Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sitaki tena Urais – Sehemu ya 34

RAIS 34 Pict

ILIKOISHIA

Zena akakasirika. Alisogea karibu akampiga kibao yule kijana aliyekuwa ananizunguka kisha akampiga na yule aliyekuwa ananipimisha jinzi.

“Wapumbavu nyie, mnataka kumuibia nani?”

Vile vibao alivyowapiga wale vijana vilisikika kwa sauti. Vilikuwa vibao vya mwanamke lakini viliwatikisa wale vijana wakayumba na kupiga kelele za maumivu.

“Twendezetu.” Zena aliniambia huku akinishika mkono.

Tukaondoka. Wale vijana walibaki pale pale wakiyumba na kupiga kelele huku wamejishika mashavu. Mlio wa vile vibao uliendelea kujirudia kama vile Zena alikuwa akiendelea kuwapiga.

SASA ENDELEA



Tulipopiga hatua kama kumi hivi niligeuza uso nikatazama nyuma. Wale vijana waliendelea kubaki pale pale wakipiga kelele kama vile walikuwa akiendelea kupigwa.

“Acha niwashikishe adabu. Wakituona tena watatukoma.” Zena aliniambia. Akaendelea kusema.

“Wao kila mtu wanamvamia. Hawajui humu kuna majini lakini wapo kama watu, kuna wachawi na kuna waganga….”

Maneno yale yakanishitua kidogo. Nikawa najiuliza, “Sasa wewe Zena ni jini au mchawi au ni mganga?”

Nikamtazama usoni. Nilimuona alikuwa binaadamu tu kama binaadamu wengine. Nikafikiri kwamba labda alikuwa mganga.

Nilishawahi kukutana na waganga wakiwa ni wasichana warembo kama Zena. Niliwaza huenda Zena alikuwa mganga wa kienyeji lakini hajaamua kuniweka wazi.

Vituko alivyokwisha nionesha tangu nikutane naye vinaonesha kwamba alikuwa na miujiza fulani kama mganga.

Zena akaniambia tuingie katika duka moja tukaingia. Lilikuwa duka la mavazi ya kiume. Kulikuwa na kila kitu kinachomfaa mwanaume mashati, tisheti,suruali, jinsi, viatu na vitu vingine.

“Chagua nguo unazozipenda nikununulie,” akaniambia.

Nilikuwa mbovu wa jinzi na tisheti. Katika duka hilo mlikuwa na vitu vikali vitupu. Jinzi na tisheti zilizokuwemo humo sikuwahi kuziona huko kwetu ingawa ni karibu na Dar.

Lakini bei ilikuwa haishikiki. Jinzi zilikuwa zinaanzia elfu hamsini kwenda juu. Tisheti elfu arobaini kwenda juu. Hakukuwa na kitu cha elfu thelathini.

Kwa vile na mimi pesa nilikuwa ninazzo nikachagua jinzi tatu, tisheti tano na viatu jozi mbili.

Pesa hizo alizilipa Zena peke yake.

“Hutaki manukato. Hupendi kunukia kama mimi?” Akaniuliza.

“Ninayataka.”

Zena akaninunulia manukato fulani ambayo bei yake ilikuwa shilingi laki  moja na nusu. Aliniambia yalikuwa ni mchanganyiko wa aina tatu za manukato bora duniani.

Baada ya kutia vitu vyangu kwenye begi tukatoka humo dukani tukaanza safari ya kurudi. Tulitokea mahali pale pale ambapo Zena aliwapiga vibao wale watu. Tulikuta kundi kubwa la watu na tuliwakuta wale vijana wawili wakiendelea kulia.

Walikuwa wakisema walikuwa wakimuona yule msichana akiendelea kuwapiga vibao na vilikuwa vinauma. Mashavu yalikuwa yamewavimba kwa maumivu.

“Twendezetu.” Zena aliniambia alipoona nilikuwa nimeshangaa nikiwatazama watu hao.

“Wale wataendelea kupigwa mpaka watakufa.” Zena akaniambia wakati tunakwenda.

“Hivi mwisho wao wale vijana ni kifo?”

“Wewe ulitaka wawe na mwisho gani?”

“Mimi nauliza tu.”

“Na mimi pia nimekuuliza ulitaka wawe na mwisho gani?”

Nikapata hofu kushindana naye. Nikaona tuachane na habari ile.

“Tufanye kama yamekwisha.”

“Unapozungumza na mimi jaribu kuwa huru kunieleza kile unachohisi.”

“Nimeona maneno yenyewe hayana maana.”

“Wale ni wezi na ni wachawi wanaokopera pesa za watu. Walikuwa wameshakuchomolea shilingi milioni moja.”

“Ni watu wabaya hasa ukizingatia ni vijana kama mimi. Wameshindwa kutafuta kazi za kuendesha maisha yao, wamekuwa wapumbavu.”

“Unadhani wale ni watu wa kuwahurumia?”

“Hapana.”

“Hivi ndivyo mimi nilivyo. Roho yangu ina utu na ina unyama. Ukinifanyia unyama utakuwa umenipeleka kule ninakokutaka. Kama wewe huko hivyo nisamehe sana.”

Nikabaki kimya wakati Zena akisema maneno yake.

“Tuchukue tena bajaj twende stendi ya Ubungo.” Zena akaniambia. Wakati ule stendi ilikuwa bado iko Ubungo.

“Sawa. Tuchukue.”

“Nilitaka tuje huku Kariakoo nikununulie zawadi kidogo.”

“Asante. Nakushukuru sana.”

Zena akasimamisha bajaj. Bajaj iliposimama tukaenda kuipanda.

“Tupeleke Ubungo.” Zena akamwambia mwendesha bajaj.

Wakati bajaj inatupeleka Ubungo Zena aliniambia.

“Na mimi nikija Morogoro uninunulie zawadi.”

“Sawa. Nitakununulia.”

Zena akacheka. “Utapata wapi pesa za kuninunullia zawadi?”

“Hizo hizo ninazopata kazini kwangu.”

“Na mimi pia nitakushukuru.”

Baja ilipotufikisha Ubungo tuliingia ndani ya basi la Morogoro mimi na Zena. Tukakaa kwenye siti kama vile tulikuwa tunasafiri sote, Tukazungumza mpaka basi lilipokuwa linakaribia kuondoka ndipo tulipoagana na Zena akashuka.

Siku ile nilirudi Morogoro huku kichwa changu kimejaa kumbukumbu za Zena. Nilipofika Morogoro nikaenda nyumbani nilikopanga chumba. Nikawa na mawazo mengi kuhusu Zena. Usiku wake wakati nimelala nikaota niko kwenye msitu nikitembea, nikatokea katika eneo lenye majabali. Jua lilikuwa kali na majabali yalikuwa yakichoma nyayo zangu.

Nikafika mahali nikaona jabali moja lilikuwa na tundu kubwa. Nikaona nijiingize kwenye tundu hilo nipumzike jua. Nikaingia na kukaa mahali palipokuwa na kivuli. Ghafla nikaona joka kubwa nalo linajiingiza katika tundu hilo. Nikajisemea kimoyomoyo sasa nakufa.

Lile joka liliponiona likaniuliza.

“Umefuata nini katika nyumba yangu?”

Kwa sababu ya hodu sukuweza kulijibu nikabaki nimelikodolea macho nikilitazama.

“Si nakuuliza wewe, umefuata nini katika nyumba yangu, hujui kama hii ni nyumba yangu?”

Nikasikia sauti ya Zena ikisema.

“Mwache nimemkaribisha mimi.”

Ghafla lile joka sikuliona tena, nikamuona Zena amekaa na mimi akinipapasa mwili wangu. Ghafla tena nikaona tumelala kwenye michanga ufukweni mwa bahari. Ghafla tena nikaona tunafanya mapenzi.

Pale nilipokuwa nataka kumaliza tendo hilo nikazinduka usingizini na kujiona niko kitandani kwangu. Ndoto ile ilifanya nisilale tena usiku huo. Asubuhi kulipokucha nikaenda zangu kazini. Zikapita kama siku tatu hivi. Zena akanipigia simu. Ilikuwa asubuhi nataka kwenda zangu kazini. Nikaona simu inaita.

Nikaipokea. “Hello.”

“Karim hujambo?”

“Sijambo. Na wewe hujambo?”

“Sijambo. Vipi hali?”

“Hali ni nzuri. Ningali nakutarajia.”

“Nitakuja leo.”

“Utakuja saa ngapi?”

“Nafikiri nitakuja usiku ili nisikusumbue. Kwa hiyo jiandae kuwa na mgeni leo.”

“Utakuja usiku saa ngapi?”

“Sijajua ila wewe zingatia nitakuja usiku.”

“Sasa nitakupokea wapi?”

“Sihitaji kupokewa.”

“Sasa utapajuaje nyumbani kwangu?”

“Nitapajua tu, usiwe na wasiwasi.”

“Mmmh….” Niliguna kimoyomoyo nikabaki kimya.

“Tutaonana hapo usiku.” Zerna akaniambia na kukata simu.

Nikaenda zangu kazini. Zena nilikuwa nampenda sana lakini vituko vyake vilikuwa vinanikosesha amani.

Jua lilipokuchwa nikaenda stensi ya mabasi kumsubiri Zena aliyeniambia atakuja usiku. Niliendelea kukaa hapo stendi nikumulika mabasi yanayotoka Dar hadi ikafika saa nne usiku. Sikumuona Zena.

Nikampigia simu ili nimuulize kama amehairisha safari yake. Simu yake haikupatikana. Nikaamua kurudi nyumbani.

Nilipofika nyumbani nikajipekua mifukoni kutazama funguo ya mlango wangu. Sikuiona. Nikashituka na kujiuliza nimeitupa wapi? Nikapenua pazia la mlangoni kwangu. Nikauona ufunguo kwenye kitasa cha mlango. Nikashituka tena na kujiuliza kama niliusahau hapo ufunguo huo tangu asubuhi. Sikupata jibu.

Nikausukuma mlango. Mlango ukafunguka. Vile mlango unafunguka kupuo la manukato anayonukia Zena likanipiga usoni. Kutupa macho humo chumbani nikamuona Zena amejilaza kitandani pangu.

Alikuwa amegeukia upande wa mlangoni akinitazama. Macho alikuwa ameyapaka wanja na sehemu ya nyusi pia aliipaka wanja. Uso wake ulikuwa umenawirika kama vile alikuwa anatoka saluni.

Nilishituka sana nilipomuona. Nikamuita.

“Zena…”

Akaniitikia kistaarabu.

“Abee…”

“Ndiye wewe?”

“Ni mimi. Kwani unamuona nani?”

“Ninakuona wewe lakini nashangaa umefikaje humu?”

“Kwani nilikwambiaje kwenye simu?”

“Uliniambia utakuja nyumbani mwenyewe.”

“Si ndiyo hivyo sasa nimekuja.”

“Unajua ninatoka stendi kukusubiri wewe tangu saa moja.”

“Umetaka mwenyewe kujisumbua. Nilikwambia usije kunipokea.”

“Niliona usingeweza kufika hapa nyumbani wewe mwenyewe.”

“Nbona nimefika?”

“Sasa sijui nikujibu nini, yaani nimeshituka kukuona hapa kwani sijui umefikaje?”

“Nimefika kwa kutumia akili yangu wala usishituke kamwe.”

“Huu ufunguo uliofungulia mlango uliupata wapi?”

Zena akacheka. “Niliuona hapo hapo kwenye mlango nikafungua na kuingia.”

“Ufunguo niliondoka nao asubuhi.”

“Sasa kama uliondoka nao niliupataje?”

“Kwa kweli siwezi kujua uliupataje? Kwa maana nina maswali mengi, hata hiki chumba changu ulikijuaje?”

“Una maswali mengi kweli. Mimi nilifikiri ungefurahi kuniona chumbani mwako, kumbe unanikaribisha kwa maswali kama mhalifu niko polisi.”

“Hapana. Mbona nimefurahi sana kukuona, wewe hujui tu.”