Prime
Fei Toto na kalamu ya dhahabu isiyohitaji mkalimani
MJADALA kuhusu hatma ya timu ya taifa ya Tanzania, umekuwa ukichukua nafasi kubwa, hasa baada ya klabu kuruhusiwa kutumia idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni katika ligi.
Wapo wanaopendekeza kupunguzwa kwa idadi hiyo ili kutoa nafasi zaidi kwa wazawa, huku wengine wakiona suluhisho ni kuanzisha michuano maalum ya wachezaji wa ndani.
Hata hivyo, hoja kubwa ambayo mara nyingi inapuuzwa ni ubora wa mchezaji mwenyewe, bila kujali anatoka wapi.
Kwa mtazamo wa kina, soka la ushindani haliwezi kujengwa kwa kulinda nafasi kwa huruma. Linahitaji ushindani halisi. Ndiyo maana ukiangalia klabu kubwa kama Yanga au Azam, hazikimbilii kusajili mabeki wa kati wa kigeni au mabeki wa pembeni bila sababu.
Hii ni kwa sababu tayari wana wazawa wenye ubora wa kushindana katika nafasi hizo. Hapa ndipo hoja ya msingi inapojitokeza, ubora ndiyo unaoamua, si uraia.
Katika muktadha huo, kuna wachezaji wachache ambao wamevuka mipaka ya mijadala hii. Mfano bora ni Feisal Salum ‘Fei Toto’. Kiungo huyu kutoka visiwani Zanzibar amejiweka katika daraja ambalo halihitaji kutetewa kwa hoja za uzawa. Amefanya kile ambacho wachezaji wengi wanashindwa, kuweka kiwango kinacholazimisha heshima.
Kwa misimu kadhaa sasa, Fei Toto amekuwa mfano wa uthabiti. Msimu wa 2023–2024 ulikuwa wa kipekee kwake alipofunga mabao 19 Ligi Kuu Bara, akibaki nyuma kidogo ya Stephane Aziz KI aliyefunga 21.
Kwa kiungo, hizi ni takwimu zinazozungumza zenyewe. Lakini hakusimama hapo. Msimu uliofuata wa 2024–2025 aligeuka kuwa kinara wa pasi za mabao kwa kutoa asisti 14, akionyesha ana uwezo wa kufunga na kutengeneza.
Msimu wa sasa umeendelea kudhihirisha ubora wake, akiwa tayari na mabao saba na pasi saba za mabao.
Hizi si takwimu tu; ni uthibitisho wa mchezaji anayebadilika kulingana na mahitaji ya timu. Zaidi ya hapo, Fei Toto ameleta burudani uwanjani, kile kitu ambacho hakipimwi kwa takwimu lakini kinaongeza thamani ya mchezo.
Wakati mwingine, wachezaji wazawa wamekuwa wakikosolewa kwa kukosa nidhamu, kujiridhisha mapema au kushindwa kupambana. Lakini uwepo wa Fei Toto unavunja simulizi hiyo. Ameonesha mchezaji wa ndani anaweza kuwa na kiu ya mafanikio, nidhamu ya hali ya juu na uthabiti wa kiwango kwa muda mrefu.
Ndiyo maana kumlinganisha na vipaji vya zamani kama Haruna Moshi “Boban” kuna mantiki. Wote wawili wana kipaji cha asili, uwezo wa kubadilisha mchezo na mvuto unaowafanya mashabiki waje uwanjani. Hawa ni aina ya wachezaji wanaojenga historia, si kujaza namba tu.
Kwa upande mwingine, uwepo wa wachezaji wa kigeni kama Pacome Zouzoua haupaswi kuonekana kama tishio. Badala yake, ni kichocheo cha ushindani. Historia imeonyesha wachezaji wazawa wanapokuwa bora, wanawaondoa wageni katika nafasi zao bila kelele.
Mfano wa wachezaji kama Pascal Msindo na Lusajo Mwaikenda unaonesha hili wazi, hawakuhitaji sheria maalum, walihitaji ubora tu.
Hivyo basi, suluhisho la kuijenga timu ya taifa halipo katika kupunguza idadi ya wageni au kulinda nafasi kwa wazawa. Lipo katika kuwekeza kwenye maendeleo ya wachezaji kuanzia akademi, miundombinu, hadi malezi ya kisaikolojia na kitaaluma.
Tukizalisha wachezaji wengi wenye kiwango cha Fei Toto, ushindani utaongezeka na timu ya taifa itanufaika moja kwa moja.
Mwisho wa siku, soka ni mchezo wa ushindani, si huruma. Kama tunataka mafanikio ya kweli, lazima tukubali ukweli huu. Na kama kuna mfano hai wa kile tunachopaswa kufikia, basi Fei Toto tayari ameonyesha njia.