Aziz: Mwenzangu alipigwa tumboni akafariki
Muktasari:
- Safari yake katika mchezo wa ngumi haikuanza kwa shangwe, wala hakupokeWa kwa mikono miwili na kila mtu aliyekuwa karibu naye. Ilianza mwaka 2017 akiwa bado mdogo, huku akitoroka na kwenda mazoezini kwa sababu tayari alikuwa ameanza kuamini kuwa ngumi ndiyo inaweza kuwa sehemu kubwa ya maisha yake.
KAMA unadhani bondia huanza safari yake kwa kupanda ulingoni na kutembea kifua mbele, basi simulizi ya Aziz Wazir Challa inaweza kubadilisha kabisa mtazamo wako.
Safari yake katika mchezo wa ngumi haikuanza kwa shangwe, wala hakupokeWa kwa mikono miwili na kila mtu aliyekuwa karibu naye. Ilianza mwaka 2017 akiwa bado mdogo, huku akitoroka na kwenda mazoezini kwa sababu tayari alikuwa ameanza kuamini kuwa ngumi ndiyo inaweza kuwa sehemu kubwa ya maisha yake.
Leo, Aziz si mgeni kwenye kazi hiyo. Amewahi kutwaa ubingwa wa Mkoa wa Dar es Salaam mara nne mfululizo katika uzito wa kilo 51, kushiriki mashindano nje ya Tanzania na kukutana na mabondia kutoka nchi mbalimbali.
Katika mazungumzo na Mwanaspoti, Aziz anafunguka kuhusu mwanzo wake, kipigo alichokutana nacho, pambano lake la kwanza, siri ya kujilinda ulingoni, familia yake, nidhamu aliyopewa na baba yake, maisha yake nje ya ngumi na ndoto yake kubwa ya kutwaa dhahabu katika Olimpiki.
MWANZO WA SAFARI
Aziz anasema aliamua kuingia kwenye mchezo wa ngumi mwaka 2017, akiwa bado mdogo. Mapenzi yake kwa mchezo huo yalikuwa makubwa kiasi kwamba wakati mwingine alilazimika kutoroka na kwenda mazoezini.
Anasema kipindi hicho aliamini kipaji alichokuwa nacho na hakutaka kukiacha kipotee, ndiyo maana licha ya umri mdogo aliendelea kutafuta nafasi ya kufanya mazoezi.
“Nilianza kucheza ngumi mwaka 2017 nikiwa bado mdogo. Kuna kipindi nilikuwa natoroka kwenda kufanya mazoezi kwa sababu nilikuwa naamini sana katika kile nilichokuwa nakifanya,” anasema Aziz.
KIPIGO HAKIKUMTISHA
Kama ilivyo kwa wengi wanaoingia kwenye michezo ya mapambano, mwanzo wa Aziz haukuwa mwepesi. Anakumbuka alivyokutana na vipigo, ikiwemo kutoka nyumbani na hata ulingoni wakati wa mazoezi.
Aziz anasema alipigwa vibaya kiasi kwamba uso ulivimba. Mjomba wake alipomwona hali hiyo alilia, huku Aziz akilazimika kutafuta sababu nyingine ya kuelezea hali yake nyumbani.
“Nilipigwa sana. Kuna siku nilifanya ‘sparring’ na Kidunda jeshini, nikapigwa mpaka uso na macho vikavimba. Mjomba wangu aliponiona alilia. Nilipofika nyumbani nikasema nina malaria ili nisieleze ukweli wa nilichopitia,” anasema.
PAMBANO LA KWANZA, HOFU KUBWA
Pambano lake la kwanza kabisa lilikuwa katika Uwanja wa Taifa, tukio ambalo Aziz hawezi kulisahau kwa sababu mazingira aliyokutana nayo kabla ya kupanda ulingoni yalikuwa mazito.
Anasema kabla ya muda wake wa kupigana, bondia mwingine aliyekuwa ametoka kwenye pambano aliumia vibaya baada ya kupigwa sehemu za tumbo na baadaye kufariki dunia akiwa njiani kwenda hospitali.
“Pambano langu la kwanza lilikuwa Uwanja wa Taifa. Kabla sijapanda ulingoni, niliona bondia mwingine ametoka kupigana, akapigwa sehemu za tumbo na baadaye akafariki akiwa njiani kwenda hospitali. Nilipata hofu sana, lakini nikajikaza na kupanda ulingoni,” anasema.
HUJUI MPINZANI HADI SIKU YA PAMBANO
Tofauti na baadhi ya mashindano ambayo mwanamichezo anaweza kujua mpinzani wake mapema na kuandaa mbinu maalumu, Aziz anaeleza kuwa katika ngumi za ridhaa mambo yanaweza kuwa tofauti.
Aziz amekuwa akifanya vizuri katika mazingira hayo na tayari amewahi kutwaa ubingwa wa Mkoa wa Dar es Salaam mara nne mfululizo katika uzito wa kilo 51.
“Katika ngumi za ridhaa hauwezi kumjua mpinzani wako mapema. Tunapimwa uzito, halafu droo inafanyika. Unaweza kuambiwa muda mfupi kabla ya pambano kwamba unapigana na bondia fulani. Hujui nguvu zake wala udhaifu wake, kwa hiyo unatakiwa uwe tayari kwa kila kitu,” anasema.
UGOMVI WA MTAA SI SEHEMU YAKE
Licha ya kuwa bondia na kujifunza namna ya kupigana, Aziz anasema hajawahi kuona sababu ya kutumia uwezo wake katika ugomvi wa mitaani.Anasema nidhamu ndiyo msingi unaomsaidia kuepuka migogoro ya aina hiyo.
“Siwezi kuona sababu ya kugombana mtaani. Ugomvi wa mtaani unaweza kuleta madhara makubwa kwa sababu haujui utaishia wapi. Mimi napenda nidhamu na najiepusha na migogoro,” anasema.
BIBI ALIMUAMINI
Aziz anasema tangu akiwa mdogo alimwambia bibi yake kuwa anatamani kuwa mchezaji mkubwa. Ndoto hiyo haikuwa maneno ya kawaida kwake kwa sababu hata baada ya kuanza mazoezi aliendelea kuamini kuwa anaweza kufika mbali.
“Nilimwambia bibi yangu tangu nikiwa mdogo kwamba nataka kuwa mchezaji mkubwa. Kabla hajafariki alinisisitiza niamini ninachokifanya. Hilo lilinipa nguvu sana,” anasema.
KENYA ILIMJENGA KUJIAMINI
Mash indano ya Kenya ni miongoni mwa matukio yaliyomjengea Aziz kujiamini zaidi. Anasema awali baadhi ya watu walikuwa wakimtazama kwa umri na kimo chake na kumchukulia kama bondia ambaye huenda asingekuwa tishio kubwa.
“Kenya ilinipa ‘confidence’ kubwa sana. Watu wengi walikuwa wananidharau kwa sababu ya umri na kimo, lakini nilipopanda ulingoni nilionyesha uwezo wangu. Kitu cha kwanza kwangu ni kuwakilisha vizuri Tanzania,” anasema.
ANAPENDA KUJILINDA
Aziz anasema nguvu yake kubwa ulingoni siyo kushambulia kwa nguvu, bali kujilinda na kutumia akili. Anasema raundi ya kwanza kwake huwa ni muhimu kwa sababu humsaidia kumchunguza mpinzani kabla ya kuongeza kasi ya mashambulizi.
“Naona niko vizuri zaidi kwenye kujilinda. Sina nguvu kubwa sana za mwili, kwa hiyo natumia spidi, akili na macho. Raundi ya kwanza namjaribu mpinzani, wakati mwingine nashusha mikono kidogo au namvutia arushe ngumi ili nijue spidi na nguvu zake. Baada ya hapo naongeza spidi,” anasema.
MEDALI ZOTE NI HESHIMA
Kwa Aziz, hakuna medali anayoweza kusema haina thamani kwa sababu kila moja ina hadithi yake na inawakilisha kazi iliyofanyika kabla ya ushindi huo.
Hata hivyo, medali alizopata nje ya Tanzania zinabaki kuwa miongoni mwa kumbukumbu zinazompa faraja zaidi, akitaja mashindano ya Afrika Kusini, Kenya, Morocco na Nigeria mwaka 2024.
“Medali zote ni bora kwangu kwa sababu kila ushindi ni heshima. Lakini medali nilizopata nje ya nchi kama Afrika Kusini, Kenya, Morocco na Nigeria mwaka 2024, zinanipa faraja kubwa. Lengo langu ni kwenda kupigania dhahabu kwenye Olimpiki na Michezo ya Jumuiya ya Madola,” anasema.
BABA ALIMJENGEA KWA NIDHAMU
Moja ya simulizi zinazogusa zaidi katika maisha ya Aziz ni namna baba yake alivyomjengea nidhamu. Anasema aliamshwa saa 10:00 asubuhi kwa ajili ya kukimbia na kufanya mazoezi kabla ya kwenda shule saa 12:00 au saa 1:00 asubuhi.
“Baba yangu alikuwa ananisisitiza sana kufanya mazoezi. Nilikuwa naamka saa 10:00 asubuhi nakimbia na kufanya mazoezi kabla ya kwenda shule. Kama sijafanya mazoezi, wakati mwingine sikupewa chakula. Ilikuwa ngumu, lakini leo naona ilinijenga sana,” anasema.
MABONDIA WA NJE
Aziz anasema kitu kikubwa alichojifunza ni nidhamu ya hali ya juu, pamoja na ukweli kwamba hakuna njia rahisi ya kuwa bingwa.
Kwa upande mwingine, amegusa pia changamoto za maamuzi katika mashindano ya kimataifa, akisema katika baadhi ya mashindano aliyoshiriki Nigeria na Afrika Kusini alimaliza nafasi ya tatu.
“Nilichojifunza ni nidhamu kubwa. Pia nimejifunza kwamba huwezi kuwa bingwa bila kumpiga bingwa. Kuna wakati unafanya vizuri lakini matokeo yanaweza kuamuliwa na majaji. Nimepata nafasi ya tatu Nigeria na Afrika Kusini, lakini hayo yote yamenifundisha zaidi,” anasema.
CHINYEMBA NDIYE ANAYEMTAKA
Kati ya mabondia wa kimataifa ambao Aziz anatamani kukutana nao ulingoni, jina la Patrick Chinyemba wa Zambia liko juu kwenye orodha yake.Sababu kubwa ni kwamba anaona wanafanana katika mambo kadhaa ya msingi yanayohusu mchezo wao, kuanzia kimo hadi spidi na matumizi ya macho.
“Natamani sana kupigana na Patrick Chinyemba wa Zambia. Tunafanana kwa kimo, spidi, matumizi ya macho na staili ya mchezo. Nadhani tukikutana lingekuwa pambano kubwa na la changamoto,” anasema.
MRITHI WA MABONDIA WAKUBWA?
Kufananishwa na mabondia wakubwa waliowahi kuitumikia Tanzania ni jambo linalompa Aziz hamasa badala ya kumuweka kwenye presha. Miongoni mwa majina anayofungamanishwa nayo ni George Constantino, ambaye Aziz anamchukulia kama kaka yake.
“Watu wakinifananisha na George Constantino inanipa faraja na hamasa. Mimi namchukulia kama kaka yangu. Ninachotaka ni kujituma ili siku moja niwe bora zaidi yake,” anasema.
MAMA ALIOGOPA
Kwa kuwa ni mtoto pekee wa kiume katika familia yao, uamuzi wa Aziz kuingia kwenye mchezo wa ngumi haukuwa jambo rahisi kwa mama yake. Aziz anasema mama yake mwanzoni hakujua anachokifanya na alipopata taarifa hizo aliingiwa na hofu kutokana na hatari zinazohusishwa na mchezo huo.
“Mama mwanzoni hakujua nilikuwa nafanya ngumi. Alipokuja kujua aliogopa sana. Baba alikuwa anajua na alikuwa ananipa ushirikiano. Baadaye mama alikubali baada ya kuona medali na mafanikio yangu,” anasema.
UJUMBE KWA VIJANA
Kwa vijana wanaotamani kuingia kwenye mchezo wa ngumi, Aziz anasema jambo la kwanza wanapaswa kulijenga ni nidhamu. Anaamini nidhamu inaanzia nyumbani kabla hata ya kufika kwenye ukumbi wa mazoezi. Pia anasisitiza kujituma na kuelewa kuwa ngumi si mchezo wa kufanya mzaha.
“Vijana wanatakiwa kuwa na nidhamu, na nidhamu inaanzia nyumbani. Pia wajitunze na wajitoe kwa dhati. Ngumi ni mchezo mzuri, lakini si wa masiara. Kama haujajiandaa vizuri unaweza kuumia vibaya au hata kupoteza maisha,” anasema.
NGUMI ZIMEMLIPA
Aziz hakubaliani na mtazamo kwamba ngumi ni mchezo ambao hauwezi kumsaidia mwanamichezo kujenga maisha yake.Kwa upande wake, anasema mchezo huo umemfungulia milango mbalimbali na kumsaidia kupata ajira rasmi pamoja na mafanikio mengine ya kimaisha.
“Ngumi zinalipa ukiwa na akili na ukijituma. Mimi kupitia mchezo huu nimeweza kupata ajira rasmi na nimepata mafanikio mengine ya kimaisha,”€anasema.
MTU WA NDANI, SI WA STAREHE
Aziz anasema ni mtu mtulivu, hapendi kuzurura wala kunywa pombe. Badala yake, wakati akiwa nyumbani anapenda kutazama video za ngumi kupitia YouTube na kujifunza mbinu mbalimbali za mchezo.
“Maisha yangu ya uraiani ni ya utulivu. Sipendi kuzurura wala kunywa pombe. Starehe yangu kubwa ni kukaa ndani na kuangalia video za ngumi na mbinu mpya YouTube,” anasema.
MTOTO WAKE ASIPIGANE?
Ingawa ngumi ndiyo imempa mafanikio, Aziz anasema kama siku moja atapata mtoto, asingependa mtoto huyo achague mchezo huo.Sababu yake ni kwamba anafahamu kwa uzoefu wake ugumu na hatari zinazoweza kuambatana na mchezo huo.
“Kwa upande wangu ningependa mwanangu asicheze ngumi kwa sababu ni mchezo mgumu na una hatari zake. Lakini kama yeye mwenyewe ataamua kucheza, sitamzuia,”€ anasema.
DHAHABU YA OLIMPIKI
Pamoja na yote aliyopitia tangu mwaka 2017, Aziz bado anaona safari yake ndiyo kwanza inaanza.Mafanikio ya ndani, medali za nje ya nchi na uzoefu alioupata dhidi ya mabondia mbalimbali havijamfanya aridhike.
“Ndoto yangu kubwa ya miaka mitano ijayo ni kushiriki Olimpiki na kushinda medali ya dhahabu. Hilo ndilo ninalolifanyia kazi,” anasema.
Kwa Aziz safari kutoka kwa kijana aliyekuwa akitoroka kwenda mazoezini hadi kuwa bondia mwenye uzoefu wa mashindano ya kimataifa haikuwa ya mkato.
Ilikuwa safari yenye vipigo, hofu, nidhamu, kujifunza na kujenga kujiamini. Sasa akiwa na ndoto ya dhahabu ya Olimpiki, kinachobaki ni kuendelea na mazoezi na kusubiri siku ambayo atapata nafasi ya kuandika sura nyingine ya historia yake ulingoni.