Ronaldo alivyojibu kwa rekodi tano za kibabe Kombe la Dunia
Muktasari:
- Nahodha huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 41 amefunga mabao mawili dhidi ya Uzberkstan na kuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya soka kufunga katika fainali sita tofauti za Kombe la Dunia.
CRISTIANO Ronaldo ni kama amewajibu waliokuwa wakimbeza kutokana na kushindwa kuiwezesha Ureno kupata ushindi katika mechi ya kwanza ya fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya DR Congo, wiki iliyopita, baada ya kuiongoza Ureno kuichapa Uzbekistan kwa mabao 5-0 na kuweka rekodi mpya.
Nahodha huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 41 amefunga mabao mawili dhidi ya Uzberkstan na kuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya soka kufunga katika fainali sita tofauti za Kombe la Dunia.
Rekodi zingine alizoweka Ronaldo ni kuwa mchezaji wa pili mwenye umri mkubwa zaidi katika historia ya Kombe la Dunia akiwa na miaka 41 na siku 138, kucheza mechi 24 za Kombe la Dunia, akifikia rekodi ya Miroslav Klose na kumpita Paolo Maldini, kufikisha mabao 10 Kombe la Dunia ikiwa ni rekodi ya juu zaidi kwa Ureno akimpita Eusebio aliyekuwa na tisa na kwa pamoja na nyota wa Argentina, Lionel Messi, wanashikilia rekodi ya muda mrefu zaidi kati ya bao la kwanza na la mwisho Kombe la Dunia miaka 20 na siku 11.
Baada ya kufunga mabao hayo, Ronaldo alisimama mbele ya kamera za televisheni na kusema, “nimerudi! nimerudi!”, ujumbe ulioonyesha kana kwamba anawalenga wale waliokuwa wakimkosoa baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya DR Congo katika mchezo wa kwanza wa Kundi K.
GARI LIMEWAKA
Ronaldo hakuhitaji muda mrefu kuonyesha ubora kwani dakika ya sita aliifungia Ureno bao la kwanza baada ya kupokea krosi kutoka Joao Cancelo.
Kabla ya mapumziko aliongeza bao la pili baada ya kupokea pasi nzuri ya Bruno Fernandes, huku akikaribia kufunga hat-trick kabla ya mapumziko lakini juhudi zake zikazuiwa kwenye mstari wa goli.
Mabao mengine ya Ureno yalifungwa na Nuno Mendes, bao la kujifunga la kipa wa Uzbekistan Abduvohid Nematov na Rafael Leao aliyefunga bao la tano mwishoni mwa mchezo.
MWENYEWE ATIA NENO
Akizungumzia kauli yake ya “nimerudi”, Ronaldo amesema ilikuwa ni kuwakumbusha wakosoaji wake kwamba bado yupo kwenye kiwango cha juu licha ya umri wake kuwa mkubwa. Ronaldo ana miaka 41
“Ni ili wasisahau, nimekuwa nikifanya hivi kwa miaka 23. Ninafurahia rekodi hizi lakini jambo muhimu zaidi ni kazi iliyofanywa na timu. Lengo langu siku zote ni kusaidia timu kufikia malengo yake,” amesema Ronaldo
MSIKIE MARTINEZ
Kocha wa Ureno, Roberto Martinez, amesema Ronaldo alikuwa na mchango mkubwa katika kuijenga upya morali ya timu baada ya matokeo ya kusikitisha dhidi ya DR Congo.
“Ukosoaji uliokuwepo ulikuwa mkubwa na kwa kiasi fulani haukuwa wa haki, Cristiano alikuwa nahodha bora, alitumia uzoefu wake mkubwa na kusaidia timu kuvuka kipindi kigumu,” amesema Martinez.
Ameongeza kuwa Ronaldo ni mfano bora kwa wachezaji vijana kutokana na nidhamu yake ya kazi na ari yake ya kujituma kila siku.
HIVI NDIVYO RONALDO ALIVYO
Mchezaji wa zamani wa Manchester United na England, Wayne Rooney, amesema mabao hayo mawili n
“Amekuwa akifanya hivi maisha yake yote, napokosolewa, hujibu kwa kufunga mabao, ana hamu ya kuwa bora kuliko wote na ndiyo sababu bado anaendelea kung'ara akiwa na miaka 41,” amesema Rooney.
KIPAJI CHAKE CHA AJABU
Nahodha wa zamani wa Manchester United, Roy Keane, amesema watu walikosea kumtilia shaka Ronaldo.
“Cristiano Ronaldo hakuwahi kupotea. Yeye ni gwiji. Ana kila kitu maishani, ameshinda karibu kila taji, ni bilionea, lakini bado ana njaa ya mafanikio, huo ndiyo mfano bora kwa vijana,” amesema Keane.
Kocha wa Uzbekistan, Fabio Cannavaro, amesema Ronaldo bado ni miongoni mwa wachezaji bora zaidi katika historia ya mchezo huo.
“Ukifika Kombe la Dunia ukiwa na miaka 41 na bado unaonyesha njaa ya mafanikio, hilo ni jambo la kipekee, ukimpa nafasi ndani ya eneo la hatari, unakuwa umejimaliza,” amesema Cannavaro.
REKODI ZENYEWE
Mchezaji wa kwanza kufunga katika Kombe la Dunia mara sita tofauti.
Mfungaji wa pili mwenye umri mkubwa zaidi katika historia ya Kombe la Dunia akiwa na miaka 41 na siku 138.
Kucheza mechi 24 za Kombe la Dunia, akifikia rekodi ya Miroslav Klose na kumpita Paolo Maldini.
Mabao 10 Kombe la Dunia, rekodi ya juu zaidi kwa Ureno, akimpita Eusebio aliyekuwa na mabao tisa.
Kwa pamoja na Lionel Messi wanashika rekodi ya muda mrefu zaidi kati ya bao la kwanza na la mwisho Kombe la Dunia, miaka 20 na siku 11.