Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Badru: Taifa Stars isiishie kumiliki mpira

BADRU Pict

Muktasari:

  • Badru ambaye amekuwa akijihusisha kwa muda mrefu na maendeleo ya vijana, amesema tofauti kubwa kati ya Taifa Stars na baadhi ya mataifa yanayofanya vizuri kimataifa ni idadi ya wachezaji wao wanaocheza nje ya nchi huku akisisitiza kuwa soka la sasa linahitaji zaidi ya kumiliki mpira.

KOCHA wa timu za vijana za Yanga, Mohamed Badru, amesema Tanzania bado ina safari ndefu kufikia kiwango cha soka la kimataifa, lakini anaamini uwekezaji unaofanyika kwenye timu za vijana unaweza kuwa msingi wa kuijenga upya Taifa Stars na kuzalisha wachezaji wengi watakaocheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Badru ambaye amekuwa akijihusisha kwa muda mrefu na maendeleo ya vijana, amesema tofauti kubwa kati ya Taifa Stars na baadhi ya mataifa yanayofanya vizuri kimataifa ni idadi ya wachezaji wao wanaocheza nje ya nchi huku akisisitiza kuwa soka la sasa linahitaji zaidi ya kumiliki mpira.

Akizungumzia michezo ya kuwania nafasi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2027’, Badru amesema timu imeonyesha baadhi ya maboresho katika namna ya kucheza, lakini bado kuna mapungufu makubwa kwenye matumizi ya nafasi na kasi ya mchezo.

“Tunatakiwa tuangalie tumetoka wapi na tunaelekea wapi. Tulipotoka na tulipo sasa ni tofauti kabisa. Angalau sasa unaweza kuona Taifa Stars inacheza mpira wa kisasa, inaweza kutengeneza nafasi, lakini bado kuna mambo mengi ya kuangalia ili kufikia levo”€  anasema Badru.

Anasema soka la kimataifa limebadilika na kwamba kumiliki mpira pekee hakutoshi kama timu haiwezi kutumia umiliki huo kupata matokeo.

“Mpira kwa sasa siyo kuhusu kumiliki ni kuhusu kushinda, mpira ni mchezo wa kushinda, siyo mchezo wa kucheza tu. Unaweza ukawa na mpira muda wote, lakini mpinzani akatumia nafasi ulizomuachia na akakufunga” anasema Badru.

Badru anasema tatizo aliloliona kwa Taifa Stars ni namna timu inavyoacha maeneo wazi wakati inapokuwa na mpira, jambo ambalo wapinzani wenye uzoefu wa kimataifa wanaweza kulitumia haraka.

Anasema hilo linatofautiana na timu za vijana za Tanzania ambazo kwa sasa zinaanza kuonyesha utofauti; “Ukiangalia U-17 na U-20, namna yao ya uchezaji inaanza kuendana na ligi za vijana na mpira wa kimataifa.”€ 

Badru anaamini kazi hiyo ikisimamiwa kwa mwendelezo, Tanzania inaweza kuanza kupata kizazi kipya cha wachezaji kitakachokuwa na uwezo wa kucheza nje ya nchi na baadaye kuongeza ushindani wa Taifa Stars.


BADR 04

YANGA NA MRADI WA VIJANA

Badru pia ameeleza namna anavyoiona kazi yake ndani ya Yanga, akisema moja ya malengo yake makubwa ni kuhakikisha vijana wanaopitia timu za chini wanafika kwenye kikosi cha kwanza badala ya kupotea njiani.

Kocha huyo anasema uzoefu alioupata alipokuwa Azam FC kwa miaka mitatu umemsaidia kuelewa umuhimu wa kuwa na mpango wa muda mrefu katika malezi ya vijana.

Anasema alipokuwa Azam, baadhi ya wachezaji aliowafundisha katika timu ya U-17 wameendelea hadi kucheza kikosi cha kwanza, wengine wamekwenda kwa mkopo kwenye ligi mbalimbali na baadhi wamefanikiwa kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania.

“Nilifanya kazi Azam kwa miaka mitatu. Nilianza na U-17, wengi wao kwa sasa wanacheza soka la kulipwa na jambo zuri ni kwamba wengine wanacheza nje ya nchi,” anasema.

Akizungumzia majukumu yake Yanga, Badru anasema bado yupo kwenye hatua za mwanzo, lakini tayari anaona dalili za kile alichokuwa anakilenga.

“Kwa upande wa Yanga bado niko kama miezi sita hivi, lakini tageti yangu ya mwanzo ilikuwa U-17 kuchukua ubingwa na kuweza kuleta ile haiba ya Yanga kuwa iko vizuri kwenye upande wa vijana,”  anasema na kuongeza:

“Kwa U-20, tageti yangu kubwa ni kutoa mchezaji mmoja au wawili na kuwa kwenye kikosi cha wakubwa Yanga, nashukuru Mungu hadi sasa nimefanikiwa mchezaji mmoja ambaye ni Kazimoto.”


BADR 07

KAZIMOTO ASITOKE KWA MKOPO

Katika mahojiano hayo, Badru amegusia pia maendeleo ya kijana Ibrahim Kazimoto, akieleza kuwa anaamini mazingira ya kikosi cha kwanza cha  Yanga yanaweza kumpa uzoefu muhimu zaidi kuliko kumpeleka haraka kwa mkopo.

Badru anasema Kazimoto ana uwezo wa kucheza kama beki wa kati, lakini pia amekuwa akitumika upande wa beki wa pembeni kutokana na uwezo wake wa kukimbia, nguvu na ukakamavu.

“Kazimoto ni beki wa katikati, lakini unaweza kuona sasa hivi anacheza pembeni. Ana ukakamavu, nguvu, kasi na uwezo mzuri wa kiufundi. Anahitaji kuendelea kuboresha zaidi upande wa kiufundi, lakini vitu hivi ndivyo vinavyomfanya aonekane bora,” anasema.

Badru anasema kwa mchezaji kijana, si kila wakati suluhisho ni kumpeleka kwa mkopo, hasa katika klabu yenye wachezaji wengi wenye uzoefu.

“Fikiria Yanga ina wachezaji wengi wakubwa, wenye uzoefu na wazuri. Ukimtoa Kazimoto ukampeleka kwa mkopo, kuna wakati unakuwa umempunguzia mazingira ya kujifunza. Yanga kuna wachezaji wengi wenye uzoefu, hivyo bila kumpeleka kwa mkopo anaweza kukua zaidi kwa kujifunza kutoka kwao,”€  anasema.

Anasema lengo la timu za vijana si kutengeneza wachezaji watakaocheza katika ngazi za chini pekee, bali kuwafikisha kwenye kiwango cha kuingia kikosi cha kwanza na baadaye kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania.


BADR 03

U-17 LENGO NI NJE

Badru anafafanua kuwa katika mpango wake, timu za vijana chini ya miaka 20 na chini ya miaka 17 zina malengo tofauti.

Kwa timu ya chini ya miaka 20, anasema lengo la kwanza ni kuzalisha wachezaji watakaoweza kupenya kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga huku timu ya chini ya miaka 17 ikiwa na lengo la kuandaa wachezaji wenye uwezo wa kwenda kucheza soka nje ya Tanzania.

“Kwa chini ya miaka 20, lengo ni kuwapeleka kwenye timu ya wakubwa. Lakini kwa chini ya miaka 17, mpango wangu siku zote ni kutengeneza wachezaji watakaoenda kufanya biashara nje, siyo kubaki kucheza ndani,”  anasema.

Hata hivyo, amesema kazi hiyo inahitaji muda kwa sababu baadhi ya wachezaji aliowakuta Yanga chini ya miaka 17 walikuwa tayari na uwezo wa kutwaa ubingwa, lakini bado hawakuwa wamefikia kiwango cha kuuzwa nje.

“Chini ya miaka 17 ni kazi kubwa sana. Msimu wa kwanza tumetwaa ubingwa, lakini kwa upande wangu ubora wa wachezaji niliowakuta ulikuwa wa kutwaa ubingwa. Hawakuwa wachezaji wa kuwapeleka nje kufanya biashara. Labda ndani ya miaka miwili tutaweza kuona kama mpango huu unafanya kazi na kuona matunda yake.” 


MAKOCHA WAZAWA

Badru pia anapinga mtazamo kwamba makocha wazawa hawana uwezo wa kufundisha timu kubwa, akisema changamoto kubwa ni kwamba bado hawajapata nafasi ya kutosha kuthibitisha uwezo wao katika mazingira yenye ushindani mkubwa.

“Makocha waliopo sasa hivi siyo wale waliokuwepo miaka 10 iliyopita. Mbinu, mfumo na mipango ya mchezo imebadilika. TFF wanafanya kazi kubwa katika kuwaendeleza makocha,”  anasema na kuongeza:

“Timu kubwa bado hazijawaamini makocha wa ndani kwa sababu bado hatujathibitisha kwamba tunastahili kuwa makocha wa timu hizo kubwa. Lakini tupo kwenye mwelekeo wa kufika huko.”

Anasema ushindani unaoonekana katika baadhi ya mechi za ligi kati ya timu kubwa na zile zenye rasilimali ndogo unaonyesha kuwa pengo la kiufundi linaweza kupunguzwa ikiwa makocha wazawa wataendelea kupata elimu na uzoefu.


BADR 02

WAGENI NA NAFASI YA WAZAWA

Kwa upande wa makocha wa kigeni, Badru amesema uwepo wao haupaswi kuonekana kama tatizo, akieleza kuwa mara nyingi wanafanya kazi katika mazingira yenye wachezaji wengi wenye uzoefu wa kimataifa.

Anasema timu kama Simba, Yanga na Azam zina wachezaji wengi wa kigeni wenye viwango na uzoefu tofauti, jambo linalomsaidia kocha kujenga kikosi chenye ushindani.

Hata hivyo, anasema hali hiyo inaibua suala la nafasi ya wachezaji wazawa, hasa katika timu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa.

“Lazima tupambane kutengeneza mazingira ambayo timu zetu kubwa zitakuwa na wachezaji wazawa bora. Tukimtengeneza mchezaji kupitia timu za vijana, akifika kwenye timu ya wakubwa anatakiwa apewe nafasi ya kucheza. TFF kuweka sheria ya vijana kupata nafasi ni kwa sababu tunataka hawa wachezaji wawakilishe Taifa Stars,”€  anasema.


BADR 05

SAMATTA BADO ANA THAMANI

Badru pia anatoa mtazamo wake kuhusu Mbwana Samatta, akisema mchezaji anayeshiriki katika ligi ya kiwango cha juu Ulaya hawezi kupuuzwa kirahisi na Taifa Stars kutokana na uzoefu anaoleta ndani ya timu.

“Kama anacheza ligi bora duniani, maana yake ana kitu ndani yake. Huwezi kumpuuza na huwezi kumuacha, kwa sababu ana kitu ambacho anaweza kukileta kwenye timu,”€  amesema.

Badru anasema hata kama Samatta hatumiki muda wote uwanjani, uwepo wake unaweza kuwa na thamani kutokana na uzoefu wake wa kucheza soka la kiwango cha juu na uelewa wa mazingira ya timu ya taifa.

“Uwepo wake tu ni kitu kizuri. Bado yupo kwenye ligi kubwa duniani. Unawezaje kumpuuza mtu kama huyu?”  anasema kocha huyo. Hata hivyo, kuhusu sababu za Samatta kutangaza kustaafu Taifa Stars, Badru anasema uamuzi huo unatakiwa kuheshimiwa kwa sababu sababu kamili zinajulikana zaidi na mchezaji mwenyewe.


BADR 06

NUHU APEWA NAFASI

Mwisho, Badru anamzungumzia kocha Haji Nuhu ambaye anaamini anaweza kuwa sehemu ya kizazi kipya cha makocha watakaokuja kuipa Tanzania mafanikio. Badru anasema Nuhu ambaye kwa sasa ni kocha wa Namungo ana tabia ya kuuliza, kujifunza na kutafuta kuelewa mambo mapya, akisema sifa hizo ni muhimu katika ukocha wa kisasa.

“Nuhu ni mtu anayependa kudadisi na kujifunza. Anauliza, anajiamini na ana ubunifu. Kujifunza ni kila kitu kwenye ukocha. Mimi namwona anaweza kuwa msaada mkubwa katika soka la Tanzania,”  anasema.

Anasema uzoefu wa Nuhu kama mchezaji wa Taifa Stars na katika klabu kubwa kama Simba na Azam unaweza kuwa msingi wa kumsaidia katika safari yake ya ukocha.