Afya ya mifupa kwa mwanasoka
Muktasari:
- Katika kupambana huko wapo wachezaji kadhaa ambao walipata majeraha mabaya ambayo yalichangia kutolewa nje na nafasi zao zikachukuliwa na wengine.
KATIKA mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya zilizochezwa jana na juzi zimeshuhudia ubora wa wachezaji wenye viwango vya juu wakichuana na wapinzani ambao wana viwango kama vyao. Mojawapo wa michezo mikali ulichezwa juzi, Jumanne, usiku, PSG ilipoibamiza Barcelona mabao 4-2. Ushindi huo haukuwa rahisi kwani wachezaji wa pande zote mbili walijiituma sana.
Katika kupambana huko wapo wachezaji kadhaa ambao walipata majeraha mabaya ambayo yalichangia kutolewa nje na nafasi zao zikachukuliwa na wengine. Wachezaji hao waliopata majeraha ni beki wa kati wa PSG, Morquinhos na winga wa kushoto, Kvaratskhelia ambaye inaelezwa majeraha yake ni mabaya. Wote tunafahamu kuwa mchezo wa soka unahusisha kukumbana kimwili, ndio maana huwa ni vigumu kukosekana kwa majeraha yatokanayo na michezo.
Leo jicho la kitabibu litaangazia afya ya mafupa kwa wanasoka kwani mifupa ndio inayotoa nafasi kwa misuli kujipachika na kuwa egemeo kuu kwa misuli na viungo vingine ikiwamo nyuzi za ligament na tendoni. Kadiri mchezaji anavyoshiriki mazoezi na michezo ndivyo pia anavyoimarisha afya ya mifupa. Ingawa hatari ya kupata majeraha ya mifupa ikiwamo mivunjuko, kuteguka na majeraha ya maungio iko pale pale.
Majeraha ya mifupa yanaweza kusababisha na mwili kupata shinikizo kubwa au kukanyagwa au kuchelewa faulo ya moja kwa moja. Kuwa na mifupa yenye afya kunaifanya kustahimili majeraha.
AFYA YA MIFUPA
Mifupa ni tishu ngumu ambayo ndiyo inasaidia mwili kuweza kuweka umbile la mwili kwa ajili ya viungo vingine kujipachika na kujihifadhi. Ukomo wake wa ukuaji ni miaka 25. Mwili wa mwanadamu una takribani mifupa 206, kati ya hiyo mifupa 26 ni ya miguuni na 54 ya mikononi ambayo ndiyo inayopata majeraha mara kwa mara kwa wanamichezo.
Mifupa ndiyo inamwezesha mwanamichezo kufanya kila kitu wakati wakucheza au kufanya mazoezi. Hii ni kutokana na misuli imejipachika katika mifupa na kutengeneza umbile la mwili.
Wakati misuli inapovutika na kujirefusha ndipo mwili huweza kutenda matendo mbalimbali ikiwamo kutembea, kukimbia na kuruka.
Ugumu wa mfupa ndiyo unaowezesha ubongo, moyo na mapafu kuwa salama kutokana na mwili kuzipa hifadhi na kuwa kama ndiyo ngao.
Vilevile ndani ya mifupa hutengenezwa seli zote za mwilini, kuhifadhi na kudhibiti madini mbalimbali ambayo ni muhimu kwa shughuli za mifumo ya mwili. Mifupa huweza kupata majeraha mbalimbali ikiwamo kuvunjika, kuteguka, kumomonyoka na kushambuliwa na magonjwa mbalimbali hivyo kuweza kuathiri utendaji wake.
Wanasoka wako katika hatari zaidi ya kupata mivunjiko ya mifupa hii kwa sababu wanatumia nguvu nyingi, wanakukumbana kimwili wakati wakucheza na huku wakipata ajali za kimichezo.
Mwanamichezo anaweza kuboresha mifupa yake kwa kuhakikisha anazingatia lishe mchanganyiko ambayo imependekezwa na wataalam lishe za wanamichezo, kuwa na mienendo na mitindo rafiki inayomwepusha na majeraha ya mifupa.
FANYA HAYA WAKATI UUGUZI MAJERAHA
Yapo mambo mbalimbali yameonekana kusaidia kuboresha uimara wa mifupa wakati wa kipindi cha uuguzi wa majeraha ya mifupa kwa wanamichezo. Mosi, ulaji wa mlo kamili na virutubisho vya ziada ni muhimu katika uponaji na ukuaji wa mifupa kwani husheheni vitamini, madini mbalimbali na protini ambavyo vyote vinahitajika katika ujenzi wa mifupa bora.
Mjeruhiwa ale zaidi mboga za majani, matunda na protini ya inayopatikana katika minofu ya samaki na nyama au jamii ya kunde.
Anywe maji mengi glasi 8-10 au lita 1.5-3 kwa siku, maji ndiyo yanayosaidia shughuli zote za mwili na pia kuupa mwili madini yanayoimarisha mifupa.
Mbili, uzito wa mwili ni lazima udhibitiwe kwa kuzingatia maelekezo ya lishe toka kwa wataalam wa lishe za wanamichezo. Muhimu kuepuka ulaji wa vyakula vya sukari, wanga na mafuta mengi.
Tatu, epuka matumizi ya tumbaku na vilevi ikiwamo pombe kwani hudhoofisha mwili na hatimaye kuingilia ukuaji wa mifupa kwani sumu za tumbaku hunyausha mishipa ya damu hivyo kuzuia damu kwenda kwa wingi katika eneo lenye mfupa wenye jeraha.
Nne, kwa aliyevunjika na kupewa matibabu ikiwamo ya bila upasuaji na upasuaji atahitajika kupumzika muda mwingi ili kuepukana na mtikisiko.
Kama ni mifupa ya mkono au mguu ndiyo iliyovunjika unyanyuaji wa vitu vizito au kuukanyagio mguu inahitajika kuepukwa kwani unapoupa shinikizo la uzito mfupa uliovunjika kabla ya kupona vizuri unaweza kusababisha mfupa huo kutounga vyema.
Tano, dhibiti matumizi holela ya dawa za maumivu ikiwamo zenye steroidi na zile zakufifisha mapigo ya kinga ya mwili kwani zina athiri ukuaji na uimara wa mifupa. Sita, epuka mambo ambayo yanaweza kukupa msongo wa mawazo kwani hali hiyo inashusha kinga ya mwili ambayo ni muhimu kipindi cha uponaji.
CHUKUA HII
Uimara wa mifupa ni muhimu kwa mwanamichezo, hivyo ni vyema kushikamana na mambo haya, kuzingatia ushauri wa daktari wa timu na mtaalamu lishe za wanamichezo. Tumia vyema fursa ya kuwa nchini Tanzania, kwa kutumia vyakula vya asili vinavyopatikana maeneo mbalimbali ambavyo vimesheheni viinilishe kwa wingi.