Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sitaki tena Urais – Sehemu ya 32

Muktasari:

  • Nikaingia bafuni  na kuivua nguo yangu ya ndani na kujimwagia maji.. Baada ya kuoga nilijifuta maji nikavaa tena ile nguo yangu ya ndani na kutoka.

“Umekwenda kuoga peke yako?” Nikamuuliza.

“Naona mwenyewe bado umelala.”

“Ngoja na mimi nikaoge.”

Nikainuka na kuelekea bafuni.

“Taulo iko huko huko,” akaniambia.

Nikaingia bafuni  na kuivua nguo yangu ya ndani na kujimwagia maji.. Baada ya kuoga nilijifuta maji nikavaa tena ile nguo yangu ya ndani na kutoka.

Nilimkuta Zena ameshavaa. Alikuwa amekaa nyuma ya kioo akipaka wanja macho yake.

Nilichukua begi langu nikatoa nguo zangu za akiba. Nilitoa suruali aina ya jinzi na Tsheti ya rangi ya bluu nikavaa.

Baada ya kuvaa nikaenda kusimama nyuma ya Zena na kumshika bega.

“Macho yamekushughulisha sana.”

“Napaka wanja.”

“Naona unatumia muda mrefu kuweka wanja.”

“Nimeshamaliza.”

Zena aliinuka akanigeukia na kuweka mikono yake miwili kwenye mabega yangu. Akanitazama usoni.

Nilipoyatazama macho yake yaliyokuwa yamekolezwa kwa wanja mzito mweusi, nilijihisi kama ninalewa pombe kwa jinsi macho hayo yalivyokuwa na mvuto wa ajabu.

“Umependeza,” nikamwambia.

“Asante. Ulikuwa ukiniambia ninapoteza muda mwingi, si nilitaka kukupendezesha wewe…”

“Sasa nimeona. Nikikutazama naona kama ninalewa pombe.”

“Hujawahi kupenda mwanamke?”

“Sijawahi kupenda mwanamke kama wewe.”

“Na hutawahi kwa sababu hutapata mwanamke mwingine kama mimi wala wa aina yangu.”

“Kwanini?”

“Utampata wapi mwanamke wa aina yangu?”

Sikumjibu nikawa namtazama. Baada ya kimya kifupi nikamuuliza.

“Niambie wewe ni nani?”

“Ukimchunguza sana kuku hutamla. Nitakuja kukwambia siku nyingine.”

“Kwani huwezi kuniambia sasa hivi?”

“Wewe bado mtoto sana. Una umri gani?”

“Kama miaka ishirini na mitano hivi.”

“Bado mtoto sana wewe ndio maana unauliza mambo unayoyaona. Hebu twende tukakae sebuleni.”

Msichana huyo akaiondoa mikono yake mabegani mwangu akanishika mkono wangu tukatoka kuelekea sebuleni.

“Tukae hapa.”

Tukakaa kwenye sofa refu.

“Una mpango gani na mimi au unataka kunichezea tu halafu urudie wasichana zako.”

“Mimi sina wasichana wowote.”

“Una maana huna wasichana huko Morogoro?”

“Sina.”

“Kama unao nitawakomesha.”

“Hivi huamini ninavyokwambia?”

“Siamini. Wanaume hawaaminiki lakini nitakuja kuona mwenyewe kwani nitakuja Morogoro.”

“Utakuja lini?”

“Siku nitakayoamua. Sasa niambie una mpango gani na mimi?”

Nikapata kigugumizi kumjibu.

“Kwani umenipenda?” Akaniuliza alipoona simpi jibu.

“Nimekupenda sana lakini naona kama unanificha kitu.”

“Umesema umenipenda sana, utanioa?”

“Sitamudu gharama ya kukuoa wewe.”

“Kwani mimi nina gharama gani jamani?”

“Si unaona maisha yako.”

“Maisha yangu yana nini?”

“Unaishi maisha ya hali ya juu, Mimi mwenzako ni masikini.”

“Sikiliza nikwambie, mapenzi hayana utajiri wala umasikini. Mapenzi ni mamlaka ya kipekee kabisa. Kama watu mmependana, utajiri na umasikini unakuwa hauna nafasi.”

“Ni kweli lakini kwa hali yangu itakuwa vigumu kukuoa wewe.”

“Si nimekupenda mwenyewe, ugumu unatoka wapi? Kwani kunioa mimi kuna gharama gani?”

“Yaani mimi sitamudu hata ile gharama ndogo na isitoshe sina maisha ya kuishi na msichana kama wewe.”

“Sasa nikwambie, kila kitu katika maisha yetu kitakuwa juu yangu mpaka gharama ya kunioa mimi itakuwa juu yangu.”

“Mahari?”

“Mahari yangu nitatoa mimi kukupa wewe. Niambie unataka shilingi ngapi?”

Nikaona Zena alikuwa akinieleza habari ya mzaha nikacheka.

“Mbona unacheka?”

“Sasa utatoaje mahari wewe wakati mimi ndio nakuoa wewe?”

“Nitatoa mimi kwa sababu wewe huna.”

“Sikiliza nikwambie, kama uko ‘serious’ nipe mimi hizo pesa halafu mimi nikutolee mahari.”

“Basi hakuna shaka, nipe mkono.”

Zena akaninyooshea mkono wake na mimi nikampa mkono wangu. Tukashikana mikono.

“Unatarajia kurudi Morogoro saa ngapi?” Akaniuliza.

“Muda wowte tu.”

“Unaonaje kama utalichukua begi lako kabisa uwe nalo mwenyewe.”

“Naweza kulichukua mwenyewe.”

“Nenda kalichukue.”

Nikainuka na kuingia mle chumbani tulimolala. Nilitia nguo zangu kwenye lile begi nikalifunga zipu na kulivaa mgongoni. Nilipotoka sebuleni Zena aliniuliza.

“Umeweka nguo zako zote?”

“Ni shati moja tu na suruali.”

“Umesahau kitu.”

“Kitu gani?”

“Katizame mchagoni mwa kitanda utakiona.”

Nikarudi tena mle chumbani huku nikijiuliza nimesahau nini.

Nilipotazama mchagoni mwa kitanda nikaona ile simu yangu.

“Nimesahau simu,” nikasema huku nikinyoosha mkono na kuichukua.

“Nilisahau simu,” nikamwambia Zena nilipokwenda sebuleni.

“Si nimekwambia umesahau kitu.”

“Umejuaje?”

“Naweza kukwambia pia umesahau hela zako kwenye suruali uliyovaa jana ambayo umeitia kwenye hilo begi.”

Nikajipapasa kwenye mifuko.

“Ni kweli. Pesa nimeziacha kwenye ile suruali.”

Nikalivua begi hilo mgongoni.

“Ziache nitakupa pesa zingine, si umeniambia huna pesa.”

“Ni kweli sina pesa.”

“Basi ziache nitakupa zingine.”

Nikalivaa tena begi langu.

“Unataka shilingi ngapi?”

“Zozote utakazotaka.”

“Hebu kaa.”

Nikakaa kwenye lile sofa.

“Mimi sitaki unijibu hivyo. Niambie unataka shilingi ngapi nikupe?”

“Shilingi milioni moja.”

“Shilingi milioni moja zitakutosha?”

“Zitanitosha.”

“Nikupe kabisa?”

“Ndiyo, nipe.”

“Nitakupa.”

Zena akainuka kwenye sofa alipokuwa ameketi akaingia mle chumbani. Baada ya dakika moja tu akatoka akiwa ameshikilia noti mkononi mwake.

Alikuja hadi pale nilipokuwa nimeketi akanipa zile pesa.

“Hizo ni milioni moja ulizotaka. Sema tu pesa zangu tumia mwenyewe, usimuhonge mwanamke mwenzangu. Umenielewa?”

“Nimekuelewa.”

“Zihesabu lakini nataka sharti langu hilo ulizingatie sana.”

“Sawa?”

Nikawa nazihesabu zile noti. Zilinichukua kama dakika tatu kumaliza kuhesabu. Ningekuwa mfanyakazi wa benki ingenichukua chini ya dakika moja kumaliza kuzihesabu.

Wakati nikihesabu, Zena alikuwa amenishikia tama akinikodolea macho.

Nilipomaliza kuhesabu nilimwambia.

“Ziko sawa.”

“Ziko sawa shilingi milioni moja?”

“Ndiyo.”

“Zitie mfukoni kabisa.”

Nikavuta juu suruali nikitaka kuzichomeka kwenye soksi.

“Mbona unataka kuziweka huko?”

“Naweza kuibiwa kwenye basi.”

“Nani alikwambia kwamba pesa zangu zinaibika?”

Tayari nusu ya pesa hizo nilikuwa nimezichomeka kwenye soksi ya mguu mmoja.

“Haziibiki?” Nikamuuliza kwa mshangao.

“Haziibiki.”

“Kwanini?”

“Wewe amini hivyo tu.”

Niliweka nusu nyingine ya pesa hizo kwenye soksi ya mguu mwingine.

“Pesa za nauli na pesa za kutumia njiani unazo mfukoni au utakuwa unatoa hapo hapo?” Akaniuliza.

“Ninazo mfukoni.”

“Sawa. Sasa naona twende zetu tukapate chai.”

“Tutakwenda kunywa chai wapi?”

“Pale tulipokula jana usiku.”

“Haya twende.”

Nikainuka. Zena naye akainuka na kunishika mkono. Katika hali ya kuonesha kunitamani alinigeukia na kunipiga kisi midomoni huku mkono wake mmoja akinipapasa kifuani kwangu.

Nikabaki nimeduwaa nikitabasamu.

“Si tunaagana. Utaondoka nyumbani kwangu hivi hivi tu?” Akaniambia.

Sikumjibu kitu akaendelea kuniambia.

“Nipige kisi na wewe lakini unishike kiuno, naweza kuanguka.”

Sikujivunga nikazungusha mikono yangu kwenye kiuno chake na kumpiga kisi. Alijisikia furaha akacheka. Alipocheka sura yake ilizidi kupendeza.

Tukaelekea kwenye mlango huku mkono wangu nimeuzungusha kwenye kiuno chake chembamba.

Tulipofika kwenye mlango akaniambia.

“Simama.”

Nikasimama na kumtazama. Yeye  pia alikuwa amesimama.

“Tutakapotoka utaona kitu si cha kawaida, nakwambia mapema usishituke.”

“Kitu gani?”

“Utakiona ila usishituke.”

“Sawa.”

Tukatoka kwenye mlango lakini sikuona kitu chochote. Lakini tulipokuwa tunatoka kwenye geti aliniambia nitangulie mimi. Nilipotoka nikajiona niko chini ya ule mti ambao usiku wa jana yake niliupanda kumsubiri Zena. Lile jumba sikuliona tena.