Sitaki tena Urais – Sehemu ya 38
ILIKOISHIA
“Na aende zake. Bora nibaki na umasikini wangu lakini niishi kwa amani.”
“Kwa hiyo humtaki huyu jini?”
“Simtaki na sitaki anifuate tena.”
“Ninunulie mbuzi mweusi na kitambaa cha sanda mita saba.”
“Na kazi yenyewe itagharimu kiasi gani?”
“Utanipa shilingi laki tatu.”
“Unanihakikishia mzee, huyu jini hatanifuata tena?”
“Hutamuona tena.”
“Sasa nilete lini hivyo vitu?”
SASA ENDELEA
“Siku yoyote utakapokuwa tayari.”
“Nakuletea kesho.”
“Lakini kazi yenyewe itafanyika usiku huko makaburini.”
“Itafanyika usiku saa ngapi?”
“Kuanzia saa saba usiku.”
“Sasa hivyo vitu nikuletee muda gani?”
“Unaweza kuniletea mchana. Halafu utarudi tena usiku.”
“Sawa.”
“Ramli yangu utalipa elfu kumi.”
Nikatoa noti ya shilingi elfu kumi na kumpa mganga huyo.
Kabla sijaondoka hapo kwa mganga, Zena akanipigia simu. Nikashituka na kumtazama yule mganga.
“Huyo msichana ananipigia simu,” nikamwambia.
“Msichana gani?”
“Huyo jini tuliyemzungumzia.”
“Ipokee simu yake halafu nipe mimi.”
Nikaipokea ile simu, bila kuzungumza chochote nikampa simu yule mganga. Mganga alipokea simu akasema.
“Halo….”
Nikasikia sauti ya mnyuso mkali kutoka simu ya upande wa pili kisha simu ikakatwa.
“Wewe nitakukomesha. Mimi ni Mtemi Wembe nitakukata tu. Siku zako zinahisabika…” Mganga akawa anaongea peke yake kwenye simu.
“Ameshakata….” Nikamwambia.
“Lakini amenisikia.”
“Aliponyusa tu akakata simu.”
“Unafikiri nina wasiwasi naye, nilitaka kumpa salamu tu akae vizuri.”
Mganga akaendelea kuniambia.
“Majini wa aina hii hawanisumbui. Nimeshapambana nao mara nyingi, hawaniwezi. Wakiniona wananikimbia. Huyu amekata simu kwa sababu ya kuniogopa na asije akakuonya ukaogopa. Anaweza kukupigia simu tena akakutisha, usiogope. Huyu anataka kukuharibia maisha yako.”
Nilikuwa nimenyamaza nikiendelea kumsikiliza mganga huyo ambaye aliendelea kuniambia.
“Kule kwetu Pemba majini ndio watumwa zetu. Tunawaweka kwenye dari za nyumba zetu kama mahindi. Wanapokwenda kinyume na vile tunavyowaagiza tunawachapa viboko. Na huyo jini wako asipoangalia naweza kumchukua nikaenda naye Pemba akawe mtumwa kama wenzake.”
Nikaona huyu mganga ni hatari sana. Anawezeje kumchukua jini na kwenda kumfanya mtumwa wakati watu wanawaogopa?
“Sasa wewe nenda uje hapo kesho.” Mganga akaniambia.
“Sawa mzee. Nitakuja kesho pamoja na hivyo vitu ulivyoniagiza.”
Nikaagana na yule mganga na kuondoka. Kile kitendo changu cha kwenda kwa mganga kikanitia wasiwasi sana. Nilikuwa nikiona kama vile Zena angeweza kunitokea ghafla na kunitisha au kunidhuru.
Usiku sikulala kwa hofu lakini kitu ambacho nilikishukuru ni kuwa Zena hakunipigia simu wala sikumuota.
Siku iliyofuata nilkwenda kununua vile vitu nilivyoagizwa kwa mganga Nilipompelekea alivikagua na kuniambia viko sawa.
“Sasa uje usiku.”
“Sawa. Nitakuja usiku.”
Nilipoondoka kwa huyo mganga nilikwenda kazini kwangu. Hata hivyo bado nilikuwa na mawazo mengi kwa vile moyo wangu ulishapata wasiwasi.
Saa mbili usiku nikaenda kwa huyo mganga. Akaniambia.
“Tutakaa hadi saa saba ndipo tutakwenda makaburini nikakushughulikie.”
Tukakaa hadi saa saba usiku. Alikuwa akiandaa vitu vyake na nilikuwa nikicheza gemu kwenye simu yangu. Saa saba tukaondoka. Tulikuwa mimi, mganga huyo na msaidizi wake mmoja.
Eneo lenyewe la makaburi lilikuwa limejitenga na makazi ya watu. Tulitembea kwa miguu mwendo wa karibu saa moja. Kwa vile ulikuwa usiku mwingi kulikuwa kimya. Eneo la makaburi lilikuwa limeota miti na kuwa na pori zuri. Usiku huo palikuwa mahali panapotisha.
Sauti iliyokuwa ikisikika mahali hapo ni ya ndege waliokuwa kwenye miti. Zaidi ya sauti za ndege palikuwa kimya sana.
Mganga na msaidizi wake walikuwa wameshachagua kaburi tangu mchana. Kaburi hilo lilikuwa katikati ya eneo hilo. Kaburi hilo lilikuwa limefukuliwa. Nafikiri walilifukua wao . Lilifukuliwa usawa wa futi moja kwenda chini lakini upana ulikuwa ni ule ule wa kaburi.
Msaidizi wa mganga akaanza kushughulika. Alinitaka nivue nguo zangu zote nibaki uchi wa mnyama. Nilishangaa kidogo nikajiuliza ulikuwa uganga wa aina gani lakini nilivyoona mahali tulipokuwa tulikuwa peke yetu na palikuwa kiza, nikavua nguo zangu zote.
Nilipobaki uchi mganga alitoa kile kitambaa cha sanda akakitandaza cjini na kunitaka nikilalie. Nikakilalia. Nikapakwa madawa yanayonukia harufu ya dawa anayotiwa maiti kabla ya kuzikwa. Kwa kweli niliogopa sana.
Nilipoona yule mganga ananishonea ile sanda nikashituka na kumuuliza.
“Mbona unaishona?”
“Ndio uganga wenyewe, wewe tulia tu.”
Nikaguna kimoyomoyo kisha nikanyamaza. Baadaye likanijia swali nikamuuliza msaidizi wa yule mganga.
“Mnataka mnizike nini?”
Msaidizi wa mganga akanijibu vilevile.
“Ndio uganga wenyewe.”
Nikabaki kimya lakini nilijiambia endapo watanizika na nikiona wananifukia nitatoka mbio. Sitataka tena huo uganga. Sanda ilikwishashonwa mwilini mwangu. Mwili wangu wote ulifinikwa kwa sanda. Kilibakishwa kilikuwa kichwa tu. Nikatiwa maji yaliyochanganywa na dawa iliyokuwa inanuka vibaya.
Wakati walipokuwa wanataka kunitia hayo maji nilimsikia yule mganga akimuuliza msaidizi wake.
“Yako wapi yale maji ya maiti.”
Msaidizi huyo akatoa dumu la maji kutoka kwenye kapu.
“Hayo ni maji yaliyooshewa maiti?” Nikamuuliza yule mganga. Mganga alikuwa ameshapandisha.
“Nyamaza wewe,” akaniambia.
Nikanyamaza kimya. Maji yalikuwa baridi yaliyosababisha nihisi mzizimo mkali. Yalitiwa hadi kichwani mwangu. Nilibana midomo yangu ili yasiniingie mdomoni mwangu.
Baada ya hapo wakanibeba. Mganga alinishika upande wa kichwani, msaidizi wake akanishika upande wa miguuni wakanitia kwenye lile kaburi. Walinilaza kichalichali.
Mikono na miguu yangu ilikuwa imefungwa kwa sanda kiasi kwamba hata kama ningetaka kutoka humo kaburini nisingeweza.
Waliponiweka ndani ya kaburi hilo watu hao wakawa wanalizunguka huku wakinisomea. Baada ya hapo wakawa wanalifukia lile kaburi kwa mikono.
“Mbona mnanifukia?” Nikawauliza kwa taharuki.
Hakukuwa na aliyenijibu. Waliendelea kufukia tu. Nikawa najaribu kuinuka na kuchomoa mikono yangu ili nitoke humo kaburini lakini sikuweza.
Waliufukia mwili wangu wote wakabakisha shingo tu na kichwa.
“Uganga gani huu?” Nikajiuliza kimoyomoyo.
Walifanya uganga wao hapo juu ya kaburi wakavunja nazi kisha mganga akamwambia msaidizi wake.
“Sasa tumfukue.”
Wakaanza kuutoa ule mchanga kwa mikono. Ile sanda ilipasuliwa kwa kisu nikatoka ndani ya lile kaburi. Mwili wote ulikuwa umekufa ganzi.
“Vaa nguo zako.” Mganga akaniambia.
Nikavaa nguo zangu na kusimama hapo hapo.
“Sasa kijana kama utamuona tena yule jini nifuate uje uchukue pesa zako. Nitakulipa hadi pesa ulizonunulia hii sanda na nitaacha uganga siku hiyo hiyo.” Mganga akaniambia.
Maneno yake yalinipa moyo sana mpaka nikajikuta natabasamu.
“Nipe zile pesa zangu tulizokubaliana.” Mganga akaniambia.
Nikatoa pesa hizo na kumpa. Mganga alizihesabu. Alipoziona zipo sawa akaniambia.
“Sasa turudini nyumbani.”
Tukarudi nyumbani kwake. Ilikuwa karibu saa kumi alfajiri.
“Sasa utakwenda nyumbani kwako au utabaki hapa hapa hadi kutakapokucha?”
“Bodaboda zipo, nitarudi nyumbani.”
“Haya uende salama.”
Nikaenda kwenye kituo kimoja cha bodaboda nikakodi pikipiki iliyonirudisha nyumbani,
Wakati nampa pesa kijana wa bodaboda, nilimuona akikunja uso na kusema.
“Nasikia harufu ya dawa kama zile anaozotiwa maiti.”
Swali lake lilinifanya nisismkwe na mwili hasa nilipofikiria kuwa maiti mwenyewe nilikuwa mimi. Lakini sikumjibu kitu, nilimlipa pesa zake nikaenda kubisha kwenye dirisha la mpangaji mwenzangu.
Baada ya kubisha mara mbili, tatu aliamka akauliza.
“Nani?”
“Mimi Karim, nifungulie mlango.”
“Karim….”
“Ndiyo.”
“Unataka nini?”
“Nataka unifungulie mlango.”
“Mlango gani?”
“Mlango wa mbele. Niko nje, ndio narudi sasa.”
“Oh nimekuelewa. Subiri nakuja.”
Baada ya sekunde chache mlango wa mbele ukafunguliwa. Nilisimama mbali kidogo na mlango.
“Karim vipi?” Mpangaji huyo akaniuliza akiwa amesimama kando ya mlango.
“Nimechelewa kidogo. Nilikuwa kwenye mziki.”
“Sawa. Ingia.”
Sikuingia mpaka alipoondoka kwenye mlango. Sikutaka asikie nanukia harufu ya ajabu ajabu.
Aliingia chumbani kwake na mimi nikaingia chumbani kwangu. Nilifikiria nikaoge lakini niliona ningeweza kuharibu miko. Tatizo lenyewe sikumuuliza yule mganga kwamba naweza kwenda kuoga.
Licha ya kutomuuliza, mimi mwenyewe pia niliona kwenda kuoga usiku ule ule ninaweza kuharibu miko. Pengine kukipambazuka ningeweza kuoga.
Kwa kweli sikulala. Nilikaa tu kwenye kochi huku nikimuwaza Zena. Kutokana na kazi niliyuiona na maneno aliyoniambia yule mganga, niliamini kuwa tatizo la Zena nilikuwa nimelimaliza.