Sitaki tena Urais – Sehemu ya 37
ILIKOISHIA
Nikazipokea pesa hizo na kumwambia.
“Asante.”
“Kumbuka kwamba nitakuja tena Moro hivi karibuni.”
“Karibu sana.”
“Nakushukuru kwa ukarimu wako.”
“Na wewe pia nakushukuru kwa wema wako.”
“Asante.”
Wakati wote tukizungumza, tabasamu lilikuwa kwenye uso wa Zena. Nikamsindikiza ndani ya basi na kuzungumza naye hadi muda wa safari ulipowadia, nikaagana naye na kutoka.
SASA ENDELEA
Basi lilipokuwa linaondoka, alinipungia mkono kupitia kwenye dirisha, na mimi nikampungia.
Nilipotoka stendi, nikaenda kazini kwangu nikiwa na shilingi milioni yangu moja mfukoni. Kazi niliyoifanya siku ile ilikuwa ni kuwachunguza marafiki wa Zena waliokuwa Facebook. Zena hakuwa na marafiki wanawake. Alikuwa na marafiki wa kiume watupu. Marafiki wenyewe walikuwa watatu, mimi nilikuwa wa nne.
Wakati nawachunguza, niligundua mmoja wao alikuwa “online”.
Nikajaribu kuwasiliana naye kwa kumuuliza hali. Alipojibu, nikajitambulisha na kumweleza mimi ni nani, kisha nikaomba namba yake ya simu. Akanipatia.
Nilipopata namba yake ya simu, nikampigia hapo hapo. Akapokea simu yangu.
“Naomba kukuuliza kidogo,” nikamwambia.
“Niulize tu.”
“Kuna msichana anaitwa Zena, yuko kwenye Facebook. Picha yako pia nimeiona kwenye Facebook yake, kwa maana kwamba mmekuwa marafiki. Sasa swali langu ni je, mlishawahi kukutana?”
“Huyo msichana, kaka, epukana naye. Ni muuaji. Alitaka nimuoe, kumbe ni jini anayetongoza binadamu.”
Maneno yake yakanishitua.
“Umesema yule msichana ni jini?”
“Ni jini yule. Nilimuomba urafiki, akanikubalia….”
Nikamkatiza. “Kwani wewe uko wapi?”
“Mimi niko Tanga, lakini wakati huo nilikuwa Arusha. Alisafiri kutoka Dar hadi Arusha kunifuata. Alikodi chumba hotelini kwa wiki nzima. Jinsi alivyo mzuri na pesa alizokuwa akinipa vilichota akili yangu sana….”
“Umeniambia kwamba ni muuaji. Ulijuaje kama ni muuaji?”
“Alimuua mke wangu, akataka kuniua na mimi.”
“Alimuua mke wako?”
“Ndiyo, alimuua. Unajua nilimdanganya kuwa sina mke. Wakati huo mke wangu alikuwa amerudi kijijini, mama yake alikuwa mgonjwa. Usiku wa siku aliyorudi, nikaota Zena anamnyonga mke wangu kitandani. Nilipoamka, mke wangu alikuwa amekufa kweli.”
Kijana huyo aliendelea kunieleza.
“Nilimpigia simu nikamueleza, akakiri kwamba amemuua eti kwa sababu hataki mshirika. Hapo ndipo aliponibainishia kwamba yeye ni jini, si binadamu. Nikaogopa sana na kukimbilia kwa waganga. Siku moja alinifuata usiku akaniambia kama nitaendelea kwenda kwa waganga, atakuja kuniua. Kwa kweli nilipata wakati mgumu sana.”
“Kwanini hukumfukuza?”
“Hafukuziki. Yaani, akishakuchunuka, unakuwa naye hadi kufa na kila msichana wako atamuua.”
“Mpaka sasa hivi bado uko naye?”
“Nashukuru, nilipata mtaalamu kutoka Tanga aliyenisaidia kumkimbiza. Sasa hivi hanifuati tena na sina mawasiliano naye kabisa. Nashukuru Mungu.”
“Sasa na mimi naona yatakuwa hayo hayo. Huyu msichana nilijuana naye kwenye Facebook. Mimi ninaishi Morogoro. Kwa jinsi nilivyomuona mzuri, nilimfuata Dar.”
Nikaendelea kumweleza vituko alivyonionesha msichana huyo hadi nilipoondoka.
“Hata mimi nilimfuata Dar nikafika nyumbani kwake. Unapotoka, unatokea kwenye mti. Mimi nilikaa kwake wiki nzima. Unapolala naye, unapitiwa na usingizi. Unafanya naye mapenzi ukiwa usingizini. Anakwambia mpaka umuoe ndipo atakuruhusu ufanye naye mapenzi waziwazi.”
“Hata mimi ni hivyo hivyo. Ninafanya mapenzi naye nikiwa usingizini. Nikipanda kitandani tu, napitiwa na usingizi hapo hapo. Nikilala, naota niko ufukweni mwa bahari nafanya mapenzi naye.”
“Mpaka sasa uko naye?”
“Niko naye. Ameondoka leo kurudi Dar. Nilikuwa naye nyumbani kwangu tangu juzi. Anataka nimuoe.”
“Usikubali, rafiki yangu. Ukioana na huyo msichana, ujue umekwisha. Ameshawaliza na kuwaua vijana wengi wenye tamaa ya wasichana warembo.”
“Sasa nitamuepuka vipi? Kutokana na maelezo yako, simuhitaji tena.”
“Tafuta wataalamu na uhame hapo nyumbani unapoishi. Akikupigia simu, usipokee.”
“Sawa. Nitajaribu kuchukua hatua. Nitakufahamisha kitakachotokea. Asante sana.”
“Jitahidi, kaka. Huyo si msichana. Mwisho wake atakuja kukuua wewe.”
“Nakushukuru kwa kunihadharisha.”
Nikakata simu. Nilipokata simu, niligundua kuwa vidole vyangu vilikuwa vikitetemeka. Hata miguu yangu ilikuwa ikitetemeka kwa hofu iliyonipata.
“Kumbe huyu msichana ni jini,” nikawa najiambia kimoyomoyo.
Nikaendelea kujiambia kwamba kama nisingempigia simu huyu jamaa, nisingeelewa kitu. Mwisho wake, yaliyompata yeye yangekuja kunipata na mimi.
Pale nikawa nafikiria kwenda kwa waganga ili watumie utaalamu wao kuniondolea lile tatizo ambalo nililiona kuwa kubwa.
Lakini kabla ya kwenda kwa mganga, nikaendelea kujiambia kwamba ni lazima kwanza nitafute chumba mahali pengine. Kama Zena atakuja ghafla, asinikute pale nyumbani.
Hapo hapo nikaona Zena ananipigia simu. Nikashituka. Nilihisi labda Zena ameshagundua kuwa niliwasiliana na mwanaume wake wa zamani na ameshanifahamu kuwa yeye ni jini.
Nikaona nisipokee ile simu. Sikuipokea. Simu iliita mpaka ikakata yenyewe. Nilikuwa naitazama tu. Ilipokata, nikaizima ili kama atapiga tena, asipate mawasiliano.
“Huyu ni chatu, sitaki hata kusikia sauti yake,” nikajiambia.
Mchana, wakati nakwenda kula chakula, nilimpitia dalali wa nyumba ambaye alikuwa rafiki yangu.
“Rafiki yangu, nataka unitafutie nyumba,” nikamwambia.
“Unataka nyumba au chumba?” akaniuliza.
“Nataka chumba.”
“Unataka wewe au kuna mtu unamtafutia?”
“Nataka mimi.”
“Pale unapoishi unataka kuhama?”
“Ndiyo, nataka kuhama. Nataka nyumba nzuri zaidi.”
“Ungependa maeneo gani?”
“Maeneo yoyote tu ya mjini.”
“Kuna nyumba moja ipo hapa karibu, ina chumba. Hebu twende sasa hivi ukaitazame.”
“Tutumie usafiri au…?”
“Tutatumia pikipiki yangu.”
Dalali huyo wa vyumba alinipakia kwenye pikipiki yake na kunipeleka katika hiyo nyumba aliyoniambia, ambayo haikuwa mbali sana na kazini kwangu.
Ilikuwa nyumba nzuri kuliko ile niliyokuwa ninaishi. Tuliingia ndani akanionesha chumba chenyewe. Jinsi nilivyoiona ile nyumba, sikutaka kumhoji mengi. Nilimuuliza:
“Kodi ni kiasi gani?”
“Shilingi elfu hamsini kwa mwezi. Wakati unaingia, mwenyewe anataka kodi ya miezi sita.”
“Kodi ya miezi sita sina. Nitalipa ya miezi minne.”
“Nitakukutanisha na mwenyewe, mtasikizana.”
“Sawa. Yuko wapi?”
“Yeye haishi hapa. Nitakupeleka anakofanya kazi muonane.”
“Sawa.”
Dalali huyo akanipakia kwenye pikipiki yake na kunipeleka alikokuwa anafanya kazi mwenye nyumba huyo. Alikuwa na duka la sonara maeneo ya stendi ya mabasi.
Nilizungumza naye, tukakubaliana nimpe kodi ya miezi minne ili nichukue kile chumba. Dalali wangu akanipakia kwenye pikipiki yake na kunipeleka nyumbani, ambako nilichukua pesa za kumlipa yeye na kulipia kile chumba. Aliponipeleka kwa mwenye nyumba, tukamalizana hapo hapo.
Jioni ya siku ile ile, nikahamisha vitu kwenye nyumba ya zamani na kuvipeleka katika nyumba mpya.
Kule nilikohama hata sikuwambia nahamia wapi na kwanini nimehama. Usiku wa siku ile nikalala kwenye nyumba niliyohamia. Usiku, kabla sijalala, Zena akanipigia simu tena. Sikuipokea.
Nilikuwa na kawaida ya kuota ninafanya naye mapenzi usiku, lakini usiku ule sikuota. Asubuhi nikaenda zangu kazini. Katika kuulizauliza, nikaelekezwa kwa mganga mmoja ambaye niliambiwa alikuwa hodari kwa kutatua matatizo ya majini. Nikaenda. Nilipokuta mganga mwenyewe alikuwa M-Pemba, nikapata matumaini kwa sababu nilisikia Wapemba ni wataalamu sana wa majini.
“Una tatizo gani?” mganga huyo akaniuliza aliponikaribisha kwenye chumba chake.
Nikamweleza tatizo langu.
“Huyo ni jini Ummy Subiani mwenye tabia ya kuchunuka watu. Majini hao wanawake huwapata binadamu wanaume, na majini kama hao wanaume huwapata wanawake,” mganga akaniambia.
Mganga akaendelea kuniambia:
“Aghalabu, majini hao wanakuwa matajiri na huwapa watu utajiri wenye masharti. Ukikiuka masharti yake, anachukua utajiri wake.”
“Ninakubali. Huyo msichana ni tajiri sana. Hilo jumba lake analoishi Dar sijawahi kuona mfano wake. Ni jumba la kifahari na ameniahidi kunijengea nyumba na kuninunulia gari.”
“Sasa tatizo lako wewe ni nini?”
“Tatizo langu sihitaji mke wa kijini wala sihitaji utajiri wenye masharti. Kuna mtu ameniambia alimuulia mke wake. Alimdanganya kuwa hana mke, kumbe alikuwa naye.”
“Tatizo lake ndiyo hilo. Hataki kudanganywa na hataki mke mwenzake. Ukiwa naye, usitongoze msichana yeyote. Ana hasira, anaweza hata kumuua msichana wako au kukuua wewe.”
“Na aende zake. Bora nibaki na umasikini wangu, lakini niishi kwa amani.”
“Kwa hiyo humtaki huyu jini?”
“Simtaki na sitaki anifuate tena.”
“Ninunulie mbuzi mweusi na kitambaa cha sanda mita saba.”
“Na kazi yenyewe itagharimu kiasi gani?”
“Utanipa shilingi laki tatu.”
“Unanihakikishia, mzee, huyu jini hatanifuata tena?”
“Hutamuona tena.”
“Sasa nilete lini hivyo vitu?”