Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sitaki tena Urais – Sehemu ya 23

Muktasari:

  • “Nimejiuliza kwanini tusiyafanye magereza kuwa moja ya sehemu za uzalishaji wakati nguvu kazi nyingi ipo pale!”

Ilikoishia

“Nimefikiria mambo kadhaa. Kwanza nimeona serikali inapoteza mamilioni ya pesa kila mwaka kwa kuwahudumia wafungwa ambao hawazalishi chochote”

“Ni kweli mheshimiwa”

“Nimejiuliza kwanini tusiyafanye magereza kuwa moja ya sehemu za uzalishaji wakati nguvu kazi nyingi ipo pale!”

Waziri mkuu alikuwa akimsikiliza Rais Shanga kwa makini.

SASA ENDELEA


Shanga aliendelea. “Nilichokusudia hapa ni kuwa wafungwa wapewe miradi ya kuzalisha mali wakiwa magerezani na sehemu ya mapato yatakayopatikana iwekwe kwenye akaunti ya mfungwa mwenyewe benki, na sehemu nyingine ihudumie familia yake iliyoko nje. Kama ana watoto, pesa zake zitumike kulipia ada zao.”

“Ni wazo zuri sana.”

“Hilo ni moja. La pili ni kwamba nisingependa kuona sheria zetu zinawafarikisha wanandoa. Mwanamke hawezi kumsubiri mume wake anayetumikia kifungo cha miaka kumi kwa sababu anahitaji huduma.

“Ni lazima atadai talaka na kuolewa na mume mwingine. Sasa kwa mpango huo wa kuyageuza magereza kuwa sehemu za uzalishaji mali, mwanamke huyo ataweza kupata huduma kutoka kwa mume wake aliyeko kifungoni. Lakini mbali na hilo, pia tunataka kuwakutanisha faragha mume na mke angalau mara moja kwa mwezi.”

“Mawazo yako nimeyaafiki moja kwa moja, mheshimiwa.”

“Sasa jukumu ninaliacha kwako la kushirikiana na wizara husika kuandaa muswada wa sheria ili kuingiza mfumo huo hapa nchini kwetu.”

“Nimelipokea jukumu hilo na nitakwenda kulifanyia kazi, mheshimiwa.”

Wakati serikali ya Rais Shanga ikiendelea kuandaa muswada wa sheria utakaoleta mabadiliko katika magereza, viongozi saba wa Freemason walikuwa wakiendelea kushikiliwa na serikali.

Ulipita mwezi mmoja na Rais Shanga alikuwa ameshaanza kusahau kuwa kulikuwa na watu aliowaweka kizuizini.

Usiku mmoja aliamshwa na mlio wa simu yake ya mkononi aliyoiweka kwenye kimeza cha pembeni mwa kitanda.

Simu iliita kwa sekunde kadhaa kabla ya Shanga kuamka usingizini. Aliwasha taa ya pembeni, akatazama saa kabla ya kuichukua simu.

Saa ilimwonyesha kuwa ilikuwa saa tisa usiku. Namba aliyoiona kwenye simu ilikuwa ya mwanawe Otis aliyekuwa akisoma nchini Canada.

“Hello, Otis!”

“Ndiyo baba, nipo kwenye matatizo! Nimetekwa nyara na watu nisiowafahamu. Wamesema...!” Sauti ikatoweka kwenye simu.

“Otis... Otis... unasemaje?”

Rais Shanga alikuwa ameshtuka.

“Baba, nipo mahali nisipopafahamu... Maisha yangu yapo hatarini!” Sauti ya Otis ilisikika kwa mbali kabla ya kutoweka tena.

“Otis, unasema uko wapi? Nani waliokuteka? Otis... Otis...?”

Shanga aligundua kuwa alikuwa akizungumza peke yake. Simu ya upande wa pili ilikuwa imeshakatwa.

Akiwa ametaharuki, Shanga alitenga shuka, akaketi kitandani na kumpigia tena mwanawe. Licha ya kujaribu kupiga mara kadhaa, simu ya upande wa pili haikupatikana.

Akamuamsha mke wake.

Joyce alipoamka, alimuuliza, “Kuna kitu gani?”

“Otis amenipigia simu sasa hivi. Ameniambia ametekwa nyara na maisha yake yako hatarini!”

“Ametekwa nyara?”

Joyce aliinuka na kuketi.

“Amesema ametekwa nyara na watu asiowafahamu na maisha yake yako hatarini.”

“Ametekwa nyara wapi?”

“Wakati namuuliza, mawasiliano yalikatika. Nimejaribu kumpigia, lakini simu yake haipatikani.”

“Labda ameizima.”

“Pengine si yeye, ni hao waliomteka.”

“Otis anataka kutuletea wasiwasi mwingine. Sasa sisi tutaelewa nini?”

“Ninaamini kuna tatizo. Asingepiga simu usiku kama huu.”

“Mtoto wetu ni huyo huyo aliyebaki. Sasa hao waliomteka watakuwa kina nani na wanataka nini?”

“Itanibidi niwasiliane na waziri wa mambo ya nchi za nje nimfahamishe afanye mawasiliano ili tupate taarifa za uhakika.”

Rais Shanga alitumia simu ya mezani kumpigia waziri wake wa mambo ya nchi za nje. Simu iliita kwa sekunde kadhaa kabla ya waziri kuipokea.

“Mheshimiwa Rais!” Sauti nzito ya mtu aliyetoka usingizini ilisikika.

Rais Shanga akamweleza kuhusu simu aliyopigiwa na mwanawe usiku ule kutoka Canada.

“Nataka ufanye mawasiliano sasa hivi na balozi wetu wa Canada tujue ni tatizo gani limemtokea mwanangu.”

“Sawa, mheshimiwa. Nitafanya mawasiliano sasa hivi.”

Waziri wa mambo ya nchi za nje naye alimpigia balozi wa Kamisa nchini Canada usiku uleule.

Kwa saa za Canada, jua lilikuwa limeshaanza kuchwa. Balozi aliipokea simu akiwa ofisini kwake.

Baada ya kuelezwa kuhusu madai ya mwana wa rais kutekwa nyara na watu wasiofahamika, balozi huyo alijibu.

“Sina taarifa yoyote.”

“Rais ametaka ufuatilie suala hili halafu utupatie majibu.”

“Sawa. Nitafuatilia.”

Balozi wa Kamisa nchini Canada, baada ya kupata agizo hilo, alichukua kitabu cha simu, akatafuta namba ya chuo alichokuwa akisoma Otis.

Alipata namba kadhaa, ikiwemo ya mkuu wa chuo hicho, akampigia.

Simu ilipopokelewa, balozi alijitambulisha na kumuuliza mkuu wa chuo hicho kuhusu Otis, mwana wa Rais wa Kamisa.

“Mimi kwa sasa nipo nyumbani, siko ofisini na sifahamu kama kuna tukio lolote,” sauti ya mkuu wa chuo hicho ilisikika kwenye simu.

“Nimepata habari zisizothibitishwa kuwa Otis ametekwa nyara na watu wasiofahamika.”

“Umepata wapi habari hizo?”

“Nimepigiwa simu sasa hivi kutoka nyumbani.”

“Wao wamejuaje?”

“Otis alimpigia simu baba yake na kumfahamisha kuwa ametekwa na yuko hatarini. Lakini mawasiliano hayakuendelea na simu ya Otis haipatikani hadi sasa.”

“Hii ni habari nzito. Subiri nifuatilie halafu nitakujibu.”

Kwa muda wa karibu saa nzima, mkuu wa chuo hicho alifanya mawasiliano ya simu na watu mbalimbali katika chuo alichokuwa akikiongoza.

Maelezo aliyoyapata kuhusu Otis ni kuwa hakuwa ameonekana chuoni kwa siku mbili na usiku uliopita hakulala katika bweni la wanafunzi.

Mkuu wa chuo hicho aliitafuta namba ya simu ya Otis na alipoipata alijaribu kumpigia, lakini simu ya Otis haikupatikana. Baada ya hapo alimpigia balozi.

“Ni kweli Otis hajaonekana chuoni kwa siku mbili na jana usiku hakulala katika bweni la chuo,” mkuu wa chuo alimwambia balozi kwenye simu.

“Itakuwa ni kweli ametekwa nyara!”

“Hatuwezi kupuuza dai hilo. Ni lazima uchunguzi ufanyike kujua yuko wapi.”

“Sasa nani atafanya uchunguzi huo?”

“Kwa vile kuna madai ya kutekwa nyara, inatubidi turipoti polisi na polisi watafanya uchunguzi huo ili kupata ukweli.”

“Sasa ningependa tukutane mimi na wewe tushughulikie suala hilo.”

“Kama uko tayari, unaweza kuamua kufika nyumbani kwangu ama mimi nifike ulipo.”

“Mimi bado niko ofisini. Nitashukuru sana kama utafika ofisini kwangu.”

“Sawa. Ninakuja sasa hivi.”

Haukupita hata muda wa nusu saa, mkuu huyo wa chuo alifika katika ofisi za ubalozi wa Kamisa nchini humo.

Baada ya kukutana na balozi wa Kamisa, walipanda magari mawili tofauti kuelekea kwenye makao ya polisi. Mkuu wa chuo, ambaye alitangulia kuondoka, aliendesha gari lake wakati balozi alitumia gari la ubalozi.

Dakika chache baadaye, watu hao wakawa ndani ya ofisi ya kamishna wa polisi wa jimbo hilo. Baada ya kujitambulisha, walimweleza tatizo lililowapeleka kwake.

“Ni lini mwanafunzi huyo alipiga simu kwa mzazi wake kumjulisha kuwa ametekwa nyara?” Kamishna wa polisi alimuuliza balozi.

“Ni leo hii,” balozi alipomjibu, kamishna huyo alimgeukia mkuu wa chuo na kumuuliza.

“Umegundua ni tangu lini kijana huyo hajaonekana hapo chuoni?”

“Leo ni siku ya pili hajaonekana.”

“Ana tabia ya kutoonekana chuoni hapo kwa siku mbili au tatu bila ruhusa?”

“Nimejulishwa kuwa hakuwa na tabia hiyo.”

Kamishna akamgeukia tena balozi.

“Huyo kijana alipiga simu kwa mzazi wake muda gani?”

“Nimeambiwa ilikuwa saa tisa usiku kwa saa za kule, ambapo kwa saa za huku huenda ilikuwa saa kumi na nusu jioni hii.”

“Unazifahamu namba za simu za huyo kijana alizotumia kumpigia baba yake?”

“Ninazifahamu. Namba zake ninazo.”

Balozi alitoa simu yake, akazitafuta namba za Otis kisha akamtajia kamishna ambaye aliziandika kwenye karatasi.

Alipomaliza kuandika, aliinua simu na kumpigia mkurugenzi wa idara ya upelelezi.

Mkurugenzi alifika baada ya muda mfupi tu. Kamishna alimtambulisha kwa wageni waliokuwa ofisini kwake na kumweleza tatizo lao.

“Sasa nenda nao ukalishughulikie suala lao,” kamishna alimwambia.

Mkurugenzi huyo alitoka na wageni hao. Kutoka ghorofa ya saba, ilikokuwa ofisi ya kamishna wa polisi, walishuka kwa lifti hadi ghorofa ya tatu, ilikokuwa ofisi ya mkurugenzi wa upelelezi.

Walipoingia ofisini humo, mkurugenzi huyo aliwauliza maswali na kuandika maelezo yao. Alipomaliza kuandika, aliwaambia waende zao.

“Nitalishughulikia suala lenu na mtapata majibu,” akawaambia. Balozi na mkuu wa chuo walipotoka, mkurugenzi huyo alimpigia simu kachero wa idara ya upelelezi, William Biro, na kumuita.

“Tafadhali fika ofisini kwangu sasa hivi. Ninakusubiri.”

“Nitarajie baada ya robo saa.”

“Sawa.” Wakati anapigiwa simu, kachero William alikuwa amekaa baa akizungumza na msichana mmoja aliyekuwa akifanya kazi hapo.

“Nimeitwa. Nitakuja kukuona usiku, sawa?” William alimwambia msichana huyo huku akinyanyuka kwenye kiti.

“Sawa,” msichana alimjibu huku akimtazama kachero huyo akiondoka.