Arsenal iko bize kusaka hivi vichwa vya kazi

Muktasari:
- Lakini, miamba hiyo ya Emirates inayonolewa na Mhispaniola Mikel Arteta baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England kwa misimu mitatu mfululizo, imekuwa ikihusishwa na mastaa kibao kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi ikijiandaa kutengeneza kikosi ambacho kitakuwa cha kishindani msimu ujao na kubeba mataji.
LONDON,ENGLAND: LISEMWALO kwa sasa ni kwamba Arsenal ipo kwenye hatua za mwisho za kunasa dili la straika Viktor Gyokeres ili akapige mzigo kwenye timu hiyo inayosaka taji la Ligi Kuu England kwa nguvu.
Lakini, miamba hiyo ya Emirates inayonolewa na Mhispaniola Mikel Arteta baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England kwa misimu mitatu mfululizo, imekuwa ikihusishwa na mastaa kibao kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi ikijiandaa kutengeneza kikosi ambacho kitakuwa cha kishindani msimu ujao na kubeba mataji.
Gyokeres si mchezaji pekee anayehusishwa na Washika Bunduki wa London Kaskazini, kuna orodha ya wakali matata kabisa wanaotajwatajwa kwenye kikosi hicho cha Emirates.
Hugo Ekitike – Eintracht Frankfurt
Gazeti la Bild la Ujerumani limefichua kwamba Arsenal imejitosa kwenye mbio za kufukuzia huduma ya straika huyo Mfaransa baada ya kufanya vizuri huko Eintracht Frankfurt. Bei ya straika huyo inadaiwa kuwa ni Pauni 85 milioni na Arsenal inaamini inaweza kuimudu licha ya kwamba bado inaangalia kwenye klabu nyingine pia kama kuna straika mzuri wa kumsajili.
Anthony Elanga – Nottingham Forest
Ripoti zinafichua kwamba Arsenal inavutiwa na kiwango cha winga Anthony Elanga wa Nottingham Forest, lakini bado haijashawishika kiasi cha kutosha kunyanyua simu kuzungumza na mkali huyo wa zamani wa Manchester United. Elanga amekuwa kwenye kiwango bora sana tangu alipojiunga na Forest, huku huduma yake ikisakwa na timu nyingi, ikiwamo Newcastle United.
Benjamin Sesko – RB Leipzig
Kwenye ishu ya straika, Arsenal bado imeamua kubaki na machaguo mengi kwenye meza yake. Kwa muda mrefu kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi imekuwa ikifanya mchakato wa kumchagua nani kati ya Benjamin Sesko na Gyokeres. Fowadi huyo wa kimataifa wa Slovenia amekuwa na kiwango bora sana huko Leipzig na ndio maana Arsenal inapambania saini yake.
Noni Madueke – Chelsea
Kwa muda mrefu kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, Arsenal imekuwa ikihusishwa na mpango wa kusajili winga na kwenye hilo, imeripotiwa mkali wa Chelsea, Noni Madueke ni moja ya wakali inawataka. Orodha ya mawinga wanaotajwa ni wengi kuanzia Eberechi Eze, Nico Williams na Rodrygo, lakini Madueke anaweza kuwa chaguo jepesi na kunaswa huko Emirates.
Cristhian Mosquera – Valencia
Arsenal ilipeleka ofa moja na kugomewa na Valencia kwa ajili ya mchezaji Cristhian Mosquera, lakini haijakata tamaa bado ipo kwenye mazungumzo na klabu hiyo ya Hispania. Kinachoelezwa ni kwamba ada ya Pauni 17 milioni inaweza kufanikisha dili hilo la kunasa saini ya beki huyo Mhispaniola, Mosquera ili akapige mzigo huko Emirates.
Eberechi Eze – Crystal Palace
Kinachoripotiwa ni kwamba Arsenal ilikutana na mawakala wa Eberechi Eze wikiendi iliyopita kujadiliana uwezekano wa winga huyo kwenda kutinga uzi wa The Gunners msimu ujao. Kilichobaki kwa sasa ni kuzungumza na klabu yake ya Crystal Palace, ambayo bila shaka Arsenal itakutana na majibu kwamba Eze anauzwa Pauni 67.5 milioni, ambayo imebainishwa kwenye mkataba wake.
Viktor Gyokeres – Sporting CP
Straika huyo wa kimataifa wa Sweden, Gyokeres alishaweka wazi kwamba anataka kuachana na Sporting kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi na kutishia kugomea mazoezi katika timu hiyo endapo kama itagomea mpango wake wa kuondoka. Ripoti za karibuni zinadai kwamba ameshafikia makubaliano ya kujiunga na Arsenal, huku kocha Arteta akihitaji mchezaji huyo atue kabla ya Julai 19.
2) Christian Norgaard – Brentford
Mwanzoni ilionekana kama vile Brentford ingehitaji pesa zaidi kutoka Arsenal kwenye mauzo ya nahodha wao, Christian Norgaard, lakini sasa ada ya Pauni 10 milioni na nyongeza nyingine inaweza kukamilisha dili hilo. Brentford haionekani kuweka ngumu kwenye uhamisho wa mchezaji huyo tofauti na hali ilivyo kwa mkali wa Cameroon, Bryan Mbeumo.
1) Martin Zubimendi – Real Sociedad
Hii ilishabainishwa wazi kwamba ni suala la muda tu kabla ya kiungo Zubimendi kwenda kutambulishwa huko Emirates kwa sababu kila kitu kimeshakamilika. Lakini, hilo litaendelea kuthibitisha usiriazi wa Arsenal kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi ikijaribu kunasa mastaa wa maana ili kupambania mataji msimu ujao, huku ada ya Pauni 51 milioni ikidaiwa itatosha kumvuta Mhispaniola huyo huko Emirates katika dirisha hili la uhamisho la majira ya kiangazi.