CAF na mlipuko wa mashindano
Muktasari:
- Mpango huo mpya na wa kushangaza unaonekana kufuata utaratibu wa mashindano mengine makubwa ya aina ya Afcon kama Euro, Copa Amerika na Kombe la Dunia.
SHIRIKISHO la soka Afrika (CAF) limetangaza kwamba mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 ndio ya mwisho kuandaliwa baada ya miaka miwili. Kuanzia mashindano yatakayofuata kila shindano litaandaliwa baada ya miaka minne.
Mpango huo mpya na wa kushangaza unaonekana kufuata utaratibu wa mashindano mengine makubwa ya aina ya Afcon kama Euro, Copa Amerika na Kombe la Dunia.
Zaidi ya mabadiliko hayo, CAF pia imetangaza ujio wa mashindano mapya yatakayoitwa Ligi ya Mataifa ya Afrika ambayo yatachezwa katikati ya Afcon moja na nyingine.
Mashindano hayo yatachukua nafasi ya mechi za kimataifa za kirafiki za tarehe ya Fifa. Ligi hiyo itachezwa kwa madaraja kama zilivyo ligi za mataifa mbalimbali.
Hivyo kutakuwa na mataifa ambayo ni ligi daraja la kwanza, daraja la pili, daraja la tatu na la nne. Hii inafuata utaratibu wa Ulaya, Uefa Nations League (Ligi ya Mataifa ya Ulaya).
MLIPUKO WA MASHINDANO
Kwa mabadiliko hayo Afrika sasa itakuwa na mashindano matatu kwa timu za taifa. Afcon (ubingwa wa mataifa ya Afrika), Ligi ya Mataifa ya Afrika (itachukua nafasi ya mechi za kirafiki), CHAN (kwa ajili ya wachezaji wa ligi za ndani). Hili ni jambo jema kwa sababu mashindano ndio uhai wa mchezo. Uhai wa mpira.
Mpira umefika ulipo kwa sababu ya mashindano. Kwa sababu ulichezwa. Kuongeza idadi ya mashindano ni kuongeza uhai wa mpira.
AFCON BAADA YA MIAKA MINNE
Kuweka Afcon kila baada ya miaka minne ni kitu kizuri kibiashara kwa sababu inaongeza hamu ya kusubiri mashindano.
Afconya kila baada ya miaka miwili inafanya mashindano kuwa kitu kinachopatikana kirahisi, hivyo kupunguza thamani yake.
Kanuni moja na muhimu ya biashara ni uadimu wa bidhaa. Bidhaa ikiwa adimu huongeza thamani yake kwa sababu hutafutwa sana. Lakini, Afcon kila baada ya miaka miwili iliyachonganisha mashindano na klabu za Ulaya.
Hii ni kwa sababu mashindano hayo hufanyika katika kipindi misimu ya ligi huendelea duniani. Wachezaji wengi wa Afrika wanaoshiriki Afcon wanachezea klabu za Ulaya. Klabu hizo huathirika kuwakosa kiasi kwamba baadhi huwaogopa wachezaji wa Afrika kwa sababu zitawakosa kila baada ya miaka miwili. Sasa angalau itapunguza hiyo presha.
LIGI YA MATAIFA YA AFRIKA
Kama ambavyo Ulaya wamefanya mashindano hayo yatachukua nafasi ya zile mechi za kirafiki za kimataifa za kalenda ya Shirikisho la Soka Dunaini (Fifa). Sasa badala ya kucheza mechi za kirafiki, mnacheza mechi za mashindano ili kuongeza thamani ya uhusika. Mechi ikiwa ya kirafiki ni kama hakuna mnachotafuta.
Mechi ikiwa ya kirafiki haitengenezi pesa au inategeneza pesa kidogo kwa sababu thamani yake ni ndogo. Kuifanya mechi ya kirafiki kuwa ya mashindano kunaiongezea thamani na hivyo kuleta pesa zaidi. Hata wachezaji watajitoa zaidi kwa hizo mechi kwa sababu zinaongeza thamani kwenye kazi yao.
CHAN
Litabaki kuwa jukwaa kuu la wachezaji wa ndani kujitangaza Afrika na kuzitangaza ligi za Afrika. Katika nyakati hizi ambazo mataifa mengi ya Afrika yanahangaika kutumia wachezaji wanaocheza nje ya nchi zao, CHAN ni mkombozi wa wachezaji wa ligi za ndani kupata uzoefu wa kimataifa kupitia timu za taifa.
MASHINDANO MFULULIZO
Utaratibu mpya wa Afcon kufanyika kila baada ya miaka minne utaanza 2028. Hii itakuwa na maana kwamba ndani ya miaka minne mfululizo Afcon itakuwa imechezwa mara tano yaani kuanzia 2024 hadi 2028 ni Afcon, Afcon, Afcon.
2024
Mashindano yalifanyika Ivory Coast. Awali yalitakiwa yafanyike 2023, lakini haikuwezekana kutokana na athari za Uviko 19, 2025 Afcon inayoendelea sasa huko Morocco ilianza Desemba 21, 2025, 2026 mashindano ya Afcon 2025 ambayo yalianza Desemba 21 yataendelea hadi 2026 na fainali itafanyika Januari 18, 2027 nchi za Tanzania, Kenya na Uganda kwa pamoja zitakuwa wenyeji wa Afcon 2027 huku kwa mara ya kwanza ikishuhudiwa nchi tatu zikiandaa kwa pamoja.
2028
Ule utaratibu mpya wa kuandaa Afcon kila baada ya miaka minne ndio utaanza. CAF hawajatangaza mashindano yatafanyika nchi gani, lakini yatafanyika mwaka huo.
Sasa pata picha ndani ya miaka mitano hii kuna Afcon nne zimechezwa na pia ndani yake kuna CHAN moja na kutakuwa na Ligi ya Mataifa ya Afrika.
Ama kwa hakika ndani ya miaka hii minne Afrika mpira utachezwa kwa kiwango kikubwa.
Kama kuna kipindi ambacho Afrika imeshuhudia mashindano mengi na mfululizo, basi ni kuanzia 2024 hadi 2028.
Hii inakaribia kidogo kilichotokea Amerika Kusini katikati ya miaka ya 2010 kwenye mashindano ya Copa America.
Mwaka 2015 yalifanyika kama utaratibu wake ulivyokuwa, halafu 2016 yakafanyika kusherehekea miaka 100 tangu yaanzishwe.
Jambo jema ni kwamba katika miaka hii minne ya mlipuko wa mashindano Afrika, Tanzania ni nchi pekee ya Afrika Mashariki imehusika kwa asilimia kubwa.
Ilifuzu Afcon 2023 iliyofanyika 2024 Ivory Coast, ikafuzu 2025 na 2026 ya Morocco na itashiriki kama mwandaaji wa Afcon 2027 huku ikitarajia kufuzu 2028.
Pia ilishiriki CHAN 2025 ikiwa mwandaaji na itashiriki Ligi ya Mataifa ya Afrika itakapoanza. Haya pia ni mafanikio kwa soka la Tanzania ambalo linazidi kujipambanua na kupaa Afrika.
KITENDAWILI NI AFL
Mwaka 2023 CAF ilianzisha mashindano mapya kwa ngazi ya klabu yaliyoitwa African Football League. Mashindano hayo yaliyoanza kwa kushirikisha timu nne yalizinduliwa Tanzania kwa mechi ya kibabe kati ya Simba na Al Ahly.
Mamelodi Sundowns kutoka Afrika Kusini wakaenda kuwa mabingwa.
Baada ya hapo ikawa kimya na hadi sasa hakuna taarifa yoyote. Hii inaonyesha upande mwingine wa udhaifu wa CAF katika kusimamia mashindano.
Je haya mashindano mapya wanayotaka kuyaanzisha ya Ligi ya Mataifa ya Afrika watayaendeleza au yatapotelea juu kwa juu kama AFL?