Anna Mariana; Mwanamke 'anayetembea na moyo' wa Casemiro
Muktasari:
- Wakati Casemiro alipohamia Real Madrid 2013, Anna alikuwa naye bega kwa bega akimsaidia kuzishinda changamoto mpya za kucheza Ulaya kwa mara ya kwanza hadi aliposhinda mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na wababe hao wa LaLiga.
KIUNGO mahiri kutokea Brazil, Carlos Casemiro, 34, amejijengea heshima kubwa katika soka hasa kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata akiwa na Real Madrid kabla ya kuhamia Manchester United 2022.
Hata hivyo, nyuma ya mafanikio ya Casemiro kuna mwanamke ambaye amekuwa nguzo muhimu katika maisha yake naye ni Anna Mariana Casemiro, 37, mzaliwa wa Brazil pia.
Uhusiano wa wawili hawa ulianza 2011 nchini Brazil, wakati huo bado Casemiro anatafuta njia ya kutoboa katika soka la kulipwa ndani ya klabu ya Sao Paulo FC ambayo aliitumikia kwa takribani miaka minne ndipo akaenda Real Madrid.
Hivyo Anna alikuwa sehemu muhimu katika safari yake tangu mwanzo, hasa wakati ambao Casemiro alikuwa bado hajafikia mafanikio makubwa. Kulingana na vyanzo mbalimbali, uhusiano wao ulikua polepole kwa misingi ya upendo, heshima na kuaminiana.
Baada ya miaka mitatu ya uhusiano wao, hatimaye Casemiro na Anna walifunga ndoa hapo Julai 28, 2014 katika sherehe ya kifahari iliyofanyika Brazil ambayo ilihudhuriwa na ndugu, familia na marafiki wa karibu.
Sasa ikiwa ni miaka zaidi ya 10 ndani ya ndoa, mastaa hao wamefanikiwa kujenga familia yenye upendo na maelewano licha ya changamoto yenye ratiba ngumu, lakini bado Casemiro na Anna wamesalia kuwa mfano wa kuigwa kwa wengi.
Wawili hao walijaaliwa kupata watoto wawili; binti aitwaye Sara aliyezaliwa 2016 na mvulana aitwaye Caio aliyezaliwa 2021. Casemiro mara kadhaa amesema kuwa familia yake ndiyo chanzo kikubwa cha nguvu na motisha katika maisha yake ya ndani na nje ya uwanja.
Kwa mujibu wa Casemiro, katika safari yake ya soka, kwa miaka mingi Anna amekuwa zaidi ya mke kwani anasimama kama mshauri, rafiki na msaidizi wa karibu. Amekuwa akimuunga mkono katika kila hatua muhimu ya maisha yake ya kikazi tangu Amerika Kusini hadi sasa barani Ulaya.
Wakati Casemiro alipohamia Real Madrid 2013, Anna alikuwa naye bega kwa bega akimsaidia kuzishinda changamoto mpya za kucheza Ulaya kwa mara ya kwanza hadi aliposhinda mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na wababe hao wa LaLiga.
Vilevile, alipofanya uamuzi mkubwa na wa muhimu wa kujiunga na Manchester United mwaka 2022, Anna aliendelea kumuunga mkono kwa kila hali na mara nyingi amekuwa akionekana uwanjani kusherehekea pamoja naye ushindi wa timu anayoichezea kwa wakati huo.
Anna haiishi tu kumuunga mkono Casemiro, bali pia humkingia kifua pale anapoona inabidi, mathalan ni pale mumewe alipokosolewa kwa madai ya kutojituma vilivyo ndani ya Manchester United, yeye Anna alijibu hilo akiposti picha za mataji yote aliyoshinda, akiwakumbusha mashabiki mafanikio makubwa ya Casemiro.
Kwa wengi, hatua hiyo ilionyesha uaminifu na upendo wake kwa mume wake, pamoja na uwezo wake wa kusimama imara katika nyakati za changamoto na kuja na suluhisho. Katika ulimwengu wa soka ambao umetawaliwa na presha na ushindani, uwepo wa Anna katika maisha ya Casemiro ni faida kubwa.
Hivi karibuni baada ya kuweka wazi kuwa ameongeza mwaka mmoja wa kusalia Manchester United, Casemiro akizungumza na tovuti rasmi ya klabu hiyo amesema anajisikia furaha sana hasa kwa upendo wa mashabiki na heshima wanayompa.
"Nashukuru kwa mapenzi haya, inanigusa sana. Natumaini sitalia siku yangu ya mwisho, kwa sababu umekuwa ni wakati mzuri mimi kuwa hapa," amesema na kuongeza:
"Mke wangu tayari alilia siku mashabiki walipokuwa wanaomba nibakie kwa mwaka mmoja zaidi. Ninachotaka sasa ni kufurahia kila wakati ambao nipo hapa, na nitabaki kuwa shabiki wa United maisha yangu yote."
Lakini, mke wa Casemiro ni nani hasa? Anna Mariana alizaliwa Julai 12, 1989 nchini Brazil, ni mwanamke mwenye elimu akiwa amehitimu shahada ya usimamizi wa biashara. Mbali na elimu yake, amejijengea sifa kama mjasiriamali wa urembo na vipodozi.
Licha ya kuwa mke wa staa mkubwa wa soka, Anna ameweza kusimama kivyake kikazi. Amefanikiwa kuendesha biashara zake na kujijengea picha nzuri kwenye mitandao ya kijamii, hasa Instagram, ambako huposti maisha yake ya kila siku, familia na kazi yake.