Sitaki tena Urais – Sehemu ya 33
ILIKOISHIA
Nikasimama na kumtazama. Yeye pia alikuwa amesimama.
“Tutakapotoka utaona kitu si cha kawaida, nakwambia mapema usishituke.”
“Kitu gani?”
“Utakiona ila usishituke.”
“Sawa.”
Tukatoka kwenye mlango lakini sikuona kitu chochote. Lakini tulipokuwa tunatoka kwenye geti aliniambia nitangulie mimi. Nilipotoka nikajiona niko chini ya ule mti ambao usiku wa jana yake niliupanda kumsubiri Zena. Lile jumba sikuliona tena.
SASA ENDELEA
Nikamuona zena akimalizia kushuka kwenye mti huo. Alikuwa Zena yule yule aliyevaa nguo zilezile.
Alipomaliza kushuka kwenye mti huo akaniambia.
“Twenzetu.”
“Mbona tumetokea hapa?” Nikamuuliza kwa mshangao.
“Si nilishakwambia kuna kitu utakiona lakini usishituke, au umesahau?”
“Nakumbuka lakini sikujua kama ingekuwa hali hii nilioiona.”
“Kila kitu kina maana yake.”
“Maana yake nini sasa?”
“Tuzungumze huku tunatembea.”
Tukaanza mwendo kuelekea barabra kuu.
“Lile jumba lako pia halipo tena,” nikamwambia.
“Sio halipo tena, sema halionekani tena.”
“Ni kwanini?”
“Nimekwambia kila kitu kina maana yake.”
“Ungenieleza nipate kuelewa.”
“Ninalinda jumba langu. Linaonekana usiku tu na pale kwenye mti ndio kuna mlango wangu. Ule mti uko kwenye kiwanja changu. Huoni hata jana usiku tulikutana juu ya mti ule.”
“Ndiyo nashangaa, inawezekanaje?”
“Utajua kila kitu. Fanya subira tu.”
Tukafika kwenye kituo cha daladala. Tukapanda tena pikipiki moja. Zena alitangulia kupanda, nikakaa nyuma yake. Sijaona msichana aliyekuwa akinukia utamu kama huyu. Nilishawahi kusikia harufu ya manukato mbalimbali maishani mwangu lakini sijawahi kusikia harufu ya manukato anayonukia msichana huyu.
Halafu kunai ile harufu ya hewa ya mwili, mbali ya manukato. Msichana huyu alikuwa na hewa nayotamanisha.
Pikipiki ikatufikisha kwenye ile hoteli tuliyokwenda jana usiku. Tulipoingia Zena aliagiza chai na vipochopocho ambavyo vingine nilikuwa sijui jina lake. Pale nilijua sambusa na khabab na bajia. Vilikuwa vimetengezewa mchuzi wa pilipili.
Kitu kilichonishangaza vitu tulivyokulla vilikuwa vya kipuuzi lakini Zena alilipa shilingi elfu ishirini na tano. Elfu ishirini na tano huko kwetu Moro huzitumia kwa mlo wa kutwa nzima kwa siku mbili.
Wakati tunatoka hapo hoteli huku tumeshikana mikono, Zena aliniambia.
“Sipendi tuachane lakini imebidi uende zako.”
“Kwani si umesema utakuja Moro?”
“Lazima nije na ninakuja kukufuata wewe.”
“Utakuja lini.”
“Sikwambii nitakuja lini. Ila nitakuja na nitakuja ghafla. Siku ninaijua mwenyewe kama ni kesho au keshokutwa au mtondogoo.”
“Kwa hiyo ukifika Moro ndio utanipigia simu?”
“Sitakupigia, tutaonana tu.”
“Sasa utajua ninaishi wapi?”
“Nitajua, usiwe na wasiwasi.”
“Utajua vipi bila mimi mwenyewe kukufahamisha?”
“Kwani unanionaje?”
“Kwa kweli bado sijakuolewa vizuri.”
Zena akacheka na kunitazama usoni.
“Nikija huko Moro ndio utanielewa vizuri.”
Ikabidi nimuitikie. “Sawa.”
“Masharti yangu unayakumbuka.”
“Nayakumbuka.”
“Nieleze nimekupa masharti yapi?”
“Umeniambia nisiwe na mahusiano na msichana mwingine.’
“Na leo nimekupa masharti yapi?”
“Leo umeniambia hizi pesa ulizonipa nisije nikampa msichana yeyote, yaani nisizihonge.”
“Kwa hiyo umekubaliana na masharti yangu?”
“Ndiyo, nimekubaliana nayo.”
“Utayatimiza?”
“Nitayatimiza bila shaka yoyote.”
“Sawa. Mimi napenda watu wanaotimiza ahadi.”
Tulikuwa tuko nje ya hoteli.
“Tutakwenda kuachana Kariakoo. Twende Kariakoo.” Zena akaniambia.
“Sawa. Twende.”
“Tutakwenda kwa bajaj.”
Bajaj ilipokuwa inapita Zena akaipungia. Bajaj ikasimama.
“Twende tukapande.”
Tukaenda kupanda bajaj. Kwanza aliingia Zena kisha nikaingia mimi.
“Tupeleke Kariakoo.” Zena akamwambia mwendesha bajaj.
Bajaj ikaondoka. “Ni muda gani sasa hujawahi kufika Dar?”
“Nina muda mrefu kidogo.”
“Unalionaje jiji lilivyobadilika?”
“Limebadilika sana. Kwa mgeni kama mimi ninaweza kupotea.”
“Siku hizi kuna barabara za juu, utakwenda kuziona.”
“Nimeshaziona wakati ninakuja.”
“Jiji limebadilika sana.”
“Sana.”
“Lakini kuishi katika jiji hili lazima uwe na pesa. Kama huna pesa unapaswa kulihama jiji hili haraka.”
“Ni kweli. Kwa maana huo usafiri peke yake utakugharimu pesa nyingi.”
“Umeona eh…?”
“Lakini wewe unamudu kuishi katika jiji hili.”
“Kwanini?”
“Kwa sababu pesa si kitu kinachokusumbua.”
Zena akatabasamu. “Umejuaje?”
“Unaonekana. Maisha yako ni ya juu, sema huna usafiri wako mwenyewe.”
“Naweza kukununulia wewe gari.”
“Wewe je?”
“Silihitaji. Ningeweza kuwa nayo hata kumi.”
“Unaridhika tu kukodi bajaj, kukodi teksi, basi?”
“Ndiyo.”
“Sasa hilo gari utaninunulia lini?”
“Siku utakapolitaka.”
“Ninalitaka.”
“Hujasema. Hapa tuko katika mazungumzo mengine, tumegusia tu kuhusu hilo gari.”
“Ni kweli lakini gari ninalitaka.”
“Utalipata. Fanya subira.”
Tahamaki tukawa tumeingia Kariakoo.
“Tushushe hapa hapa.” Zena akamwambia mwendesha bajaj.
Bajaj ikasimama. Tukashuka. Zena alimlipa mwendesha bajaj tukaanza kutembea kwa miguu huku tukipishana na makundi ya watu mbalimbali.
Kando kando ya barabara tuliyokuwa tunapita kulikuwa na machinga wengi waliokuwa wameshika nguo. Nilikuwa nikizikodolea macho jinzi na tisheti mpaka vijana hao wakawa wanatufuata fuata kutuonesha nguo zao.
Kulikuwa na mahali ambapo nililazimika kusimama ili kutazama jinzi moja aliyonipa machinga mmoja niiangalie kama inanifaa. Wakati naangalia ile jinsi kulikuwa na kijana mwingine aliyekuwa ameshika mfuko akinizunguka huku akicheza.
Zena alikuwa amesimama mbele yangu akinitazama. Nikampungia mkono kumuita. Nilitaka nishauriane naye ninunue ile jinzi.
Akawa ananifanyia ishara ya mikono kwamba nisinunue, twendezetu.
Nikairudisha ile jinsi kwa machinga.
“Basi,” nikamwambia.
“Kwanini. Jinzi safi sana hii.”
“Sina pesa. Tajiri yangu amekataa.”
Machinga akachukua jinzi yake na kuondoka. Nikamfuata Zena.
“Sasa ulikuwa unafanya nini?” Zena akaniuliza huku amenishikia kiuno.
“Nilikuwa natazama ile jinzi.”
“Ulitaka kuinunua?”
“Ndiyo nilitaka kuinunua lakini wewe umekataa nikaiacha.”
“Wewe unajua mambo ya jiji hili?”
“Mambo gani?”
“Karim unaonekana kuwa mshamba. Hebu tazama zile pesa nilizokupa.”
“Zile shilingi milioni moja?”
“Ndiyo.”
Nikainama na kuivuta suruali yangu juu ili nizitoe zile pesa kwenye soksi. Nikashangaa nilipoona pesa hizo hazikuwepo. Nikatazama kwenye mguu mwingine. Pia hazikuwepo. Zimekwenda wapi wakati nilizipachika kwenye soksi?
“Mbona hazipo?” Nikamuuliza Zena.
“Mimi nataka nikuulize wewe, mbona unaniuliza mimi?”
“Nashangaa zile pesa sizioni wakati nilizitia kwenye soksi. Wewe mwenyewe pia uliona.”
“Wewe hujui mambo ya jiji hili. Wale wenzako wamekuchezea.”
Nikageuka nyuma.
“Wenzangu kina nani?”
“Yule aliyejifanya anakuuzia jinzi na yule mwenzake aliyekuwa ameshika mfuko huku anakuzunguka. Alikuwa anakukopera.”
Nikashituka na kujishika kichwa kwa mikono mwili.
“Mama yangu, yaani zile pesa zote zimekwenda?”
“Twendezetu. Wameruka patupu.”
“Sasa twendezetu vipi wakati pesa zetu zimechukuliwa?”
Zena akafungua mkoba wake na kutoa vibunda viwili vya noti.
“Pesa zako hizi hapa, shika.” Zena akaniambia huku akinipa vile vibunda vya noti. Nikabaki mdomo wazi.
“Si nilikwambia hizi pesa haziwezi kuibika hata kwa uchawi. Umeamini sasa?”
“Yaani imekuwaje?”
“Wamezikopera lakini hazikwenda kwao zimekuja kwangu.”
Nikawa nazitazama huku nikitabasamu.
“Kweli haziibiki.”
“Zitie mifukoni tu.”
Nikazichomeka mifukoni. Tukawaona wale vijana wakija mbio.
“Hao wanakuja,” nikamwambia Zena.
“Wameona pesa zimewakimbia, wanakufuata tena.”
Walipotufikia yule kijana mmoja akanizunguka tena. Yule mwenzake alisimama mbele yangu akinionesha lile jinzi.
“Rafiki yangu unaiacha hili jinzi. Saizi yako kabisa…”
Akawa kama anaipimisha kwenye kiuno changu.
Zena akakasirika. Alisogea karibu akampiga kibao yule kijana aliyekuwa ananizunguka kisha akampiga na yule aliyekuwa ananipimisha jinzi.
“Wapumbavu nyie, mnataka kumuibia nani?”
Vile vibao alivyowapiga wale vijana vilisikika kwa sauti. Vilikuwa vibao vya mwanamke lakini viliwatikisa wale vijana wakayumba na kupiga kelele za maumivu.
“Twendezetu.” Zena aliniambia huku akinishika mkono.
Tukaondoka. Wale vijana walibaki pale pale wakiyumba na kupiga kelele huku wamejishika mashavu. Mlio wa vile vibao uliendelea kujirudia kama vile Zena alikuwa akiendelea kuwapiga.