Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Cape Verde 'muujiza wa soka' Kombe la Dunia 2026

CAPE VERDE Pict

Muktasari:

  • Cape Verde kwa jina la utani 'Blue Sharks' kwa kimombo wakiwa na maana ya Papa wa Bluu au Papa wa Samawati sio nchi yenye watu wengi, sio taifa lenye uchumi mkubwa, wala haipo katika orodha ya mataifa yenye ligi 10 bora Afrika ambazo Tanzania imekuwa ikijivunia.

PRAIA, CAPE VERDE: Julai 5,1975, bendera ya Cape Verde ilipepea kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Várzea katika mji mkuu wa Praia, ikiwa ni siku ambayo taifa hilo lilipata uhuru wake kutoka kwa Ureno. Wakati huo hawakuwa na timu ya taifa, wala kuonyesha kama kuna kitu kinakuja.

Siku 100, baada ya kusherehekea miaka 50 ya uhuru wao, bendera ya nchi hiyo ilipepea tena kwenye uwanja uleule wananchi wa nchi hiyo walijitokeza uwanjani kusherehekea Cape Verde ikiweka historia ya kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza Kombe la Dunia baada ya kuichapa Eswatini kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa. Kisiwa hicho kilichopo katika pwani ya Senegal, kina wakazi 529,630, inakuwa nchi ya pili ndogo kufuzu kwa Kombe la Dunia baada ya Iceland kufanya hivyo mwaka 2018.

Cape Verde kwa jina la utani 'Blue Sharks' kwa kimombo wakiwa na maana ya Papa wa Bluu au Papa wa Samawati sio nchi yenye watu wengi, sio taifa lenye uchumi mkubwa, wala haipo katika orodha ya mataifa yenye ligi 10 bora Afrika ambazo Tanzania imekuwa ikijivunia.

Hata hivyo, ndani ya miaka michache iliyopita taifa hilo limejijenga utaratibu na kuwa moja ya timu zinazoheshimika. Safari yao ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 imekuwa ishara kuwa katika soka, nidhamu, maono, umoja na mipango sahihi vinaweza kuifanya nchi ndogo kuishangaza dunia.

CAPE 01

TAIFA DOGO LENYE NDOTO KUBWA

Cape Verde licha ya kuwa na idadi ya ndogo ya watu, lakini taifa hilo limeweza kuzalisha vipaji vikubwa vya soka vinavyocheza katika ligi mbalimbali za Ulaya.

Kitu kinachofanya Cape Verde kuwa ya kipekee ni kwamba wachezaji wengi wa timu yao ya taifa wamezaliwa nje ya nchi hiyo. Wapo waliokulia Ufaransa, Ureno, Uholanzi na hata Marekani, lakini wameamua kuitumikia nchi yao ya asili.

Hali hiyo imeifanya Cape Verde kupata mchanganyiko wa wachezaji wenye malezi ya soka la Ulaya, lakini wenye moyo wa Kiafrika. Ndiyo maana timu yao imekuwa ngumu kuifunga na mara nyingi imekuwa ikipewa heshima kubwa hata inapokutana na mataifa makubwa.

Safari yao ya soka ilianza kwa tabu kubwa. Mechi yao ya kwanza ya kimataifa mwaka 1978 walipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Guinea. Kwa miaka mingi walikuwa wakionekana kama timu ya kawaida tu ya Afrika Magharibi, lakini hatua kwa hatua wakaanza kubadilika.

CAPE 02

CAPE VERDE ILIVYOBADILIKA

Baada ya juhudi zao za kwenda Ulaya kushindwa kufua dafu, mwanzoni mwa 2000, Cape Verde waliamua kuanza kushiriki mashindano ya Afrika ndipo ilipoanza kuonyesha mabadiliko. Taifa hilo lilianza kuwasaka wachezaji wenye asili ya Cape Verde waliokuwa wakicheza Ulaya. Wengine walikuwa wamefundishwa katika akademi kubwa za Ureno na Ufaransa, hivyo walikuja na uzoefu mkubwa.

Mabadiliko hayo yaliifanya Cape Verde kuanza kushindana vizuri katika michuano ya kufuzu AFCON na Kombe la Dunia. Walianza kupata ushindi dhidi ya timu zilizokuwa zinaheshimika Afrika, jambo lililowapa kujiamini.

Mwaka 2010, walicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Ureno iliyokuwa na mastaa kama Cristiano Ronaldo, lakini Cape Verde walishangaza wengi kwa kutoka suluhu (0-0). Hiyo ilikuwa ishara kuwa taifa hilo lilikuwa linaanza kukua.

Miaka michache baadaye walifuzu kwa mara ya kwanza kucheza AFCON 2013 baada ya kuiondoa Cameroon. Ushindi huo uliishtua Afrika nzima. Cape Verde waliingia mashindanoni kama wageni lakini wakafika robo fainali, wakionyesha uwezo mkubwa dhidi ya timu zilizokuwa na historia kubwa zaidi.

Kuanzia hapo, 'Blue Sharks' wakaanza kuonekana kama moja ya timu hatari zaidi barani Afrika.

CAPE 03

SAFARI YAO 2026

Kufuzu kwa Cape Verde kwenye Kombe la Dunia 2026 ni moja ya hadithi kubwa kabisa katika soka la Afrika. Katika kinyang'anyiro cha kufuzu walionyesha uimara mkubwa kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Walipata ushindi muhimu dhidi ya Mauritius, Angola, Cameroon na Eswatini.

Sare yao ya mabao 3-3 wakiwa ugenini dhidi ya Libya pia ilionyesha jinsi timu hiyo ilivyokuwa na moyo wa kupambana.

Kilichowafanya kuwa tofauti ni nidhamu yao ya kiuchezaji. Cape Verde hawana mastaa wengi wanaocheza klabu kubwa duniani, lakini wana timu iliyoungana na yenye kujituma.

Kocha Pedro Leitão Brito 'Bubista' amekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio hayo. Amejenga timu yenye mfumo wa kisasa wa kucheza, inayojilinda vizuri, pia inayotumia nafasi chache kupata mabao.

Mashabiki wa Cape Verde walisherehekea kufuzu kwao kama ushindi wa taifa zima. Vyombo vya habari duniani vilielezea mafanikio hayo kama “muujiza wa soka”. Hili lilikuwa jambo kubwa zaidi nchini humo tangu kupata uhuru.


RYAN MENDES

Kama kuna jina moja ambalo haliwezi kuondolewa katika historia ya soka la Cape Verde basi ni Ryan Mendes. Nahodha huyo ndiye mchezaji mwenye mechi nyingi zaidi na mfungaji bora wa muda wote wa taifa hilo.

Kufikia Machi 2026 alikuwa amecheza mechi 96 za kimataifa na kufunga mabao 22 kwa Cape Verde, takwimu zinazomfanya kuwa mmoja wa mastaa wakubwa kuwahi kulitumikia taifa hilo.

Mendes alianza kuchezea Cape Verde 2010 na tangu hapo amekuwa nembo ya kizazi kilichobadilisha historia ya timu hiyo. Katika AFCON 2023 alikuwa mmoja wa viongozi wakubwa wa kikosi hicho kilichofika robo fainali huku akifunga bao muhimu dhidi ya Msumbiji na pia penalti ya ushindi dhidi ya Mauritania hatua ya 16 bora.

Mbali na rekodi zake za kimataifa, Mendes ambaye kwa sasa anaichezea Igdir FK ya Uturuki pia ana uzoefu mkubwa wa kucheza soka la kulipwa  Ufaransa na Falme za Kiarabu.

Garry Rodrigues ambaye anaichezea  Apol. Limassol ya Cyprus naye ni moja ya silaha kubwa za Cape Verde, amecheza mechi 60 za kimataifa na kufunga mabao tisa. Ndiye aliyefunga bao la ushindi dhidi ya Ghana katika AFCON 2023, ushindi uliowapa Cape Verde mwanzo mzuri wa mashindano hayo.

Mshambuliaji Dailon Livramento anayeichezea Casa Pia ya Ureno ni mmoja wa vijana wanaokuja kwa kasi ndani ya timu hiyo, amefunga mabao saba katika mechi 20 pekee za kimataifa.

CAPE 04

HESHIMA YAO

Kabla ya kufuzu Kombe la Dunia, Cape Verde tayari walikuwa wameonyesha ubora kwenye AFCON 2023 iliyofanyika Ivory Coast.

Walianza kwa kuifunga Ghana kwa mabao 2-1, wakaitandika Msumbiji mabao 3-0 na kisha kutoka sare 2-2 dhidi ya Misri. Walimaliza hatua ya makundi bila kupoteza mechi hata moja.

Katika hatua ya 16 bora waliiondoa Mauritania kwa bao 1-0 kabla ya kutolewa kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Afrika Kusini katika robo fainali.

Mashindano hayo yaliifanya dunia kutambua kuwa Cape Verde sio timu ya kuibeza.

CAPE 05

KOMBE LA DUNIA 2026

Katika Kombe la Dunia 2026, Cape Verde imepangwa Kundi H pamoja na Hispania, Uruguay na Saudi Arabia.

Hilo ni kundi gumu kwao kwa sababu wapo pamoja na mabingwa wa zamani wa Kombe la Dunia, Hispania na Uruguay pamoja na Saudi Arabia ambayo katika fainali zilizopita za Kombe la Dunia iliushangaza ulimwengu kwa kuifunga Argentina.

Hata hivyo, Cape Verde hawatakuwa na hofu kubwa. Wameonyesha mara nyingi kuwa wana uwezo wa kushindana na timu kubwa. Katika AFCON waliwahi kuisumbua Ghana, Misri na Cameroon, hivyo wanaamini wanaweza kufanya jambo la kushangaza tena.

Mechi yao dhidi ya Hispania, Juni 15, 2026 itakuwa ya kihistoria. Hiyo itakuwa mara ya kwanza taifa hilo dogo kucheza dhidi ya bingwa wa zamani wa Kombe la Dunia.

CAPE 06

CHANGAMOTO KUBWA

Pamoja na ubora wao, Cape Verde wanakabiliwa na changamoto kadhaa.

Kwanza, hawana kikosi kipana kama mataifa makubwa. Kuumia kwa baadhi ya nyota wao kunaweza kuathiri timu kwa kiasi kikubwa.

Pili, kukosa uzoefu wa kucheza Kombe la Dunia pamoja na presha kubwa kutokana na matarajio ya mashabiki wao.


KIBARUA KILICHOPO

Cape Verde tayari wameandika historia kwa kufuzu Kombe la Dunia. Lakini wana nafasi ya kufanya zaidi.

Iwapo watavuka hatua ya makundi, itakuwa moja ya hadithi kubwa kabisa kuwahi kutokea katika soka la Afrika.

Taifa hilo dogo linaweza kuwa mfano kwa nchi nyingine ndogo kuwa mafanikio yanawezekana bila kuwa na uchumi mkubwa.