Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fatma Said Ally; Waziri aliyeikabili kadhia ya upangaji matokeo Ligi Kuu

FATMA Pict

Muktasari:

  • Kipindi hicho miaka ya 1980 na 1990, mashabiki wengi wa soka waliona haikuwa sahihi kwa Rais Ali Hassan Mwinyi kumbebesha mwanamke mzigo huo.

MWANAMKE aliyeweka historia ya kuwa waziri wa kwanza kuongoza wizara yenye dhamana ya michezo Tanzania ni Fatma Said Ally.

Kipindi hicho miaka ya 1980 na 1990, mashabiki wengi wa soka waliona haikuwa sahihi kwa Rais Ali Hassan Mwinyi kumbebesha mwanamke mzigo huo.

Mwanamke aliyekulia katika utamaduni na mila za watu wa Zanzibar kupewa wizara ya michezo huku mchezo mkuu ukiwa ni soka ambao viongozi wengi, mashabiki na wachezaji ni wanaume, haikuwa sahihi kwa Fatma Said Ally kubebeshwa jukumu hilo.

Kwa wale waliomjua Fatma Said Ally walikuwa na mtazamo tofauti. Waliona amepewa jukumu sahihi kwani mbali na kujulikana kuwa mwanamichezo, shabiki na mpenzi wa soka, pia alikuwa mwamuzi wa netiboli ambaye aliwahi kuucheza mchezo huo.

Akizungumzia enzi zake kwenye netiboli, Fatma, mama wa watoto wanne na ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 77, anasema mavazi yanayotumika kwenye netiboli yalimpa tabu.

Anafafanua kuwa mbele ya wengi hasa wanaume alionekana ni msichana mwenye kikiuka maadili kwa kwenda kinyume na mila na tamaduni za watu wa Zanzibar.

Mtazamo huo japo ulimpa tabu haukumtoa katika netiboli na ushabiki wake kwenye soka, hadi alipokuwa mtu mzima ingawa ameendelea kuwa mwanamichezo na shabiki wa soka na netiboli.

Akiwa waziri wa michezo, wakati huo wizara hiyo pia ilihusika na mambo ya utamaduni na maendeleo ya vijana, mwaka 1987 alijikuta katika kipindi kigumu kwenye mechi za mwisho mwisho za Ligi Kuu Bara (wakati huo Ligi Daraja la Kwanza). Ni mwaka ambao timu ya Simba ilikuwa ikipata matokeo mabaya hadi kufikia hatua ya kupambana kufa na kupona kujinasua na janga la kushuka daraja.

FAT 01

Kila mikakati ilivyopangwa ndivyo mambo yalivyozidi kuwa magumu, timu iliendelea kupata matokeo mabaya mechi baada ya mechi huku mgogoro mkubwa ukifukuta bila kupoa.

Viongozi wa wakati huo, walizongwa na kusakamwa na wanachama, waliotaka mkutano mkuu, wengine wakitaka uchaguzi na wengine wakitaka uongozi ung’olewe.

Suala la Simba kushuka daraja ilikuwa kama kuhesabu siku kwa namna msimamo wa ligi ulivyokuwa, mechi ya kufunga msimu wa ligi mwaka huo, Simba ilikuwa ikicheza na Tukuyu Stars ya Mbeya.

Ni mechi iliyobeba hatma ya Simba, ilikuwa lazima ishinde na kama ni sare iwe ya mabao mengi ili kuziacha mbali timu nyingine, pia ilikuwa lazima kujua matokeo ya mechi nyingine hususan idadi ya mabao.

Timu tatu zilikuwa zikichungulia kaburi la kushuka daraja; Biashara, Simba na kwa mbali Nyota Nyekundu au Red Star wakati Reli ilikuwa tayari imeshuka na inasubiri timu ya kuungana nayo.

Siku ya siku ikafika, Simba wakacheza na Tukuyu na mechi ikaisha kwa sare ya mabao 5-5, matokeo yaliyoiokoa Simba na janga la kushuka daraja.

Matokeo hayo yaliyoonekana kuipaisha Simba kwa faida ya mabao dhidi ya mpinzani wake katika janga hilo, timu ya Biashara.

Nje ya uwanja ikaibuka hadithi siku hiyo hiyo kwamba matokeo ya mechi ya Simba na Tukuyu yalipangwa.

FAT 02

Kilichozungumzwa ni kwamba Simba na Tukuyu walikubaliana kutoka sare ya 5-5, lengo likiwa ni kuifanya BIashara iungane na Reli kushuka daraja ili kuinusuru Simba.

Habari ya mechi ya Simba na Tukuyu kupanga matokeo ilikuwa gumzo kote Tanzania, mtu pekee aliyekuwa akisubiriwa kwa hamu kutoa kauli ni waziri mwenye dhamana ya michezo, Fatma Said Ally.

Pengine ingekuwa zama hizi za mitandao ya kijamii mijadala ingekuwa mikubwa zaidi kwenye Facebook, Instagram na kwingineko na si vijiweni pekee kama ilivyokuwa wakati huo.

Ukiachana na mechi hiyo habari ya upangaji matokeo pia ilihusishwa katika mechi ya Pamba na Nyota Nyekundu, ilidaiwa timu hizo zilicheza mechi yao ya mwisho kwa makubaliano.

Pamba walidaiwa kuusaka ushindi wakafanya kikao maalumu na viongozi wa Nyota Nyekundu ili kuhakikisha wanapata ushindi.

Pamba waliokuwa moto wakiusaka ubingwa, washindani wao wakuu zilikuwa timu mbili; Majimaji ya Songea na Yanga waliokuwa wakishika usukani wa ligi.

Nyota Nyekundu hata hivyo waliangalia mbali, walirekodi mazungumzo yao na Pamba na baadaye wakayatumia kama ushahidi kwa waziri ili kujinasua na janga la kushuka daraja kwa kuzidiwa pointi na Biashara.

Biashara nao wakahusishwa na sakata hilo hilo la upangaji matokeo kwenye mechi yao ya mwisho dhidi ya RTC Kigoma.

Biashara walihitaji ushindi, waliamini mabao mengi yangewatoa katika janga la kushuka daraja na kuwaachia Nyota Nyekundu au Simba, moja ya timu hizo ingeungana na Reli.

Biashara, timu iliyokuwa dhaifu katika mechi yake ya mwisho ya ligi  iliifunga RTC Kigoma 5-2, matokeo yaliyoacha maswali na hoja kubwa ilikuwa ni hisia kwamba timu hizo pia zilipanga matokeo.

Matukio yote hayo yaliwafanya mashabiki kuongeza shauku ya kutaka kusikia uamuzi utakaochukuliwa dhidi ya wapanga matokeo.

Mtoaji wa hukumu au adhabu hiyo hakuwa mwingine, bali ni Fatma Said Ally, mwanamama aliyekuwa na dhamana ya juu kwenye michezo.

FAT 03

Fatma Said Ally akaja na uamuzi tofauti, alifuta matokeo ya mechi zote za mwisho za ligi, uamuzi ulioifanya Biashara iungane na Reli kushuka daraja, Simba na Nyota Nyekundu zikapona na kubaki kwenye ligi.

Uamuzi huo haukuacha kujadiliwa, wapo walidai ulikuwa wa kuibeba Simba lakini wapo waliousifia na kuona kuwa ni wa busara kwa kuwa uliangalia kwenye tatizo na kukabiliana nalo moja kwa moja.

Wapo ambao pia walitoa lawama zao kwa sababu tu waziri alikuwa mwanamke na kuonekana kama hakuwa mtu sahihi wa kupewa wizara hiyo na hata maamuzi yake hayakuwa sahihi.

Tukio hilo ni moja ya matukio ambayo yapo katika kumbukumbu za Waziri Fatma Said Ally katika utekelezaji majukumu kwenye wizara ya  michezo na utamaduni.

Fatma Said Ally ambaye alipata shahada ya kwanza ya elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1977 hadi 1980 na baada ya hapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Southampton nchini Uingereza na kusoma shahada ya pili pia katika elimu, pia akiwa waziri anakumbukwa kwa namna alivyozipamba nywele zake kwa kuziweka ‘kalikiti’, staili iliyopamba moto enzi hizo kwa wanawake wengi hasa wa mjini.

Waliokuwa wakimnanga walihoji inakuwaje waziri Mtanzania mwenye dhamana ya utamaduni anaweka nywele kalikiti, utamaduni ambao si wa Kitanzania wala wa Kiafrika, ni utamaduni wa kigeni, wa kuiga na kutaka kuonekana mzungu.

Nilipomuuliza kuhusu hilo alicheka kidogo akionekana kulikumbuka jambo hilo lakini alisema ilikuwa ni ujana na ndio kwanza alikuwa ametoka masomoni Uingereza.

“Unajua mambo ya ujana, ndio kwanza nilikuwa nimetoka Uingereza sasa kuna mambo kutokana na ujana yanakuwa ya kawaida,” anasema.

Fatma Said Ally ambaye hakuwa tayari kuweka wazi ushabiki wake kwa timu za Simba na Yanga, akiwa waziri pia hakufurahishwa na nguvu kubwa ya timu hizo kwenye soka la Tanzania, aliona kama timu nyingine zinaachwa nyuma.

Aliamini jambo hilo linapunguza ushindani katika soka na wizara yake ina wajibu na kila sababu ya kuzisaidia timu nyingine ili kuongeza ushindani na kusaidia kukuza soka.

Walianza kuzitafutia baadhi ya timu makocha na mojawapo ni timu ya Majimaji waliyoisaidia kupata kocha Samsarov kutoka Bulgaria.

Aliomba msaada kwa rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere akiamini nguvu na ushawishi wa Mwalimu vingesaidia kuikabili nguvu kubwa ya Simba na Yanga.

Aliamini kauli ya Mwalimu ingewafanya viongozi washtuke na kusaidia kuimaisha timu zao hasa mikoani badala ya kushiriki kuzisaidia Yanga na Simba pekee. Baada ya kupata habari kwamba Mwalimu alikuwa Songea kikazi, Waziri Fatma Said Ally anasema walisafiri usiku ili tu wakutane na Mwalimu na kuzungumza naye jambo hilo.

“Kipindi kile barabara zilikuwa mbovu lakini hatukujali tulisafiri usiku kwa gari aina ya Land Rover, siku iliyofuata tukakutana na Mwalimu na kufanya naye kikao,” anasema.

Waziri Fatma Said Ally anafafanua kuwa katika kikao hicho walikuwapo viongozi wa michezo na wale wa chama na serikali.

Baada ya kumuelezea Mwalimu jambo lile, Mwalimu naye alimwambia pale pale kuwa hata wale viongozi tuliokua nao ni mashabiki wa Simba na Yanga na wasingeweza kumsaidia.

Mwalimu alinisikiliza kisha akasema wazi wazi, “hata hawa ulionao hapa kwenye kikao wanakudanganya, nao ni mashabiki wa Simba au Yanga hawataweza kukusaidia lolote,”’ anasema.

Anasema baada ya kikao kile ndipo alipobaini ugumu wa alichokuwa akijaribu kukipigania na hadi leo hashangai kuona Simba na Yanga zinavyoendelea kuwa na nguvu kubwa kwenye soka la Tanzania.