Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chicharito aitaka Mexico kuanza kwa kishindo Kombe la Dunia 2026

MEXICO Pict

Muktasari:

  • Hernandez ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa Mexico akiwa na mabao 52, alisema mchezo wa kwanza dhidi ya Afrika Kusini utakuwa muhimu katika safari ya timu hiyo ndani ya mashindano hayo makubwa yatakayofanyika Marekani, Mexico na Canada.

MEXICO CITY, MEXICO: MSHAMBULIAJI wa zamani wa timu ya taifa ya Mexico, Javier ‘Chicharito’ Hernandez anaamini Mexico inaweza kufanya vizuri katika Kombe la Dunia 2026, lakini jambo muhimu zaidi ni kuanza mashindano hayo kwa ushindi ili kujenga morali na kujiamini kwa timu.

Hernandez ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa Mexico akiwa na mabao 52, alisema mchezo wa kwanza dhidi ya Afrika Kusini utakuwa muhimu katika safari ya timu hiyo ndani ya mashindano hayo makubwa yatakayofanyika Marekani, Mexico na Canada.

Kwa mujibu wa nyota huyo wa zamani wa Manchester United, maandalizi mazuri pamoja na kuimarika kwa ushirikiano wa wachezaji ndani ya kikosi hicho vinaweza kuifanya Mexico kuwa moja ya timu zitakazotoa ushindani mkubwa katika michuano hiyo.

MEXI 01

“Hofu yangu kubwa ni kuona timu inaanza vibaya. Ukiianza vizuri michuano kama hii unapata nguvu, morali na kujiamini. Nina matumaini Mexico itaingia vizuri na kupata matokeo mazuri,” anasema Hernandez.

Katika Kombe la Dunia 2026, Hernandez hatakuwa sehemu ya kikosi kama mchezaji, bali atakuwa mchambuzi wa soka katika kituo cha Fox Sports, kazi ambayo amesema anaingojea kwa hamasa kubwa.

Nyota huyo anasema uzoefu huo utakuwa mpya kwake kwa sababu kwa mara ya kwanza atakuwa akifuatilia Kombe la Dunia akiwa nje ya uwanja huku akitoa maoni na uchambuzi kuhusu timu na wachezaji mbalimbali.

“Nina furaha sana. Itakuwa tofauti kabisa kwa sababu sitakuwa tena uwanjani. Nitakuwa na kipaza sauti nikizungumzia wachezaji, timu za taifa na mashindano ambayo naamini yatakuwa Kombe la Dunia bora zaidi kuwahi kufanyika,” anasema.

MEXI 02

Anasema moja ya sababu zilizomshawishi kukubali kazi hiyo ni kufanya uchambuzi kwa lugha ya Kiingereza, jambo analoliona kama hatua kubwa kwa watu wa Mexico.

“Kwangu ilikuwa nafasi ya kipekee kwa sababu nitakuwa nikizungumza Kiingereza kuhusu mchezo mkubwa zaidi duniani. Watu wengi wa Mexico wataona inawezekana kufanya mambo makubwa hata nje ya nchi yao,” anasema.

Chicharito ni mmoja wa wachezaji watatu pekee wa Mexico waliofanikiwa kufunga mabao katika Kombe la Dunia mara tatu tofauti mwaka 2010 nchini Afrika Kusini, 2014 Brazil na 2018 Russia.

Katika Kombe la Dunia 2010, Hernandez aliweka historia baada ya kufunga dhidi ya Ufaransa, jambo lililokuwa la kipekee zaidi kwa sababu babu yake pia aliwahi kuifungia Mexico dhidi ya Ufaransa kwenye Kombe la Dunia la mwaka 1954.

MEXI 03

Nyota huyo anasema kumbukumbu zake kubwa zaidi ni ushindi walioupata dhidi ya Ujerumani katika Kombe la Dunia 2018 nchini Russia.

Kwa mujibu wa Hernandez, kikosi cha Mexico cha mwaka 2018 kilikuwa kizazi bora zaidi kuwahi kutokea kutokana na idadi kubwa ya wachezaji waliokuwa wakicheza soka la kulipwa Ulaya.

“Tulikuwa na karibu wachezaji 15 wanaocheza Ulaya na wengi wao walikuwa wakicheza mara kwa mara katika timu zao. Tulikuwa na kikosi imara sana,” anasema.

Anaongeza kuwa kuisikia nyimbo ya taifa ya Mexico ikiimbwa kwa nguvu ndani ya uwanja uliokuwa umejaa mashabiki mjini Moscow ilikuwa moja ya nyakati za kipekee kabisa katika maisha yake ya soka.

Akizungumzia safu ya ushambuliaji ya Mexico ya sasa, Hernandez anasema washambuliaji Raul Jimenez, Santiago Gimenez na Armando Gonzalez wana uwezo mkubwa wa kuibeba timu hiyo.

MEXI 04

Kwa upande wake, anamuelezea Jimenez kama mshambuliaji mwenye uzoefu mkubwa huku Gimenez akiwa mchezaji anayeweza kubadilisha mchezo wakati wowote.

Pia anasema Gonzalez ana uwezo wa kufunga mabao hata anapotokea benchi na kwamba uwezo wao wa kuendana na mifumo tofauti ya uchezaji ni faida kwa Mexico.

Hernandez pia anampongeza kocha Javier Aguirre akimtaja kuwa mmoja wa makocha bora zaidi kuwahi kutokea nchini Mexico.

Kwa mujibu wa mshambuliaji huyo, Aguirre amekuwa akiboresha uwezo wake wa ukocha kwa miaka mingi na ana uwezo mkubwa wa kupanga timu pamoja na kuwatoa ubora wachezaji wake katika nyakati muhimu.

“Makombe makubwa yanahitaji makocha wakubwa na wachezaji wakubwa kujitokeza katika wakati muhimu. Nina matumaini Mexico itafanya hivyo,” anasema.

MEXI 05

Mbali na Mexico, Hernandez anasema pia atakuwa akifuatilia kwa karibu timu ya taifa ya Ureno kwa sababu anaamini Kombe la Dunia 2026 linaweza kuwa la mwisho kwa staa Cristiano Ronaldo.

Anasema anatarajia kumuona Ronaldo akijaribu kuhitimisha safari yake ya Kombe la Dunia kwa mafanikio.

Pia anasema mabingwa watetezi Argentina wakiongozwa na Lionel Messi pamoja na Ufaransa yenye nyota Kylian Mbappé zitakuwa miongoni mwa timu zitakazovuta hisia kubwa za mashabiki duniani.

Kwa upande mwingine, Hernandez amesema ana fahari kubwa kuona Mexico ikiandaa Kombe la Dunia kwa mara ya tatu katika historia yake baada ya kufanya hivyo mwaka 1970 na 1986.

MEXI 06

Anasema safari hii ni ya kipekee zaidi kwake kwa sababu familia yake ina historia kubwa ndani ya mashindano hayo ambapo baba yake na babu yake waliwahi kuwa sehemu ya soka la Mexico katika vipindi tofauti vya Kombe la Dunia.

“Ni jambo maalumu sana. Nilisikia hadithi nyingi kutoka kwa baba na babu yangu kuhusu Kombe la Dunia zilizofanyika Mexico. Sasa nami nitakuwa sehemu ya historia hiyo kwa namna tofauti,” anasema Hernandez.


HISTORIA YA MEXICO

Soka nchini Mexico lilianza kuchezwa mwanzoni mwa karne ya 20 kupitia makundi ya wahamiaji wa Ulaya, hasa wachimba migodi kutoka Cornwall nchini Uingereza pamoja na Wahispania waliokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Hispania.

Mechi ya kwanza ya timu ya taifa ya Mexico ilichezwa Desemba 9, 1923 katika uwanja wa Parque Espana jijini Mexico City. Mexico iliifunga Guatemala mabao 2–1 na hiyo ilikuwa mwanzo wa mfululizo wa mechi za kirafiki dhidi ya Guatemala. Mechi ya pili iliyochezwa Desemba 12 Mexico ilishinda 2–0 na ya mwisho Desemba 16 ikamalizika kwa sare ya 3–3. Baada ya miaka minne, Mexico ilirejea tena kucheza mechi za kimataifa za kirafiki, ikicheza dhidi ya Hispania na kutoka sare ya mabao 3–3 mwaka 1927. Pia walicheza dhidi ya Montevideo na kupoteza kwa mabao 1–3. Mwaka 1927, shirikisho la kwanza rasmi la soka nchini Mexico lilianzishwa na 1928 Mexico ilishiriki mashindano ya Olimpiki kwa mara ya kwanza ambapo ilipoteza kwa mabao 7-1 dhidi ya Hispania katika hatua ya 16 bora.

Mexico ilishiriki Kombe la Dunia la kwanza mwaka 1930 nchini Uruguay ikiwa kwenye kundi na Argentina, Chile na Ufaransa.

Mechi ya kwanza ya Kombe la Dunia kwa Mexico ilikuwa dhidi ya Ufaransa ambapo ilipoteza kwa mabao 4–1 lakini bao la kwanza la Mexico katika historia ya Kombe la Dunia lilifungwa na Juan Carreno.

MEXI 07

Mechi ya pili walipoteza 3–0 dhidi ya Chile na ya tatu walipoteza 6–3 dhidi ya Argentina ambapo Mexico ilipata penalti ya kwanza ya mashindano ikifungwa na Manuel Rosas.

Huo ulikuwa mwanzo wa safari ndefu ya kushiriki mara kwa mara fainali hizo za Kombe la Dunia miaka mingine waliyoshiriki ni 1950, 1954, 1958, 1962, 1966, 1970, 1978, 1986, 1994, 1998, 2002, 2006, 2010, 2014, 2018 na 2022.



DONDOO 

Imecheza Kombe la Dunia mara 18

Mexico ni moja ya mataifa yaliyoshiriki Kombe la Dunia mara nyingi zaidi duniani.


Hii ni mara ya tatu

Mexico iliandaa Kombe la Dunia mwaka 1970 na 1986 na 2026 itakuwa mara ya tatu.


Robo fainali mara mbili

Mexico ilifika robo fainali za Kombe la Dunia mwaka 1970 na 1986.


Bingwa wa CONCACAF

Mexico ni moja ya timu zilizotwaa mataji mengi zaidi ya CONCACAF Gold Cup baada ya kutwaa ubingwa mara 12 katika miaka ya 1965, 1971, 1977, 1993, 1996, 1998, 2003, 2009, 2011, 2015, 2019 na 2023.


Estadio Azteca yaweka historia

Estadio Azteca ni uwanja wa kwanza duniani kuandaa fainali mbili za Kombe la Dunia (1970 na 1986).