Prime
Bara kuna Simba na Yanga, halafu Kagere na Tambwe
KATIKA soka la Tanzania kuna Ligi Kuu Bara, halafu kuna ligi ya Simba na Yanga. Ndizo timu zinazoifanya Ligi Kuu na michuano mingine ichangamke. Hata mamlaka ya soka nchini akili na nguvu zao huzielekeza zaidi kwa timu hizo kutokana na kusaidia kuwaingizia fedha nyingi.
Halisemwi wazi, lakini ndivyo ukweli ulivyo bila ya Simba na Yanga ni kama soka la Tanzania halipo.
Katika Ligi Kuu Bara na hata michuano mingine ya ndani ikiwamo Ngao ya Jamii, ASFC, Kombe la Mapinduzi na mingine ndizo timu zinazoleta msisimko kutokana na kuchuana kubeba mataji.
Katika fainali za msimu huu za Kombe la Mapinduzi, waandaaji walikakariwa wakikerwa na namna timu hizo zilivyopeleka vikosi dhaifu na kutolewa mapema michuanoni. Wenyewe walitamani kuona fainali ikipigwa kati ya Simba na Yanga ili wavune fedha badala ya kuzishuhudia Mlandege na Singida BS.
Simba na Yanga ndio baba lao la soka katika ukanda wa Afrika Mashariki, CECAFA inaumia sana kuona timu hizo zisiposhiriki michuano ya Kombe la Kagame. Nani hakumbuki tukio la mwaka 2008, Yanga iliposusia mechi ya mshindi wa tatu dhidi ya Simba na namna Katibu Mkuu wa Cecafa wakati huo Nicholas Musonye alivyowaka. Akajitutumia kuifungia Yanga, lakini ilikuwa ni kama hukumu hewa tu, kwani adhabu hiyo ilifutwa kiaina. Huu ndio ukubwa wa Simba na Yanga.
Simba ndio mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo ikibeba mataji sita ikilingana na AFC Leopards ya Kenya, kisha zinafuatiwa na Yanga na Tusker Kenya na Gor Mahia za Kenya kila mmoja ikibeba mara tano tano.
Sasa achana na vita hiyo ya Simba na Yanga, unaambiwa katika Ligi Kuu Bara kuna kaligi kengine kadogo baina ya Meddie Kagere na Amissi Tambwe. Wachezaji hao wakongwe kutoka nchi jirani za Rwanda na Burundi wamewahi kupita Simba na Yanga. Msimu uliopita waliicheza pamoja katika timu ya Singida Big Stars (sasa Singida Fountain Gate).
Hao ndio wachezaji wa kigeni waliocheza kwa muda mrefu Ligi Kuu Bara na kufunga mabao mengi katika ligi hiyo kwa miaka ya karibuni wakiwaacha mbali watangulizi wao Emmanuel Okwi, Hamis Kiiza 'Diego' na Kipre Tchetche aliyewahi kujiwekea ufalme pale Chamazi, alipokuwa na Azam FC.
Hapo chini ni rekodi na namba ambazo nyota hao wawili walipoziweka katika misimu ya Ligi Kuu Bara tangu walipotua nchini. Endelea nayo....
BALAA LA TAMBWE
Nyota huyo kutoka Burundi alisajiliwa na Simba mwaka 2013 akitokea Vital'O ya nchini kwao akitoka kubeba ubingwa wa michuano ya Kombe la Kagame lililofanyikia Sudan akiwa kinara wa mabao akifunga sita. Katika michuano hii, Simba na Yanga hazikwenda kushiriki kutokana na hofu ya kiusalama na Vital'O ikafanya kweli kwa kubeba ubingwa na Tambwe kubeba tuzo ya Mfungaji Bora.
Simba alianza kuitumikia Simba msimu wa 2013-2014 na kufanikiwa kumaliza kama Mfungaji Bora akifunga jumla ya mabao 19, ingawa ubingwa ulienda kwa Azam FC. Lakini msimu huo alitwaa na Simba taji la Nani Mtaji Jembe kwa kuifunga Yanga mabao 3-1, huku yeye akitupia mawili kambani.
Msimu uliofuata aliifunga Simba bao moja tu kisha kutemwa kitatanishi kwenye dirisha dogo na kuibukia Yanga iliyomsajili fasta na kumaliza nao msimu huo wa 2014-2015 akiwa na mabao 14 nyuma ya Simon Msuva aliyefunga 17 na vijana wa Jangwani kubeba ubingwa wa Ligi Kuu. Msimu huo licha ya kutopewa nafasi na Kocha Patrick Phiri, lakini Tambwe alibeba taji la Nani Mtani Jembe 2014 kwa ushindi 2-0 kabla ya kutemwa dirisha dogo na kukimbilia Yanga.
Msimu wa tatu, mwamba alifanya kweli kwa kuiwezesha Yanga kutetea ubingwa wa Ligi Kuu kwa msimu wa pili mfululizo na kuwapa Ngao ya jamii, huku mwenyewe akimaliza Mfungaji Bora akifunga mabao 21.
Msimu wa nne Tambwe alipunguzwa makali kwa majeraha aliyokuwa nayo, kwani alifunga mabao 11 tu, lakini timu ya Yanga ilitetea taji kwa msimu wa tatu mfululizo na msimu uliofuata iliokuwa wa tano kwake ulikuwa mbaya zaiidi kwani majeraha yalimweka nje na kumaliza msimu bila bao lolote.
Haukuwa msimu mzuri kwa Tambwe tu, bali hata Yanga ilishindwa kutetea taji na kushuhudia Simba iliyokuwa haijabeba ubingwa wa ligi hiyo kwa misimu mitano mfululizo ikizinduka na kutwaa taji hilo na kuja kulitetea msimu wa mwisho wa Tambwe akiwa Jangwani, ambapo straika huyo alifunga mabao manane kabla ya kutimka zake Oman kujiunga na FC Fanja kisha kuibukia Police Djibouti.
Ndipo misimu miwili iliyopita alirejea nchini na kujiunga na Singida (enzi ikiwa Championship ikitumia jina la DTB) akamaliza kama kinara wa mabao na kuipandisha Ligi Kuu Bara na kuifungia mabao mawili tu.
Rekodi zinaonyesha ameicheza Ligi Kuu Bara kwa misimu saba tofauti na kufunga jumla ya mabao 75 akitwaa mataji matatu ya Ligi Kuu Bara, moja ya ASFC na Ngao ya Jamii moja. Akibeba tuzo mbili za Mfungaji Bora wa Ligi Kuu 2013-2014 na 2015-2016. Pia alitwaa mataji mawili ya Nani Mtaji Jembe akiwa na Simba 2013 na 2014. Mechi ya kwanza ambayo Simba ilishinda 3-1, Tambwe alifunga mawili.
Mabao 75 aliyofunga Tambwe kwenye Ligi Kuu inamfanya awe mchezaji wa kigeni anayeongoza kwa idadi kubwa ya mabao, lakini akiwa pia ameweka rekodi ya kufunga hat trick sita katika misimu hiyo.
KAGERE NOMA ZAIDI
Mashabiki wa Simba walimpa jina la MK14 a.k.a Terminator kutokana na umahiri wake wa kucheka na nyavu, kwani msimu wake wa kwanza tu tangu atue Mshimbazi kutoka Gor Mahia ya Kenya, kidume kiliweka rekodi ya kufunga jumla ya mabao 23 na kutwaa Tuzo ya Mfungaji Bora.
Mabao aliyofunga yalivunja rekodi ya Tambwe kwa wachezaji wa kigeni kufunga mabao mengi katika Ligi Kuu Bara, kwani yalikuwa ni mawili zaidi na yale ya Mrundi aliyefunga 21 msimu wa 2015-2016, huku akifunga bao lililoisaidia kuipa Simba Ngao ya Jamii mbele ya Mtibwa Sugar, mechi iliyoipigwa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Balaa la Kagere alikuwa kwenye Ligi Kuu Bara tu, lakini hata kwenye Ligi ya mabingwa Afrika jamaa alitisha kwa kuibeba Simba iliyoandikisha rekodi ya kufika robo fainali kwa mara ya kwanza.
Msimu wa pili akiwa anavaa jezi ya Simba, Kagere alitwaa tena Ngao ya Jamii na timu hiyo ilipoilaza Azam mabao 4-2, kisha akamaliza kwa kubeba Ligi Kuu Bara ikiwa ni msimu wa tatu mfululizo kwa Simba, huku yeye akitetea tuzo ya Mfungaji Bora akitupia kambani mabao 22.
Msimu huo pia Simba ilitwaa Kombe la Shirikisho (ASFC) iliyolitetea tena msimu wa 2020-2021 baada ya awali kutetea Ngao ya Jamii kwa msimu wa nne mfululizo, huku akimaliza msimu huo na mabao 13 tu baada ya kupunguzwa kasi kwakutopewa nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Msimu wa mwisho kuvaa jezi za Simba ulikuwa 2021-2022 na kidume hicho kilimaliza na mabao saba, huku Yanga ikibeba kila kitu katika Ligi Kuu, Ngao ya Jamii na ASFC kabla ya msimu uliopita kuibukia Singida Big Stars alimaliza kama mfungaji wa pili kinara wa timu kwa mabao manane nyuma ya Mbrazili, Bruno Gomes aliyemaliza na mabao 10.
Rekodi zinaonyesha katika misimu mitano mfululizo kwa Kagere kucheza Ligi Kuu Bara amefunga jumla ya mabao 73, mawili pungufu na aliyonayo Tambwe aliyetumia misimu saba.
Kagere pia ametwaa mataji matatu ya Ligi Kuu Bara kama Tambwe, lakini akimzidi mwenzake kwenye Ngao ya Jamii aliyobeba matatu, huku mawili yakiwa ya ASFC na pia ana taji moja la michuano ya Kombe la Mapinduzi 2022 ambayo alimaliza kama Mfungaji Bora wa michuano hiyo.
REKODI ZILIVYO
Amissi Tambwe
2013-2014 (Simba)
Mabao 19
2014-2015 (Simba/Yanga)
Mabao 14
2015-2016 (Yanga)
Mabao 21
2016-2017 (Yanga)
Mabao 11
2017-2018 (Yanga)
Mabao 0
2018-2019 (Yanga)
Mabao 8
2022-2023 (Singida)
Mabao 2
Jumla mabao ya Ligi, 75
Mataji:
Ligi Kuu 3
Ngao 1
ASFC 1
Mtani Jembe 2
Tuzo:
Mfungaji Bora
2013-2014
2015-2016
Meddie Kagere
2018-2019 (Simba)
Mabao 23
2019-2020
Mabao 22
2020-2021
Mabao 13
2021-2022
Mabao 7
2022-2023 (Singida BS)
Mabao 8