Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ratiba hii ya ligi bado inafikirisha

NONDO Pict

Muktasari:

  • Ligi ilisimama kwa takriban wiki mbili kupisha mechi za timu ya taifa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), huku zikiwa zimechezeshwa jumla ya mechi 39 tu kati ya 240 zinazotakiwa kupigwa msimu huu wa 2025-2026 ulioanza rasmi Septemba 17.

LIGI Kuu Bara inarejea tena wikiendi hii, ikienda sambamba na ratiba ya mechi za michuano ya kimataifa ya CAF kwa maana ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.

Ligi ilisimama kwa takriban wiki mbili kupisha mechi za timu ya taifa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), huku zikiwa zimechezeshwa jumla ya mechi 39 tu kati ya 240 zinazotakiwa kupigwa msimu huu wa 2025-2026 ulioanza rasmi Septemba 17.

Kwa kuwa kuna jumla ya klabu 16 zinazoshiriki ligi hiyo, kila moja inapaswa kuchezwa mechi 30 ikiwa na maana duru la kwanza 15 na duru la mwisho 15 na kwa jumla yake msimu mzima unapaswa kupigwa mechi 240 na ilipangwa msimu umalizike Mei 23 mwakani.

Hata hivyo, kabla hata ligi haijachangamka, Bodi ya Ligi imetangaza mabadiliko mengine madogo ya ligi hiyo ambayo imekuwa ikipanguliwa na kusimamia bila mpangilio tangu msimu ulipoanza na sasa huenda ligi ikamalizika Mei 29 na msimu ukitarajiwa kuisha mwishoni mwa Juni kwa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) baada ya kumalizika kwa play-off za kupanda daraja.

Ukiangalia msimamo wa ligi hiyo, utaona kuna timu zimecheza mechi za raundi sita, nyingine tano na zipo zilizocheza nne kama Yanga na Tanzania Prisons, halafu kuna zilizocheza mechi tatu tu, ikiwamo Simba, Azam FC, Singida Black Stars na TRA United.

NOND 01

Kama hujui, ligi ilichelewa kuanza kutokana na kuwepo michuano ya Kombe la Mabingwa wa Afrika (Chan) 2024 zilizoandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda na hata ilipoanza ilisimama ndani ya muda mfupi kutokana na uwepo na mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2026 zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico.

Baada ya hapo ikarudi kwa mechi chache kabla ya kukwama kutokana na kilichotokea katika uchaguzi mkuu wa taifa na kutibua baadhi ya mechi kuchezwa, kisha kuwepo kwa kalenda ya mechi za timu za taifa kwa mujibu wa Fifa na sasa imerejea tena kwa mechi chache.

Ndiyo, ni mechi chache kwa vile itachezwa hadi Desemba 7 kama hakutakuwa na mabadiliko mengine na kusimama kwa ajili ya kupisha maandalizi kwa timu ya taifa itakayoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zitakazoanza Desemba 21 hadi Januari 18 mwakani.

Kwa hesabu, baada ya mechi chache za Desemba, ligi itasimama hadi Februari mwakani wakati klabu shiriki zikiwa hazijacheza hata mechi 10 kwani ratiba inaonyesha baadhi zitacheza hadi nane na zile zenye mechi chache zitafikisha angalau tano hadi sita tu!

NOND 04

Hapo hatuzungumzii uwepo wa michuano ya Kombe la Muungano itakayochezwa Aprili wala mechi za Kombe la Shirikisho (FA) zinazoanza kupigwa Desemba kwa raundi ya 64 Bora na kumbuka Simba, Yanga, Azam na Singida zinashiriki mechi za makundi za michuano ya CAF.

Kama zitapenya kwenda robo fainali au mbele zaidi ni wazi ratiba ya ligi itazidi kuvurugika tofauti na kilichotangazwa na Bodi ya Ligi msimu utamalizika Juni 14 kwa mechi za play-off za kuwania kupanda na kushuka daraja. Hii ni kwa sababu tarehe ya fainali ya FA haijatangazwa.

Kutokana na kusuasua huko kwa ligi, kuna baadhi wameanza kuhoji kwa nini ligi yetu inasimama kupisha kalenda ya Fifa au Caf wakati mataifa mengine ikiwemo Kenya na DR Congo ligi zao zikiendelea kupigwa licha ya timu za taifa kukipiga?

Pia wanahoji kuna wiki zinapita vigogo Simba na Yanga zinakuwa mjini na hazichezi mechi zozote kwa maelezo zinajiandaa na mechi za kimataifa, lakini wapinzani wao wanaochuana nao huko CAF wanaendelea na ratiba zao kama kawaida na huoni tofauti yoyote zikikutana uwanjani?!

NOND 02

Hata hivyo, ni kweli kwa tariba ilivyo, ni ngumu kutoboa kirahisi kwa matarajio ya wengi, ila Bodi ya Ligi haipaswi kunyooshewa kidole. Iachwe ifanye kazi kwa sababu sio matarajio yao.

Kwa mfumo wa uundwaji wa timu yetu ya taifa inayotegemea asilimia 90 na zaidi ya kikosi chake kutokana na wachezaji wanazotoka katika klabu zetu.

Hivyo kuendelea kwa ligi kama ambavyo wenzetu wanaendelea kutazua migongano zaidi ya kifikra baina ya klabu kufikia malengo waliyojiwekea kwa msimu husika kwa kuanza kunyang’anyana wachezaji na timu ya taifa.

Kama ligi itaendelea huku timu ya taifa ikiwa na majukumu yake wachezaji watalazimika kuchagua klabu au timu ya taifa, kitu ambacho si kizuri kwa ukuaji wa taifa letu katika hatua zake za kisoka.

Wanaotaka ligi iendelee huku timu ya taifa ikiwa katika majukumu yake, nadhani hawazingatii athari zitakazojitokeza kwa klabu zinazochangia wachezaji wengi timu ya taifa na mbaya zaidi namna zinavyosajili pia wachezaji wa kigeni ambao wanaitwa pia kwenda kutumikia mataifa yao na ndio wachezaji tegemeo katika vikosi hivyo.

NOND 03

Ndiyo maana naona kwa muundo wa klabu zetu na timu ya taifa hatuwezi kuendelea kucheza ligi huku timu za taifa zikiendelea na majukumu hasa timu yetu ya taifa inapokua ikishiriki michuano ya Caf au Fifa.

Ni kweli kuna wakati Bodi ya Ligi inahitaji kubeba lawama kuhusu ratiba ya ligi kutokwenda vizuri, lakini kwa hili ipumzishwe ifanye majukumu yake kuhakikisha mbali na mrundikano wa michuano kwa timu ya taifa bado ligi inachezwa na kumalizika.

Miaka ya nyuma ilikua rahisi wakati michuano mikubwa kama Afcon inachezwa sisi tulikuwa tunaendelea na ligi zetu za ndani sababu hatukuwa tunashiriki michuano kwa ngazi hizo na hizi ndizo athari za ukuaji kuanzia klabu na timu za taifa.

Klabu zetu zinavyoshinda Afrika na timu yetu ya taifa ndipo tunatengeneza viporo kwa klabu zinazotuwakilisha na kusimama kwa ligi kupisha timu ya taifa, ndio maana nasema bodi iachwe!