Serengeti Boys kamili kado Kombe la Dunia U-17
Muktasari:
- Serengeti Boys inayoshiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo, imepangwa Kundi I pamoja na Brazil, Costa Rica na Jamhuri ya Ireland katika fainali hizo zinazoanza Novemba 19 hadi Desemba 13, 2026.
KOCHA wa Serengeti Boys, Elieneza Nsanganzelu amesema mechi tatu za maandalizi walizocheza Dubai zimewasaidia wachezaji kupata muunganiko na kuzoea mazingira ya ushindani kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 17 (U-17).
Serengeti Boys inayoshiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo, imepangwa Kundi I pamoja na Brazil, Costa Rica na Jamhuri ya Ireland katika fainali hizo zinazoanza Novemba 19 hadi Desemba 13, 2026.
Nsanganzelu amesema maandalizi yaliyofanyika katika mazingira tofauti ya ushindani yamewapa nafasi ya kupima uwezo wa wachezaji kimwili na kisaikolojia, huku yakisaidia kujenga muunganiko ndani ya kikosi.
Amesema michezo hiyo imewapa picha halisi ya uwezo wa timu na kuwafanya wachezaji kuzoea mazingira ya mashindano makubwa, jambo linaloweza kuwasaidia kuanza vizuri fainali hizo.
“Mechi za kirafiki zimetupa mtihani. Tukiwa katika mazingira ya mashindano, tumepima uwezo wa kimwili na kisaikolojia, jambo ambalo limetusaidia kuwa tayari na kutufanya mazingira haya yasiwe mageni. Hii itatupa mwanzo mzuri,” amesema Nsanganzelu.
Kauli ya kocha huyo inakuja baada ya Serengeti Boys kukamilisha michezo mitatu ya kirafiki katika mashindano ya Dubai Youth Challenge, ambako ilianza kwa kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Venezuela, ikafuatiwa na sare ya bao 1-1 dhidi ya Australia kabla ya kuhitimisha kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tajikistan.
Michezo hiyo ni sehemu ya maandalizi ya muda mrefu yaliyohusisha pia safari za China, England na Korea Kusini, ikiwa ni mkakati wa kuwazoesha vijana hao mazingira na mitindo tofauti ya soka kabla ya kushiriki Kombe la Dunia.
Katika mashindano ya Vertex Cup yaliyofanyika England, Serengeti Boys ilianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya China, bao lililofungwa na Luqman Ally.
Serengeti Boys inaingia kwenye fainali hizo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya mashindano ya AFCON U-17 yaliyofanyika Morocco mwaka 2026, ambako ilifika fainali na kumaliza katika nafasi ya pili.
Katika mchezo huo wa fainali, Tanzania ilipoteza kwa mikwaju ya penalti 4-2 dhidi ya Senegal baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 120.