Penzi la Araujo, Abigail lilianzia kanisani
Muktasari:
Wawili hao ambao tayari ni wazazi wa watoto wawili wa kike, Aitana (2021) na Adara (2024), wamekuwa pamoja tangu mwaka 2016 baada ya kukutana kanisani, hivyo familia yao wameijenga pia katika msingi wa imani.
BEKI wa kimataifa wa Uruguay, Ronald Araujo, 26, ni miongoni mwa wachezaji muhimu katika kikosi cha Barcelona. Mbali na mafanikio ya uwanjani, maisha yake binafsi yanavutia watu hasa uhusiano wake na mkewe Abigail Olivera.
Wawili hao ambao tayari ni wazazi wa watoto wawili wa kike, Aitana (2021) na Adara (2024), wamekuwa pamoja tangu mwaka 2016 baada ya kukutana kanisani, hivyo familia yao wameijenga pia katika msingi wa imani.
Abigail Olivera, 26, ni mwanamke mrembo kutokea Uruguay kama mumewe, lakini licha ya kuishi maisha ya kifahari, haonekani sana hadharani na pia si mtu anayejishughulisha mara kwa mara na mitandao ya kijamii.
Mrembo huyo alizaliwa Septemba 18, 1999, hivyo ana umri wa miaka 26, umri unaokaribiana na mume wake Araujo, ambaye alizaliwa Machi 7, 1999.
Kazi yake ni ubunifu wa mapambo ya ndani ya nyumba (interior designer), hivyo ni mtaalamu wa kupanga na kupamba sehemu mbalimbali ndani ya nyumba ili ziwe na muonekano wa kuvutia.
Mbali na kazi yake, Abigail pia anapenda sana mitindo ya mavazi. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, wafuasi wake wengi wameweza kupata mawazo ya mitindo mizuri kutokana na namna anavyovaa.
Abigail ambaye amejipambanua kama mtu anayependa maisha ya utulivu na faragha, hajatoa taarifa nyingi kuhusu wazazi wake wala ndugu zake, jambo linalofanya maisha yake binafsi kubaki kuwa siri.
Sasa picha linaanza mnamo Januari 2025, ambapo Araujo anasaini mkataba mpya ambao utamweka Barcelona hadi 2031, na siku hiyo hiyo ndipo alipomvisha Abigail pete ya uchumba!
Ikumbukwe beki huyo aliyesajiliwa na Barcelona B mwaka 2018 akitokea klabu ya Boston River ya Uruguay, tangu wakati huo ameendelea kukua na kuwa sehemu muhimu ya kikosi cha wababe hao wa Catalonia.
Uwezo wake ndani na nje ya uwanja umevutia wachambuzi wengi wa soka la Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), ambao wanasema hatima yake imebeba mambo makubwa kwa kasi anayoendelea nayo.
Kabla ya kutua Barcelona, tayari Araujo alikuwa amefahamiana na Abigail tangu mwaka 2016, na walikutana wote wakiwa na umri wa miaka 16. Kinachofanya hadithi yao iwe ya kipekee ni mahali walipokutana kwa mara ya kwanza kanisani.
Abigail mwenyewe ndiye alieleza jambo hilo katika mjadala wa maswali na majibu aliyoufanya kwenye mitandao yake ya kijamii, ambapo alisimulia chanzo cha uhusiano wake na beki huyo.
“Tulikutana kanisani tulipokuwa na umri wa miaka 16,” alijibu Abigail. Ujumbe huo mfupi unaeleza mengi kuhusu maisha yao kama wanandoa, ukiwatambulisha kama watu wenye imani na wenye kujitoa.
Ni wazi kuwa dini na mambo ya kiroho ni nguzo muhimu katika maisha yao wote wawili tangu awali kabisa, hivyo kukutana kwao katika mazingira ya imani kulikuwa mwanzo wa uhusiano ulio imara.
Katika maswali na majibu hayo hayo, Abigail alitaja mstari anaoupenda zaidi kutoka katika Biblia: “Kwa wale wanaompenda Mungu, Mungu amewaandalia mambo ambayo hakuna mtu aliyewahi kuyaona, kuyasikia wala kuyawaza.”
Vilevile alijibu maswali mengine kuhusu maisha yake binafsi. Alipoulizwa kama wanapanga kuongeza watoto zaidi, alijibu; Sio kwa sasa. Alipoulizwa kuhusu ndoto zake maishani, alisema angependa kuja kuisaidia jamii.
“Ningependa kusaidia zaidi watu wenye uhitaji, kuwa na shirika lisilo la kiserikali au taasisi ya kusaidia watu,” alisema Abigail, kauli inayoonyesha kuwa ana moyo wa kujitolea.
Katika ulimwengu wa soka ambapo mara nyingi huzungumzwa zaidi mafanikio na migogoro kuliko maadili, Abigail na Araujo ni mfano mzuri wa maisha yenye utulivu.
Baada ya kuvishwa pete ya uchumba hapo Januari 2025, Abigail aliposti mtandaoni picha za tukio hilo akishukuru kwa hatua hiyo na kueleza kuwa jibu lake lilikuwa yes, yaani ndiyo, nimekubali.
Hatimaye Julai 21, 2025, Araujo na Abigail wakafunga ndoa katika kanisa la Methodist jijini Montevideo, na harusi yao ilikuwa ya faragha, ikihudhuriwa na marafiki wa karibu na familia.
Harusi yao ilikuwa tukio lililovutia wengi. Abigail alivaa gauni la kifahari lililotengenezwa kwa ustadi mkubwa huku likipambwa kwa maua na vito. Wawili hao walitangaza rasmi ndoa yao kupitia Instagram kwa kuandika; Just married.
Ikumbukwe walifunga ndoa wakiwa tayari wana watoto wao wawili ambao kupitia mitandao ya kijamii wamekuwa wakionekana mara nyingi katika picha za familia wakifurahia maisha pamoja na wazazi wao.