Sitaki tena Urais – Sehemu ya 13
UTANGULIZI
Asubuhi kulipokucha Shanga alizuia taarifa ya kifo cha mwanawe isitolewe kwenye vymbo vya habari mpaka kwanza wapokee taarifa ya uchunguzi wa polisi wa Canada kuhusiana na kupote kwa mwili wa mwanawe hoyo.
Lakini vyombo vya habari vya nje vilianza kuliripoti tukio hilo wakati ikulu ya Kamisa ikiwa kimya.
Mpaka inafika saa saba mchana Rais Shanga alipokea taarifa ya maandishi ya uchunguzi wa awali wa polisi wa Canada juu ya kupotea kwa mwili wa marehemu Jimmy ukiwa katika chumba cha maiti katika hospitali ya serikali nchini humo.
SASA ENDELEA
Taarifa ilieleza kuwa kulihitajika uchunguzi zaidi kuhusu kupotea kwa mwili huo, kwani kupotea kwake kulikuwa kwa kimiujiza. Polisi walieleza kuwa hawajajua mwili huo ulipoteaje na wanaendelea kuwahoji madaktari walioupokea pamoja na wafanyakazi wa chumba cha maiti.
Shanga akamweleza mke wake kuhusu taarifa iliyotoka Canada.
“Sasa tutazika nini?” mke wake akamuuliza kwa mshangao. “Maiti inapoteaje? Basi mwanangu hakufa!”
“Kifo chake kimeshathibitishwa, isipokuwa mwili wake ndio hauonekani.”
“Mwili wa mtu utapoteaje mpaka polisi washindwe kufahamu!”
“Ndiyo, hatuwezi kuelewa, mke wangu. Inabidi tuendelee kusubiri uchunguzi wa polisi.”
“Sasa tutazika nini?”
“Ondoa shaka, suala hili linashughulikiwa.”
Ilikuwa siku ya tatu tangu kutokea kwa tukio hilo. Ikulu ya Kamisa iliamua kutoa taarifa ya kifo cha Jimmy na ubalozi wa Canada ukatoa taarifa ya serikali ya Canada ya kuiomba radhi serikali ya Kamisa kutokana na kupotea kwa mwili wa mwana wa Rais Shanga uliokuwa umewekwa mochwari katika hospitali ya serikali nchini humo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa polisi nchini humo wanaendelea na uchunguzi ili kujua mwili huo umepoteaje na watatoa taarifa kwa serikali ya Canada mara tu uchunguzi huo utakapokamilika.
Wiki moja baadaye, Rais Shanga na mke wake, wakishirikiana na viongozi wa kanisa lao, walifanya taratibu zote za mazishi bila kuwepo kwa mwili wa marehemu. Walichukua hatua hiyo baada ya kutoona dalili yoyote ya kupatikana kwa mwili wa marehemu Jimmy.
Pia Shanga alimzuia mwanawe Otis aliyekuwa Canada kutokwenda nchini humo kuomboleza msiba wa kaka yake kwa hofu kwamba watu wa kundi alilojiunga nao wangemuona.
Baada ya kumalizika kwa msiba huo, ambao ulihitimishwa bila ya kupatikana kwa mwili wa marehemu, Shanga aliwaita wale wasaidizi wake wawili wa Ikulu na kuwaambia.
“Nimewaita kuwaeleza kuwa kitendo kilichofanyika cha kumla mwanangu kimeniuma sana na kimenifanya nifikirie upya ushiriki wangu katika chama chenu.”
“Lakini, mheshimiwa, hilo ni suala tulilokubaliana kabla. Wewe mwenyewe ulikubali kumtoa mwanao,” mmoja wa maafisa hao alimwambia.
“Kwani nyinyi si mlijua mwanangu anasoma Canada?”
“Ndiyo, tulijua.”
“Sasa kwa nini mlifanya vile?”
“Yalikuwa ndiyo masharti ya wewe kupata urais,” afisa mwingine akamjibu Shanga.
“Si mngesubiri nimtoe mwenyewe?”
“Muda ulikuwa umeshafika wa kutimiza sharti letu.”
“Kumbe ndivyo mnavyofanya hivyo?”
“Ndiyo, mheshimiwa.”
“Sasa mimi ninawaambia kuwa ninajitoa katika kundi lenu na si mwanachama wenu tena!”
“Kama umeshajiunga, huwezi kujitoa tena,” maafisa wote wawili walimjibu kwa pamoja.
“Kwa nini nisiweze? Nani atanilazimisha?”
“Ndiyo sheria zetu, mheshimiwa,” mmoja wa maafisa hao alimwambia huku sauti yake ikionyesha utulivu.
“Mimi silazimiki kufuata sheria zenu. Nilijiunga kwa hiari yangu na ninajitoa kwa hiari yangu.”
“Haitawezekana, mheshimiwa. Umeshakuwa rais.”
“Wananchi ndio wamenichagua niwe rais wao, si nyinyi!”
“Sisi ndio tumetia ushawishi kwa wananchi.”
Shanga akatikisa kichwa kwa hamaki.
“Hakuna kitu kama hicho!” Sauti ya Shanga ilizidi kupanda.
“Nimefanya kampeni nchi nzima kuwashawishi wananchi wanichague na wamenichagua. Nyinyi mnasema nini?”
Maafisa hao aliokuwa akibishana nao wakanyamaza kimya.
“Ninawaambia wazi kuwa sikubaliani na kitendo mlichofanya na kimeniuma sana. Kwa hiyo nimeamua kujiengua kutoka kwenu. Kuanzia sasa mimi si mwanachama wenu. Nendeni mkamwambie Osaka,” Shanga akamaliza.
Asubuhi ya siku iliyofuata, rais huyo aliamka akiwa na mawazo mengine. Alikuwa amefikiria kwamba asingeweza kuwa karibu na watu hao kwa sababu ya kuwaona kuwa ni watu hatari. Hivyo akawafukuza kazi.
Juma moja baada ya tukio hilo, ujumbe wa maafisa kumi wa serikali ya Kamisa, ukiongozwa na waziri wa mambo ya nchi za nje, ulikuwa na ziara ya kutembelea nchi kadhaa za Ulaya, ikiwemo Marekani na Canada.
Madhumuni ya ziara hiyo yalikuwa kutangaza fursa za vitega uchumi vilivyokuwemo nchini humo pamoja na vivutio vya kitalii. Pia, kupanua wigo wa biashara kati ya nchi ya Kamisa na nchi za Ulaya, Marekani na Canada.
Kadhalika, Rais Shanga alikuwa amemtuma mjumbe maalumu kwenda Canada kwa ajili ya kupata taarifa kamili juu ya kupotea kwa mwili wa mwanawe Jimmy na kueleza kusikitishwa kwake kuhusu tukio hilo.
Ujumbe huo uliondoka na ndege saa nne usiku kuelekea Canada na kisha Marekani kabla ya kuzuru nchi za Ulaya.
Kabla ya kwenda uwanja wa ndege, ujumbe huo ulikuwa Ikulu ambapo Rais Shanga aliusisitizia kuwa madhumuni makubwa ya kuwatuma huko ni kutangaza fursa za vitega uchumi vilivyokuwemo nchini humo.
“Nataka mkazitangazie nchi hizo fursa tulizonazo za vitega uchumi katika sekta ya madini. Tunayo madini ya aina mbalimbali nchini kwetu.
“Pia, katika sekta ya kilimo tuna ardhi nzuri yenye rutuba na tunapata mvua za kutosha kwa mwaka. Katika sekta ya utalii tuna maeneo mengi yenye vivutio vya kitalii, ikiwemo mbuga za wanyama,” Rais Shanga aliuambia ujumbe huo.
Ndege iliyoupakia ujumbe huo iliondoka saa nne kamili usiku kuelekea Canada. Walitarajia kwamba wangefika Canada saa mbili asubuhi.
Ilipofika saa sita usiku, Rais Shanga aliamshwa usingizini kwa mlio wa simu.
Shanga alishtuka na kuinuka kitandani. Akaketi na kuwasha taa kabla ya kuunyakua mkono wa simu ambao ulikuwa umeunganishwa na mtandao wa Ikulu.
“Hello!” Shanga alisema kwa sauti nzito ya mtu aliyetoka usingizini.
“Mheshimiwa, kuna taarifa ya kushtua kidogo. Samahani kwa kukuamsha, lakini inabidi tukupe taarifa hii usiku huu,” sauti kutoka upande wa pili wa simu ikasikika.
“Taarifa gani?” Shanga aliuliza huku akiizuia sauti yake isionyeshe mshangao.
“Ndege iliyokuwa imeupakia ujumbe wetu kuelekea Canada usiku huu imekata mawasiliano mara tu baada ya kuruka na inahisiwa kwamba huenda imeanguka mahali pasipojulikana.”
“Imepatwa na hitilafu gani?”
“Haijajulikana hadi sasa ni hitilafu gani iliyotokea.”
“Umesema inakisiwa kuwa imeanguka?”
“Ndiyo, mheshimiwa.”
“Nani waliokisia hivyo?”
“Waongoza ndege wameiambia Ikulu.”
“Hilo tukio limetokea muda gani?”
“Dakika chache tu baada ya kuruka. Natumaini ilikuwa ni saa nne na dakika kadhaa.”
Shanga akatazama saa.
“Hivi sasa inakaribia kuwa saa sita. Kwa nini mmechelewa kunifahamisha?”
“Kabla ya habari hizi kutolewa, waongoza ndege walikuwa wanajaribu kupata mawasiliano na ndege hiyo. Baada ya juhudi hizo kutofanikiwa, ndipo tukaletewa taarifa.”
“Sasa nini kinafanyika hadi sasa?”
“Kuna helikopta mbili za jeshi zilizotumwa kuitafuta ndege hiyo, lakini bado hazijaleta taarifa yoyote.”
Kuanzia hapo Shanga hakulala tena.
Mpaka ilipofika saa nane usiku, Shanga alipigiwa tena simu na kuarifiwa kuwa ndege iliyokuwa inatafutwa imeonekana.
“Imeanguka katika eneo la milima ya Binzii, katika mji wa Koto ulioko kaskazini mwa Kamisa,” msemaji wa Ikulu alimwambia kwenye simu.
“Imekutwa ikiwa katika hali gani?”
“Imekutwa ikiwa vipandevipande na inawaka moto.”
Shanga akatikisa kichwa kwa masikitiko.
“Hakuna dalili kuwa kuna mtu aliyepona,” msemaji wa Ikulu aliendelea kumweleza.
“Ni pigo kubwa kwa taifa letu. Ninahitaji helikopta ili niweze kufika katika eneo hilo.”
“Helikopta tano zimeshaelekea huko. Tutawasiliana na mkuu wa Jeshi la Polisi atupatie helikopta moja.”
Baada ya muda wa saa moja, helikopta ya polisi ilitua kwenye kiwanja cha Ikulu. Rais Shanga na waziri wa mambo ya ndani pamoja na maafisa kadhaa wa Ikulu walikuwa wameshafika eneo la Ikulu.
Walipakiwa katika helikopta na kupelekwa katika eneo la tukio. Wakati wakilikaribia eneo hilo, tangu wakiwa juu waliweza kuyaona mabaki ya ndege ambayo bado yalikuwa yanawaka moto katika eneo la milima ya Binzii.
Helikopta ilitua chini. Kulikuwa na helikopta nyingine kadhaa, zikiwemo za Jeshi la Ulinzi na Polisi.
Kulikuwa na vikosi vya wanajeshi waliokuwa wakijaribu kutafuta miili ya watu, pengine wakitarajia wanaweza kumpata mtu aliyekuwa hai.
Rais Shanga na maafisa wake walisimama kando ya helikopta na kuangalia kazi iliyokuwa ikifanywa na wanajeshi hao.
Mkuu wa Jeshi la Ulinzi na mkuu wa Jeshi la Polisi walikuwa wakisimamia zoezi hilo na walipomwona Rais Shanga walimfuata.
Wakuu hao walimpigia saluti Rais Shanga na kupeana naye mikono.
“Mnaendeleaje na zoezi hili?” Shanga akawauliza, uso wake ukiwa umefadhaika.
“Tunaendelea kwa taabu kwa sababu moto unawaka na hatuwezi kuuzima,” mkuu wa Jeshi la Ulinzi alimjibu Shanga na kuongeza.