Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

BAB'KUBWA... Pedro alivyokwepa  mtego wa Waarabu

YANGA Pict

Muktasari:

  • Bao la Prince Dube dakika ya 56, ndilo limeipa heshima hiyo Yanga ikiichapa AS FAR Rabat ya Morocco katika mechi ya kwanza ya Kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa jana Jumamosi kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

YANGA imeanza na ushindi kwa mara ya kwanza katika hatua ya makundi michuano ya CAF, hayo yamefanyika chini ya kocha Pedro Goncalves, raia wa Ureno.

Bao la Prince Dube dakika ya 56, ndilo limeipa heshima hiyo Yanga ikiichapa AS FAR Rabat ya Morocco katika mechi ya kwanza ya Kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa jana Jumamosi kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.


YANG 05

KABLA YA UJIO WA PEDRO

Rekodi zinaonyesha, kabla Pedro hajatambulishwa Yanga, Oktoba 25 mwaka huu, timu hiyo ilikuwa haijawahi kushinda mechi ya kwanza hatua ya makundi CAF tangu mwaka 2016.

Mara zote ilifungwa na timu zenye asili ya Waarabu ambazo ni MO Bejaia (2016), USM Alger (2018), US Monastir (2023), CR Belouizdad (2024) na Al Hilal (2024).

Katika mechi hizo tano zilizopita dhidi ya Waarabu, Yanga mbali na kupoteza zote, pia ilikuwa haijafunga bao lolote.

Ilianza Juni 19, 2016, Yanga iliposhiriki Kombe la Shirikisho na mechi ya kwanza ya kundi ilianza na MO Bejaia ya Algeria na kupoteza kwa bao 1-0. Yanga ilikuwa inafundishwa na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm.

Mei 6, 2018, Yanga ilishiriki tena Kombe la Shirikisho na ilianza makundi dhidi ya USM Alger pia ya Algeria na ikapoteza kwa mabao 4-0. Kikosi kiliongozwa na makocha wasaidizi Shadrack Nsajigwa na Noel Mwandila, baada ya kocha mkuu, Mzambia George Lwandamina kuondoka.

JICH 02

Msimu wa 2022-2023, Yanga ilianzia Ligi ya Mabingwa, lakini ikaangukia Shirikisho baada ya kutolewa na Al Hilal, hatua ya pili, ikakutana na Club Africain, ikaitoa kwa jumla ya bao 1-0 na kufuzu makundi.

Hatua ya makundi, mechi ya kwanza ilikutana na US Monastir ya Tunisia na kupoteza 2-0 chini ya kocha Nasreddine Nabi.

Msimu wa 2023-2024 ikinolewa na Miguel Gamondi katika Ligi ya Mabingwa Yanga ilianza na kichapo cha 3-0 kutoka kwa CR Belouizdad ya Algeria, kisha msimu uliopita ikinolewa na Sead Ramovic aliyempokea Gamondi aliyeiingiza makundi, ilianza na kichapo cha 2-0 kutoka kwa Al Hilal ya Sudan.


YANG 04

SAYANSI YA MPIRA ILIVYOJIBU

Pedro anayetambulika kama Kocha wa Sayansi ya Mpira, amefanya yasiyowezekana kuwa yanawezekana baada ya kuanza na ushindi huo wa kibabe.

Akiwa na siku 28 tu tangu ajiunge kikosini hapo kutoka Oktoba 25, 2025 hadi Novemba 22, 2025, Pedro ameiongoza Yanga mechi tatu na zote amepata ushindi.

Katika mechi hizo tatu, kuna mastaa saba hawajakosekana kwenye kikosi chake ambao ni Djigui Diarra, Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Dickson Job, Duke Abuya, Maxi Nzengeli na Prince Dube.

Pedro mechi mbili za kwanza zilikuwa za Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar na KMC, ambapo alifanya mabadiliko ya mchezaji mmoja tu kikosini, huku wengine wakiwa walewale.

Dhidi ya Mtibwa Sugar wakati Yanga inashinda mabao 2-0, kikosi kilikuwa hivi; Djigui Diarra, Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Duke Abuya, Edmund John, Maxi Nzengeli, Prince Dube, Mohamed Doumbia na Offen Chilola.

Mechi iliyofuata dhidi ya KMC, Yanga ilishinda 4-1, hapo Pedro alimuanzisha Pacome Zouzoua aliyechukua nafasi ya Edmund John.

Kikosi kilikuwa hivi; Djigui Diarra, Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Duke Abuya, Offen Chilola, Maxi Nzengeli, Prince Dube, Mohamed Doumbia na Pacome Zouzoua.

Mechi ya tatu dhidi ya AS FAR Rabat, Pedro alifanya mabadiliko ya wachezaji watatu kutoka kikosi kilichoifunga KMC mabao 4-1 katika Ligi Kuu Bara.

Ibrahim Bacca alichukua nafasi ya Bakari Mwamnyeto, Offen Chikola akampisha Celestine Ecua, huku Mudathir Yahya akianza badala ya Mohamed Doumbia.

Kikosi kilikuwa hivi; Djigui Diarra, Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Prince Dube, Pacome Zouzoua na Celestine Ecua.


YANG 02

DUKE, MUDATHIR, MAXI WATU WA KAZI

Siku moja kabla ya kucheza na AS FAR Rabat, Pedro alifika kwenye Uwanja wa New Amaan akiwa na kikosi cha Yanga kufanya mazoezi na mwisho.

Kabla ya mazoezi kuanza, kulikuwa na mazungumzo baina ya benchi la ufundi na wachezaji wote. Kisha baada ya hapo, Pedro akakaa pembeni na viungo watatu, Duke Abuya, Mudathir Yahya na Maxi Nzengeli.

Akiwa na viungo hao, Pedro alionekana kujadiliana nao kwa msisitizo na kuweka mikakati ya kuizuia FAR Rabat. Hawakuwa wakisikika wanachokizungumza, lakini vitendo vya mikono yao ilidhihirisha kulikuwa na kitu muhimu sana wanajadili na kuwekeana msisitizo fulani.

Siku ya mechi, Pedro aliwaanzisha viungo hao katika kikosi cha kwanza. Duke akicheza namba sita, Mudathir na Maxi wakiwa juu wakipishana. Wanapotengeneza mashambulizi, mmoja anakuwa namba kumi mwingine namba nane, wakirudi kujilinda, wote wanashuka chini kusaidiana na Duke.

YANG 09

Walicheza kwa mtindo huo hadi dakika ya 65, Pedro alipomtoa Mudathir ambaye alicheza vyena na kutoa asisti ya bao la Prince Dube na kuingia Lassine Kouma, kisha dakika ya 85, Mousa Balla Conte akachukua nafasi ya Maxi.

Wakati mabadiliko hayo yote yanafanyika, Yanga ilikuwa mbele kwa bao hilo 1-0, hivyo Pedro akawa analinda ushindi wake na kufanikiwa.

Kwa muda waliocheza pamoja viungo hao, walifanya kazi kubwa sana kumiliki eneo la kati ya uwanja na kuwapa shida nyota wa FAR Rabat kupenya. Ilishuhudiwa dakika 45 za kwanza, FAR Rabat ikishindwa kutengeneza shambulizi lolote la hatari. Shuti lao la kwanza kulenga lango lilikuja katika dakika ya 53, likitokea pembeni kwa kupigwa krosi. Pale kati palikuwa pagumu kupitika.


YANG 10

BOLI LINAPIGWA HASWA

Katika mechi tatu tu, Wanayanga wameonyesha imani kubwa na kocha huyo kwani ukiwasikia wanavyozungumza, hivi sasa wanaona soka safi likichezwa.

Pedro kwa kiasi fulani amerudisha ile Yanga ya kuuchezea sana mpira kiasi kwamba mashabiki wanafurahia kuiangalia timu inapocheza tofauti na awali wakati kocha Romain Folz alipokuwepo, wengi walionyesha kutofurahia uchezaji wa timu hata iliposhinda.

Yanga soka inacheza kulingana na mpinzani anavyokuja. Ukiweka mpira chini wanacheza na wewe, ukija na mfumo wa mipira ya juu wanaruka na wewe. Pedro anaijenga Yanga inayocheza staili zote za wapinzani.

YANG 01

Yanga mbali na kutawala mchezo kwa asilimia 51 dhidi ya 49 za Rabat, ilipiga mashuti tisa yaliyolenga lango dhidi ya moja tu la wageni, huku kiujumla Yanga ikipiga mashuti 15 kwa matano.

Uchezaji wa Yanga umemfanya kocha wa AS FAR Rabat kukiri wapinzani wao hao ni wagumu akisema: “Tulimaliza kipindi cha kwanza kwa sare ya 0-0 na tuliendelea kupambana. Tuliendelea kwa kufanya baadhi ya mabadiliko, tukabadilisha baadhi ya wachezaji.

“Pia tulibadilisha mambo kadhaa ili kupata udhibiti zaidi wa mpira, kumiliki mpira zaidi. Nadhani tulifanikiwa. Lakini Yanga walikuwa imara pia.

“Kama nilivyosema, ilikuwa mechi ya ushindani mkubwa, ngumu sana, na tunapaswa kuinuka tena, kuelekeza macho yetu kwenye mechi inayofuata. Tutajiandaa kwa mechi ijayo na kuusahau haraka huu mchezo.”


YANG 08

KAULI YA PEDRO

Kocha Pedro amezungumzia namna anavyoendelea kuijenga Yanga akisema ndani ya kikosi hicho, bado ana kazi ya kuimarisha viwango vya wachezaji taratibu huku akifurahishwa na mwendeo wa timu.

“Tunafanyia kazi suala la kujitoa kwa pamoja kama timu. Hilo ni jambo muhimu sana. Bila shaka, kwao ni muhimu kucheza vizuri kama mchezaji mmoja mmoja, lakini wanapaswa kutambua kuwa wao ni sehemu ya timu, klabu, na familia yenye msaada. Kwa hiyo, jambo la muhimu zaidi mwishoni ni timu kufanikisha malengo yake.

“Bado tunaendelea kuiimarisha timu na kupitia hizi mechi tunazoendelea kucheza za mashindano tutazidi kuimarika kwani hatuna muda mwingi wa kujiandaa.

“Ukiangalia baada ya mimi kuja, tulicheza kidogo, tukasimama kwa wiki moja, baada ya hapo ikaja kalenda ya FIFA, wachezaji wakaenda kwenye timu zao za taifa. Hapo unaona namna ratiba inavyobana lakini tunaendelea kupambana.”

YANG 06

Kuhusu namna alivyojipanga kuwadhibiti FAR Rabat na kufanikiwa, Pedro amesema: “Mimi na Alexandre (kocha wa FAR Rabat) tunafahamiana vizuri sana. Ukiangalia, wachezaji wa timu hizi mbili ni tofauti.

“Falsafa za klabu nazo ni tofauti, pia maendeleo ya klabu yapo katika viwango tofauti, lakini namna ya kuandaa mbinu za kucheza mpira tunafanana sana. Kwa hiyo tulijua watajaribu kucheza soka kama sisi, na tulijiandaa na mpango wa kuweka presha ya juu, halafu kujaribu kutumia nafasi mapema iwezekanavyo, au kudhibiti kasi ya mchezo, kumiliki mpira, kuwa na akili, kumtafuta mchezaji aliye huru ili apige shuti au kutengeneza nafasi ya kufunga.

“Ilikuwa ni furaha kucheza naye, pamoja na timu yake. Pia, kwa Carneiro (beki wa FAR Rabat raia wa Angola), ambaye ni mchezaji niliyemfundisha kwa miaka mingi sana.

“Ndio hivyo soka lilivyo, wakati mwingine tunakuwa upande mmoja, wakati mwingine tunakuwa wapinzani, lakini daima kwa heshima, na kila mmoja anajaribu kufanya vyema ili kutawala uwanja.”

Yanga imeanza kwa kushika nafasi ya pili katika Kundio B nyuma ya mabingwa mara 12 wa michuano hii, Al Ahly ya Misri ambao waliifunga JS Kabylie ya Algeria kwa mabao 4-1 jana pia na kukaa kileleni.

Mechi ijayo, Yanga itaenda ugenini dhidi ya JS Kabylie Ijumaa hii saa 4:00 usiku.


YANG 07

KUNDI B

                     P        W       D       L        F        A       PTS

1. Al Ahly     1         1         0       0       4        1         3

2. Yanga       1         1         0       0       1         0       3

3. Rabat       1         0       0       1         0       1         0

4. Kabylie     1         0       0       1         1         4        0


Mechi zijazo:

Nov 28, 2025

JS Kabylie    v Yanga (Saa 4:00 usiku)

Far Rabat     v Al Ahly (Saa 4:00 usiku)