AFCON 2027 tuige tunayoyaweza Morocco
Muktasari:
- Ni fainali ambazo wengi tunakubaliana kwamba ndio bora zaidi kulinganisha na nyingine za hapo nyuma na sio kwamba tunazibeza ila kiukweli Morocco wamefanikiwa.
TUMEWAONA Morocco namna walivyoziandaa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazoendelea hivi sasa zikisubiria hatua ya 16 bora.
Ni fainali ambazo wengi tunakubaliana kwamba ndio bora zaidi kulinganisha na nyingine za hapo nyuma na sio kwamba tunazibeza ila kiukweli Morocco wamefanikiwa.
Viwanja vyao ni vya hali ya juu kiasi ambacho kinafanya boli litembee na timu zionyeshane uwezo wa kimbinu na kiufundi hata pale ambapo mvua inanyesha.
Walioenda huko na hata taarifa kutoka vyombo mbalimbali vya habari zinatuonyesha kuwa wenyeji wamewapa mapokezi mazuri wageni na mastaa wa timu nyingi zinazoshiriki mashindano hayo wamesifu namna Morocco ilivyojiandaa kwa ajili ya mashindano hayo.
Kwa namna hapa kijiweni tunavyotazama fainali za AFCON 2025 zinazoendelea Morocco, tunaona kama jamaa wanatupa deni na kutuchonganisha sisi ambao tutaandaa fainali zinazofuata kwa maana ya AFCON 2027.
Katika hiki kipindi cha muda uliobaki kabla ya fainali zitakazofuata za AFCON, tunapaswa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha viwanja vyetu na miundombinu mingine inakamilika kwa wakati na inakuwa na ubora stahiki.
Sio lazima tuwe kama Morocco kwa vile wao wenzetu wametuacha mbali kiuchumi lakini tunapaswa viwe na ubora wa kuchezeka kulingana na vigezo ambavyo CAF imeviweka katika matumizi ya viwanja.
Lakini kitu kingine cha muhimu ni kuhakikisha tunashawishi watu wahamasike na washiriki kwa idadi kubwa katika fainali zijazo za AFCON ili ziweze kuwa na vaibu ambalo tunaweza kulitumia kama jambo la kujivunia.
Jambo ambalo tunapaswa kulizingatia ni kwamba aibu au sifa za kuandaa AFCON 2027, zitaenda kwa nchi na sio mtu mmoja.