Senegal yamtimua kocha Pape Thiaw
Muktasari:
- Thiaw aliyekiinoa kikosi cha Simba Teranga tangu Desemba 2024, alishindwa kuiongoza Senegal kufanya vizuri katika mashindano hayo baada ya kupoteza mechi mbili za mwanzo za Kundi dhidi ya Ufaransa na Norway.
DAKAR, SENEGAL: SHIRIKISHO la Soka la Senegal (FSF) limemfuta kazi kocha mkuu Pape Thiaw kufuatia kushindwa kwa timu hiyo kuvuka hatua ya 32 Bora kwenye Kombe la Dunia 2026.
Thiaw aliyekiinoa kikosi cha Simba Teranga tangu Desemba 2024, alishindwa kuiongoza Senegal kufanya vizuri katika mashindano hayo baada ya kupoteza mechi mbili za mwanzo za Kundi dhidi ya Ufaransa na Norway.
Hata hivyo, Senegal ilifufua matumaini kwa kuichapa Iraq mabao 5-0 katika mchezo wa mwisho wa makundi na kufuzu hatua ya mtoano kama moja ya timu bora zilizomaliza nafasi ya tatu.
Safari yao iliishia kwa maumivu katika hatua ya 32 Bora walipokutana na Ubelgiji. Senegal ilikuwa mbele kwa mabao 2-0, lakini ilipoteza dira dakika za mwisho kwa kuruhusu mabao mawili ya kusawazisha kabla ya kufungwa kwa penalti katika dakika za nyongeza na kupoteza mchezo huo 3-2.
Baada ya kipigo hicho, kiungo Pape Gueye alitangaza kuwa atasitisha kwa muda kuitumikia timu ya taifa ya Senegal ikiwa benchi la ufundi lingeendelea kubaki madarakani.
Katika taarifa rasmi, FSF ilieleza kuwa uamuzi wa kumtimua Thiaw umefikiwa baada ya kufanya tathmini ya kina kuhusu matokeo ya timu pamoja na mustakabali wa kikosi hicho.
"Baada ya tathmini ya kina ya matokeo ya timu ya taifa na mwelekeo wake wa baadaye, Shirikisho limeamua kumaliza ushirikiano na kocha Pape Thiaw kwa maslahi mapana ya soka la Senegal," ilieleza taarifa hiyo.
Sakata la AFCON bado halijaisha
Kuondolewa kwa Thiaw kunakuja miezi michache baada ya kuhusika katika sakata kubwa la Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Senegal ilikuwa imetwaa ubingwa huo uwanjani, lakini baadaye ilinyang'anywa taji na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutokana na tukio la utata lililotokea kwenye fainali dhidi ya Morocco.
Katika dakika za mwisho za mchezo huo, Morocco ilipewa penalti ya utata, hatua iliyomfanya Thiaw kuwaamuru wachezaji wake watoke uwanjani kupinga uamuzi wa mwamuzi.
Baada ya kusimama kwa takribani dakika 17, Senegal ilirejea uwanjani. Brahim Diaz alikosa penalti hiyo, kisha Pape Gueye akaifungia Senegal bao la ushindi katika muda wa nyongeza.
Hata hivyo, mwezi Machi, CAF ilibatilisha matokeo ya fainali hiyo na kuitangaza Morocco kuwa mabingwa rasmi, ikieleza kuwa kitendo cha Senegal kutoka uwanjani kilikiuka kanuni za mashindano.
Kwa sasa, Senegal imewasilisha rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ikitarajia kurejeshewa ubingwa wake wa AFCON, huku ikianza pia ukurasa mpya baada ya kumtimua Thiaw.