Aturo aweka malengo makubwa Simba Queens, aitaka Afrika
Muktasari:
- Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, kipa huyo amezungumzia kurejea kwake Simba, uzoefu alioupata akiwa Tausi, ushindani WPL, malengo na ndoto ya kuifikisha Simba kwenye hatua kubwa ya soka la wanawake Afrika, huku akigusia sababu zinazoifanya WPL na Ligi Kuu Bara kuwa kimbilio la mastaa wengi wa kigeni.
BAADA ya msimu mmoja wa kuitumikia Simba Queens, kipa raia wa Uganda, Ruth Aturo anaingia msimu mpya akiwa na kiu kubwa ya mafanikio. Aturo kabla ya kutua Msimbazi aliichezea Tausi iliyopanda kutoka Ligi Daraja la Kwanza Bara hadi Ligi Kuu ya Wanawake Bara (WPL).
Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, kipa huyo amezungumzia kurejea kwake Simba, uzoefu alioupata akiwa Tausi, ushindani WPL, malengo na ndoto ya kuifikisha Simba kwenye hatua kubwa ya soka la wanawake Afrika, huku akigusia sababu zinazoifanya WPL na Ligi Kuu Bara kuwa kimbilio la mastaa wengi wa kigeni.
TOFAUTI ZA LIGI
Kipa huyo amecheza ligi mbalimbali nje ya Tanzania, akipita Kawempe Muslim na UCU Lady Cardinals za Uganda, FC KTP ya Finland, Al Shabab na Altaqadum za Saudia Arabia pamoja na Vihiga Queens ya Kenya.
Pia, ndiye kipa namba moja katika timu ya taifa ya Uganda na amekuwa na mafanikio ikiwemo kuchukua tuzo ya Mchezaji Bora wa Kike Uganda (2018).
Aturo anasema tofauti ya ligi alizocheza ni fedha akitoa mfano Kenya ambako hakuna mishahara ya kudumu kwa wachezaji, lakini kwa Tanzania mchezaji analipwa kwa wakati pamoja na posho.
“Tofauti ni pesa tu mfano Tanzania hapa ndio maana wachezaji wanakuja wengi kwa sababu kuna uhakika wa malipo tofauti na Kenya, lakini Finland na Saudi Arabia wako kitaaluma sana, hawana mchezo na maslahi ya mchezaji, wanaendesha timu vizuri sana,” anasema kipa huyo.
SIMBA KLABU KUBWA
Aturo anasema uamuzi wa kujiunga na Simba umechangiwa kwa kiasi kikubwa na ukubwa wa timu hiyo pamoja na mazingira yake ya ushindani.
“Najisikia vizuri sana kuwa hapa kwa msimu mwingine nikiwa na Simba Queens. Napenda kila kitu kuhusu Simba. Ni moja ya timu kubwa sana, nafikiri, katika ukanda wa Afrika Mashariki,” anasema.
Kipa huyo anaongeza mbali na timu hiyo kuwa na jina kubwa kwenye soka la Tanzania pia ni klabu yenye utamaduni wa kutafuta mafanikio na kushindana katika kila mashindano.
TAUSI ILIMPA UZOEFU
Kabla ya kutambulishwa Simba, Aturo alicheza Tausi msimu wa 2024/25 akiipandisha kutoka Ligi Daraja la Kwanza hadi Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania.
Anasema kucheza Tausi kulimsaidia kuelewa mazingira ya soka la wanawake nchini, aina ya ushindani uliopo na namna wachezaji wanavyopambana kila siku kutafuta mafanikio.
“Nafikiri ilikuwa hatua nzuri kwangu kwa sababu nilipata nafasi ya kucheza na kujifunza zaidi kuhusu ligi na mazingira ya Tanzania,” anasema.
Licha ya kuwa Tausi ilikuwa timu iliyokuwa imepanda daraja, Aturo anasema alifurahia uzoefu huo na sasa anatamani kufanya zaidi ya alichoonyesha ili kuwapa furaha mashabiki wa Simba ambao wamekuwa na matarajio makubwa ya timu yao kila msimu.
LIGI BONGO INAKUA
Aturo anasema Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania ni mashindano yenye ushindani mkubwa na ambayo yanaendelea kukua siku hadi siku.
Kwa nafasi yake ya golikipa, anasema ligi hiyo imemsaidia kukutana na wachezaji wenye uwezo tofauti, jambo linalomlazimisha kuendelea kujifunza na kuboresha kiwango chake.
“Ni ligi nzuri na yenye ushindani mkubwa sana, ikiwa na wachezaji wengi wenye uzoefu ambao wanaifanya iwe na ushindani wa kweli. Tangu nilipojiunga, nimeona ni ligi nzuri inayomfanya mtu ajifunze zaidi,” anasema.
Anaongeza uwepo wa wachezaji kutoka mataifa mbalimbali pia umeongeza ushindani katika ligi hiyo, huku klabu zikiongeza nguvu usajili wa wachezaji wenye uzoefu wa kimataifa.
Aturo anaamini hali hiyo inaweza kuendelea kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi inayokuza maendeleo ya soka la wanawake Afrika Mashariki.
MALENGO MAKUBWA
Anasema hajashangazwa na matarajio yaliyopo ndani ya klabu hiyo kwa sababu anafahamu vizuri ukubwa wa Simba na mahitaji ya mashabiki wake.
“Simba Queens wana matarajio makubwa kila msimu. Niko tayari kabisa kwa changamoto hiyo na ninaifanyia kazi,Lengo langu la kwanza ni kushinda na kwenda kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika,” anasisitiza.
CECAFA NJIA AFRIKA
Simba Queens kwa sasa inaelekeza nguvu zake kwenye maandalizi ya michuano ya CECAFA inayotarajiwa kufanyika Rwanda.
Kwa Aturo, mashindano hayo ni muhimu kwa sababu yanaweza kuwa hatua ya kwanza kuelekea kutimiza ndoto ya kushiriki michuano mikubwa ya klabu barani Afrika.
“Naamini tukifanya vizuri kwenye michuano mikubwa kama hii tunaweza kufikia malengo yetu. Nataka kusaidia timu kushinda na kufikia hatua kubwa zaidi,” anasema.
“Ninalenga kufanya vizuri zaidi kuliko nilivyokuwa Tausi. Kwa sasa akili yangu yote ipo hapa kusaidia timu kufikia malengo yake,” anasema.
WASHAMBULIAJI
Anasema msimu uliopita amekutana na washambuliaji wengi lakini anawataja Jamila Rajabu wa JKT Queens, Jeaninne Mukandayisenga wa Yanga Princess kuwa walimsumbua walipokutana kwenye mechi.
“Ligi ina wachezaji wengi wazuri lakini kwa wachezaji wa timu nyingine niliokutana nao nafikiri hao ndio hatari zaidi ni wachezaji wengi sana wakatili langoni,” anasema Aturo
SIRI YA UREMBO
Kipa huyo ni miongoni mwa wachezaji warembo kwenye ligi na hapa anaeleza siri nyuma ya ulimbwende wake.
Anasema: “Napenda sana kuonekana wa tofauti naondoa ile fikra ya wachezaji wa kike kuonekana wa kiume mpira wa miguu usitufanye tuonekane watu wa tofauti naamini mimi ni kioo cha wachezaji wengine wa kike hivyo natamani niwe mfano bora ndio maana napenda kujiweka nadhifu.”
UJUMBE MASHABIKI
Aturo anawataka mashabiki wa Simba Queens kuendelea kuwaunga mkono wachezaji kipindi chote cha msimu iwe kigumu au kizuri.
Anasema sapoti ya mashabiki inaweza kuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya timu hasa inapokuwa inakabiliwa na mechi ngumu.
“Nataka mashabiki waendelee kutuamini na kutupa sapoti. Tunajua matarajio yao ni makubwa na sisi kama wachezaji tunataka kuwafurahisha kwa kufanya vizuri,” anasema.