi zaidi yake)

Feitoto alicheza akiwa amevaa glovu siku hiyo na ndicho alichokimaanisha shabiki huyu. Haya yalikuwa baadhi tu ya maoni ya mashabiki wa soka wa Afrika Kusini baada ya mchezo ule.

Ukweli ni kwamba Feitoto hakucheza vizuri mechi ile...alicheza chini sana ya kiwango chake. Na hii sio mechi ile tu. Feisal Salum amekuwa na kiwango cha chini sana katika kipindi chote cha mwaka 2025. Mojawapo ya ushahidi ni kwamba hajafunga bao lolote ndani ya mwala huu wa 2025. Mtu ambaye alikuwa bora sana mwaka 2024, amebadilika na kuwa wa kawaida sana mwaka 2025. Ama kwa hakika Feitoto alikuwa mchezaji bora wa Tanzania kwa mwaka 2024.

Alikuwa kwenye kiwango bora sana na kila alichofanya kiligeuka dhahabu. Lakini ulipoisha mwaka huo na yeye kila kitu kitu kiliisha. Sasa hivi ameongezeka mwili na kumsababishia uzito...Feitoto amekuwa mzito sana.

PUM 04

Zaidi ya kutofunga hata bao moja mwaka huu. Feitoto amekuwa mcheza madhambi kiasi mwaka huu pekee hadi sasa ameshapati kadi nne za njano.

Mechi ya mwisho ya ligi dhidi ya Fountain Gate mjini Babati. Feitoto  hakusafiri na timu kwa sababu alikuwa na kadi tatu za njano. Yaani Feitoto ana kadi nyingi mwaka 2025 kuliko mabao na asisti kwa pamoja. Na hili unaweza moja kwa moja ukalielekeza kwa vyombo vya habari. Vimekuwa vikimhusisha na klabu nyingine kila wakati kiasi cha kumnyima utulivu.

Vyombo vya habari vimeuandama uhamisho wa Feitoto utadhani wana mgao kwenye ada.

Hii imemfanya hata yeye mwenyewe kujikuta anakosa utulivu na kuweka mawazo yake yote kwenye mpira na kujikuta akiwa njiapanda. Hajasaini mkataba mpya na timu yake na hakuna ofa iliyokuja mezani kutaka huduma yake.

PUM 05

Yawezekana anapigiwa simu nyingi na kukaa vikao vingine na wote wanaotajwa kwenye uhamisho wake. Na kama ni hivyo, basi ule msemo wa miluzi mingi hupoteza mbwa, ndipo unapokuja.

Feitoto wa mwaka 2025 amepotezwa na miluzi mingi. Anatakiwa afanye maamuzi mapema, kama anaendelea kubaki Azam au anaondoka. Na kama anaondoka basi hao wanaomtaka wapeleke ofa mezani kwa Azam. Bila hivyo mwaka huu utaisha hivi hivi na utakaoanza utakuwa mbaya zaidi kwake.