Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sitaki tena Urais – Sehemu ya 22

RAIS 22 Pict

ILIKOISHIA

Kabla ya kuifikia ofisi ya Master kulikuwa na sebule na hapo ndipo walipomkuta Master ameketi akiangalia tv iliyounganishwa na kamera iliyokuwa inamulika geti.

Tv hiyo ilikuwa ikimuonesha mlinzi aliyekuwa kando ya geti akisikitika peke yake. Pengine ni wa sababu ya wale makachero kumzidi nguvu na kuingia ndani.

SASA ENDELEA


WALIPOIONA ile tv makachero hao walitambua kuwa wakati wanazozana na yule mlinzi kwenye geti mtu huyo alikuwa akiwaona. Lakini hata hivyo hakuonesha kugutuka au kuwa na wasiwasi.

Alikuwa mtu mwenye maungo makubwa aliyekwishapituka umri wa miaka sitini. Uso wake mpana ulikuwa na ndevu zilizochongwa vizuri kwa mtindo wa O. Nywele zake zilikuwa ndefu zenye mvi na zilizokatwa vizuri.

Alikuwa amevaa suti nyeusi. Na katika mkono wake wa kulia alishika kifimbo kilichokuwa kinameremeta.

Kachero Shamla na mwenzake walipoingia katika sebule hiyo. Mtu huyo aligeuza kichwa taratibu na kuwatazama.

“Master!” Shamla akamuita akiwa na hakika kwamba alikuwa ni yeye.

“Nyinyi ni kina nani?” Mtu huyo aliwauliza kwa sauti tulivu. Lakini ilikuwa sauti nzito ya kukwaruza.

“Sisi ni maofisa wa polisi.” Shamla alimjibu huku yeye na kachero mwenzake wakitoa vitambulisho na kumuonesha.

“Mnataka nini hapa?”

“Tumekuja kukukamata wewe, kutoka sasa uko chini ya ulinzi!”

“Sawa. Subirini hapo hapo!”

Mtu huyo alinyanyuka haraka akaingia katika ofisi yake.na kufunga mlango.

“Tumfuate. Huwezi kujua atatoka na nini” Shamla akamwambia mwenzake.

Makachero hao waliharakisha kuingia katika chumba hicho. Walipofungua mlango tu walikutana na moshi uliouwa unapalia na kuwasha macho. Walishituka, wakauacha wazi mlango na kurudi nyuma.

“Moshi huu unatokea wapi?” Shamala akauliza huku akikohoa na kufinya macho. Kwa vile yeye ndiye aliyefungua ule mlango moshi huo ulimpata vizuri.

“Kuna kitu amechoma” Kachero mwenzake alimwambia.

“Kweli?”

“Sasa unafikiri ni moshi wa nini?”

“Bila shaka anataka tusimfuate”

Moshi huo ulikuwa unapungua.

“Unaona unaanza kupungua” Shamala akasema.

Walisimama hapo kando ya mlango kwa sekunde zisizopungua thelathini. Moshi huo ukaisha kabisa. Wakaingia tena ndani ya ile ofisi. Cha ajabu ni kwamba hawakukuta mtu yeyote. Ofisi ilikuwa tupu!

Kama kungekuwa na mlango mwingine wangehisi kuwa mtu huyo alitokea kwa mlango huo. Lakini hakukuwa na mlango mwingine. Pia hakukuwa na dirisha lenye uwazi wa kupenyeza hata paka achilia mbali mtu mzima!

Shamla na mwenzake wakatazamana.

“Jamaa hayumo!”

“Lakini si aliingia humu?”

“Sasa yuko wapi?”

“Hayumo!”

“Na ule moshi ulikuwa unatokea wapi?”

“Haijulikani!”

“Sasa hii ni miujiza. Twenzetu”

“Twende tukapekue katika vyumba vingine. Tunaweza kumkuta”

“Kama ameweza kutoweka hapa, hatashindwa kufanya hivyo katika vyumba vingine”

“Basi twenzetu”

“Inaonekana huyu hatutaweza kumkamata”

Walitoka katika ile ofisi wakiwa wametaharuki.

“Unafikiri nini kimetokea Shamla?”

“Sijui na mazingaombwe….sijui ni nguvu za giza…sijui ni nini!”

Walishuka ngazi na kutoka kwenye lango la jumba hilo.

Lile gari lililokuwa kwenye banda hawakuliona.

“Ile benzi imekwendawapi?” Shamla akamuuliza mwenzake.

“Ameshaondoka nayo!”

“Ngoja tumuulize mlinzi”

Walimfuata mlinzi huyo aliyekuwa ameketi kando ya geti.

“Ile benz nyeusi iliyokuwa kwenye banda iko wapi?” Shamla akamuuliza.

Mlinzi huyo alipotupa macho kwenye banda hilo alishituka.

“Oh! Sijui limekwenda wapi na sijasikia gari likiwashwa!”

Uso wa Shamla ukahamaki.

“Sikiliza wewe! Unajua tunaweza ukuweka ndani na kukufungulia kesi…!”

“Nimefanya nini…?”

“Kwanini hutaki kusema ukweli?”

“Mnaweza kudhani ninasema uongo lakini ukweli wangu ndio huo. Lile gari ndio sasa nagundua halipo!”

“Hakutoka nalo hapa?” Shamla akamuuliza.

“Hakuna gari lililotoka hapa”

“Na mwenye gari hukumuona?”

“Sijamuona1”

Shamla na mwenzake wakatoka na kujipakia kwenye gari lao walilokuwa wameliacha mbele ya geti.

“Mimi naamini yule mlinzi anasema ukweli,” Shamla alisema wakati analiwasha gari.

“Kwa hiyo lile gari nalo limetoweka kama alivyotoweka mwenyewe?”

“Ameondoka nalo kimiujiza bila kuonekana”

“Itakuwa ni kweli Shamla”

“Nitakwenda kumueleza mkurugenzi. Hii kazi ya kumkamata huyu mtu itakuwa ngumu!”

                                              ***************

Simu ya mkuu wa jeshi la polisi ilipoita juu ya meza yake, afisa huyo alikuwa amesimama kando ya dirisha akiwaza. Aliposikia simu inaita alirudi kwenye kiti akaketi na kuipokea.

Ilikuwa simu iliyotoka kwa mkurugenzi wa upelelezi.

“Niambie nini kinaendelea hapo ofisini kwako?”

“Nina taarifa ya kiongozi wa freemasons aliyetakiwa kukamatwa”

“Ameshaamatwa”

“Hapana, alishindikana kukamatwa. Alitoweka kimiujiza mbele ya vijana wangu na kugeuka moshi unaowasha!”

“Unasemaje?”

Mkurugenzi wa upelelezi alimueleza kwa undani kuhusu tukio hilo kama alivyoelezwa na Shamla.

“Unataka uniambie anatumia uchawi?”

“Kusema kweli hatuna vigezo vya kutambua uchawi na hatujajua anatumia nini!”

“Inasemekana wanajihusisha na vitu kama hivyo. Inawezekana kuwa ni kweli. Sasa acha kwanza hili suala nimueleze rais”

“Sawa afande”

Mara tu mkuu huyo alipomaliza kuzungumza na mkurugenzi wa upelelezi alipiga simu ikulu na kuomba kuzungumza na rais. Simu yake iliunganishwa na simu ya rais.

“Mheshimiwa rais habari ya muda huu?”

“Nzuri tu, mnaendeleaje na kazi?”

“Tumepatwa na tatizo kidogo”

“Tatizo gani?”

Mkuu wa jeshi la polisi akamueleza rais kuhusu mkasa uliowatokea kina Shamla.

“Hii inadhihirisha ukweli wa madai yanayotolewa kwamba watu hao wanajihusisha na ibada za mashetani” Rais Shanga alimwambia mkuu wa jeshi la polisi baada ya kumsikiliza wa makini.

“Ni kweli lakini katika usajili wao walijiandiisha kama taasisi ya kimataifa inayotoa misaada kwa jamii”

“Hapo mwanzo walifahamika hivyo lakini hivi sasa serikali imeshawatambua kuwa wanajihusisha na ibada za kimashetani”

“Kuna madai pia kwamba hawaingilii dini ya mwanachama wao awe muislamu, mkristo au pagani”

“Lakini unapoabudu shetani, maana yake umeshajitoa kwenye dini yako. Unakuwa katika dini ya kuabudu shetani. Watu wengi wamejiunga nao kwa tamaa ya kupata utajiri”

“Ilikuwa ni sahihi kuzuia shughuli zao hapa nchini kwetu. Uchunguzi umeonesha kuwa vijana wengi walikuwa mbioni kujiunga na kundi hilo”

“Ni kweli…sasa sikiliza…”

“Ndiyo mheshimiwa”

“Huyo kiongozi wao asiwasumbue, muacheni. Umenielewa?”

“Nimekuelewa”

“Sawa”

Shanga alirudisha mkono wa simu na kuendelea na kazi zake nyingine.

Mchana wa siku ile Shanga alikuwa akifanya ziara katika magereza ya Maloto ili kujionea hali halisi ya magereza pamoja na kuzungumza na wafungwa.

Katika ziara yake Shanga pia alizungumza na mwanamke mmoja aliyefika katika gereza moja kumtembelea mume wake aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka kumi. Mwanamke huyo alifika katika gereza hilo akiwa na watoto watatu.

Alimueleza rais matatizo aliyokuwa anakabiliana nayo tangu mumewe awe kifungoni.

“Ameniachia watoto wanne ambao hivi sasa hawapati huduma yake. Hawa wawili wakubwa wamekatisha masomo kwa sababu ya ukosefu wa ada, hivi sasa wanazurura tu mitaani kuombaomba na ni watoto wa kike. Nina hofu kuwa wanangu watakuja kubakwa au kupata mimba za utotoni,” mwanamke huyo alimueleza Rais Shanga na kuongeza.

‘’Tunapopata nafasi kama hivi huwa tunakuja kumtembelea kujua hali yake laini haitupi matumaini yeyote kwa maisha yetu.”

Rais Shanga baada ya kumsikiliza yule mwanamke aliagana naye. Aliporudi ofisini kwake alimuita waziri mkuu na kumueleza juu ya ziara yake aliyoifanya kwenye magereza.

“Nimepata wazo moja la msingi sana. Mfumo uliopo sasa wa kuwapa adhabu za vifungo watu wanaopatikana na hatia una kasoro kubwa”

“Una kasoro gani mheshimiwa?” Waziri mkuu akamuuliza.

“Huu mfumo hautoi adhabu kwa mfungwa peke yake bali unatoa adhabu hata kwa watu wasiohusika na lile kosa”

Rais Shanga alitoa mfano wa yule mwaname aliyezungumza naye gerezani ambaye watoto wake wamekatizwa masomo kwa sababu ya ukosefu wa ada na kuanza kuwa ombaomba.

“Adhabu ya huyu baba tayari imeshaleta athari kwa maisha ya sasa na ya baadaye ya watoto wake na familia yake kwa ujumla”

“Ni kweli mheshimiwa lakini hali hii ndiyo ipo katika nchi nyingi za Kifrika”

“Sasa mimi nataka tubadili huu mfumo, watu wasiohusika wasiteseke kwa makosa ya watu wengine. Au kwa maneno mengine wafungwa wenye familia waweze kuzihudumia familia zao wakiwa vifungoni”

“Mfumo huo utakuwaje mheshimiwa?”

“Nimefikiria mambo kadhaa. Kwanza nimeona serikali inapoteza mamilioni ya pesa kila mwaka kwa kuwahudumia wafungwa ambao hawazalishi chochote”

“Ni kweli mheshimiwa”

“Nimejiuliza kwanini tusiyafanye magereza kuwa moja ya sehemu za uzalishaji wakati nguvu kazi nyingi ipo pale!”

Waziri mkuu alikuwa akimsikiliza Rais Shanga kwa makini.