Charlie Chaplin: Anaendelea kuishi kwa uchale wake

Muktasari:
- Mchekeshaji huyu wa Uingereza aliyependwa kila pembe ya dunia aliwahi kufukuzwa Marekani kwa kauli zake za kupinga kuundwa taifa la Israel.
MASHAMBULIZI ya Palestina yanayofanywa na Israel yaliyoua mamia ya watu, huku zaidi ya milioni 2, wakikosa makazibaada ya nyumba zao kuharibiwa, yamewakumbusha watu wa Ulaya na Marekani alichosema msanii wa karne ya 20, Charlie Chaplin.
Mchekeshaji huyu wa Uingereza aliyependwa kila pembe ya dunia aliwahi kufukuzwa Marekani kwa kauli zake za kupinga kuundwa taifa la Israel.
Baadaye Mei 1, 1944 alishitakiwa kwa kufanya uchochezi wa kuwataka Waingereza kupinga kuundwa kwa Israel.
Alipokuwa mahakamani alisema Wayahudi ambao walisakwa kama paka mwizi na maelfu kuuliwa na dikteta wa Ujermani, Adolf Hitler, watakuja kufanya mauaji ya halaiki zaidi ya waliyofanyiwa kwani ni watu majahili na waliokosa ubinaadamu.
Kwa kile kinachotokea Gaza sasa waandamanaji wanabeba picha za Chaplin na kupiga kanda za matamshi yake yasemayo: “Ulimwengu utanikumbuka, Wayahudi watapokusanya nguvu na kufanya ujahili Palestina. Tuchukue tahadhari sasa kuzuia uonevu watakaofanyiwa watu wa Gaza.”
Sauti hii inayosikika tena Ulaya katika maandamano, karibu miaka 80 tangu Chaplin kuitamka inasemekana ndiyo iliyosababisha shinikizo kwa Norway, Finland na Hispania kulitambua rasmi taifa la Israel hivi karibuni.
Wakati huo huo, patafanyika Paris, Ufaransa, mwezi wa Julai tamasha la kuenzi maisha ya Charlie Champlin kwa kukemea udikteta na maonevu katika filamu zake na michezo ya kuigiza.
Katika jamii za Waswahili na hasa Zanzibar anapotokea mtu kueleza jambo kwa mzaha utasikia anaambiwa acha kufanya uchale.
Asili ya neno chale ni jina la huyu mchekeshaji wa michezo ya sinema, Charlie Chaplin na alipopata umaarufu kwa kuchekesha Waswahili wakabuni neno chale kumueleza mchekeshaji..
Katika nchi nyingi hufanywa matamasha ya kukumbuka visa na mikasa yake, hasa inapofika tarehe yake ya kuzaliwa.
Charles Spencer ‘Charlie’ Chaplin alizaliwa Uingereza 1889 na kufariki dunia 1977.
Kwa miaka 75 alishiriki katika michezo zaidi ya 50 ya sinema tangu akiwa mdogo na kuvutia wakubwa na wadogo duniani kote.
Tangu akiwa hai na baada ya kuiaga dunia watu wamekuwa wakifurika kwenye majengo ya sinema kuona michezo yake.
Wengine wanazo nyumbani video za michezo yake na vituo vya runinga katika nchi nyingi havichukui muda mrefu bila ya kuonyesha michezo yake.
Ukipanda boti zinazosafiri kati ya Dar es Salaam na Zanzibar au mabasi ya kwenda mikoani, michezo ya Chaplin inaonyeshwa ili kuwafurahisha abiria.
Chaplin anatajwa ni mchekeshaji maarufu kuliko wenzake wote wa fani hiyo duniani.
Ninakumbuka nilipokuwa mdogo jinsi watu walivyofurika sinema mchezo wa Charlie Chaplin ulipoonyeshwa.
Waswahili walivutiwa na sura yake iliyochekesha na hasa alipokuwa katika kivazi alichokipenda cha panjama (nguo za kulalia).
Miongoni mwa michezo iliyonivutia katika miaka ya 1950 ni wa kuigiza ujahili wa dikteta wa Kijerumani Adolf Hitler uliotwa The Great Dictator (Dikteta aliyebobea).
Mchezo huu uliopata tunzo nyingi ulifundisha hatari za udikteta, iwe katika familia , jamii au nchi na kuonya Wayahudi ni watu hatari.
Mchezo wake mwegine uliovutia ni Crying in the rain (Kilio wakati mvua). Katika mchezo huo Chaplin alisema ukilia wakati maji ya mvua yanakuangukia watu hawaoni machozi yako na hivyo aibu yako inafichika.
Ijapokuwa Chaplin aliweka mzaha mbele kuliko mambo mengine alitoa ushauri wa maana na mfunzo kwa jamii na serikali ziliojikita katika udikteta, rushwa na ufisadi.
Miongoni mwa matamshi yake muhimu ni pale aliposema “You’ll never find a rainbow if you’re looking down” (Hutauona upinde wa mvua kama utaangalia chini”.
Nukuu yake moja maarufu inasema “Nothing is permanent in this wicked world, not even our troubles” (Hapana jambo la kudumu katika dunia hii iliojaa maovu, hata kwa matatizo tuliokuwa nayo.”
Alizaliwa Aprili 16, 1889 na kuwa na maisha magumu alipokuwa mdogo na hali kuwa mbaya mama yake aliyekuwa mjane alipopata matatizo ya akili.
Akiwa na miaka 9 alipelekwa nyumba ya mayatima na huko alianza kufanya kazi kama mtoto mchekeshaji kwenye kumbi za burdani na haikuchukua muda alipata umaarufu.
Baadaye baadhi ya michezo yake ilimpatia umarufu duniani na watu waliopenda kuchekesha wenzao waliitwa Charlie Chaplin.
Chaplin alitengeneza, kuongoza, kuhariri na kutia muziki michezo yake.
Baadhi ya kauli zake za kukosoa nchi za Magharibi zilimpelekea aambiwe ni mkomunisti na Shirikika la Ujasusi la Marekani (FBI) lilimfukuze Marekani katika mwaka 1952.
Alipoelezwa kuwa mtu hatari alisema kama kutetea watu masikini, kukemea maovu na kulaani wasiojali maisha ya wanyonge ni kitu kibaya basi alifurahi na kuona fahari kuambiwa hivyo.
Alirudi Marekani 1972 pale chuo cha michezo ya sinema, Academy of Motion Pictures, kilipompa tuzo maalumu kwa mchango wake katika fani ya usanii.
Baadhi ya michezo yake, kuanzia alipokuwa mdogo hadi mzee, imeigizwa na wachezaji sinema wengi duniani.
Chaplin alifunga ndoa na Oona, mtoto wa mwandishi wa michezo ya sinema Eugene O’Neill. Wakati walipofunga ndoa Oona alikuwa na miaka 18 na yeye 54.
Alipoulizwa kwa nini alifunga ndoa na msichana alisema: “Raha ya maisha ni kuwa na dogo dogo pembeni.
“Unapokuwa na msichana mdogo karibu yako damu yako huchangamka na kuwa kijana,” alisema.
Chaplin na mkewe waliondoka Marekani na kuishi pamoja hadi 1977 alipofariki dunia akiwa Uswisi na maombolezo yake kufanyika katika nchi nyingi.
Dunia imeshuhudia wacheza sinema wengi wanaochekesha, lakini wengi wanaamini hadi sasa hakuna aliyempiku Charlie Chaplin.
Hii ndio sababu hadi leo siku yake ya kuzaliwa inaadhimishwa katika nchi nyingi na sasa kauli yake ni sehemu ya kampeni ya kupiga uvamizi wa Gaza unaofanywa na Israel.
Watu wengi wanaamini hatatokea mtu wa aina ya Charlie Chaplin.