Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dunia imepoteza tamasha la World XI

MAGWIJI Pict

Muktasari:

  • Desemba 1997, Uwanja wa Velodrome jijini Marseille, Ufaransa, uligeuka kuwa jukwaa la kipekee baada ya timu za Europe XI na Rest of the World kukutana katika mchezo wa kirafiki uliokusanya baadhi ya wachezaji bora duniani.

LONDON, ENGLAND: KULIKUWA na kipindi ambacho mashabiki wa soka walipata nafasi ya kuwaona mastaa wakubwa duniani wakicheza timu moja, licha ya kutoka mataifa tofauti na kuwa wapinzani kwenye mashindano rasmi. Hata hivyo, utamaduni huo wa mechi za mastaa wa dunia (World XI) umepotea kutokana na mabadiliko makubwa ya biashara ya soka.

Desemba 1997, Uwanja wa Velodrome jijini Marseille, Ufaransa, uligeuka kuwa jukwaa la kipekee baada ya timu za Europe XI na Rest of the World kukutana katika mchezo wa kirafiki uliokusanya baadhi ya wachezaji bora duniani.

Miongoni mwa nyota waliokuwapo ni Ronaldo de Lima, Gabriel Batistuta, Zinedine Zidane, Fernando Hierro, Alessandro Costacurta, Paul Ince, Patrick Kluivert na Alen Boksic.

Mchezo huo ulikuwa sehemu ya maandalizi kuelekea droo ya Kombe la Dunia la mwaka 1998, ambapo kila taifa lililokuwa likishiriki lilikuwa na mwakilishi wake katika kikosi hicho cha nyota.

Hata hivyo, mmoja wa wachezaji waliopata nafasi ya kushiriki alikuwa beki wa Denmark, Soren Colding, ambaye hakutarajia kuitwa katika kikosi kilichokuwa kimejaa majina makubwa ya soka duniani.

Colding, aliyekuwa akiichezea Brondby, alisimulia namna alivyopokea mwaliko huo na kujikuta akicheza pamoja na mastaa aliokuwa akiwaona kama magwiji wa mchezo huo.

MAGWI 01

“Bila shaka, unapoona majina yale, unahisi kama ndoto imetimia,” alisema Colding, ambaye baadaye aliichezea Denmark mechi 27 na kushiriki Kombe la Dunia la 1998 pamoja na Euro 2000.

Alisimulia pia namna alivyofikishwa Ufaransa kwa ndege na kupelekwa hotelini kwa gari maalumu, ambako alikuta zawadi mbalimbali za FIFA, ikiwemo vifaa vya michezo.

Hata hivyo, aliposhuka kwenda kula chakula cha mchana akiwa amevalia mavazi ya mazoezi ya Adidas, alijikuta akiwa tofauti na wachezaji wengine waliokuwa wameketi pamoja na mawakala, wake, familia na marafiki zao.

“Nilikuta begi kubwa zaidi la Adidas ambalo sijawahi kuliona maishani mwangu. Ndani yake kulikuwa na mavazi ya mazoezi, nikayavaa na kwenda kula chakula cha mchana. Nilipofika nikawakuta wachezaji wengine wameketi kwenye meza zao wakiwa na mawakala, wake, familia na marafiki zao, wamevaa nguo za kawaida. Halafu yule Mdenmark akaingia akiwa amevalia mavazi ya mazoezi ya Adidas! Hakuna anayemjua,” alisimulia kwa utani.

Katika mchezo huo, mashabiki 38,000 walijitokeza kumshuhudia Ronaldo, ambaye wakati huo alikuwa katika kiwango cha juu baada ya kuhamia Inter Milan akitokea Barcelona kwa ada iliyoweka rekodi ya dunia.

Mshambuliaji huyo alikuwa ametoka kufunga mabao 47 katika mechi 49 akiwa Barcelona, jambo lililomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa wakivutia zaidi duniani.

MAGWI 02

Akiwa nahodha wa Rest of the World, Ronaldo alionyesha ubora wake kwa kufunga mabao mawili na kutoa pasi za mabao matatu katika ushindi wa 5-2 dhidi ya Europe XI. Batistuta naye alifunga mabao mawili, huku Zidane akifunga bao moja kwa upande wa Ulaya.

Colding, ambaye aliwahi kukutana na Ronaldo katika mechi ya timu za vijana chini ya miaka 21 kati ya Denmark na Brazil kabla ya Michezo ya Olimpiki ya 1996, alisema kasi, nguvu na uwezo wa mshambuliaji huyo vilikuwa vya kiwango kingine.

Alikumbuka pia namna Ronaldo alivyokuwa mtu mwenye aibu na asiye na makuu licha ya kuzungukwa na watu wengi waliokuwa wakimlinda na kumfuatilia.


MAGWI 05

MARADONA ALIVYOTUA WEMBLEY

Michezo ya timu za nyota duniani haikuanza mwaka 1997, bali ilikuwa na historia ndefu iliyoanzia mwaka 1963, wakati England ilipoadhimisha miaka 100 ya Shirikisho lake la Soka (FA) kwa kuandaa mchezo wa timu ya nyota dhidi ya England.

Mchezo huo ulivutia mashabiki takribani 100,000 waliojazana katika Uwanja wa Wembley, na baadaye mechi za aina hiyo zikawa zikifanyika mara kwa mara kwa ajili ya kuchangisha fedha au kuadhimisha mafanikio ya wachezaji.

Katika nyakati tofauti, mastaa kama Eusebio, Zico na Roberto Baggio walipata nafasi ya kushiriki michezo hiyo.

Hata hivyo, miongoni mwa matukio yaliyokumbukwa zaidi ni ujio wa Diego Maradona katika Uwanja wa Wembley mwaka 1987, mwaka mmoja baada ya kuiongoza Argentina kutwaa Kombe la Dunia la 1986 na kufunga bao maarufu la ‘Mkono wa Mungu’ dhidi ya England.

Wakati huo, Maradona alialikwa kucheza katika mchezo wa kuadhimisha miaka 100 ya Ligi ya Soka England (Football League), akiikabili timu iliyokuwa na wachezaji wa ligi hiyo.

Kwa mujibu wa Jon Smith, aliyekuwa mwakilishi wa Maradona, nyota huyo alilipwa takribani pauni 250,000 na kusafirishwa kutoka Napoli kwa ndege binafsi.

Smith alisema Maradona alitaka pia kupeana mikono na wachezaji wa England na kuwaomba radhi wale waliohisi kukerwa na bao lake la ‘Mkono wa Mungu’.

MAGWI 06

“Kwa kweli, alitaka kupeana mikono na timu hiyo na kusema, ‘Samahani kama niliwaudhi.’ Aliamini kipaji chake alipewa na Mungu,” alisema Smith.

Alieleza kuwa Maradona alikuwa na sura mbili tofauti, kwani nje ya uwanja alikuwa mtu mpole na mwenye urafiki, lakini alipoingia uwanjani alibadilika na kuwa Maradona ambaye dunia ilimfahamu.

Katika mchezo huo, timu ya Football League ilishinda mabao 3-0, Bryan Robson akifunga mawili na Norman Whiteside akiongeza jingine.

Smith alikumbuka pia tukio la kumtambulisha Maradona kwa kocha Bobby Robson, ambaye alikataa kupeana naye mkono wa kushoto kutokana na tukio la bao la ‘Mkono wa Mungu’, lakini baadaye wakapeana mkono mwingine.


MAGWI 04

TAMASHA LA MWISHO LA MASTAA

Mojawapo ya michezo mikubwa ya mwisho ya aina hiyo ilifanyika Februari 2005 katika Uwanja wa Nou Camp, Barcelona, ambapo timu ya Ronaldinho ilicheza dhidi ya kikosi cha Andriy Shevchenko kwa ajili ya kuchangisha fedha kwa wahanga wa tsunami iliyotokea mwaka 2004.

Timu ya Shevchenko ilikuwa na mastaa kama Zidane, David Beckham, Alessandro Del Piero, Thierry Henry, Raul, Paolo Maldini na Steven Gerrard.

Kwa upande wa Ronaldinho, kikosi chake kilikuwa na Ronaldo, Kaka, Cafu, Adriano, Javier Zanetti, Didier Drogba na Samuel Eto’o.

Hata hivyo, mshambuliaji wa Southampton, Henri Camara, ndiye aliyekuwa shujaa wa mchezo huo kwa kufunga mabao mawili katika ushindi wa 6-3 wa timu ya Ronaldinho.

Pamoja na mvuto wa michezo hiyo, mabadiliko ya soka la kisasa yamefanya iwe vigumu kwa wachezaji wakubwa kuruhusiwa kushiriki mechi za maonyesho.

Jon Smith alisema biashara ya soka imekua kwa kiwango kikubwa, tofauti na zamani ambapo wachezaji walikuwa wakipata mishahara mizuri lakini si mikubwa kama ilivyo sasa.

MAGWI 03

Alieleza kuwa klabu haziwezi kuhatarisha afya za wachezaji wao kwa kuwaruhusu kucheza mechi zisizo sehemu ya ratiba rasmi, hasa kutokana na uwezekano wa kupata majeraha ambayo yanaweza kuathiri shughuli za timu.

Pia, baadhi ya wachezaji sasa wanamilikiwa au kusimamiwa na makampuni makubwa na wawekezaji wenye nguvu za kifedha, hali inayofanya uamuzi ya kushiriki michezo hiyo kuwa magumu zaidi.


COLDING BADO ANAILINDA JEZI YAKE

Licha ya kupita takribani miaka 30 tangu mchezo wa Marseille, Colding bado anaihifadhi jezi aliyovaa wakati wa kuwakabili mastaa kama Ronaldo na Batistuta na kucheza pamoja na Zidane.

Alisema mchezo huo ulikuwa zaidi ya fedha, kwani wachezaji walipata nafasi ya kuiwakilisha nchi zao, kufurahia soka na kuonyesha mshikamano kati ya wachezaji kutoka mataifa tofauti.

Alisisitiza kuwa licha ya kuwa wapinzani wanapokutana katika mashindano rasmi, soka linaweza kuwaunganisha na kuwafanya kuwa marafiki nje ya uwanja.

Kwa Colding, michezo hiyo ilikuwa na ujumbe mkubwa kwa mashabiki na kizazi kipya cha wachezaji, kwamba soka si biashara na ushindani pekee, bali pia ni mchezo unaopaswa kuleta furaha na kuunganisha watu.

Alisema hata anapowaonyesha watoto wake jezi hiyo na kuwasimulia namna alivyocheza pamoja na Zidane na kukabiliana na Ronaldo na Batistuta, wakati mwingine huwa hawaamini kuwa kweli alikuwa sehemu ya kikosi hicho.