Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sitaki tena Urais – Sehemu ya 39

RAIS 39 Pict

ILIKOISHIA

Sikuingia mpaka alipoondoka kwenye mlango. Sikutaka asikie nanukia harufu ya ajabu ajabu.

Aliingia chumbani kwake na mimi nikaingia chumbani kwangu. Nilifikiria nikaoge lakini niliona ningeweza kuharibu miko. Tatizo lenyewe sikumuuliza yule mganga kwamba naweza kwenda kuoga.

Licha ya kutomuuliza, mimi mwenyewe pia niliona kwenda kuoga usiku ule ule ninaweza kuharibu miko. Pengine kukipambazuka ningeweza kuoga.

Kwa kweli sikulala. Nilikaa tu kwenye kochi huku nikimuwaza Zena. Kutokana na kazi niliyuiona na maneno aliyoniambia yule mganga, niliamini  kuwa tatizo la Zena nilikuwa nimelimaliza.


SASA ENDELEA



ILIPASA nimshukuru Mungu kumpata mganga yule mwenye ujuzi wa majini, vinginevyo ningeendelea kupata mateso na mwisho wake ningeuawa na Zena.

Nilikuwa na kawaida kila ninapolala humuota Zena, hasa huota tukifanya mapenzi ufukweni mwa bahari. Usiku ule sikuota kabisa kitu ambacho kiliniongezea imani kuwa Zena ameshakuwa mbalimbali na mimi.

Asubuhi nilioga nikaondoa zile dawa za maiti ziliokuwa na harufu mbaya. Si kawaida yangu kujipulizia manukato lakini siku ile nilijipulizia kuondoa ile harufu. Nikaenda zangu kazini.

Kusema kweli jinsi nilivyokuwa mchangamfu na mwenye furaha nilionekana wazi kuwa nilikuwa na kitu. Na kitu hicho si kingine bali ni ile furaha ya kumpoteza Zena. Najua wako watu ambao wanaweza kuniona nilikuwa bwege kupata msichana mwenye utajiri kama yule na halafu kumwendea kwa mganga na kumtimua. Utajiri wake na uzuri wake usingekuwa na maana yeyote kwangu kama hatima yake ni kuja kuutoa uhai wangu. Sitaweza kutii majini hata siku moja.

Wakati wa mchana nilikuwa nimeingia Facebook nikiangalia posti za marafiki zangu. Ghafla nikaona Zena ametuma maneno yanayosomeka kama ifuatavyo.

“MIMI NAJUA KUPENDA TU, SIJUI KUACHA. NIKISHAKUCHUNUKA HUWEZI KUNIEPUKA

Nikashituka na kujiuliza, Zena alikuwa akimwambia nani maneno hayo? Alikuwa akiniambia mimi au mtu mwingine? Niliamini kwa wakati ule mpenzi wake nilikuwa mimi. Hakuwa na mwingine. Na pia kwa kadiri nilivyojua jini hachunuki watu wawili kwa wakati mmoja.

Kama mpenzzi wake nilikuwa mimi na maneno hayo alikuwa akiniambia mimi.

Nikajiuliza kama alikuwa akiniambia mimi maneno hayo ataniambiaje kuwa hawezi kuniepuka wakati tayari tumeshapitisha kafara la kumuondoa tangu jana. Ina maana alikuwa hajajua bado?

Nikatamani nirudi kwa yule  mganga nikamueleze lakini nikasita. Nilisita baada ya kufikiri kwamba mganga huyo anaweza kuona nilikuwa mpumbavu kutiwa wasiwasi na maneno hayo ya Zena.

Nilihisi anaweza kuniambia, watu hujipachikia maneno tu kwenye Facebook hata yasiyo na maana. Au angeweza kuniambia kuwa Zena ameweka maneno hayo kunitisha tu baada ya kugundua siingiliki tena.

Nikaona nisiende kwa huyo mganga kwani sikuwa na sababu za msingi za kwenda kwake.

Siku iliyofuata ilikuwa jumapili, sikwenda kazini. Niliamua kubaki nyumbani. Nilipoamka asubuhi nilifua. Nilipomaliza kufua nilioga ndipo nikachemsha chai chumbani mwangu. Baada ya kunywa chai na mkate nikakaa kwenye kochi nikitazama televisheni.

Mlango wa chumbani mwangu ukabishwa.

“Nani?” Nikauliza lakini sikupata jibu. Mlango ukabishwa tena. Nikainuka kwenda kuufungua.

Unadhani alikuwa nani? Alikuwa Zena! Nilishitika na moyo ukapiga kwa kishindo.

Nikabaki nimeduwaa kwenye mlango.

“Hujambo Karim?” Akanisalimia huku akinitolea tabasamu.

“Sijambo. Karibu.” Nikamkaribisha.

Zena akaingia chumbani. Wakati anaingia mimi nilitoka. Nilitoka nje nikaenda kwenye kituo cha bodaboda kukodi pikipiki iliyonipeleka kwa yule mganga.

“Una tatizo gani?” Mganga akaniuliza alipoona jinsi nilivyohamanika.

“Yule msichana amekuja tena,” nikamwambia.

“Amekuja tena wapi?”

“Amekuja nyumbani kwangu.”

“Amekuja lini?”

“Amekuja sasa hivi. Alivyoingia chumbani mwangu, mimi nilitoka nikaja hapa kwako.”

“Siamini kama yule msichana amekuja tena kwako.”

“Amini ninavyokwambia. Hivi sasa yuko chumbani kwangu.”


“Tunaweza kwenda ili nikamuone?”

“Ndio nataka twende ukamuone.”

“Subiri kidogo.”

Mganga akajitayarisha. Baada ya dakika tatu tu akawa tayari nikaondoka naye akiwa na kapu lake. Nilikodi bajaj. Tukiwa njiani nilimuuliza yule mganga.

“Zena amepajuaje nyumbani ninapoishi. Ile nyumba anayoijua sio hii ninayoishi sasa. Amekijua mpaka chumba changu.”

“Yule ni jinni, usiulize amejuaje. Wewe twende nikaonane naye mimi mwenyewe.” Tukafika nyumbani. Tulishuka kwenye bajaj tukaingia ndani.

“Fungua mlango.” Mganga akaniambia.

“Fungua wewe.”

Mganga akaufungua mlango huo na kuingia ndani ndipo na mimi nikaingia.

Chumba kilikuwa kitupu. Zena hakuwemo chumbani.

“Yuko wapi?” Mganga akaniuliza.

“Sijui. Nilimuacha humu humu chumbani.”

“Amekimbia alipogimdua nakuja au amejificha mvunguni. Hebu tazama mvunguni.”

Nikapiga goti na kuchungulia mvunguni mwa kitanda. Hamkuwa na kitu.

“Hayumo.”

“Basi amekimbia, hatakuja tena.”

“Hatakuja tena?”

“Kesho nitakupa hirizi uiweke humu chumbani mwako.”

“Utanipa kesho? Kwanini usinipe leo?”

“Itabidi turudi nyumbani nikakupe.”

Nilikuwa nimeshasimama, wasiwasi ukanifanya nipige goti tena na kuchungulia mvunguni kuhakikiksha kuwa Zena hakujificha humo.

“Au wewe uliona msichana mwingine?” Mganga akaniuliza.

“Nilimuona Zena si msichana mwingine.”

“Sasa yuko wapi na ulisema umemuacha humu chumbani.”

“Labda ameondoka na kama unavyosema wewe amekukimbia wewe.”

“Basi twende nyumbani.”

Nikatoka tena na yule mganga. Nilifunga mlango wangu tukaenda kupanda bajaj nyingine tukarudi nyumbani kwa mganga.

Mganga huyo akanitengezea hirizi mbili, akaniambia moja nitembee nayo mfukoni na nyingine niiweke mahali popote chumbani mwangu.

“Ukiwa nayo hirizi hii mfukoni, huyo jini hatakufuata kabisa na hii nyingine ukiiweka chumbani mwako Zena hataingia katika chumba chako. Ukihama hama nayo.” Mganga akaniambia.

Nikarudi nyumbani na zile hirizi mbili. Hirizi moja niliitia kwenye pochi yangu ili isipotee na hirizi ya kuweka chumbani niliining’iniza juu ya mlango wa chumbani mwangu.

Kwa vile moyo wa kishirikina ulikuwa umeshanipata, nikawa sina wasiwasi tena baada ya kupewa hirizi hizo.

Usiku nililala bila wasiwasi na sikuota ndoto zozote. Siku iliyofuata nilikwenda kazini kwangu. Nikafanya kazi hadi saa saba mchana. Nikaenda zangu kula chakula. Baada ya kula ugali kwa mchuzi wa perege nikatoka kurudi kazini.

Wakati natembea, ghafla nikaona pikipiki inasimama mbele yangu. Nikamuona msichana aliyekuwa amepakiwa akishuka haraka haraka. Nilipomtazama msichana mwenyewe nikaona alikuwa Zena. Alikuwa amependeza kuliko maelezo.

Nilishituka nikamkwepa na kugeuka upande mwingine kisha nikaendelea na safari nikijifanya kama sikumuona. Wakati natembea nikazisikia hatua za Zena nyuma yangu. Alikuwa akitembea haraka haraka kunifuata, mimi nilizidi kwenda. Ghafla nikamuona yuko sambamba na mimi upande wangu wa kulia, tumefuatana kama tuliokuwa safati moja. Bado nilijifanya sigeuki, naendelea kwenda tu.

Nikasimama ghafla nikajifanya nanunua gazeti na yeye akasimama. Wakati napokea gazeti, yeye akatoa  pesa ya gazeti.

Hapo ilibidi nigeuke nimtazame. Nikajifanya kama namuona sasa.

“Habari yako?” Nikajikuta namsalimia bila kupenda.

“Nzuri. Kumbe unapenda kusoma magazeti.”

“Kiasi tu si sana.”

“Unakwenda wapi?”

“Ninakwenda kazini kwangu.”

Zena akashituka. “Umeweka nini kwenye pochi yako?” Akaniuliza.

Na mimi nikashituka. ”Sikuweka kitu.”

“Hapana. Umeweka kitu. Hebu toa pochi yako.”

Nikaitoa mfukoni. “Ifungue,” akaniambia uso akiwa ameukunja.

Nikafungua ile pochi. Nikaona ile hirizi inaaguka chini.

“Nini hiyo?”

Nikainama na kuiokota.

“Nini hiyo?” Akaniuliza tena.

Sikuwa hata na la kujibu.

“Itupe mbali sana,” akaniambia.

Wakati akiniambia hivyo alikuwa amenishika mkono mmoja. Nilikuwa natetemeka.

“Itupe.”

Nikairusha upande wa pili wa barabara.

“Sasa twende zetu.”

Nikaifunga ile pochi na kuirudisha mfukoni. Tukaanza kutembea. Muuza magazeti alikuwa akitutazama.

“Mimi nakwenda kazini,” nikajikuta nikimwambia hivyo.

“Nakusindikiza. Usijali.”

Nikanyamaza kimya. Moyoni mwangu nilikuwa nikijiambia, yule mganga aliniambia nikiwa na ile hirizi Zena hatanifuata tena, sasa mbona amenifuata na kunilazimisha niitupe?

“Utarudi nyumbani saa ngapi?” Zena akaniuliza.

“Nitarudi jioni.”

“Nipe ufunguo wa chumbani mwako, ukirudi utanikuta chumbani.”

Nikaguna kimoyomoyo kisha nikajifanya kama sikumsikia vizuri nikamuuliza.

“Unasemaje?”

“Nimekwambia nipe ufunguo wa chumbani kwako.”

“Halafu nikishakupa…?”

“Ukirudi kazini jioni utanikuta chumbani mwako.”

Sikutaka kumpa huo ufunguo lakini sikuwa na jinsi. Sikuweza kumkatalia, nikampa.

Nilipompa alitabasamu na kuniaga akaondoka. Alipoondoka hapakuniweka tena. Niliondoka kazini bila kuomba ruhusa. Kwa lugha nyingine nilitoroka kazini.