Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Misimu 15 ya Azam Bara sio mchezo

LIGI Kuu Bara msimu wa 2023-2024 unatarajiwa kuanza kati ya Agosti na Septemba ikishirikisha jumla ya timu 16, zikiwamo tatu zilizopanda daraja kutoka Ligi ya Championship. Timu hizo zilizopanda daraja ni JKT Tanzania, Kitayosce (itakayofahamika kama Tabora United) na Mashujaa, ambap zinaunga na watetezi, Yanga, Simba, Azam, Singida Big Stars (itakayofahamika kama Singida Fountain Gate), Namungo, Geita Gold, Ihefu, Kagera Sugar, Tanzania Prisons, Dodoma Jiji, KMC, Mtibwa Sugar na Coastal Union zilizoishiriki ligi ya msimu uliopita.

Huu utakuwa ni msimu wa 60 tangu kuasisiwa kwa Ligi ya Bara mnamo mwaka 1965, huku Yanga ikiendelea kushikilia rekodi ya kutwaa mara nyingi taji la michuano hiyo ikibeba mara 29, ikifuatiwa na Simba ilitobeba mataji 22, ikifuatiwa na Mtibwa Sugar yenye mawili.

Timu nyingine zilizobeba mataji ya ligi katika misimu 59 iliyopita ni pamoja na Mseto, Pan African, Tukuyu Stars ya Mbeya, Coastal Union na Azam FC.

Azam ndio klabu ya mwisho nje ya Simba na Yanga kubeba ubingwa na ikifanya hivyo msimu wa 2013-2014 ikitwaa bila kupoteza ikiifikia rekodi iliyokuwa imewekwa na Simba 2009-2010 ambayo nayo ilibeba taji bila kupoteza kabla ya Yanga kuifikia nao misimu miwili iliyopita.

Kama hujui Azam ilipanda Ligi Kuu msimu wa 2008-2009 baada ya kufanya kweli kwenye Ligi ya Taifa mwaka 2007 ilipoifumua Majimaji kwa mabao 2-0  katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma, moja ya vituo viwili vilivyotumiwa kwenye ligi hiyo kwa msimu huo. Kituo kingine cha ligi hiyo kilikuwa mkoani Mara, ambapo Villa Squad ya Kinondoni ilipanda kupitia huko na kuungana na Azam kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza 2008-2009.


MABAO YA BOCCO
Kwa wasiokumbuka kituo cha Dodoma kilikuwa na timu za Kijiweni Mbeya, Majimaji Songea, Azam na Mbagala Market (sasa African Lyon), ilihali kituo cha Musoma, Mara kilikuwa na timu za AFF Arusha, Villa Squad, Polisi Tabora na Mwanza United.

Azam ilianza kwa kulazimishwa suluhu na Mbagala Market, ikaifumua Kijiweni kwa mabao 3-0 kisha ndipo ikavaana na Majimaji katika mechi iliyopigwa Julai 27, 2007 na mabao mawili na John Bocco 'Adebayor'.
Bocco kabla ya kusajiliwa Azam alikuwa akiichezea Cosmopolitan katika Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam ambapo Azam iliifungwa mabao 2-0 timu hiyo kwenye pambano lililopigwa Uwanja wa Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, mabao yakiwekwa na Bocco, lakini Cosmo ilishindwa kuizuia Azam isiende Dodoma.

Umahiri wa straika huyo ngongoti aliyekuwa moto kwenye Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam iliwafanya Azam imsajili kuongeza nguvu kwenye mechi za Ligi ya Taifa na usajili huo ulilipa kwa nyota huyo kuifungia mabao mawili yaliyoipandisha timu hiyo Ligi Kuu Bara msimu wa 2008-2009.

Bocco alifunga mabao hayo kwa friikikii na kuifanya Azam kumaliza mechi za kituo hicho ikiwa na pointi saba na kuungana na Villa kupanda Ligi Kuu zote zikiwa ni kwa mara ya kwanza kwao kwa msimu huo.

Tangu ilipopanda daraja Azam haijawahi kushuka na msimu uliomalizika hivi karibuni, ulikuwa ni wa 15 kwao katika Ligi Kuu, huku ikifanikiwa kubeba taji mara moja tu msimu wa 2013-2014 na mawili ya Kombe la Kagame ikifanya hivyo 2015 na 2018.
Lakini imebeba taji moja la Kombe la FA (sasa ASFC) 2018-2019 kwa kuicharaza Lipuli FC kwa bao 1-0 lililofungwa na Mzambia Obrey Chirwa, pia imenyakua Ngao ya Jamii mara moja ilipofunga Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-1 baada ya sare ya mabao 2-2 na imebeba Kombe la Mapinduzi mara tano ikiwa ni rekodi kwenye michuano hiyo. Azam ilibeba taji hilo mwaka 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019.

KIKOSI KAZI
Azam imedumu katika Ligi Kuu kwa misimu yote 15 na kufanikiwa kubeba mataji 10 ya michuano mbalimbali, kwa kazi kubwa iliyofanya na kikosi kazi kilichoipandisha daraja ndani ya mwezi kama huu, lakini mwaka 2007.

Katika mechi ile ambayo Bocco alitupia mabao mawili na kuibeba Wanalambalamba katika Ligi Kuu kikosi kiliundwa na wachezaji wafuatao; Idd Abubakar, Malika Ndeule, Paulo Nyangwe a.k.a Mitindo, Luckson Kakolaki, Boniface Pawasa aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho, Adam Ngido ‘Popa’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Steven Nyenge, John Bocco ‘Adebayor’, Kassim Kilungo na James Adriano, huku kocha akiwa ni Mohammed Seif 'King' nyota wa zamani wa kimataifa aliyewahi kuwika na Small Simba akisaidiwa na Habib Kondo.
Ni Bocco na Sure Boy ambao wote walioongezwa kwenye kikosi cha Azam kilichofuzu fainali ya Ligi ya Taifa msimu huo wa 2007 na wote kusaidia kuipandisha daraja, ndio pekee kwa sasa wanaocheza soka la ushindani.

Bocco akiwa ndiye nahodha wa Simba, aliyojiunga nayo misimu sita iliyopita baada ya kuitumikia Azam kwa misimu tisa mfululizo hadi 2017-2018 alipohama kwenda Msimbazi sambamba na kipa Aishi Manula, Erasto Nyoni na Shomary Kapombe. Manula na Kapombe bado wapo Simba, wakati Nyoni amepewa 'Thank You' hivi karibuni na tayari ameshasajiliwa na Namungo kwa msimu wa 2023-2024.

Katika misimu sita ya kukipiga Msimbazi, Bocco amenyakua mataji manne ya Ligi Kuu Bara, Kombe la ASFC mara mbili, Ngao ya Jamii mara tatu na Kombe la Mapinduzi mara moja.
Kwa upande wa Sure Boy kwa sasa anakipiga Yanga, baada ya kusajiliwa kupitia dirisha dogo la misimu miwili iliyopita, akiwa ameitumikia Azam kwa misimu 13 na nusu mfululizo.
Katika misimu miwili ndani ya Yanga, kiungo mshambuliaji huyo, amenyakua mataji mawili ya Ligi Kuu, mawili ya ASFC, Ngao ya Jamii (2) na Kombe la Mapinduzi mara moja.
Wachezaji wengine walioipandisha daraja Azam pale Jamhuri, Dodoma wengi wamestaafu na kugeukia ukocha akiwamo Idd Abubakar, Boniface Pawasa, huku Kakolaki akiwa ni Meneja wa sasa wa timu hiyo iliyoamaliza nafasi ya tatu msimu uliopita na kukata tiketi ya michuano ya CAF.

MSIMU 15 YA KIBABE
Rekodi zinaonyesha tangu Azam ilipopanda daraja ni mara moja tu katika msimu wa kwanza tu wa Ligi Kuu Bara 2008-2009 ndio ilimaliza nje ya Nne Bora. Katika msimu huo wa kwanza pengine kwa ugeni wa ligi hiyo ilijikuta ikimaliza nafasi ya nane kwa kukusanya pointi 26 tu kupitia mechi 22.
Baada ya hapo Azam ilirudi kwa msimu wa pili wa ligi hiyo kwa kuzishtua klabu kongwe zilizokuwa kwenye msimu huo kwa kumaliza nafasi ya tatu, ikikusanya jumla ya pointi 33 katika mechi 22 ikizidiwa ujanja na Simba iliyobeba ubingwa bila kupoteza na Yanga ilikuwa ya pili.
Msimu wa tatu wa Azam iliendelea kuganda nafasi ya tatu nyuma ya Yanga iliyobeba ubingwa na Simba iliyokamata nafasi ya pili. Azam ilivuna jumla ya pointi 43 kwa idadi ya mechi 22 na ikaenda kujipanga vyema na iliporudi kwenye msimu wa nne wa 2011-2012 walipindua meza ikimaliza ya pili.
Katika msimu huo ambao Simba ilirejesha tena taji kutoka kwa Yanga iliyomaliza nafasi ya tatu, Azam ilikusanya jumla ya pointi 56 katika mechi 26 na katika msimu wa tano ilimaliza ya pili pia kwa kuvuna 54 katika mechi 26, nyuma ya Yanga iliyonyakua ubingwa wa ligi kwa msimu huo.

NDOO PEKEE BARA
Ndipo msimu wa sita kwa timu hiyo ikiwa kwenye Ligi Kuu Bara ilifanya kweli kwa kubeba ubingwa ikifikia rekodi ya Simba ya 2009-2010 ya kubeba taji bila kupoteza kwa kukusanya jumla ya pointi 62 kupitia mechi 26, ikiizidi akili Yanga iliyomaliza nafasi ya pili, huku timu iliyokuwa imepanda daraja msimu huo, Mbeya City ikishika nafasi ya tatu mbele ya Simba iliyokuwa ya nne. Hilo ndilo taji pekee la Ligi Kuu kunyakuliwa na Azam FC, kwani baada ya hapo imekuwa ikipambana bila mafanikio.
Ikicheza Ligi Kuu kwa msimu wa saba mfululizo, Azam ilishindwa kutetea taji na kujikuta 2014-2015 ikimaliza nafasi ya pili kwa kukusanya pointi 49 kwa mechi 26, ikiwa nyuma ya Yanga, huku Simba ikishika nafasi ya tatu na kufuatiwa na Mbeya City iliyoshindwa kushikilia bomba baada ya kupanda na mkwara msimu uliopita wakati huo.
Katika msimu wa nane wa Azam katika Ligi Kuu aliendelea kuganda nafasi ya pili nyuma ya Yanga iliyotetea tena ubingwa, baada ya Wanalambalamba kukusanya jumla ya pointi 64 kwa mechi 30,  Simba ikishika nafasi ya tatu na TZ Prisons ikifunga dimba la Nne Bora msimu huo wa 2015-2016.
Msimu wa tisa kwa Azam iliyumba kidogo kwa kuporomoka hadi nafasi ya nne ikikusanya pointi 52 kupitia mechi 30, huku Yanga ikitetea taji kwa msimu wa tatu mfululizo ikifuatiwa na Simba kisha Kagera Sugar ikamaliza nafasi ya tatu, juu ya Wanalambalamba.
Azam ilienda kujiuliza kisha kujipanga na kurudi kwenye msimu wa 10 wa 2017-2018 wakati ikiwa imeondokewa na majembe yake ya maana wanne waliohamia Msimbazi na kumaliza nafasi ya pili ikikusanya jumla ya pointi 58 katika mechi 30, nyuma ya Simba iliyebeba taji, huku Yanga ikiwa ya tatu na Tanzania Prisons ikishika nafasi ya nne.
Msimu wa 11 Azam  ilirudi nyuma kidogo kwa kumaliza nafasi ya tatu, wakati Simba ikitetea taji kwa mara ya pili mfululizo. Azam ilikusanya pointi 75 kupitia mechi 38, huku Yanga ikiwa ya pili na KMC iliyokuwa imepanda daraja msimu huo wa 2018-2019 kumaliza nafasi ya nne.

Misimu minne mfululizo iliyofuata Azam imeganda kwenye nafasi hiyo hiyo ya tatu ikizipisha Simba na Yanga kubadilishana nafasi mbili za juu, 2019-2020 iliyokuwa msimu wa 12 kwa Azam ilikusanya pointi 70 kwa mechi 38, nyuma ya Simba iliyotetea taji kwa msimu wa tatu na Yanga iliyokuwa ya pili, huku Namungo iliyokuwa ikicheza ligi kwa msimu wa kwanza kumaliza nafasi ya nne.
Msimu wa 13 kwa Azam ilikusanya pointi 68 katika mechi 34 na kumaliza nafasi ya tatu nyuma ya Simba iliyotetea taji kwa msimu wa nne mfululiza kisha Yanga na Biashara United ikamaliza ya nne na msimu wa 14 kwa Wanalambalamba ilivuna pointi 49 kwa mechi 30.

Msimu huo wa 2021-2022, Yanga ndio iliyobeba ubingwa bila kupoteza, ikafuatiwa na Simba, huku Geita Gold ikimaliza kwenye nafasi ya nne na msimu uliopita, Azam ilimaliza ya tatu tena kwa kukusanya pointi 59 katika mechi 30 ikiwa juu ya Singida Big Stars iliyopanda daraja, huku Yanga ikitetea taji kwa msimu wa pili mfululizo mbele ya Simba iliyokuwa ya pili.

UFUNGAJI BORA
Rekodi zinaonyesha katika misimu 15 mfululizo kwa Azam katika Ligi Kuu Bara mbali na kuzitetemesha vigogo Simba na Yanga kwa kukomaa nafasi za juu, lakini ilifanikiwa kutoa Wafungaji Bora katika misimu mitatu mfululizo ikiwa ni rekodi kipindi hicho kabla ya Yanga kuifikia rekodi hiyo kwa kutwaa tuzo hiyo misimu mitatu mfululizo pia, ndipo Simba ikaja kupindua meza misimu ya karibuni ikibeba tuzo hiyo mara nne mfululizo ikiivunja rekodi hiyo ya Azam na Yanga.

Azam ilitoa Mfungaji wa kwanza wa Ligi Kuu msimu wa 2010-2011, ikiwa ni msimu wa tatu kwao kuwepo kwenye ligi hiyo kwa kiungo mshambuliaji, Mrisho Ngassa kunyakua tuzo kwa kufunga jumla ya mabao 18, kisha msimu wa 2011-2012, John Bocco alinyakua tena akifunga jumla ya mabao 19 kabla ya Kipre Tchetche kuirejesha tena tuzo hizo Chamazi msimu wa 2012-2013 kwa mabao 17 aliyofunga.
Yanga iliifikia rekodi hiyo baada ya Simon Msuva kubeba mara mbili (2014-2015 na ule wa 2016-2017 alipofunga mabao 17 na 14 mtawalia, huku Amissi Tambwe akifanya yake 2015-2016 alipofunga mabao 21.
Hata hivyo, Simba ilikuja kuvunja rekodi hiyo kwa kutwaa kwa nyota wake watatu tofauti akizana Emmanuel Okwi aliyebeba msimu wa 2017-2018 kwa mabao 20, kisha Meddie Kagere kunyakua mara mbili mfululizo ikiwa ni rekodi akitwaa 2018-2019 akifunga 23 na kurudia tena 2019-2020 kwa mabao 22, kisha John Bocco akaipeleka tena tuzo hiyo Msimbazi msimu wa 2020-2021 kwa mabao 16.


UTILITY
2004 Mwaka ambao Azam FC iliasisiwa ikifahamika kama Mzizima FC kabla ya kubadili jina baadae

10 Idadi ya mataji iliyotwaa Azam ikiwamo Ligi Kuu, Ngao ya Jamii, ASFC, Kagame na Mapinduzi.

2007 Mwaka ambao Azam ilipanda daraja kupitia Ligi ya Taifa ikiifumua Majimaji kwa mabao 2-0.

2015 Mwaka ambao Azam ilibeba taji la kwanza la michuano ya kombe la Kagame ikiilaza Gor Mahia.

05 Mataji ya Kombe la Mapinduzi iliyobeba Azam ikishukilia rekodi ya kubeba mara nyingi zaidi.