Sitaki tena Urais – Sehemu ya 36
Muktasari:
- Nikashuka kitandani na kujifunga taulo. Nilitoka uani nikapiga mswaki na kuoga kisha nikarudi chumbani mwangu. Zena alikuwa bado amejinyoosha kitandani.
Ilikoishia
Nikashuka kitandani na kujifunga taulo. Nilitoka uani nikapiga mswaki na kuoga kisha nikarudi chumbani mwangu. Zena alikuwa bado amejinyoosha kitandani.
Nilivaa nguo zangu. Nilipokuwa tayari nikamuuliza Zena.
“Kwahiyo?”
“Wewe nenda kazini kwako, tutaonana utakaporudi.”
“Sasa utakula nini?”
“Usijali Karim, nitakula tu.”
“Kwa kawaida nikitoka asubuhi ninarudi jioni lakini kwa sababu yako nitakuja mchana kukuangalia.”
“Sawa. Njoo tu.”
SASA ENDELEA
NIKAONDOKA na kumuacha Zena mle chumbani. Nilikwenda kazini kwangu nikiwa na mawazo mengi. Mawazo yangu yalihusu yule rafiki yangu aliyeniuliza usiku uliopita nazungumza na nani na jinsi Zena alivyoniambia rafiki yangu hawezi kumuona kwa vile sijamuoa.
Kilichojidhihirisha kwenye mawazo yangu ni kuwa Zena hakuwa binaadamu wa kawaida.
Hicho kilijidhihirisha kwa jinsi nilivyoona ameota vinywelea tumboni na kifuani kama mwanaume hali ambayo haikuwa ya kawaida kwa binaadamu mwenye jinsia ya kike.
Mawazo yangu pia yalihusu vile nilivyoshituka usiku na kusikia sauti yake ikitokea nyuma ya nyumba. Nikajiuliza Zena alikuwa akizungumza na nani wakati alikuwa ni mgeni katika nyumba ile. Ni nani aliyekuwa akimwambia
“Nimeshakwambia neda katekeleze kazi niliyokutuma. Usirudi tena kunisumbua. Mume wangu mtarajiwa amelala, sitaki kumwamsha.”
Halafu ilikuwaje ile taa ya chumbani ikazimika yenyewe na ghafla nikapitiwa na usingizi?
Kama hivyo havitoshi, niliendelea kuwaza, ni kwanini aniambie sitamfaidi mpaka nimuoe? Jibu la swali hilo lilikuwa rahisi. Muda ule aliponiambia hivyo nililala nikaota ninafanya naye mapenzi.
Kinachojionesha ni kuwa Zena hataruhusu nifante naye mapenzi ya waziwazi mpaka nimuoe.
Nikaendelea kujiuliza. Nitamuoaje msichana wa aina ile ambaye tabia zake haziko kibinaadamu?
Nikajiambia ninapaswa nifanye uchunguzi nijue Zena alikuwa jini au mchawi. Kama ni jini, niliendelea kujiambia, nilipaswa kumkimbia haraka. Au kama ni mchawi pia sitoweza kuendelea kuwa naye.
Nilipofika kazini kwangu nilifanya kazi hadi saa saba mchana. Ule muda wa kwenda kula chakula nikarudi nyumbani. Niliujaribu mlango nikakuta umefungwa kwa ndani. Nikaugonga. Baada ya muda kidogo mlango ukafunguliwa. Nikaingia ndani.
Zena alikuwa amesimama kando ya mlango akiwa amejifunga shuka za kitandani.
“Yaani bado umelala tu.?” Nikamuuliza.
“Sasa nifanyeje Karim, niende wapi wakati nimekuja kwako?”
“Utachoka haraka.”
“Siwezi kuchoka, nimeshazzoea kukaa ndani.”
“Sasa kuhusu kula. Utakula nini?”
“Nitakula chakula. Usijali nitatoka kwenda kula chakula.”
“Utakwenda kula wapi?”
“Mwenye bodaboda atanipeleka kwenye hoteli safi halafu atanirudisha.”
“Sawa. Nimekuja mara moja tu kukutazama. Ninarudi zangu kazini. Ukitoka utafunga mlango.”
“Ninajua. Siku hizi wizi mwingi.”
“Haya natoka.”
“Nenda urudi salama mpenzi wangu.”
Wakati nataka kugeuka, Zena aliwahi kunishika akashumu kwenye shavu langu kisha akaniachia.
“Nimekutia nguvu za kwenda kazini.”
“Na kweli. Mwili umenisisimka.”
Zena akacheka nikageuka na kutoka. Wakati natembea kurudi kazini nilikuwa nikijiambia. “Zena nampenda lakini nina wasiwasi naye, si binaadamu wa kawaida.”
“Ana umbo zuri, ana pesa na ana mapenzi,” nilijiambia hizo ndizo sifa anazotakiwa awe nazo mwanamke na Zena anazo.
Ghafla nikasikia sauti ya msichana akiniita nyuma yangu.
“Karim,”
Nikasimama na kugeuka nyuma. Nikamuona msichana mmoja niliyekuwa nikimfahamu ambaye zamani alikuwa akiishi jirani na nyumba ninayoishi. Alikuwa akiitwa Halima.
“Karim vipi?” Akaniuliza aliponifikia.
“Safi. Niambie….”
“Unakwenda wapi?”
“Nakwenda kazini.”
“Ngoja tufuatane. Na mimi naelekea huko huko.”
Tukawa tunatembea huku tunazungumza.
“Naona umependeza, unaelekea wapi?” Nikamuuliza.
“Niko kwenye mishe zangu. Mwenzangu si unajua ninakopesha.”
“Unakopesha nini?”
“Vitu mbalimbali, viatu, mikoba na nguo.”
“Duka lako liko wapi?”
“Napitishia wateja wangu majumbani na maofisini.”
“Mbona uko mikono mitupu?”
“Leo nakwenda kudai tu.”
“Hebu nipe namba yako.”
Halima akanipa namba yake. Nikaitia kwenye simu yangu kisha nikampigia hapo hapo.
“Namba yangu ndiyo hiyo. Iko siku naweza kuhitaji kitu nikakupigia.”
“Sawa.”
Tulipofika mbele kidogo tukaachana. Yeye alikata kushoto mimi nikaendelea na safari.
Nilipofika kazini kwangu Halima akanipigia simu.
“Karim. Pale tulipoachana tu ametokea msichana mmoja ameniambia eti wewe ni mpenzi wake. Akaniuliza tulikuwa tunaongea nini?”
Moyo wangu ukapiga kwa kishindo.
“Ni msichana gani huyo?” Nikamuuliza.
“Aliniambia eti anaitwa Zena.”
“Alipokuuliza hivyo ulimjibu nini?”
“Nilimwambi asiniulize mimi, aje akuulize wewe kama ni mpenzi wake. Nilipomwambia hivyo akanitolea ukali na kunitishia maisha yangu. Ameniambia eti nikukome. Na mimi nimemwambia utakomesha wasichana wangapi. Yaani anadhani wewe ni mwanaume wangu.”
“Zena ninamfahamu. Achana naye, ana wivu mwingi.”
“Sasa wewe ndio umkomeshe yeye asione kila msichana unayesimama naye mwanamke wako.”
“Nitamwambia, samahani sana.”
Halima akakata simu. Nikawa najiuliza Zena nimemuacha nyumbani amejuaje kama nilikuwa nimefuatana na msichana na alifikaje mahali nilipoachana na Halima?
Hapo shaka yangu kwake ikazidi kuongezeka. Jioni nilipokuwa narudi nyumbani nilikuwa nimeshapanga maneno ya kumwambia Zena andapo ataniuliza nilikuwa nimefuatana na nani.
Nilipofika nyumbani nikamkuta Zena bado amelala.
“Habari ya saa hizi?” Nikamsalimia.
“Nzuri. Na wewe habari ya kazini?”
“Pia ni nzuri.”
Nikakaa kwenye kochi langu.
“Ulikwenda kula chakula?”
“Sijatoka bado. Nimeona nitoke usiku.”
Maneno yake yakanishangaza kidogo. “Kama hajatoka, Halima alikutana na msichana gani?” Nikajiuliza.
“Kama nakumbuka vizuri aliniambia msichana mwenyewe anaitwa Zena.” Nikawaza.
“Yaani utashinda na njaa hadi usiku?” Nikamuuliza Zena huku moyoni mwangu nikiyawaza yale maneno ya Halima.
“Haina tatizo. Sipendi kula sana naogopa kunenepa.”
“Subiri nikakununulie chips.”
“Hapana, usisumbuke. Chips tutakula usiku.”
“Lakini ujue kuwa unajitesa.”
“Sijitesi. Mimi sipendelei kula sana mchana. Nielewe Karim. Mbona uko hivyo?”
“Una maana hujatoka humu chumbani?”
“Sijatoka.”
“Mbona niliona mtu kama wewe barabarani?” Nilijaribu kuchota akili yake.
“Si kweli. Sijatoka bado.”
Nikaguna. Sijui kama Zena alinielewa ninaguna nini lakini wewe unayenisoma umeshaelewa.
Tukaendelea kuzungumza na Zena hadi usiku lakini hakukubali kutoka mle chumbani hadi ilipofika saa sita usiku watu wakiwa wamelala ndipo nilitoka naye uani. Akaenda bafuni kuoga. Alipomaliza nilirudi naye chumbani akavaa kisha akaniambia tutoke. Nikatoka naye.
Tulikodi bajaj tukaenda katika hoteli ile ile tuliyokwenda usiku wa jana yake, tukala chipsi na nyama ya kuku hadi tukashiba. Tukarudi tena nyumbani. Tulipoingia chumbani kumbukumbu zangu zilikuwa kwenye kuvua nguo, kilichoendelea baada ya hapo sikukijua.
Nikiwa nimelala nikaota niko na Zena kwenye ufukwe wa bahari ya Zanzibar tunafanya mapenzi. Asubihi alianiamsha yeye Zena.
“Umeamkaje?” Akaniuliza.
“Nimeamka vyema, sijui wewe.”
“Mimi pia nimeamka vyema. Nilitoka peke yangu wakati wa alfajiri nikaenda kuoga kabisa. Unajua hii asubuhi ninaondoka kurudi Dar.”
“Unaondoka leo?” Nikamuuliza.
“Naondoka leo.”
“Subiri na mimi nikaoge.”
“Nenda kaoge.”
Nikatoka uani kwenda kuoga. Niliporudi chumbani nilimkuta Zena ameshavaa. Na mimi nikavaa nguo zangu. Nilipomaliza kuvaa nikamuuliza Zena kama alikuwa tayari tutoke.
“Mimi niko tayari ila…”
“Ila nini…”
“Zawadi zangu. Tulikubaliana nikija Morogoro siku ya kuondoka utanipa zawadi au umesahau?”
“Nakumbuka ila umenishitukizia sana. Ilipasa uniambie tangu jana kuwa leo utakwenda zako ili nikuandalie zawadi.”
“Hii si mara ya mwisho. Nitakuja tena. Zawadi zangu niwekee.”
“Kwa hapo tumeelewana.”
Tukatoka. Tulikodi bajaj tukaenda hadi stendi ya mabasi. Nikamkatia Zena tikiti. Alipopokea tikiti akanipa shilingi milioni moja.
“Chukua hii, itakusaidia,” akaniambia.
Nikazipokea pesa hizo na kumwambia.
“Asante.”
“Kumbuka kwamba nitakuja tena Moro hivi karibuni.”
“Karibu sana.”
“Nakushukuru kwa ukarimu wako.”
“Na wewe pia nakushukuru kwa wema wako.”
“Asante.”
Wakati wote tukizungumza, tabasamu lilikuwa kwenye uso wa Zena. Nikamsindikiza ndani ya basi na kuzungumza naye hadi muda wa safari ulipowadia, nikaagana naye na kutoka.