Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga v Ruvu Ilikuwa shoo shoo!

Yanga v Ruvu Ilikuwa shoo shoo!

MASHABIKI wa Yanga wana kila sababu ya kutembea vifua mbele kutokana na jinsi chama lao linavyowapa raha baada ya juzi kupata ushindi wa tano mfululizo katika Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting.

Katika mchezo huo uliokuwa mkali uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Yanga ilizidi kuimarika kwani ni mara ya kwanza msimu huu katika ligi na mechi za mashindano kupata ushindi wa zaidi ya mabao mawili.

Ushindi huo umeifanya kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha pointi 15 na mabao tisa ya kufunga na kuruhusu bao moja ikiwafanya mashabiki wake kuwatambia wenzao wakijinadi huu ni msimu wao wa kurejesha ufalme na mataji yaliyowakimbia kwa misimu minne mfululizo.

Licha ya kupata ushindi huo, lakini mechi ya juzi Yanga ililazimika kupambana kwani wapinzani Ruvu Shooting walionekana wamepania kuwatibulia kwa bao la mapema, lakini kosa la nahodha wao, Santos Mazengo kumchezea vibaya Fiston Mayele na kulimwa kadi nyekundu liliwapa mwaya Yanga kusawazisha na kuongeza mengine yaliyoihakikishia pointi tatu.

Kilichowatia kiburi wana Yanga ni namna kikosi kwa sasa kilivyo kipana kiasi kwamba mchezaji yeyote akikosekana hakuonyeshi pengo tofauti na ilivyokuwa misimu kadhaa iliyopita - yaani nje mtiti na ndani mtiti.


DJIGUI ACHAFUA REKODI

Kipa Diara Djigui ambaye alicheza mechi nne bila kuruhusu bao kwenye mchezo wa tano alijikuta akiruhusu nyavu ziguswe kupitia bao la Shaban Msala aliyefunga mapema tu.

Msala alifanya hivyo kwa shuti la chinichini lililombabatiza Kibwana Shomary na kuubadilishia mwelekeo wa mpira ulioingia wavuni. Mapema hadi jana jioni kipa pekee aliyekuwa hajaruhusu bao alikuwa Aishi Manula wa Simba.


MUKOKO AREJEA, ATUPIA

Kiungo Mukoko Tonombe alirejea kwa mara ya kwanza kikosini tangu alipoonekana mara ya mwisho uwanjani kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Azam dhidi ya Simba alikoonyeshwa kadi nyekundu.

Mukoko alicheza kama kiungo mchezeshaji na kuwa kwenye bato zito na kiungo wa Ruvu Shooting, Ally Kombo ambaye alikuwa anacheza naye bega kwa bega.

Licha ya kuwa katika ulinzi mkali, Mukoko alifunga bao wakati huohuo kwenye kiungo alikuwa anasaidiana na Yannick Bangala eneo la ukabaji kuhakikisha anakuwa huru kufanya kazi yake.


RUVU YAPAKI BASI

Kitendo cha beki wa Ruvu Shooting, Santos Mazengo kulimwa kadi nyekundu dakika ya 23 kiliwafanya wenzake wacheze kwa woga ili wasiruhusu mabao mengi zaidi.

Kucheza kwao kwa kurudi nyuma kulichangia Yanga kupata wakati mzuri kushambulia kwa sababu walikuwa wanapeleka mashambulizi mara kwa mara, huku Ruvu wakifanya yale ya kushtukiza.

Yanga ilipata bao la pili na la tatu kutokana na Ruvu kucheza zaidi nyuma ikijilinda na kuwafanya wapinzani wao kuwachezesha nusu uwanja baada ya mabeki kusogea mpaka katikati.


SAIDO NDO HIVYO

Kufuatia Yacouba Sogne kuumia katika mchezo huo dakika ya 30 kulimfanya Saido Ntibazonkiza aingie na kucheza kushoto.

Saido inakuwa ni mara ya kwanza kuonekana na jezi ya Yanga msimu huu katika ligi, lakini bado alionyesha umahiri wake wa kupiga pasi na spidi ya kuingiza mashambulizi ndani ya boksi.

Majeraha ya goti aliyoyapata Yacouba hata kama yakiwa makubwa kwa uwezo aliouonyesha Saido bila shaka mchezaji huyo amejihakikishia kurejea katika kikosi cha kwanza.


BRYSON GARI LIMEWAKA

Beki wa kushoto David Bryson aliingia katika mchezo huo akichukua nafasi ya Kibwana Shomari dakika ya 65 ili kwenda kuongeza mashambulizi na alifanikiwa.

Bryson alionyesha umakini kupeleka mbele mashambulizi mara kwa mara akitokea kushoto na ubora wake ulikuwa katika kupiga krosi zenye macho ndani ya boksi. Urejeo wa spidi kwa Bryson kunazidi kuweka wakati mgumu kwenye timu hiyo kwa sababu yupo Kibwana ambaye ameonyesha kiwango bora sawa na Adeyum Saleh wakati huohuo Yassin Mustapha anarejea kutoka majeruhi.


CHILAMBO HABARI NYINGINE

Beki wa Ruvu Shooting, Nathaniel Chilambo alionyesha umahiri kupeleka mashambulizi mbele akitokea kulia na alionekana kumzidi spidi mara kwa mara Kibwana.

Chilambo alionyesha pia umahiri kuchezea mpira hasa katika kipindi cha kwanza baada ya kupiga chenga mara kwa mara huku akisonga mbele kwenda kupeleka mashambulizi katika kipindi cha kwanza.

Pia, kipindi cha pili beki huyo alipotea lakini ilipofika dakika ya 60 walipoanza kushambulia alirejea katika uchezaji wake akipeleka mashambulizi hali iliyowalazimu Yanga kumuingiza Bryson ambaye naye ni mzuri kwenye kushambulia na kumfanya Chilambo apunguze kushambulia.


NABI AFUNGUKA

Kocha mkuu wa Yanga, Nesreddine Nabi alisema kikosi chake kinazidi kuimarika kadri siku zinavyokwenda mbele na wachezaji wote wana nafasi ya kucheza.

Nabi alisema amefurahishwa na kiwango cha Bryson aliyeingia na kushambulia vizuri akitokea kushoto uwanjani.

“Wachezaji wote ni wazuri na wameonyesha kiwango kizuri. Bryson ni mzuri kwenye kushambulia na alifanya hivyo alivyoingia uwanjani. Hata upande wa Saido naye pia ameonyesha kitu,” alisema Nabi.

Akizungumzia upande wa timu yake kuruhusu bao, Nabi alisema: “Ni jambo la kawaida kuruhusu bao, lakini kikubwa hatujapoteza katika mchezo huu na tumepata pointi tatu muhimu, ila pia tumeongeza mabao ya kufunga leo.”


WASIKIE WADAU

Aliyekuwa katibu mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Angetile Osiah alisema kocha Nabi ana uwezo wa kutambua kipaji cha wachezaji wake na ndicho ambacho kinamsaidia katika kuwabadilisha inapohitajika kufanya hivyo.

Akizungumzia mabadiliko ya timu kucheza kandanda safi, alisema hilo limetokana na kocha kupata wachezaji sahihi katika kila eneo na kazi yake kufanikiwa.

“Msimu huu wamepata wachezaji wazuri na ndio maana unaona Yanga wanacheza mpira. Msimu uliopita walikuwa wanatumia zaidi mipira mirefu, lakini msimu huu Aucho (Khalid) na Bangala (Yanick) wameituliza timu kwa kuichezesha,” alisema.

Naye aliyekuwa meneja wa zamani Azam, Philip Alando alisema Nabi anastahili pongezi kwa sababu ukiachana na ushindi ambao Yanga wanaupata, kocha huyo anainua wachezaji wa kawaida na kung’ara kikosini.

Alando alisema hakukuwa na mtu anayejua Kibwana anaweza kucheza upande wa kushoto, lakini alimpa nafasi na mchezaji huyo amepambana kuonyesha uwezo mkubwa, kwani kama angebaki kulia inawezekana angekosa nafasi.

“Farid Mussa na yeye anazidi kuimarika kadri siku zinavyokwenda mbele, tofauti na alivyokuwa katika msimu uliopita na hapa ndio unaona anazidi kuwabadilisha wachezaji,” alisema Alando.

“Yanga kwa sasa hakuna mchezaji anayejiona mkubwa bali kila mtu yupo sawa na mwenzake, wakiwa uwanjani wanacheza soka la kuvutia na hata mashabiki ndio maana wanaenda kuwaangalia.”